Kupaa kwa Bwana Mbinguni. Kupaa kwa Bwana Mbinguni. 

Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni:Mtakuwa mashahidi wangu

Yesu anaenda mbinguni,baada ya siku 40 ya kukufuka lakini hatuachi peke yetu duniani.Anatuahidia ujio wa Roho Mtakatifu lakini pia anaahidi uwepo wake.“Tazama,mimi nipo pamoja nanyi siku zote,hata ukamilifu wa dahari."Yuko pamoja nasi kila mara.Kwa hiyo,tunahitaji kumkaribia Yesu,tunapaswa kushikamana naye na kumfuata.Hakuna kitu kinachoweza kututenganisha na upendo wake.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News katika tafakari ya liturgia ya Neno la Mungu Sherehe ya Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni siku 40 baada ya kufufuka kwake. Bwana wetu Yesu Kristo sasa ameketi mkono wa kuume wa Baba, Ameenda kutuandalia makao. Yesu amepaa mbinguni katika ubinadamu wake na katika umungu wake. Kwa kupaa kwake, tuna matumaini,  kwamba tutafufuka, na hivyo mbinguni itakuwa nyumba yetu ya milele..

Katika somo la kwanza Matendo ya Mitume 1:1-11, tunasikia Yesu akiwaambia wanafunzi wake “wasiondoke Yerusalemu, bali waingojee ahadi” ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Pia somo hili linasimulia matukio ya dakika za mwisho na kukutana kwa Kristo na mitume wake kabla ya kupaa kwake mbinguni.  Tena Kristo anawatia moyo wanafunzi wake wabaki waminifu. Muhimu zaidi, anawakumbusha kwamba mafanikio yao yatategemea uwezo wao wa kutembea na Roho Mtakatifu. Maagizo haya yamekusudiwa kwetu pia. Baada ya kuwapa maagizo hayo alichukuliwa kwenda mbinguni. Je Wakristo wa kwanza walifanya nini baada ya Yesu kuinuliwa mbinguni?. Walifanya kile ambacho Yesu aliwaambia wafanye. Walirudi Yerusalemu pamoja na Maria Mama yake, wakatumia maisha yao kusali pamoja na kusubiri zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo aliwaahidia. Hivi ndivyo Kanisa limeishi siku zote. Hivi ndivyo tunavyohitaji kuishi hadi sasa. Kukaa karibu na Yesu kwa njia ya sala, karibu na Maria Mama wa Mungu na mama yetu.

Kupaa kwa Bwana Mbinguni
Kupaa kwa Bwana Mbinguni

Mpendwa katika Kristo, kabla ya kupaa mbinguni Yesu alilipatia Kanisa lake utume huu duniani, kama tunavyosoma Injili ya Matayo 28:19-20 na pia Marko 16:15-16: “Nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kushika yote niliyowaamuru ninyi.” Yesu alikuja kuunda familia, kuunda ufalme wa Mungu. Na huo ufalme wa Mungu ni kwa mataifa yote ya ulimwengu, anataka kufanya familia moja, sisi sote watoto wa Mfalme mmoja ambaye ni Kristo. Alitaka tubatizwe kwa jina la Utatu Mtakatifu - Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mimi na wewe, kaka na dada - kila mmoja wetu ana sehemu ya kutekeleza katika kuijenga familia hiyo hapa duniani. Tuna wito mtukufu! Haijalishi wewe ni nani, uwe mwanandoa, mtawa au mkleri au kijana, wote tunautume huu  wa kwenda kutangaza habari njema ya Yesu Kristo na kuleta wokovu kwa wengine. Wokovu huja kwa kumjua Yesu. Kila kitu kinabadilika Yesu anapokuja maishani mwetu. Yeye ni mwanga, yeye ni ukweli, yeye ni uzima. Yeye ndiye njia pekee ya kupata furaha na anataka kila mmoja wetu ajue hilo. Kila mmoja wetu ameitwa kuwa mfuasi mmisionari. Ndiyo maana Yesu anasema kwa wanafunzi wake, "Mtakuwa mashahidi wangu hata miisho ya dunia." Luka 24:48.

Yesu anaenda mbinguni, lakini hatuachi peke yetu duniani. Anatuahidia ujio wa Roho Mtakatifu lakini pia anaahidi uwepo wake. "Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari." Yuko pamoja nasi kila mara. Kwa hiyo, ndugu zangu, tunahitaji kumkaribia Yesu, tunapaswa kushikamana naye na kumfuata. Hakuna kitu kinachoweza kututenganisha na upendo wake. Tuombe neema ya kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu katika maisha yetu.

