Tafuta

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 

Siku ya 59 ya Kuombea Miito: Changamoto Za Miito Mitakatifu

Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022, Mwaliko ni kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Sinodi, Kanisa linalomsikiliza Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 anawaalika waamini kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalomsikiliza Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi. Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika Tafakari ya changamoto kupata vijana katika miito ya Utawa na Upadre leo. Dominika ya 4 ya Pasaka ni Dominika ya Mchungaji mwema. Dominika ya kuombea Miito Mitakatifu katika Kanisa. Kuwaombea ambao tayari wapo katika miito hiyo lakini pia kuombea kupata watendakazi wengi katika shamba la Bwana. Leo tutatafakari kwa ufupi juu ya changamoto za kupata vijana wenye miito mitakatifu katika Kanisa kwa nyakati za sasa hasa nchini Tanzania, pamoja na kwamba bado hatuna shida sana kama ilivyo katika nchi za Ulaya na Amerika kaskazini. Lakini kama wanavyosema changamoto ya mwenzako iwe pia ni fursa kujipanga ili usikumbwe na tatizo lile lile. Hata hivyo kadri tunavyoendelea hali hiyo inakuja kwetu kutokana na sababu nitakazoeleza hapo chini.  Tunapoongolea miito mitakatifu tunamaanisha: Ndoa, Daraja Takatifu na Utawa. Lakini katika miito hiyo kuna wale ambayo tayari wapo kwenye hiyo miito na wale ambayo wapo njiani yaani malezini na wale ambao wanasubiriwa kuingia katika miito hiyo.

Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu
Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu

Mimi nitaongelea changamoto za kupata vijana katika miito hiyo ingawa pia nitagusia wale ambao wapo malezini na pia wale ambao tayari wapo ndani ya miito hiyo.  Baada ya kuona changamoto zilizopo tutajaribu kuona namna gani tufanye ili kunusuru upungufu wa watenda kazi katika shamba la Bwana. Kwa nyakati za sasa kanisa limeanza kupungukiwa watenda kazi katika shamba lake yaani watu waliokwenye miito hiyo mitakatifu. Kwa mfano miaka ya sasa ni wachache wanaofunga ndoa na kuishi kwa uaminifu katika ndoa. Ndoa ni mahali ambapo tunapata miito ya Utawa, Upadre na pia wanandoa wengine. Yaani miito yote inaanza kwenye familia. Hivyo familia ndiyo chimbuko la miito yote. Familiia inapolega lega miito mitakatifu italega lega. Miaka ya sasa ni wachache wanapata upadre katika majimbo mengine Tanzania kuna miaka inapita bila kupadrisha hata padre mmoja na pia hata mashirika baadhi mwaka unapita bila kupadrisha na pia hata nadhiri. Hebu tuone sasa namna gani familia inaweza kuchangia kuwa chanjo cha kupungukiwa na miito mitakatifu. Lakini pia mapadre na watawa nao kushiriki kwa namna fulani kufifisha miito katika kanisa. Tunaanza na familia kuwa chanjo kikubwa.

Mpendwa msikilizaji: Leo familia nyingi hazina nafasi ya kusali pamoja, hata kupeleka watoto au kufuatilia watoto kama wameenda kanisani hakupo. Familia nyingine hazijishughulishi na malezi bora kwa watoto wao, kila mmoja bize na kazi na wakirudi bize na simu na watoto wanasimu zao. Kila mmoja anahangaika na mawasiliano ya watu mbalimbali walio mbali na nyumbani, lakini pale nyumbani hakuna hata kuongea. Hivyo hawafuatilii maadili ya watoto wao. Kutokana na hilo kumepelekea kuporomoka kwa maadili katika familia. Hapa ni kwamba wazazi maadili yao wenyewe si mazuri hivyo huwezi kutegemea watoto wakawa na maadili mazuri. Mti mzuri hujulikana kwa matunda yake, na mti mbaya hujulikana kwa matunda mabaya.  Kwa mfano wazazi wote walevi, au wezi, au waongo, hawajiheshimu wenyewe, wanaongea maneno ya ovyo mbele ya watoto wao nk. Hawawezi kukemea wanapoona watoto wao wanafanya yale yale wanayofanya wao. Jambo jingine kwenye familia ni kwamba wazazi wengine hawawi tayari kuruhusu watoto wao kuingia maisha ya utawa au upadre kwa sababu ya kupunguza ukoo. Hivyo wengi wameshindwa na wanashindwa hata kama wana wito wa upadre au utawa lakini kwa sababu wazazi wamekataa na hawajapata msaada mwingine namna ya kufanya, wanakwama kuitikia wito wao na wanaingia wito mwingine. Lakini wapo wengine kinyume chake kijana anakuwa hana wito wa kuwa padre au mtawa.

