Tafuta

2021.05.26 Utatu katika sanaa 2021.05.26 Utatu katika sanaa 

Sherehe ya Utatu Mtakatifu:tunamkiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika nafsi tatu

Kristo mwenyewe katika mafundisho yake ameuzungumzia Utatu Mtakatifu kama makao,makao ambayo Yeye yumo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yake katika ushirika wa Roho Mtakatifu.Haya ni makao ambayo ni kilele cha wafuasi wake na kila anayemwamini anaalikwa kuyaingia na kuyashiriki.Naye anasema“mtu akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda;nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake” (Yoh 17:21-23).

Na Padre William Bahitwa -Vatican.

Dominika hii Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Ni sherehe ambayo kwa njia yake tunamkiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Mithali(Mith 8:22-31). Hiki ni mojawapo ya vitabu saba vya Agano la Kale vinavyoitwa vitabu vya Hekima. Waisraeli, kama hata ilivyo kwetu leo, waliitukuza sana hekima. Waliitambua kama ni uzoefu wa maisha na kipawa kinachomwezesha mtu kung’amua mambo na kumsaidia kuishi vizuri na watu. Zaidi ya hapo, Waisraeli waliihaisha hekima, yaani waliitukuza kiasi cha kuiona kama ni nafsi ya mtu anayeishi. Na kwa jinsi hii hekima aliweza kuongea na kuingia katika mazungumzo na watu. Katika somo letu hili la kwanza, hekima anajipambanua kama nafsi inayotoka kwa Mungu mwenyewe na zaidi ya hapo ni nafsi iliyokuwapo tangu hata kabla ya kuumbwa ulimwengu. Ilikuwapo kabla ya kuwepo vilindi, kabla ya milima, kabla mbingu hazijathibitishwa, kabla ya kuwako nchi na yote yanayoonekana. Utenzi huu ambao kimsingi unaitukuza hekima, unatuonesha pia kuwa ulimwengu na misingi yake yote pamoja na vyote vikubwa na vidogo vilivyomo kuna wakati havikuwapo. Vyote vilikuja kuumbwa na kuwekwa jinsi vilivyo. Na aliyefanya yote hayo ni Bwana Mungu aliyekuwa pamoja na hekima. Katika dominika hii ya Utatu Mtakatifu, somo hili linatupatia ufunuo wa Mungu Baba kama muumbaji, ufunuo ambao tangu kale waisraeli waliukiri na hekima yao iliwaonesha waziwazi kuwa ulimwengu na vyote vilivyomo viliumbwa. Ni somo linalodokeza kazi ya uumbaji ya Baba.

Somo la pili ni kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi(Rum 5:1-5 ). Katika kifungu hiki Mtume Paulo anazidi kufafanua fundisho lake kuwa tunakombolewa na kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na si kwa matendo ya Sheria au Torati. Anaonesha kuwa katika kuifikia neema hii ya kukombolewa na kuhesabiwa haki, Kristo ndiye njia. Ni kwa njia ya imani kwa Kristo ndipo mtu anaweza kuifikia neema hii. Nayo ni neema inayompa mtu amani na tena si amani tu bali sababu ya kufurahi katika dhiki kwa sababu kwa njia ya Kristo dhiki hiyo huleta saburi na saburi huleta uthabiti wa moyo na uthabiti wa moyo huleta tumaini, tumaini ambalo haliwezi kumdanganya mtu. Tunaona pia katika somo hili dokezo kuhusi nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu, yaani Bwana Wetu Yesu Kristo ambaye ndiye anayewahakikishia watu ukombozi na kuhesabiwa haki.

