Sherehe ya Ekaristi Takatifu 2022 Sherehe ya Ekaristi Takatifu 2022 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu:Ekaristi ni jumla na muhtasari mzima wa imani yetu!

Adhimisho la Ekaristi Takatifu ni mwaliko pia wa kuiishi Ekaristi.Kufufua ndani yetu kiu na hamu ya kushiriki mara nyingi iwezekanavyo Misa Takatifu hasa siku ya Dominika.Ni mwaliko kufufua ndani yetu kiu ya kuipokea Ekaristi Takatifu tena kwa moyo safi na kushiriki ibada za kuabudu,zile za pamoja na zile za binafsi.

Na Padre Wiliam Baitwa, - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Dominika ya wiki hii Kanisa linaadhimisha sherehe ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo
Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo

Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Mwanzo (Mwa 14: 18-20) ambapo somo hili linaelezea tukio la Abramu kukutana na Melkizedeki (wakati huo hakuwa bado amebadilishiwa jina na Mungu na kuitwa Abrahamu). Abramu alikuwa akitoka vitani kupambana dhidi ya wafalme wanne walioivamia nchi yake. Alipokuwa akirudi Melkizedeki akaja kumlaki. Huyu alikuwa ni mfalme wa Salemu na pia alikuwa ni kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Alimpa Abramu mkate na divai na kisha akambariki. Abramu kwa upande wake anamtolea Melkizedeki zaka, moja ya kumi ya vitu alivyochukua mateka vitani. Kwa tendo hili Melkizedeki naye alibarikiwa. Yalianza kutimia maneno ya Mungu kwa Abramu kuwa ”wote watakaokubariki nitawabariki” (Mwa 12:3).

Tendo hili lilikumbukwa sana na wayahudi wa vizazi vyote vilivyofuatia. Walimuona Melkizedeki kama mfano wa ufalme ambapo utawala na uchaji wa Mungu havipingani. Yeye alikuwa mfalme na hapo hapo kuhani. Katika Agano Jipya Melkizedeki anatajwa kama kuhani mkuu ambaye ukuhani wake ni mkubwa kuliko ule wa Haruni na hivi ukuhani wote wa Agano la Kale. Kwa jinsi hii ukuhani wa Melkizedeki unatajwa kuwa ni mfano wa ukuhani wa Kristo. Sababu ya ukuhani wa Melkizedeki kuwa mkubwa kuliko ule wa Haruni ni kile kilichooneshwa katika somo la leo, katika  tendo la Abramu kutoa Zaka, moja ya kumi, kwa Melkizedeki. Hii ilionesha kuwa Abramu ni mdogo kuliko Melkizedeki na hivi Haruni ambaye ni uzao wa Abrahamu hawezi kuwa mkubwa kuliko Melkizedeki na uzao wake kwa sababu Abramu baba yake ni mdogo kwa Melkizedeki.  Ni katika sura hii Melkizedeki anakuwa ni mfano wa Kristo na tendo lake la kutolea mkate na divai kwa Abramu pamoja na kutamka maneno ya baraka yanakuwa ni kiashirio cha Ekaristi ambapo Yesu mwenyewe atatoa mwili wake kama chakula na damu yake kama kinywaji kama tendo la shukrani kwa Mungu na baraka za ulimwengu mzima.

Somo la pili ni kutoka waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto (1Kor 11:23-36). Sehemu kubwa ya waraka huu ulikuwa ni kurekebisha mpasuko uliokuwapo katika kanisa la Korinto pamoja na kurekebisha utovu wa maadili na kufuru za kiibada. Wakati wa Misa kwa mfano walikuwa wameshapoteza utakatifu wa adhimisho na ile sura ya upamoja. Badala yake Misa ikawa ni mahala pa maonyesho, vurugu na kufuru. Katika somo hili Paulo anawaonesha kuwa adhimisho la Misa ni adhimisho la mateso, kifo na ufufuko wa Yesu mwenyewe. Ni adhimisho la maanani sana: sio maigizo, mzaha au kumbukumbu tu ya kawaida bali kila aulaye “ule mkate”, anakula mwili kweli wa Kristo na kila ainywaye “ile divai” anakunywa damu kweli ya Kristo. Hivyo aliwaalika kuishiriki inavyostahili ili wajiepushe na hatia ya kukufuru.

Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo
Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo

Injili ya leo kutoka kwa Mwinjili Luka Injili (Lk 9:11b-17) ambapo Yesu anaulisha umati wa watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Ni muujiza na hapo hapo ni ishara. Ni ishara inayoashiria tendo la Yesu kujitoa mwenyewe kama chakula cha kuwashibisha watu wake.

TAFAKARI

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Ekaristi Takatifu ni adhimisho la uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika mwili na damu yake chini ya maumbo ya mkate na divai.  Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK 1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Kumbukumbu rasmi ya kuwekwa kwa Ekaristi ni siku ya Alhamisi Kuu. Lakini kama tunavyofahamu ilivyo nidhamu ya maadhimisho ya Juma Kuu hasa zile siku tatu kuu za Pasaka, hatuwezi kuadhimisha siku hiyo kwa shangwe kuu pamoja na maandamano ya kutangaza ukuu wa fumbo hili ambalo Kristo ameliachia Kanisa. Ndiyo maana ikatengwa siku nyingine baada ya sherehe za Pasaka kwa ajili ya adhimisho hili kubwa la Ekaristi pamoja na maandamano ya hadharani ili kukiri wazi na kutangaza ufahari wa imani yetu hii kubwa juu ya Ekaristi Takatifu.

Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo
Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo

Adhimisho hili ni mwaliko pia wa kuiishi Ekaristi. Kufufua ndani yetu kiu na hamu ya kushiriki mara nyingi iwezekanavyo Misa Takatifu hasa siku ya dominika. Ni mwaliko kufufua ndani yetu kiu ya kuipokea Ekaristi Takatifu tena kwa moyo safi na kushiriki ibada za kuabudu, zile za pamoja na zile za binafsi. Katika mazingira ambapo tunajikuta tumejifungia kupokea Ekaristi, adhimisho la leo linatupa mwaliko tusiridhike na hali hiyo wala kukata tamaa bali tuendelee bila kuchoka kutumia misaada yote kanisa linayoweka mbele yetu ili kuurudia muungano wetu ndiyo komunio na Kristo. Ni mwaliko wa kukuza imani yetu kuwa Yesu yupo daima na sisi hata mwisho wa nyakati. Amina

TAFAKARI YA SIKU KUU YA EKARISTI TAKATIFU:YESU MWENYEWE ANATOA MWILI WAKE
16 June 2022, 16:51