Tafuta

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. anasema changamoto za kiuchumi, zinachangia sana kwa wazee kupata huduma duni za afya, malazi, chakula na mavazi na hivyo kujikatia tamaa ya maisha. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. anasema changamoto za kiuchumi, zinachangia sana kwa wazee kupata huduma duni za afya, malazi, chakula na mavazi na hivyo kujikatia tamaa ya maisha. 

Askofu Lazarus Msimbe Mauaji Ya Wazee ni Kinyume Cha Haki Msingi za Binadamu Na Utu wema

Changamoto za kiuchumi, zinachangia sana kwa wazee kupata huduma duni za afya, malazi, chakula na mavazi. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni kati ya mambo yanayopelekea mauaji ya wazee na vikongwe. Vyombo vya ulinzi na usalama, lakini hasa jamii nzima inapaswa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sababu na vichocheo vya mauaji ya wazee na vikongwe ndani ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Wazee na Wajukuu Duniani Dominika tarehe 24 Julai 2022 yananogeshwa na kauli mbiu: “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea wazee ili waweze kuongoka na kuwa ni waalimu wa huruma na upendo; ili uzoefu na mang’amuzi yao, yaweze kuwasaidia wazee kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na uwajibikaji. Uzee ni kipindi cha neema na baraka; wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii, mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni pamoja na: imani na mang’amuzi ya maisha. Wazazi na walezi kwa kushirikiana na wazee, warithishe imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.  Watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, wazazi wawasaidie vijana na watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa na kutunzwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi uzee stahiki.

Jengeni na kudumisha utamaduni na Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.
Jengeni na kudumisha utamaduni na Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii, maendeleo na mafao ya wengi.   Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki la Morogoro katika mahojiano maalum na Radio Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Sku ya II ya Wazee na wajukuu anasema, wazee ni sehemu muhimu sana ya maisha ya jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii katika ulimwengu mamboleo. Wazee wanapaswa kusikilizwa kwa makini, ili wasaidie kuchangia miongozo na dira makini za maisha. Wazee waheshimiwe, wathaminiwe na kuendelezwa, ili wao pia waendelee kuchangia kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wapewe huduma bora na rafiki hasa katika huduma ya matibabu, malazi na chakula.

Wazee walindwe, watunzwe na kuheshimia na jamii inayowazunguka
Wazee walindwe, watunzwe na kuheshimia na jamii inayowazunguka

Wazee wengi wanalalamika kwamba, mazingira wanamoishi kwa sasa ni tete na ya hatari na yamewafanya wengi kupoteza maisha kabla hata ya kulemewa na uzee wao, wapo wanaouawa kwa imani za kishirikina na baadhi kutelekezwa na familia zao na hivyo kujikuta wakikosa mahitaji msingi na baadaye kupoteza, matumaini ya kuendelea kuishi. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. anasema, changamoto za kiuchumi, zinachangia sana kwa wazee kupata huduma duni za afya, malazi, chakula na mavazi. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni kati ya mambo ambayo yanapelekea mauaji ya wazee na vikongwe. Vyombo vya ulinzi na usalama, lakini hasa jamii nzima inapaswa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sababu na vichocheo vya mauaji ya wazee na vikongwe ikiwa ni pamoja na kuwabaini wahusika wanaopanga na kutekeleza mauaji haya ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, na pale inapothibika wahusika wachukuliwe hatua kali ili kutokomeza kabisa vitendo hivi vya kikatili vinavyokwenda kinyume cha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tafiti zilizopo zinaonesha mauaji na ukatili dhidi ya wazee yanachochewa na imani za kishirikina pamoja na migogoro ya ardhi. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki la Morogoro anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unadhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mauaji ya wazee
23 July 2022, 16:12