Sherehe ya Kupaa Bwana:mbona mmesimama, mkitazama mbinguni?
Padre Paschal Ighondo – Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu katika sherehe ya kupaa Bwana, mwaka C wa kiliturujia. Tunasherehekea kupaa mbinguni kwa Yesu mwili na roho, ukamilifu wa umasiha wake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti, silaha za shetani. Hili ni adhimisho la tendo la ukombozi ambapo Kristo baada ya kufufuka kutoka wafu na kuingia katika utukufu wake na kuendelea kuwatokea wafuasi wake kwa siku arobaini/muda wa kutosha akiwaimarisha kiimani, alitoweka rasmi katika upeo wa macho yao wasimuone tena, zaidi ya kumtokea Saulo katika barabara ya Dameski (Mdo.9:1-9).
Somo la kwanza la matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11); ni wosia wa Yesu kwa Mitume kabla hajapaa mbinguni. Katika wosia huu Yesu anawaambia Mitume kuwa wanapaswa kuhubiri habari njema duniani kote pia anawaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu atakayewakumbusha yote aliyowafundisha na kuwaongoza siku zote katika kuitangaza habari njema ya wokovu. Baada ya maagizo haya Yesu “aliyochukuliwa/akainuliwa juu na wingu likampokea wasimwone tena. Na walipokuwa wakitazama mbinguni watu wawili wakawaambia; “mbona mmesimama, mkitazama mbinguni? Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja vivyo hivyo mlivyomuona akienda zake mbinguni”. Nacho kiitikiko cha wimbo wa katikati kutoka (Zab. 47:5) kinaimba; “Mungu amepaa kwa kelele za shangwe na Bwana kwa sauti ya baragumu.”
Somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef.1:17-23); ni sala ya Mitume inayotupa fundisho juu ya uweza na utajiri wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo. Mungu alimfufua Yesu Kristo toka wafu akamweka kuwa Kichwa cha Kanisa na ulimwengu. Yesu akiwa kichwa cha Kanisa yu pamoja na Kanisa daima. Yeye yuko juu ya vyote vilivyoumbwa na Mungu.
Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:46-53); Yesu kabla ya kupaa mbinguni anawakumbusha kuwa kifo, ufufuko na uenezaji wa Injili yake duniani kote, vilitabiriwa na manabii toka zamani katika Agano la Kale akisema; “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari za toba na ondoleo la dhambi”. Na nguvu ya Roho Mtakatifu itawawezesha wafuasi kuieneza Injili kwa furaha duniani kote. Baada ya kuwakumbusha habari hizi na kuwaahidi zawadi ya Roho mtakatifu akawaongoza mpaka Bethania kijiji cha Lazaro aliyemfufua, akawabariki, na kisha kuwabariki akachukuliwa juu mbinguni.
Katika lugha ya kibiblia neno kupaa ni kuhama kwa mwili wa utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, kutoka duniani na kuingia Mbinguni. Ni hali ya kutukuzwa kwa Yesu, kuwa mkuu na mmiliki wa vitu vyote mbinguni na duniani. Ni kuwa juu ya vitu vyote. Ni kurudia utukufu aliokuwa nao kabla ya umwilisho, yaani kuchukua mwili kwa mama Bikira Maria. Ni kuvikwa taji ya ushindi. Kristo ni mshindi ameshinda dhambi na mauti (Mk 16:19). Itakumbukwa kuwa; “Mmojawapo wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja na Yesu alimwambia; “Ee Bwana unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Naye Yesu akamwambia; “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mahali pema peponi” (Lk 23:42-43). Kwa maneno haya ni dhahiri kuwa hakukuwa na wakati fulani uliopita kutoka ufufuko mpaka kupaa katika maana ya kuwa na hali ya utukufu. Kwa ufufuko Yesu alitoka kaburini akiwa na mwili wa utukufu, usiofungwa na nguvu za maumbile, ndiyo maana aliweza kuingia katika chumba walimokuwamo mitume hata milango ilipokuwa imefungwa kwa kuwa alikuwa na mwili wa utukufu.
