Askofu Mkuu Paulo Ruzoka: Tukutane IFUCHA 25 Septemba 2022: Tuna Jambo Letu!
Na Godfrey Mahonge, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.
Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, tarehe 20 Julai 2022 ametimiza miaka arobaini na saba tangu (47) alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Julai 1975, Kumbukumbu ya Mtakatifu Eliya, Nabii ambaye ni kati ya Manabii wakuu wa Agano la Kale. Alitangaza na kushuhudia imani thabiti kwa Mungu aliye hai. Katika hafla fupi ya kumbukizi hizi uaskofuni Tabora, Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka amewashukuru wote waliomsindikiza na wanaoendelea kufanya hivyo, wakimwombea na kumtia shime katika maisha na utume utume wake tangu akiwa Jimbo Katoliki la Kigoma na hata sasa jimboni Tabora. Alisema yeye alikuwa Padre mzalendo wa sita kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tangu kuanzishwa Jimbo Katoliki la Kigoma. Katika kipindi kile sehemu kubwa ya Tanzania ikiwa na mapadre wengi kutoka nje ya Afrika, yaani wamisionari haikuwa rahisi hata kidogo kwa vijana wazalendo kufuasa wito wa upadre. Lakini kijana Paulo Ruzoka, enzi hizo, hakuteteleka wala kubabaika na lolote, na kwa sala, sadaka, kujitoa na kujitolea; akafanya jamala kuonesha kwa matendo nia yake ya kumtumikia Mungu kama Padre wa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Akitafakari sana juu ya safari yake ya wito wa upadre akisema kwamba miaka yake 47 ya upadre imechagizwa na tumaini kwamba mapenzi ya Mungu hayana mipaka, nayo humkaribisha kila huyo kwa namna yake.
Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka anawashukuru kwa namna ya pekee wazazi wake waliomjengea msingi thabiti wa imani na matumaini. Anawashukuru walezi, ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo kwa msaada wa sala na maombezi yao. Watu wateule na watakatifu wa Mungu Jimboni Tabora wanampongeza sana Askofu mkuu Paulo Ruzoka na kumwombea kheri la baraka tele katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, kama kielelezo cha uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Paulo Ruzoka, alizaliwa kunako mwaka 1948 huko Nyakayenzi, Kigoma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 20 Julai 1975 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa kuwekewa mikono na Askofu Alphons Daniel Nsabi wa Jimbo Katoliki la Kigoma, akiwa ni Padre wa sita mzalendo, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, matendo makuu ya Mungu. Tarehe 10 Novemba 1989, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma na kuwekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1990 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 25 Novemba 2006, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na kusimikwa rasmi tarehe 28 Januari 2007. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora wanasema tarehe 25 Septemba 2022 tunalo jambo letu moyoni. Tunajiandaa kwenda Ifunyang’olo, kutuliza mioyo! Waswahili wangesema, eti kuliza ball ya maisha ya kiroho! Usikose hata kidogo!