Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Mazingira Bora & Injili ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo
Na Na Angela Andrew Kibwana, DSM & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
AMECEA inasema, Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda, kutunza na kutetea mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu. Ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anahimiza umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaitaka jamii kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Itakumbukwa kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, kuanzia tarehe 10-18 Julai 2022 linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 20 Jijini Dar es Salaam. Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.”
Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Serikali ya Tanzania imetia nia ya kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo AMECEA katika mchakato wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unahudhuriwa na wajumbe zaidi 270 kutoka ndani na nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Watu wa Mungu wanahimizwa: Kuona, Kuhukumu na Kutenda kadiri ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote,” ili kuokoa mazingira nyumba ya wote, changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Paulo VI. Watu wa Mungu wasiposimama kidete kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote, hathari zake ni kubwa sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kazi za binadamu zimeendelea kuchangia katika uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
Mababa wa AMECEA wanasema, Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na: Ujenzi wa dhamiri adilifu, kanuni maadili na utu wema; Imani inayomwilishwa katika vipaumbele vya mwanadamu, ili kupambana na uharibifu pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Huu ni wakati wa kufanya maamuzi makubwa, kwa kujikita katika toba, wongofu wa kiikolojia na utakatifu wa maisha, unaomwilishwa kwa vitendo mambo msingi yanayopania kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Ignatius Chama wa Jimbo kuu la Kasama, Zambia, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, ZCCB. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA wajenge utamaduni wa kupanda na kutunza miti. Waepukane na tabia chafu ya kuchoma misitu kwa moto pamoja na kuchafua mazingira. Wongofu wa ikolojia ya mazingira, uchumi, tamaduni na maisha ya kila mtu kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi hadi familia nzima ya watu wa Mungu, Ukanda wa AMECEA, Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake usaidie kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Kutokana na ukame wa kutisha, mafuriko, ongezeko la joto duniani sanjari na kupanda kwa kina cha maji baharini, uhakika na usalama wa chakula kwa siku za usoni uko mashakani.
Kwa upande wake, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, anasema, maendeleo, sera na mikakati isiyozingatia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tishio kwa maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Watu wa Mungu wajifunze na kumwilisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira, ili kurejesha tena uoto wa asili, kwa kupanda na kutunza miti; kwa kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji; ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula sanjari na afya bora. Wananchi wajifunze mbinu za kilimo bora na ufugaji wa kisasa sanjari na matumizi ya teknolojia rafiki, itakayookoa misitu inayokatwa ovyo kwa ajili ya kutengeneza kuni na mkaa. Wananchi wasipopata nishati mbadala na teknolojia rafiki, wataendelea kukata miti ovyo na kuchoma mkaa. Kumbe, elimu bora ya mazingira na ushirikishwaji wa umma katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mambo muhimu sana. Binadamu kwa mikono yake mwenyewe amechangia kiasi kikubwa kuleta athari za mabadiliko ya tabianchi, kumbe, anaweza pia kushiriki kikamilifu katika kuganga na kuponya majeraha ya uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Elimu ya utunzaji bora wa mazingira ianzie kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, parokia, jimbo na hatimaye kuwahusisha kikamilifu watu wote wa Mungu. Ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali ni muhimu sana katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Wakati huo huo Padre Charles Kisima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA nchini Tanzania imekuwa ni fursa kwa kwa familia ya Mungu Ukanda wa AMECEA kutafakari na kujadili kwa kina kuhusu utunzaji bora wa mazingira, matumizi na jinsi ya kuyaendeleza, ili yawe ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu. Mwanadamu ataendelea kuyatumia mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini jambo la msingi ni kuwa na sera, mipango na mikakati itakayosaidia kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ambao ni wajibu wa kijamii na kimaadili kwa kusukumwa na dhamiri adilifu. Watu wajenge utamaduni wa kuheshimu na kuthamini kazi ya uumbaji, huku wakiongozwa na dhamiri adilifu, ili misingi ya haki, amani na udugu wa kibinadamu viweze kunogeshwa zaidi katika jamii. Madhara ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira Barani Afrika yanajionesha wazi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa baa la umaskini, njaa, maradhi, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kwa sasa Mababa wa AMECEA wamejifungia ili kuandaa ujumbe kwa watu wa Mungu na mada kuu itakayofanyiwa kazi wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA kunako mwaka 2026.