Ghasia nchini Nigeria:Padre Vitus Borogo auawa
Vatican News
Katika ukurasa wa twitter wa Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji, limetoa mwaliko wa kuiombea roho ya Marehemu Padre Vitus Borogo, aliyeuawa nchini Nigeria na watu wenye silaha kwenye shamba la Magereza, kando ya Barabara ya Kaduna-Kachia. Padre Vitus alikuwa Padre wa jumuiya katoliki ya Chuo Kikuu cha Jimbo la Kaduna na kwamba haya ni mauaji ya pili nchini Nigeria na ya nne barani Afrika tangu Mosi Januari 2022.
Mnamo tarehe 19 Juni watu wasiopungua watatu waliuawa na takriban watu arobaini walitekwa nyara katika shambulio dhidi ya waamini wa Kanisa katoliki la Mtakatifu Moses, Robuh, katika jimbo la Kaduna. Nchi hiyo ya Nigeria imetikiswa na mashambulizi ya kusikitisha kwa miezi kadhaa. Siku ya Jumapili tarehe 5 Juni 2022 waamini wapatao arobaini walipoteza maisha katika shambulio dhidi ya Kanisa la Mtakatifu Francis Xavier huko Owo, katika jimbo la Ondo, kusini magharibi mwa Nigeria.