Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Fahari ya Msalaba, kiwe ni kipaumbele katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Fahari ya Msalaba, kiwe ni kipaumbele katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu 

Wakristo Wanatumwa Kutangaza Habari Njema ya Wokovu: Msalaba

Mama Kanisa katika masomo ya dominika ya 14 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisaanatukumbusha kuwa kwa Sakramenti ya ubatizo na kipaimara sisi sote tumeitwa kuihuburi Injili kwa kuishi ukristo wetu vyema sio kwa sheria za maumbile bali kwa kuwa viumbe vipya ndani ya Kristo na kuona fahari juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Msalaba.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Mama Kanisa katika masomo ya dominika hii anatukumbusha kuwa kwa Sakramenti ya Ubatizo na kipaimara sisi sote tumeitwa kuihuburi Injili kwa kuishi ukristo wetu vyema sio kwa sheria za maumbile bali kwa kuwa viumbe vipya ndani ya Kristo na kuona fahari juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Somo la kwanza kutoka sura ya mwisho ya kitabu cha Nabii Isaya (Isa 66:10-14); linatupa matumaini na faraja ya kushangilia na kufurahi kwa kuwa Mungu atasimamisha ufalme mpya wenye haki kwa wale wampendao na kumcha. Hii ni kusema kwamba wenye haki watashiriki baraka za milele katika dunia mpya na mbingu mpya yaani uzima wa milele. Utabiri huu wa nabii Isaya unatimilika katika Kristo kwa kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kazi imebaki kwetu kuyaishi vyema maisha yetu ya kikristo kwa kuzishika ahadi zetu za ubatizo, kumkataa shetani na mambo yake yote na fahari zake zote ili baada ya maisha ya hapa duniani tuweze kushirikishwa uzima wa milele.

Somo la pili ni hitimisho la barua ya Mtume Paulo kwa Wagalatia (Gal 6: 14-18). Ujumbe wa somo hili una mazingira yake. Wakati wa enzi za mitume jumuiya zilizoipokea Injili zilikuwa na hamasa kubwa na hivyo ziliikumbatia Imani. Furaha iliijaza mioyo yao. Walikuwa wachache kwa idadi, lakini waliishi imani hiyo kiaminifu na kwa furaha kubwa. Furaha hiyo iliongezeka kadiri idadi yao ilivyoongezeka kwani wengi walipendezwa na maisha yao wakaamini na kubatizwa. Lakini taratibu, ile hamasa ilianza kufifia, ugomvi na mpasuko kati yao ukaanza kutokea, wengi wakaanza kurudi nyuma katika imani yao. Wakristo katika Kanisa la Galatia nao walikata tamaa na kuanza kurudi nyuma kiimani. Katika mazingira hayo Paulo anawakemea akiwaambia; “Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaloga?” Maneno haya makali ya Paulo ni kuwataka Wagalatia na sisi tuujue ukweli na tusipotoshwe na mafundisho ya uongo na upotoshaji.

Kwa Ubatizo na Kipaimara, wakristo wanatumwa kuinjilisha
Kwa Ubatizo na Kipaimara, wakristo wanatumwa kuinjilisha

Itakumbukwa kuwa Paulo aliwahubiria watu wa Galatia katika safari yake ya kwanza ya kimisionari (Mdo 13:14-14:23). Baada ya yeye kuondoka, kikundi cha Wayahudi walioongokea ukristo walifika, wakahubiri kuwa ni lazima watu wa Mataifa yaani wapagani, watu wasio wayahudi watimize kwanza sheria za Musa ili wapate kuokoka na kuwa wakaristo. Paulo anapinga mafundisho hayo kwa kuonyesha umuhimu wa Imani kwa ajili ya wokovu akitolea mfano wa Ibrahamu baba wa Imani aliyeishi miaka 400 kabla ya sheria ya Musa kutolewa, alivyookolewa kwa imani yake kwa Mungu. Paulo anasisitiza kuwa kushika sheria tu bila kuwa na Imani hakuwezi kumwokoa mtu na yeye mwenyewe Paulo ni mfano hai aliyeongoka na kuokolewa kwa neema ya Mungu katika kumwamini Kristo. Kumbe tunahesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani na tunakuwa watoto wa Mungu kwa imani. Kwa kuwa Kristo ametuweka huru, basi tusimruhusu mtu yeyote aturudishe kwenye mawazo ya kudhania kuwa matendo ya kisheria yanatosha kutupatia wokovu.

Kama watu waliookolewa kwa neema, tuna wajibu wa kuishi maisha yanayolingana na imani yetu. Ndiyo maana Paulo anasema; “Mimi hasha sioni fahari juu ya kitu cho chote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa Yeye ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu. Kwa maana katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! Tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu”. Itakumbukwa kuwa nyakati za Paulo, mabwana waliwapiga chapa watumwa wao kwa kutumia chuma ya moto. Ikiwa mtumwa alitoroka, alijulikana mara, na kurudhishwa kwa Bwana wake. Akitumia lugha ya kupigwa chapa Paulo anasema kwamba Kristo ameshampiga chapa, kwa kutumia ishara ya Msalaba. Msalaba si ishara ya aibu au utumwa, bali ni ushindi, utukufu na uhuru wa kweli. Yesu alitukomboa kwa Msalaba wake, nasi tunapaswa kumdhihirisha katika maisha yetu kwa kuikumbatia misalaba yetu, yaani, kuyapokea mateso na mahangaiko ya kimaisha kwa uvumilivu kwa ajili ya Kristo.