Kupaa kwa Bwana Mbinguni
Kupaa kwa Bwana Mbinguni

Katika injili ya Luka 24:46-53 ambayo inasomwa katika Sherehe ya Kupaa Kwa Bwana Mwaka C. Yesu alijua kwamba mitume wake walihitaji msaada ili kufanikiwa. Kwa hiyo akawaagiza: “... kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Kama tulivyosikia pia katika somo la Kwanza.  Lazima tutafute nguvu hii ili kuwezesha utume wetu kuwa na ufanisi zaidi.   Kwa hiyo, lazima tuzingatie kile Yesu alichowaambia mitume wake kabla ya kupaa kwake.  Bwana anajua jinsi kazi yetu ilivyo ngumu na kile kinachohitajika ili kufanikiwa. Anajua kwamba ni Roho Mtakatifu pekee anayeweza kutusaidia. Kwa hiyo, Kupaa kunaashiria mwanzo wa utimilifu wa ahadi ya Kristo kwetu. Kwa hiyo, tunapoadhimisha sherehe ya Kupaa, Yesu anatukumbusha kwamba bila kujali ujuzi wetu na uwezo wetu wa kibinadamu tunahitaji msaada wa Mungu ili kufanikiwa. Msaada huu wa kimungu utatoka kwa Roho Mtakatifu ambaye tunapaswa kuzingatia kila wakati. Kwa hiyo, tunapoadhimisha Kupaa kwa Kristo na kutarajia utimilifu wa ahadi yake siku ya sherehe ya Pentekoste, tuombe hivi: “Ee Bwana, tuma Roho wako, ukaufanye upya uso wa nchi.

Ndugu zangu, tunahitaji kukaa pamoja, kusali pamoja, ndiyo maana tunajumuiya ndogo ndogo, ambalo ni mojawapo ya matunda ya AMECEA. Tuombee mkutano wa AMECEA utakaofanyika siku za karibuni Tanzania uwe na mafaniko makubwa. Lakini pia tunaendelea na mchakato wa kanisa la kisinodi lenye kutembea pamoja. Tunahitaji mshikamano wa kweli kama familia moja, mwili mmoja, kusikiliza sauti ya Mungu kama kanisa. Mtakatifu Paulo kwa waefeso 1:17-23 anatuambia katika somo la pili kwamba Kanisa ni mwili wa Kristo duniani na kwamba yeye ndiye kichwa. Ikiwa Kristo ndiye kichwa chetu, hiyo ina maana kwamba tunapaswa daima kujitahidi kuwa na nia ya Kristo - kufikiri kama Kristo na kutenda kama Kristo; anavyotaka tumpenda Mungu na kupendana sisi kwa sisi. Tunahitaji kupenda kama Yesu Kristo. Kwa hiyo ndugu zangu wapendwa, leo tumekuwa mashahidi wa kile ambacho Mtakatifu Paulo anakiita “ukuu wa uweza wake sisi tuaminio”.

Kupaa kwa Bwana Mbinguni
Kupaa kwa Bwana Mbinguni

Yesu alishuka kutoka mbinguni ili kushiriki maisha yetu ya kibinadamu, katika mateso na furaha zetu zote. Leo anapaa mbinguni ili tuweze kumfuata. Yeye ni njia inayongoza kwenda mbinguni, ikiwa tunatembea na Yesu anayekwenda pamoja nasi. Kwa hiyo tuendelee kutembea pamoja naye. Paulo anasali akimwomba Mungu atupelekee Roho Mtakatifu: “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo awape ninyi Roho wa hekima na utambuzi wa mambo yaliyofunuliwa, ili kuwaletea maarifa yake kamili. Ni lazima tumwalike Roho Mtakatifu atuongoze katika  utume wetu. Ni lazima tumwalike atie nuru kwenye giza ya maisha yetu jinsi Paulo anavyoomba: “Na ayatie nuru macho ya nia zenu, mpate kuona tumaini ambalo mwito wake unalo kwa ajili yenu...” Ef.1:18  Ni lazima tumwombe aongoze njia zetu.  

Na wiki hii, tunaposubiri ujio wa Roho Mtakatifu katika Sherehe ya Pentekoste, tumwombe Bikira Maria, Mama wa Kanisa, atuombee tupate kila neema katika maisha yetu ili tuweze kutekeleza utume tuliokabidhiwa - kuwa wanafunzi wamisionari, tukiishi kwa utukufu wa Mungu na wokovu wa roho za watu. Kupaa ni sherehe inayodumisha tumaini la Wakristo kwamba siku moja tutakuwa pale Kristo alipo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (665-667), inafundisha kwamba: "... Yesu Kristo kichwa cha Kanisa hututangulia kuingia katika ufalme wa utukufu wa Baba yake, ili sisi viungo vya mwili wake tupate kuishi katika matumaini ya siku moja kuwa naye milele."

28 May 2022, 11:09