Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa sala na kazi; maisha ya kiroho na kimwili kwa ajili ya ustawi wa maisha ya mtu mzima. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa sala na kazi; maisha ya kiroho na kimwili kwa ajili ya ustawi wa maisha ya mtu mzima. 

Tafakari Neno la Mungu Dominika 16 Mwaka C: Sala na Kazi: Mwili

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaweza uwiano sawa kati ya sala na kazi; kati ya maisha ya kiroho na kimwili, kwani haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana kwa ajili ya maendeleo na mafao ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Waamini wasali kwa bidii na wafanye kazi kwa juhudi na maarifa.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Yesu akasema: “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi, kinatakiwa lakini kitu kimoja tu; na Maria amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.” Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunakwenda kuyasoma na kuyafafanua masomo ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 16 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo ndani yake tunaupokea mwaliko wa Yesu: kulitafuta na kulichagua fungu lililo jema katika maisha yetu. Ufafanuzi wa masomo: Kama ilivyo kawaida ya kipindi hiki, tunaanza kwa kuyapitia masomo yote matatu ya dominika na kuyapatia ufafanuzi. Somo la kwanza linatupeleka katika tukio moja katika maisha ya Abrahamu. Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo 18:1-10a Abrahamu yupo nje ya hema lake, mchana wakati wa jua kali, wanamjia watu watatu. Katika mazingira ya nchi ya jangwa kitendo cha kuwakarimu wageni kilisisitizwa sana. Hii ni kwa sababu pia wengi wa wageni walikuwa ni wasafiri, walisafiri kwa miguu au kwa wanyama, na walipopita katika miji ya watu ilikuwa ni jambo jema kuwakirimu kwa chakula na malazi ili waweze kuendelea na safari. Abrahamu anawakaribisha na anawaonesha ukarimu. Kwa Abrahamu, kitendo hicho ambacho ni cha kawaida na cha kiungwana kinakuwa si cha kawaida kwa sababu wageni wale watatu wanaonekana kuwa si wageni wa kawaida. Ni wageni wanaojua ahadi Mungu aliyokuwa amempa Abrahamu, ahadi ya mtoto, na wanamwambia Abrahamu “wakati kama huu mwakani Sara mkeo atapata mtoto wa kiume.”

Maisha ya waamini yarutubishwe kwa Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa
Maisha ya waamini yarutubishwe kwa Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa

Wageni hawa walikuwa ni akina nani? Baadhi ya wachambuzi wa Maandiko Matakatifu wanasema inawezekana ujio wa wageni hao watatu ulikuwa ni ujio wa Mungu mwenyewe katika Utatu Mtakatifu kwa maana walikuwa ni watatu lakini walizungumza na Abrahamu kama mtu mmoja. Biblia ambayo daima huwa inajifafanua yenyewe, yaani baadhi ya vifungu vyake vinafafanuliwa kwa vifungu vingine ndani ya Biblia, tunaona kuwa waraka kwa Waebrania 13:2 unaeleza “msisahau kuwafadhili wageni, maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua” Kifungu hiki cha Waraka kwa Waebrania ndicho kinadokeza tendo la Abrahamu. Kinaweka pamoja fadhila ya kibinadamu: ukarimu na utimilifu wa ahadi au mpango wa Mwenyezi Mungu. Na neno linalotoka kama fundisho ni kuwa kuna wakati ambapo Mwenyezi Mungu anapitisha neema zake, anatekeleza ahadi zake kwa mwanadamu kupitia matendo yale ya fadhila za kibinadamu. Matendo mema ni mfereji wa kuvuta neema za Mwenyezi Mungu. Tuingie sasa katika somo la pili. Kama ilivyokuwa katika dominika iliyopita, hata katika dominika hii somo la pili linatoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 1:24-28). Tunasikia maneno ya Paulo akisema “nayatimiliza katika mwili wangu yale yanayopungua ya mateso ya Kristo.” Ni nini anachomaanisha Paulo? Kwanza inabidi kufafanua kuwa mateso aliyoteseka Kristo hadi kufa msalabani, ni mateso yaliyotosha kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Ukombozi alimletea mwanadamu kwa njia ya mateso yake ulikuwa ukombozi kamili, haukuwa ukombozi pungufu. Ni kwa upande wa mwanadamu ambaye katika kuupokea ukombozi huo, ataupokea ukamilifu wake si hapa duniani bali katika makao ya Baba mbinguni.

