Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Tafakari Dominika XV ya Mwaka C: Injili ya Huruma na Upendo Inamwilishwa Katika Matendo

Mungu Muumba wetu ametupatia Neno lake, Neno ambalo ni taa ya kutuongoza na hapo hapo ni sheria ya kuifuata katika maisha yetu. Masomo ya dominika hii yanakuja kutuonesha kile kilicho kiini cha Neno la Mungu, kiini cha sheria ya Mungu. Kiini hicho ni huruma na upendo: huruma inayojimwilisha katika matendo. Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha ya mwamini.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu, tafakari inayotupatia nafasi ya kuyasoma na kuyapatia ufafanuzi masomo ya dominika. Mungu Muumba wetu ametupatia Neno lake, neno ambalo ni taa ya kutuongoza na hapo hapo ni sheria ya kuifuata katika maisha yetu. Masomo ya dominika hii yanakuja kutuonesha kile kilicho kiini cha Neno la Mungu, kiini cha sheria ya Mungu. Kiini hicho ni huruma na upendo: huruma inayojimwilisha katika upendo. Tuyapitie sasa na kuyafafanua masomo yote matatu ya dominika hii. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kum 30:10-14) katika kile ambacho kinafahamika kama ni hotuba ya mwisho ya Musa kwa waisraeli. Musa akijua kwamba hatavuka na waisraeli kwenda nchi ya ahadi, anatimiza bado wajibu wake wa kinabii kuwaandaa waisraeli kuingia na kuishi vema katika nchi hiyo. Hapa anawaambia Waisraeli kuwa Neno la Mungu, maagizo ambayo Mungu amewapa, sheria ya Mungu; vyote hivyo Mungu ameviweka ndani yao. Vyote vipo ndani ya moyo wa mtu. Hawana sababu ya kusema hatujui Mungu anataka nini katika maisha yetu, hatujui Mungu anataka tuishi vipi ili kumpendeza; wala kusema ni nani atakayeenda huko mbali liliko Neno la Mungu atuletee. Ile kiu ya kutafuta na kuelekea katika yampendezayo Mungu, ipo ndani ya moyo wa kila mtu, ndani ya kile tunachoita dhamiri.

Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.
Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.

Jambo hili linahitaji kufafanuliwa kwa sababu anaweza mtu akasema kama mambo ndio yako hivyo basi kila ambacho moyo unamtuma mtu kufanya ni sahihi na kinapendeza machoni pa Mungu na hakuna mwingine wa kumuambia kama ni chema au la. Hakuna aliye na ukweli wote kwa pamoja ndani yake. Sote tunakua na kuvutwa kuuelekea ukweli wa kimungu hatua kwa hatua. Musa anachowafundisha waisraeli na kutukumbusha sisi sote ni kuwa Mungu ameweka ndani yetu ile kiu ya kumtafuta na kiu ya kutenda yale yampendezayo na dhamiri yetu njema, dhamiri iliyoundwa ndiyo ile sauti ya Mungu inayotushitaki tunapopotea njia na ndiyo inayoridhia pale tunapokwenda katika njia sahihi. Mungu yu upande wa wote wamtafutao Kutoka somo la kwanza, tuliangalie sasa somo la pili. Hili linatoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 1:15-20). Somo hili linaeleza kwa njia ya utenzi mojawapo ya kiri ya imani kuhusu Kristo, yaani, kile ambacho Kanisa limeamini na limefundisha kuhusu Kristo tangu kipindi cha wakristo wa kwanza. Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, si katika ngazi ya uzao kama walivyo watoto wa familia moja. Ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kuwa msingi na yule aliyewezesha wazaliwa wengine yaani sisi, kuwepo kwa maana ni katika yeye vitu vyote viliumbwa. Kwa nafasi yake ya kuwa msingi wa kazi yote ya uumbaji, ndiye aliyetwaa mwili akashuka duniani ili kuvipatanisha viumbe hivyo na Mungu baada ya dhambi kuingia na kuharibu uhusiano kati ya viumbe na Mungu. Naye Kristo ameufanya upatanisho huo kwa kumwaga damu yake msalabani.

Neno la Mungu litangazwe na kutolewa ushuhuda wenye mvuto na mashiko
Neno la Mungu litangazwe na kutolewa ushuhuda wenye mvuto na mashiko