Injili ya leo ni kutoka kwa mwinjili Yohane(Yoh 16:12-15). Inaeleza sehemu ya wosia wa Yesu kwa wanafunzi wake, sehemu inayoendeleza ufunuo wa Mungu Roho Mtakatifu. Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa anayo bado mengi ya kuwaambia lakini anaona kuwa kwa wakati huo hawataweza kuyastahimili. Jambo ambalo mtu hawezi kulistahimili ni jambo zito. Yesu anawaonesha wanafunzi wake kuwa huko mbeleni utume na maisha yao kwa ujumla vitakumbwa na mambo mazito. Na kama tunavyojua uzito wa jambo mtu huusikia pale jambo lenyewe linapompata na si pale anapoelezwa, Yesu anawaonesha ni wakati huo huo atakapokuwapo pamoja nao Roho Mtakatifu. Kumbe Yesu anamwonesha Roho Mtakatifu kama yule atakayewapa mitume ustahimilivu katika magumu, na katika mtazamo mpana zaidi Roho Mtakatifu anaoneshwa kama ndiye ambaye utume ujao wa wafuasi na mambo yajayo ya kanisa yapo mikononi mwake. Ni katika mwono huu tunayaelewa maneno Yesu anayosema baadaye kuwa Roho Mtakatifu atawaongoza katika ukweli, atanena kutoka yale aliyofundisha Yesu na atamtukuza Yesu mwenyewe na kumtukuza Baba. Katika dominika hii ya Utatu Mtakatifu, injili ya leo inafunua kazi za Roho Mtakatifu katika maisha ya wafuasi na katika kanisa kwa ujumla.

Tafakari

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe tunayoadhimisha leo ni sherehe inayogusa fundisho kuu juu ya Mungu mwenyewe. Ni fundisho la imani na hapohapo ni fumbo, kwamba Mungu wa kweli na wa pekee ni mmoja katika nafsi tatu ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.  Tunaamini juu ya fumbo la Utatu Mtakatifu kwa sababu Mungu mwenyewe amelifunua. Amelifunua  hatua kwa hatua katika historia ya wokovu; katika fumbo la uumbaji, katika fumbo la ukombozi wa mwanadamu na katika fumbo la kumtuma Roho Mtakatifu. Katika mpango huu wa ukombozi kila nafsi ya Mungu inatekeleza kazi yake ya pamoja kufuatana na hali yake kama nafsi. Ndiyo maana tunamtaja Baba kama muumbaji, Mwana kama mkombozi na Roho Mtakatifu kama mfariji anayetakatifuza. Hata hivyo hii yote ni kazi ya pamoja ya nafsi tatu za Mungu kwa sababu hizi ni nafsi zenye asili moja na kwa sababu hiyo zina utendaji mmoja ulio sawa. Na maisha yote ya kikristo ni ushirika wa kila nafsi ya Mungu bila kuzitenganisha kwa namna yoyote. Anayemtukuza Baba hufanya hivyo kwa njia ya Mwana katika Roho Mtakatifu; anayemfuata Kristo anafanya hivyo kwa sababu Baba anamvuta na kwa sababu Roho Mtakatifu anamwongoza.

Kristo mwenyewe katika mafundisho yake ameuzungumzia Utatu Mtakatifu kama makao, makao ambayo Yeye yumo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yake katika ushirika wa Roho Mtakatifu. Haya ni makao ambayo ni kilele cha wafuasi wake na kila anayemwamini anaalikwa kuyaingia na kuyashiriki. Naye anasema “mtu akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake” (Yoh 17:21-23). Nasi tunapata matumaini ya kuyaingia kwa njia ya Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, ndani ya upendo wa Mungu Baba na katika ushirika wa Roho Mtakatifu.

Makao haya ya Mungu katika utatu Mtakatifu, yanaakisi pia makao yetu hapa duniani katika familia, jumuiya na taasisi zetu. Neema, upendo na ushirika ndani ya Utatu Mtakatifu na kwa njia ya Utatu Mtakatifu ni mwaliko wa kwetu kuziishi tunu hizi katika familia zetu, jumuiya zetu na katika taasisi zetu. Maadhimisho ya leo yawe kichocheo kwetu cha kujenga familia na jumuiya zinazojitahidi kutunza neema zilizopata kwa njia Kristo, familia na jumuiya zinazoiga siku kwa siku upendo wa Baba na kwa mfano wa upendo huo kupendana wao kwa wao: familia na jumuiya zinazoishi kwa kushirikiana na kusaidiana hasa katika nyakati ngumu ambapo mmoja wa wanafamilia au wanafamilia wote wanapokuwa wanapita katika kipindi kigumu cha maisha. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe nasi katika familia na jumuiya zetu zote. Amina.

TAFAKARI YA SHEREHE ZA UTATU MTAKATIFU 2022

 

11 June 2022, 19:40