Mtume Paulo anahitimisha akisema; “Na wote watakaoenenda katika kanuni hii, amani na iwe nao kwa rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina” (Gal 6:16). Kumbe hatuwezi kuwa na Bwana mwingine kuliko Kristo. Paulo anatualika Wakristo tujikabidhi kwa moyo wote na imani kuu kwa Kristo, na ni katika kujikabidhi kwake na kumwamini Yeye kuwa Bwana na mwokozi wetu tutaishi kwa furaha na amani licha ya matatizo na mahangaiko ya kimaisha yanayotukabili kila siku. Tukiwa wakristo vuguvugu hatuendi popote. Furaha na amani ya Kristo ni kwa wale walio wake, waliojitoa kikamilifu. Mkristo ni yule anayejitoa na kubaki shupavu katika maisha ya Kiroho ndani ya moyo wake, anayekaa upande wa Kristo, bila kuangalia gharama.

 Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu

Katika Injili, Mwinjili Luka (Lk 10:1-12,17-20) anasema; “Bwana aliweka wengine 72 nje na wanafunzi 12 (Mt.10:5-14, Mk.6:7-13, Lk.9:1-6), akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda katika kila mji alipokusudia kwenda mwenyewe. Ni Luka peke yake ndiye anayesimulia tukio hili. Namba 72 inasimama mahali pa makabila 72 au koo zilizotokana na wana watatu wa Noa yaani Shemu, Hamu na Yafethi, baada ya gharika kuu (Mwanzo 10). Hii ni namba kamili kama walivyofikiri Wayahudi, ikiwakilisha Makabila au Koo zote za dunia kwa wakati ule. Huu ni ujumbe kuwa kutangaza habari njema ni jukumu la kila mmoja wetu. Hivyo kila mbatizwa anawajibu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo popote pale alipo katika maisha yake. Wazazi wana jukumu la kuwarithisha na kuwafundisha watoto wao imani. Watoto nao wanaowajibu kwa wazazi wao kuishuhudia imani waliyoipokea kwao kwa kuishi nao vizuri wakiwatunza katika uzee wao kama anavyosisitiza Papa Francisko. Mume anaalikwa kumpenda na kumwinjilisha mkewe, kadhalika mke naye anao wajibu kwa Mumewe kuona kwamba imani ndani ya familia inakuwa na kupewa kipau mbele hususani kwa makuzi ya watoto. Ndugu katika familia kila mmoja anapaswa kuwa mfano bora wa kuiishi Injili/Habari Njema ya wokovu. Hivyo kila mwanafamilia mbatizwa ni Mmisionari kwa mwenzake.

Tukishirikiana na maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa na makatekista tumpeleke Kristo katika maisha ya watu ili wauonje upendo wake na faraja yake katika mahangaiko ya kimaisha. Kristo anatoa masharti katika kumtangulia akisema; “Msimwamkie mtu njiani” ili tusichelewe pia tusiweke matumaini yetu katika watu au vitu: “Msichukue mfuko wala fedha, wala viatu”. Si fedha, wala elimu, wala mamlaka ya kibinadamu inayohitajika katika kumhubiri Kristo bali upendo na huruma yake. Kinachohitajika ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo na kuona fahari juu ya Msalaba. Tunaitwa kuwa mabalozi wa amani na Upendo: ndiyo maana Kristo anasisitiza; katika kuenenda kwenu hii iwe ni salamu yenu: “Amani iwe ndani ya nyumba hii”. Kila Mkristo anapaswa kuwa mleta amani na mpatanishi wakati wote. Hatuwezi kuwa waleta amani au wapatanishi ikiwa amani ya Kristo haimo ndani yetu. Tuombe daima amani hiyo na upendo wa Kristo utawale katika mioyo yetu na katika jumuiya zetu.

Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa huruma, upendo na mshikamano
Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa huruma, upendo na mshikamano

Tuwe wajasiri na tusiokata tamaa katika kumshuhudia Kristo kwani anatuambia; “Na mji wowote mtakaoingia, nao hawakuwakaribisha, tokeni humo nanyi mkipita katika njia zake semeni, hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandama na miguu yetu, tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili; “Ufalme wa Mungu umekaribia”. Hatupaswi hata mara moja kukata tamaa, wala kuogopa. Daima tukumbuke kwamba kuwaleta watu kwa Yesu kunaleta furaha kuu ndani ya mtu binafsi na katika Jumuiya. Wote wanaojitahidi kuwaweka watu huru kutoka utumwa wa shetani, wanapata nguvu kutoka kwa Mungu wanazohitaji katika shughuli hiyo ya kumshinda shetani wakati wa majaribu. Lakini furaha kubwa zaidi ni kuuridhi ufalme wa mbinguni ndivyo anavyotumbia Yesu: “Msifurahi kwa vile pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Tafakari Dominika 14
01 July 2022, 15:06