Somo hili linahusiana vipi na somo la kwanza? Uhusiano upo, tena mkubwa kabisa. Somo la kwanza limezungumza kuhusu sheria ya Mungu, sheria ambayo ni Neno la Mungu. Somo hili linakuja kutuonesha kuwa Kristo ndilo hilo Neno la Mungu na ndiyo sheria ya Mungu iliyotwaa mwili. Kristo ni ushuhuda kuwa Neno la Mungu linashikika na sheria ya Mungu inatekelezeka. Vyote hivyo sio vitu vya nadharia, sio kanuni tu ambazo hazina mashiko wala uhalisia bali ni vitu halisi katika mazingira halisi ya mwanadamu. Injili ya dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa ni ile inayofahamika kama “injili ya Msamaria Mwema”. Katika mazingira ambapo tunatafakari juu ya sheria ya Mungu, Yesu anakutana na mwanasheria anayemuuliza afanye nini ili aurithi uzima wa milele. Mwanasheria huyu analifahamu agizo la kumpenda Mungu na kumpenda jirani lakini hajui jirani yake ni nani. Hajui kukiweka katika uhalisia wa maisha yake ya kila siku kile anachokifahamu akilini kwa nadharia. Kumfafanulia mwanasheria huyo nini maana ya sheria hiyo ya Mungu, Yesu anatoa simulizi la mtu aliyekuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, njiani akautana na majambazi, wakampiga, wakamnyang’anya vyote alivyokuwa navyo, wakamwacha akiwa mahututi.

Katika njia ile walipita kuhani na mlawi lakini hawakumsaidia chochote. Kuhani na mlawi ni wawakilishi wa upendo wa Mungu kwa watu wake. Ni watu ambao kwa utume wao wanamleta Mungu karibu na watu, wanamfanya Mungu awe jirani na watu, lakini wao katika mazingira hayo wanakuwa mbali na majeruhi huyo. Anapita msamaria. Leo hii neno msamaria ni jina zuri na lenye sifa ya mtu mwema anayejali wahitaji. Katika mazingira ya Yesu haikuwa hivyo. Msamaria lilikuwa ni kama tusi kwa sababu ya uadui uliokuwapo kati ya Israeli na nchi ya Samaria. Msamaria, yaani aliyetokea Samaria alionekana kama ni mtu asiye mstaarabu, asiyejua chochote, mtu wa kudharaulika na wa kuepukika kabisa. Sasa ni huyo ambaye katika mfano wa leo anachukua jukumu la kumsaidia majeruhi; anamuonea huruma. Na ni kwa mfano wa alichokifanya yeye, Yesu anamwambia mwanasheria “enenda zako nawe ukafanye vivyo hivyo.” Ni msamaria, mtu mwenye sifa tulizozitaja hapo juu ndiye anayewafundisha kuhani, mlawi na mwanasheria kiini cha sheria ya Mungu: huruma na upendo. Kati ya mambo ambayo injili hii inatuambia ni kuwa haitoshi tu kufahamu mambo, hasa haya yahusuyo imani yetu. Haitoshi kujua kwa ufasaha Neno la Mungu, kujua amri za Mungu zinasemaje; wala haitoshi kuwa na uwezo wa kuzifafanua, kuzifundisha, kuzisali na kadhalika kama tunapokuja katika mazingira yanayotuhitaji tuyaweke katika matendo tunageukia upande mwingine. Ni injili kumbe inayotualika kushuka chini, kuweka katika uhalisia Neno lile tunalolifahamu na tunaloliamini. Ni mwaliko, kama tunavyoweza kusema, kulipeleka mitaani kwetu Neno la Mungu na kuishusha ardhini sheria ya Mungu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhidia Injili ya huruma ya Mungu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhidia Injili ya huruma ya Mungu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika Maandiko Matakatifu ambayo dominika hii ya 15 inatupatia, ninaguswa kutafakari nanyi swali lile ambalo mwanasheria anamuuliza Yesu: “nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele.” Katika mazingira ya wakati wa Yesu, mwanasheria ndio alikuwa kipimo cha juu cha mtu ambaye ni msomi, mtu aliyestaarabika, mtu mwenye uwezo na nafasi ya juu katika jamii. Sasa huyo ndio mtu ambaye kati ya maswali aliyonayo ni hilo linalohusu anachotakiwa kufanya ili aurithi uzima wa milele. Ninarudi katika mazingira tuliyomo, mazingira ya mtanzania wa leo na ninajiuliza; mtanzania msomi, mwenye kiwango cha juu au mwenye nafasi ya juu katika jamii suala la kuwa afanye nini ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu ni mojawapo ya masuala yanayomuwangisha kichwa? Hii ninaipokea kama changamoto na kukushirikisha nawe ndugu msomaji na msililizaji wa Vatican News kuwa kiu ya kuutafuta ufalme wa Mungu, Mungu mwenyewe ameiweka ndani yetu. Tusiizime, tusiipuuzie kwa kutafuta vipaumbele vingine katika maisha yetu. Maandiko Matakatifu yanatukumbusha daima kuwa kumcha Bwana ndio chanzo cha maarifa. Kumbe katika harakati, mipango, kazi na mahangaiko yote tuliyonayo kama watu wengine wowote, tusisahau kuiitikia kiu ambayo Mungu ameiweka ndani yetu, kiu ya kumjua, kumpenda, kumtumikia ili tuweze kuurithi uzima wa milele na kufika kwake mbinguni.

Liturujia D15

 

 

08 July 2022, 17:32