Kuna changamoto nyingi katika miito mitakatifu, sala ni muhimu sana.
Kuna changamoto nyingi katika miito mitakatifu, sala ni muhimu sana.

Wazazi wanamlazimisha kijana aingie maisha hayo ambayo yeye hajisikii. Kwa hiyo kijana anakubali kwa kuwa wazazi wanataka anaenda huko. Wazazi wanataka aingie huko ili ionekane familia yao imetoa mtawa au padre. Kwa wazazi ni faraja na sifa. Hivyo wengine wanavumilia hadi mwisho na baadaye akianza utume tatizo linaanza, na ukifuatilia historia yake naye akisema alilazimishwa na wazazi, alitaka kuwaridhisha wao lakini si wito wake. Jambo jingine linalokwamisha kupata vijana katika miito mitakatifu hasa ya upadre na utawa ni umaskini kwenye familia zetu. Wapo ambao wanatamani kuingia katika utawa au upadre lakini kwa sababu wanapaswa wawe wamesoma kidato cha nne au cha sita. Lakini wazazi hawawezi kumudu kuwalipia ada na gharama nyingine, na wanashindwa kuendelea na sekondari na matokeo yake hata ndoto ya wito wao inapotea. Pia wapo ambao wanaingia katika miito mitakatifu na wakaanza malezi pengine wakaenda sekondari wakisaidiwa na shirika au parokia lakini wakimaliza na wakafaulu vizuri na wanaona upo uwezekano wa kupata kazi wanasema hana wito au wanasema hawawezi endelea sababu wanataka kusaidia familia zao. Wapo walioacha kwa sababu hiyo na wakaenda kusaidia lakini pia wapo walioacha kwa sababu hiyo na hawajawa msaada kwa familia.

Kwa upande mwingine wapo wanaotamani kuingia maisha ya kitawa au upadre baada ya kushindwa njia nyingine kwa mfano "amefeli" kidato cha nne au cha sita hana uwezekano wa kuendelea na chuo kikuu unasikia wakiulizia mashirika wakisema walau wawe mabradha. Mara kadhaa nimewauliza nani alisema “Mabradha” ni watu waliofeli ambao hawana uwezekano wa kuendelea na Chuo kikuu au kupata ajira. Kwa hiyo inakuwa kuingia wito ni baada ya kushindwa maisha mengine kumbe, si hivyo. Inakuwa maisha ya utawa au upadre kama sehemu ya maisha ya watu ambao hawakupata fursa nzuri kwa maisha ya kawaida, kumbe, utawa au upadre ni wito siyo kazi ya mshahara. Shule wanazopitia. Wapo vijana ambao baada ya kukosa mwongozo mzuri kwenye familia wanaweza kupata msaada kwenye shule wanazosoma; shule ya msingi na hata sekondari. Lakini huko wanakosoma hakuna kupata vipindi vya dini katoliki wanapata elimu dunia tu na wakati mwingine madhehebu mengine wanafundisha vipindi vya dini lakini wakatoliki hakuna. Na kuna baadhi ya shule unakuta wanafunzi wenyewe kama kuna TYCS wanafundishana wao kwa wao hata kama hawana uelewa mpana. Kwa hali kama hiyo si wote watavutiwa kwenda huko na pia hakuna wakuelezea juu ya miito mitakatifu. Lakini kama kungekuwa na padre, bradha, sista au katekista anafundisha dini na kuelezea miito mitakatifu ingesaidia. Wapo pia ambao wanakuwa na mategemeo makubwa sana kuwa wakiwa watawa au mapadre kuna mambo watapata. Lakini wakifikia wanakuta ni tofauti na yale matarajio.