Kumbe tunapoadhimisha sikukuu hii siku ya 40 baada ya ufufuko haimaanishi kuwa Yesu aliingia katika hali ya utukufu siku 40 baada ya kufufuka. Itakumbukwa kuwa namba 40 katika bibilia ni namba ya ukamilifu. Gharika kuu mvua ilinyesha siku 40 usiku na mchana (Mw. 7:17; 8:6). Waisraeli waliingia nchi ya ahadi baada ya miaka 40 ya kutangatanga jangwani. Nabii Eliya alitembea siku 40 jangwani baada ya kupewa chakula na malaika wa Bwana. Yesu alifunga siku 40 kabla ya kuanza kazi yake ya kuhubiri. Yesu aliendelea kujionesha kwa wafuasi wake kwa siku 40 baada ya kufufuka kwake. Kumbe namba 40 ilitumika kuonesha kwamba jambo limetendeka katika ukamilifu wake yaani kadiri ya mpango wa Mungu. Kusema kwamba Yesu aliwatokea mitume kwa siku 40 kwamaanisha kwamba Yesu aliwatokea mitume kadiri ya mpango wa Mungu, na kisha hakufanya hivyo tena. Na tunaposema Yesu mfufuka alipaa mbinguni siku ya arobaini, tunamaanisha siku ambapo alionana ana kwa ana, uso kwa uso, macho kwa macho na wanafunzi wake kwa mara ya mwisho na kuwapa maagizo ya kuihubiri injili ulimwenguni mwote mpaka ukamilifu wa dahari na baada ya hapo hakuonekana tena. Na siku arobaini hapa zina maana ya muda wa kutosha, ambao Yesu mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwaimarisha ili waweze kushuhudia ufufuko wake kwa watu wote.
Kupaa juu mbinguni kwa Yesu mfufuka haimaanishi kuwa Yesu alisafiri kwenda juu angani. Kwenda juu mbinguni ni lugha ya picha inayoashiria ukuu na utukufu wake. Ni namna ya kusema kuwa Yesu amerudi katika makao yake ya milele katika hali ya utukufu wa kimungu. Wayahudi waliamini kuwa makao ya Mungu yako juu angani ndiyo maana kilele cha mlima ilichukuliwa kuwa ni sehemu ya karibu zaidi na Mungu na ni sehemu ya kukutana, kumuabudu na kumsikiliza Mungu. Ndiyo maana Mungu alimtokea Musa katika kichaka kilichowaka moto katika mlima Horebu/Sinai (Kut.3:1-6), mahali alipopokea Amri kumi za Mungu/Torah (Kut.24:12-18) na mfalme Sulemani alijenga hekalu la Mungu juu ya mlima Sayuni, mlima huo ukawa mahali pa pekee pa kukutana na Mungu. Baadaye Sayuni ukawa mji wa mfalme/Masiha kama walivyotabiri manabii (Isa.2:1-3, Zek.14:16–19; Ebr.12:22; Uf.14:1).
Itakumbukwa pia kuwa kwa wayahudi neno Juu au mbinguni pia ni jina mbadala la Mungu. Malaika Gabrieli alipompasha habari Bikira Maria alimwambia usihofu, kwa maana “Roho Mtakatifu atakujia juu yako na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli (Lk. 1:35). Zakaria katika wimbo wa kinabii anasema; “Naye mtoto ataitwa nabii wake Aliye Juu” (Lk. 1: 76). Yesu katika kuhubiri anasema; “Tubuni kwa maana ufalmwe wa Mbinguni umekaribia”. Na kabla ya kupaa, aliwaambia wanafunzi wake wasitoke Yerusalemu mpaka watakapovikwa uweza na nguvu kutoka Juu naye alichukuliwa kwenda Juu mbinguni (yaani kwa Mungu).
Sherehe hii ya kupaa Bwana mbinguni inatukumbusha kuwa maisha ya hapa duniani ni ya mda tu. Maisha ya umilele yako mbinguni Kristo aliko na ni hamu yetu kufika huko ndiyo maana sala zote katika liturujia ya sherehe hii zinatuelekeza mbinguni. Katika koleta Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.” Katika sala ya kuombea dhambihu anasali; “Ee Bwana tunaleta sasa kwa unyenyekevu sadaka yetu kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba utujalie kila tunapoyapokea mafumbo haya matakatifu, tuzidi kuyajongea ya mbinguni. Na katika sala baada ya komunio anasali; “Ee Mungu mwenyezi, wewe watujalia sisi tulio hapa duniani kushughulika na mambo ya mbinguni. Tunakuomba uuelekeze moyo wetu wa ibada huko aliko Bwana wetu, Mungu-mtu”.
Sasa ili tuweze kufika Mbinguni aliko Kristo, yatupasa tufuate agizo lake; “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Mt. 28: 19). Hili ni jukumu la kila mbatizwa. Kumbe kuihubiri injili kwa maneno na matendo yetu, kusali, kulisoma, kulitafakari na kuliishi neno la Mungu, kupokea sakramenti kwa kustahili na kutenda matendo mema ndiyo masurufu yetu ya njiani kuelekea juu mbinguni. Tuombe neema ya kuyafanya haya ili mwisho nasi tupae kwende kwa juu mbinguni aliko Yesu Kristo Bwana na Mkombozi wa maisha yetu, tukaishi naye milele yote.