Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. 

Sherehe Ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Ushuhuda Wa Fumbo La Imani

Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba, kwenye uzima na furaha ya milele pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwa kupaa mbinguni, Kristo Yesu amemfungulia mwanadamu njia, ili akae na kuamini, kwamba, waamini ambao ni viungo vya mwili wake, amewatangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu. Rej. KKK 659-662.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho! Maana yake ni kwamba, Kristo Yesu anakamilisha mchakato wote wa uwepo wake wa kibinadamu na hivyo sasa anarudi katika utukufu wa Mungu unaojionesha katika sura ya wingu na mbingu. Lk 24:51 na tangu hapo ameketi kuume kwa Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu aliyepaa mbinguni kwa Baba ila Yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa mtu. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba, kwenye uzima na furaha ya milele pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwa kupaa mbinguni, Kristo Yesu amemfungulia mwanadamu njia, ili akae na kuamini, kwamba, waamini ambao ni viungo vya mwili wake, amewatangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu. Rej. KKK 659-662. Huyu ndiye Kristo Yesu aliyeinuliwa juu ya Msalaba, ili kuwavuta wote kwake. Ni Kuhani wa Agano Jipya na la milele anayewaombea binadamu wote mbele za Mwenyezi. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu ambapo tunatafakari masomo ya Misa ya sherehe ya Kupaa Bwana.

Sherehe ya Kupaa Bwana Ni Sehemu ya Mafumbo ya Kanisa
Sherehe ya Kupaa Bwana Ni Sehemu ya Mafumbo ya Kanisa

MASOMO KWA UFUPI: Adhimisho la Kupaa Bwana ni mojawapo ya maadhimisho ya mafumbo makubwa ya imani yetu. Na kwa kuwa ni Fumbo la Imani ni vigumu kupata maneno au maelezo ya kulifumbua au kulifafanua kinagaubaga au kwa ufasaha wa mantiki.Tunasaidiwa kwa kiasi kikubwa sana na mwanga wa imani. Ni kwa mantiki hii, masomo ambayo Kanisa linatupatia katika adhimisho hili yanatumia maneno tofauti tofauti ili kutujengea katika ufahamu wetu picha ya fumbo la kupaa Bwana kama tukio. Katika somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 1:1-11), tukio hili linawekwa ndani ya kipindi maalumu cha muda;  Siku 40 baada ya ufufuko. Zaidi ya hapo, tukio lenyewe linaelezwa kama kuchukuliwa, kuinuliwa na kupokelewa na wingu. Somo la Injili linaongeza “akachukuliwa juu mbinguni”. Hii yote ni lugha inayoleta maana kuwa kupaa Bwana ni kitendo cha Yesu kuchukuliwa kwenda juu, kuinuliwa na kupokelewa mbinguni. Na hapa mbinguni inachukuliwa kumaanisha yalipo makao ya Mungu au kumaanisha umungu wenyewe. Wayahudi mara nyingi kwa kuepuka kulitaja jina la Mungu walitumia neno mbingu kumaanisha Mungu. Kumbe, hapa Maandiko yanaposema Yesu alipokelewa mbinguni tunapata dokezo kuwa kwa kupaa kwake, Yesu alienda kuutwaa ule umungu ambao tunaweza kusema aliposhuka duniani hakuudhihirisha katika utukufu wake.

Amepaa Mbinguni ili apate kuwashirikisha waja wake Umungu wake
Amepaa Mbinguni ili apate kuwashirikisha waja wake Umungu wake

Somo la pili lenyewe linatumia lugha ya kikuhani. Tunasoma katika waraka kwa Waebrania (Ebr 9:24-28, 10:19-23) ambapo Kupaa Bwana kunafananishwa na kitendo cha kuhani mkuu kuingia madhabahuni kumtolea Mungu sadaka kwa ajili ya taifa lake lote. Hapa picha inayotolewa ni kuwa Yesu kupaa ni kitendo cha yeye kuingia katika madhabahu ya mbinguni. Sio katika madhabahu ya kawaida ya duniani, madhabahu iliyotengenezwa kwa mikono ya kibinadamu na madhabahu ambayo makuhani wakuu walizoea kuingina. Yeye ameingia madhabahu halisi ya mbinguni ili akutane uso kwa uso na Mungu amtolee sadaka kwa ajili yetu. Na sadaka anayotoa sio sadaka ya kumwaga damu ya wanyawa. Yeye anatoa sadaka ya kumwaga damu yake mwenyewe. Ni kwa sababu hiyo, sadaka anayotoa yeye ni sadaka inayofanyika mara moja tu na inatosha. Hapa tunaona wazi, kama alivyofundisha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa fumbo la Kupaa Bwana halielezwi na kifungu kimoja tu. Ni Maandiko Matakatifu yote katika ujumla wake yanayotoa ushuhuda wa fumbo hili kwa namna mbalimbali. Masomo haya pamoja na kutumia lugha ya picha kulielezea Fumbo la Kupaa Bwana, yanaeleza pia jinsi ambavyo Mitume na Kanisa la mwanzo walilipokea na kulitafsiri. Yaani, kwa mitume na kwa kanisa la mwanzo, Fumbo la kupaa Bwana lilimaanisha nini katika utume na maisha yao kwa ujumla? Kinachojitokeza waziwazi ni kuwa kwao, kupaa Bwana kulimaanisha mwanzo wa kipindi cha ushuhuda.

Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaleta maneno ya Yesu: “nanyi mtakuwa mashahidi wangu ... hadi mwisho wa dunia.” Mitume na kanisa zima walitambua kuwa Yesu sasa amemaliza kazi ya kupanda mbengu njema ya Neno la Mungu duniani. Amemaliza kazi ya ukombozi. Ni wao sasa wanapaswa kuchukua jukumu la kuieneza Habari Njema na kuendeleza kazi ya Kristo ya ukombozi. Na huku ndiko kuwa mashahidi wake.  Jambo la pili ni ahadi ya Roho Mtakatifu. Mitume na Kanisa la mwanzo linaelewa kuwa baada ya kifo cha Yesu hawawezi kuwa naye tena kama walivyokuwa wamezoea. Hawawezi kumuona kwa macho, kula naye, kuongea naye n.k kama walivyofanya mwanzo. Hata hivyo Yeye hapotei. Uwepo wake unahakikishwa kwa uwepo wa Roho Mtakatifu. Somo la kwanza na somo la Injili yote kwa pamoja yanaleta ahadi hiyo ya ujio wa Roho Mtakatifu. Naye anaelezwa kama nguvu kutoka juu itakayowafanya wawe mashahidi. Injili inatumia neno ambalo linahitaji kidogo ufafanuzi. Yesu anawaambia wanafunzi “kaeni humu mjini, yaani Yerusalemu, hadi mvikwe uwezo kutoka juu”. Anamwongelea Roho Mtakatifu kama vazi, vazi ambalo mitume watavikwa kutoka juu. Vazi hili linatukumbusha lile vazi la kwanza ambalo Mungu alimvika mwanadamu. Baada ya dhambi ya Adamu na Eva, mwanadamu alipoteza utukufu wa Mungu (Rejea Rom 3:23) akajikuta yuko uchi. Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo (Mwa 3:21) kuwa Mungu aliamua kumtengenezea vazi la ngozi na kumvika. Baada ya Kristo kumkomboa mwanadamu, vazi hilo la ngozi haliendani na hadhi mpya ya mwanadamu aliyekombolewa. Mungu anamvika vazi jipya, vazi kutoka juu, vazi ambalo ni Roho Mtakatifu. Kupaa Bwana kunaashiria sasa mwanzo mpya wa maisha na hadhi ya mwanadamu aliyekombolewa.

Fumbo la Kupaa Bwana Mbinguni Ni Sehemu ya Kanuni ya Imani ya Kanisa
Fumbo la Kupaa Bwana Mbinguni Ni Sehemu ya Kanuni ya Imani ya Kanisa

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Fumbo hili la imani ambalo tunalitafakari siku hii ya leo, Fumbo la Kupaa Bwana linanizungumzia kitu gani katika maisha yangu ya leo? Katika ufafanuzi wa masomo tumeona picha mbalimbali ambazo Biblia inazitumia kulielezea, tumeona pia namna ambavyo mitume wenyewe na Kanisa la mwanzo walivyolichukulia na sasa ni zamu ya kujiangalia wenyewe katika mazingira yetu ya sasa na katika maisha yetu ya sasa ya imani na kuona kile ambacho tunaweza kukichota na kuendelea kukichota. Binafsi ninavutwa kulitafakari fumbo hili katika nafasi mbili tofauti. Nafasi ya kwanza ni ile ambayo Mitume wenyewe mapema kabisa waliitambua. Kwamba kupaa Bwana kunaashiria mwanzo wa kipindi cha ushuhuda. Kristo haonekani tena katika mwili wake. Anahitaji kuchukua mwili wa wafuasi wake ili kwa njia yao uwepo wake uendelee kudhihirika duniani na ili kupitia wao kazi yake ya ukombozi iendelee kutendeka hadi atakaporudi. Na hapa msisitizo unakuwa si kusubiri hadi atakaporudi. Msisitizo ni kwamba wakati kanisa linasubiri Kristo arudi: linaishi, linatekeleza utume na linamshuhudia Kristo.

Ndiyo maana Kanisa katika mafundisho yake linasisitiza kutambua kuwa Kristo amepaa lakini uwepo wake unaendelea kudhihirishwa ndani ya Kanisa kwa namna mbalimbali. Wimbo maarufu wa Liturujiaunaofahamika wa jina la “Kaa nasi” unaakisi fundisho hili unapoonesha kuwa Kristo anakaa nasi katika Sakramenti zake, katika Ekaristi kwa namna ya pekee, katika watumishi wake (watumishi wa daraja), katika Jumuiya ya waamini na katika Neno lake. Nafasi ya pili inayonivuta kulitafakari fumbo hili la kupaa Bwana ni kuwa kwa kupaa kwake, Kristo ametupatia matumaini ya kutazama juu na kutazamia kutoka juu. Tunapata matumaini ya kutazama juu kwa sababu huko ndiko iliko hatima yetu. Yeye ambaye alishuka chini na kuuvaa ubinadamu wetu ametuonesha kuwa ubinadamu huu wetu hatima yake si hapa duniani tu. Ubinadamu una lengo kubwa linalovuka haya tunayoishi sasa, haya tunayoyaona sasa na haya tunayopitia sasa. Tunapata matumaini ya kutazamia kutoka juu: Kristo anatuonesha sasa kuwa tunaweza kumtumainia yeye kutoka juu atusaidie kwa neema zake katika safari yetu ya maisha ya hapa duniani. Ni kwa matumaini haya tunainua macho juu kuomba huruma, tunainua mikono juu kupeleka sala na maombi yetu mbalimbali tunapaaza sauti zetu juu kuimba, kusifu na kushukuru ukuu wa Mungu unaotuangalia na kutuongoza kutoka juu. Tumsifu Yesu Kristo.

Liturujia Kupaa Bwana
NIFUNDISHE YESU
11 May 2022, 09:03