Kanisa linawahitaji mashuhuda amini wa uinjilishaji, ili kuwavuta vijana katika utawa.
Kanisa linawahitaji mashuhuda amini wa uinjilishaji, ili kuwavuta vijana katika utawa.

Baadhi yao huacha wito wao hata kama wamepadrishwa au kufunga nadhiri za daima. Hiyo ni kwa sababu waliingia wakiwa na matarajio fulani ya malimwengu. Mifano mibaya ya waliotangulia katika miito hiyo upadre au utawa lakini pia hata wanandoa. Kwa mfano mapadre au watawa kujiingiza katika ulevi hadi wakati mwingine “network” zinakatika. Mifano mibaya kama wanaposikia kashfa "Scandal" ya padre fulani au mtawa fulani, au pengine namna padre anavyoishi parokiani, mahusiano yake na waamini yakoje, kwa wengine pengine muda wote ni kugomba tu, wengine kila siku ni manunguniko tu awe padre au mtawa, kwake hakuna siku ataonesha anafurahia wito wake bali daima ni mateso katika wito. Wapo baadhi ya mapadre kila akihubiri anakazia na kugomba kuhusu sadaka na zaka kuwa hazitoshi na hiyo inafanya vijana wasiguswe na wito. Mapadre kama hawa wanaitwa "Mapadre wa michongo." Unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto kama ilivyotokea katika nchi za wenzetu kesi za kulawiti watoto hasa watumishi wa altare na hao pengine walikuwa na wito inafika mahali hawaoni sababu tena ya kukuza wito wao. Hali hiyo inakwaza vijana, hatuombei itokee katika maeneo yetu. Kukosa watu wakuwasindikiza katika wito. Watu wakuwasaidia kupambanua vema wito wao kwa mwanga wa Roho Mtakatifu kama alivyofanya Eli kwa Samweli, Yesu kwa wafuasi wawili wa Emau nk. Vijana wanaonesha nia ya wito lakini wanakatishwa na wale wanaoambiwa ili wawape mwanga hawawasaidii. Changamoto nyingine ni gharama za kusomesha waseminari kwa sasa.

Zamani Seminari nyingi zilikuwa zinapata ufadhili toka nje na wazazi walikuwa hawahangaiki na malipo ya waseminari hasa seminari kubwa. Pia seminari ndogo walikuwa wanalipa kidogo, sasa seminari ndogo gharama ni kubwa na wenye kugharimia ni wazazi na hao wazazi hawana uwezo mkubwa, watoto wa familia maskini ni vigumu kusoma. Ukienda seminari kuu kwa sasa gharama pia ni kubwa sababu wale wafadhili hawasaidii tena. Kwa hiyo sasa waseminari wanalipiwa na majimbo yao au mashirika yao. Kwenye majimbo kinachofanyika kuchangisha maparokiani kila mwaka. Hiyo pia si parokia zote zinafanikisha kuchangia sababu katika parokia mahitaji ni mengi. Wanaohusika ni waamini hao hao ambao hata mahitaji yao kupata ni shida. Hivyo inakuwa ngumu sana. Mbaya zaidi yule ambaye walikuwa wakimlipia wakasikia kuwa haendelei na wito inawakatisha tamaa zaidi. Uhuru wa mitandao ya kijamii ambayo imetoa uhuru wa kupata taarifa zo zote na kupost zo zote kadri mtu anavyojisikia. Katika taarifa hizo yamo mambo ambayo ni kinyume cha maadili ya kikristo. Vijana wamekuwa huru kutumia mitandao hiyo tangu utoto wao kama tulivyoona huko juu, wakiwa wakubwa wapo seminarini au kwenye nyumba za malezi na wakati huo walishazoea baadhi ya tabia ambazo kimsingi hazipaswi kukuzwa kwa vijana wanaotarajia kuwa mapadre au watawa kwani kanisa linahitaji watawa au mapadre wenye maadili na utu wema. Hivyo vijana hao kwa mazoea waliyokuwa nayo kabla hujikuta wanawakati mgumu katika malezi yao na pia walezi wanakuwa na mahangaiko namna ya kuwasaidia. Na wakati mwingine wengine wanaweza kujifanya wamebadilika wapo vizuri wakishapata upadre au kuweka nadhiri za daima tayari shida wanaingia kwenye kashifa za ajabu ajabu. Moja wapo kuwa na matumizi mabaya ya mitandao.