Ni mateso gani sasa anayozungumzia Mtume Paulo? Paulo anazungumzia mateso ya mwili wa Kristo ambao ni Kanisa; mwili wa Kristo ambao ni wale wote wanaomwamini Kristo. Tunakumbuka wakati Kristo anamtokea Paulo, wakati huo akiitwa Saulo, anamwambia “Saulo, Saulo mbona wanitesa?” Saulo anauliza, “ni nani wewe Bwana ninayekutesa?” Na Yesu anajibu “mimi ndimi Yesu unayenitesa” (rej. Mdo 9:4-6) kumwambia kuwa mateso ya waamini wa Kristo ni mateso ya Kristo mwenyewe. Sasa fundisho lililo ndani ya maneno haya ya Paulo kwamba anakamilisha katika mwili wake kile kinachopungua katika mateso ya Kristo ni kuwa kama vile Kristo alivyoukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso, mkristo  anaalikwa kuuchuchumalia ukombozi kwa njia ya mateso, yaani kwa njia ya kuyashinda majaribu, kuushinda ulimwengu n.k. Sasa Paulo anapojipima katika njia hiyo ya kuyashinda majaribu, njia ya kuushinda ulimwengu ambayo ni njia ngumu ya mateso, anaona bado anadaiwa kupiga hatua zaidi, ni kama anasema niko tayari kuipambannia imani yangu, niko tayari kuyapokea mateso zaidi ili kujazilizia kinachopungua bado katika safari yangu ya ukombozi. Na hii ndiyo inapaswa kuwa itikadi yetu sote tunaomwamini Kristo. Katika somo la Injili, Yesu amekaribishwa ugeni katika nyumba ya Martha na Maria, dada wa Lazaro. Dada hawa wawili wanakuwa na namna mbili tofauti za kumkirimu mgeni. Martha anaingia jikoni kujishughulisha na kumuandalia chakula lakini Maria anaketi karibu naye kumsikiliza. Inaonekana shughuli zinamuelemea Martha na anakuja kwa Yesu akimlalamikia dada yake Maria aende kumsaidia. Na Yesu anatoa jibu lile ambalo tumelinukuu mwanzo wa kipindi hiki.

Waamini wawe tayari kushiriki katika mateso ya Kristo kwa ukarimu
Waamini wawe tayari kushiriki katika mateso ya Kristo kwa ukarimu

Tukilisoma somo hili katika mwanga wa masomo mawili yaliyotangulia, lile la ukarimu wa Abrahamu na utayari wa Paulo kuyapokea mateso kama Kristo alivyoteseka, tunaona kuwa dada hawa wawili wanaunganisha pamoja tunu hizo mbili: ukarimu wa kibinadamu na kujifunza kutoka kwa Kristo; shughuli za kimwili na mahitaji ya kiroho; au kama alivyofundisha Mt. Agostino, kazi za mikono na maisha ya sala, maisha ya kusikiliza Neno la Mungu. Vitu hivi viwili havipingani, vinaenda pamoja, vinategemeana. Kimoja huelekeza kwa kingine na kingine hukamilika kikijumuisha kimoja. Mtakatifu Benedikto abate alifundisha “sala na kazi” katika kanuni yake ya maisha ya kitawa. Ni somo basi linalokuja kutufundisha kuwa hatuwezi kuishi maisha ya kikristo katika ukamilifu wake kwa kuegemea upande mmoja tu wa kazi, matendo ya nje au shughuli za kimwili. Hizi zote tunahitaji kuzifanya katika muungano na shughuli za kiroho. Hali kadhalika hatuwezi kuuishi ukristo katika ukamilifu wake kama tutabaki katika maisha ya kiroho tu; sala, nyimbo, sifa n.k tukajitenga na kupuuzia yahusuyo mwili. Tunapaswa kuyapa yote uwiano unaostahili.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kutoka katika Maandiko Matakatifu ambayo dominika hii ya 16 inatupatia, ninaguswa kutafakari nanyi sehemu ya fundisho la somo la Injili. Katika mazingira yetu ya leo ambapo tunapenda kuona matokeo ya mipango au kazi zetu kuna kishawishi kikubwa cha kutokuyapa uzito yale yasiyoonekana, yale yasiyoweza kupimwa kwa macho au yale yasiyokuwa na mguso au kama tunavyozoea kusema “mashiko” kwa watu. Yesu anampomsifu Maria, na kusema fungu alilochagua yeye, kuketi miguuni na kumsikiliza, anatukumbusha nasi kuupa uzito upande huo muhimu katika maisha: kulisikiliza Neno lake, kulitafakari Neno lake na kuliona Neno lake kama msingi wa utendaji wetu. Kwetu sisi ambao tuna nafasi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu au kufundisha imani tulipe nafasi ya kutosha Neno la Mungu. Tuwape watu nafasi ya kumsikiliza Kristo anayeongea katika Maandiko Matakatifu. Vinginevyo mafundisho yetu yatakuwa kama uchambuzi wa kijamii ambao  anaweza kuufanya mwanasosholojia yoyote au wale tunawaowaita “wazungumzaji wanaotia motisha” (motivational speakers).

Sala na tafakari ya kina, viwe ni utambulisho wa mwamini
Sala na tafakari ya kina, viwe ni utambulisho wa mwamini

Na tukikosa kujikita katika msingi imara wa Neno la Mungu, tutayumbishwa na upepo uleule unaoziyumbisha jamii zetu na kushindwa kutoa lishe bora kwa manufaa ya kiroho na ya kimwili kwa watu wa Mungu. Hali kadhalika katika utendaji wetu. Utendaji unaojikita katika mambo ya nje tu haujakamilika kama haugusi ustawi wa roho. Tunaona Martha anafanya kazi nzuri kwa sababu mgeni atahitaji pia chakula. Lakini kazi ile nzuri anayofanya haimridhishi yeye mwenyewe, inamchosha, inakuwa ni mahangaiko kwa sababu hathamini mchango wa yale ambayo yanaleta ustawi wa roho. Bila ustawi wa roho kazi zetu njema zinahatari ya kushia alipoishia Martha: kuwa ni mahangaiko na usumbufu usioisha, mahangaiko yasiyoleta utulivu. Mwanadamu ni mwili na roho. Mwanadamu si kamili akiwa na roho bila mwili na si kamili akiwa na mwili bila roho. Ni hayo Martha na Maria katika umoja wao wanayotufundisha leo.

Liturujia D16
15 July 2022, 17:39