Miito Mitakatifu inapata chimbuko lake ndani ya familia.
Miito Mitakatifu inapata chimbuko lake ndani ya familia.

Tufanye nini ili kunusuru; ukuzaji wa miito unapaswa kupewa kipaumbele kwa jamii na kwa kanisa ambalo msingi wake mkuu kupata watenda kazi katika shamba la Bwana, walio wema, watakatifu, hodari wenye ari na moyo wa utume. Kuimarisha familia katika misingi ya Kikristo. Familia kusali pamoja, kujikita katika malezi bora ya watoto wao. Wazazi kuongea na watoto wao na kujua wanasemaje juu ya wito wao. Familia kutoa mfano mzuri kwa watoto wao. Yaani wazazi wawe na maadili mazuri na hii itasaidia kuwafundisha watoto wao kwa matendo yao. Mapadre na watawa kujipa nafasi kufundisha vipindi vya dini mashuleni yaani shule za msingi na sekondari.  Hiyo itasaidia vijana kuguswa na wito wanapoona padre au mtawa katika mazingira yao ya shuleni na pia kuwafundisha. Hata kama si wengi lakini baadhi watasikia sauti ya Mungu kupitia padre au sista. Huko mashuleni kuongea pia juu ya wito. Mapadre na watawa kama ilivyo kwa wanandoa kutoa mfano bora wa maadili na maisha ya wito kwa ujumla. Tusiwe ni sababu ya vijana kukwazika.  Na wale wanaohusika na malezi kuwasaidia vijana kupambanua vema wito wao. Wawe pia ni baba au katika malezi yao, kuongea nao vizuri kwa nia ya kuwasaidia kupambanua wito wao.

Kuzeni moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana ili kuganga majeraha ya binadamu
Kuzeni moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana ili kuganga majeraha ya binadamu

Kusali kwa ajili ya kuombea miito kwani mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache, hivyo hatuna budi kuomba Mungu aongeze watenda kazi. Kama tunavyosoma injili ya Luka 10:2 na pia Mathayo 9:37-38 mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache ombeni Bwana wa mavuno aongeze watenda kazi katika shamba lake. Vijana wanao jitokeza kuwa wana wito wasaidiwe vema kupambanua wito wao kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Wasaidiwe kama alivyofanya Eli kumsaidia Samweli kutambua wito wake kupambanua. Eli alimsaidia Samweli baada ya kuona ni Mungu anamwita anampa mwongozo namna ya kufanya. “ukisikitia tena sema: Nena Bwana mtumishi wako anasikia” (1Samweli 3:9) au pia kuwa karibu ni vijina wanamna hiyo kama alivyofanya Yesu kwa wafuasi wawili wa Emaus, kutembea pamoja kwa kutoa maelekezo lakini pia msaada wa kuelewa (Lk.24;13-35). Maparokiani huko watawa, mapadre na makatekista tuwasadie vijana kuwaelekeza mashirika mbalimbali kwa wale wanaotaka utawa na kuwaeleza pia taratibu zinazotakia kwa wale wanaotaka kuwa mapadre wa majimbo. Tusiwe wachoyo.

Siku ya 59 Miito
NINAFUNGUA MOYO WANGU
06 May 2022, 14:54