Tafakari Neno la Mungu Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukarimu kwa wahitaji ni chanzo cha neema, baraka na utakatifu kutoka kwa Mungu Tafakari Neno la Mungu Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukarimu kwa wahitaji ni chanzo cha neema, baraka na utakatifu kutoka kwa Mungu 

Tafakari Neno la Mungu Dominika 16 Mwaka C: Ukarimu Chanzo Cha Neema na Baraka!

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inatuhamasisha tuwe na moyo wa ukarimu kama alama ya huduma na utumishi kwa wengine hasa wageni na usikivu kwa Neno la Mungu ili tuweze kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu.. Waamini wajitahidi kuchota nguvu kutoka katika Neno la Mungu na maisha ya sala kwa ajili ya huduma kwa wahitaji.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa tuwe na moyo wa ukarimu kama alama ya huduma na utumishi kwa wengine hasa wageni na usikivu kwa neno la Mungu ili tuweze kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu. Somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo (Mwa 18:1-10a), linatusimulia jinsi Ibrahimu baba wa imani alivyoonyesha fadhila ya ukarimu kwa kuwapokea wageni na kuwahudumia. Kwa tendo hili alimpendeza Mungu hata akaahidiwa kupata mtoto katika uzee wake, licha ya kuwa mkewe Sara naye alikuwa tasa na alishazeeka kiasi kwamba kibayolojia asingeweza kuzaa. Lakini kwa Mungu yote yawezekana. Kumbe huduma tunayowapatia wengine zinakuwa ni chanzo cha neema na baraka machoni pa Mungu kwani ni ukarimu unaotoka ndani ya moyo uliojaa upendo unaakisi neema na baraka toka kwa Mungu. Katika somo la pili la Waraka wake kwa Wakolosai (Kol. 1:24-28), Mtume Paulo anatufundisha kuwa Kristo ameteswa kwa ajili ya watu wote ili auweke ufalme wa Mungu. Nao wote wanaoendeleza kazi ya Kristo lazima washiriki mateso yake katika kuwahudumia wengine. Yeye Paulo ni mfano wa utumishi bora kwa wengine kwa kuyatoa maisha yake kwa kuvumilia taabu na mahangaiko ili upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo uweze kudhihirishwa kwa njia yake.

Ndiyo maana anasema; “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa lake. Na hii ndiyo siri iliyofichwa kwa wamchao Mungu, yaani Watakatifu wake. Ni siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, na sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake. Ni kwa siri hii, nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliyopewa kwa faida ya watu, nikilitimiza neno la Mungu” (Kol.1:24-25). Haya yote yanaunganishwa kwa neno moja ukarimu unaoongozwa kwa upendo. Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 10:38-42), ni simulizi la Maria na Martha kumkaribisha Yesu nyumbani kwao. Simulizi hili linasisitiza kuwa huduma na utumishi kwa wengine visitufanye tushindwe kusikiliza neno la Mungu ndiyo maana Yesu anamkaripia Martha si kwa sababu ya huduma yake bali kwa sababu anajishughulisha mno na mambo yanayohusu mwili na kuayaacha ya wokovu wa roho. Kumbe huduma kwa wengine hazipaswi kuwa katika mahitaji ya kimwili tu bali pia kiroho. Tukumbuke kuwa ukarimu na upendo vyote vinapaswa kuambatana pamoja.

Waamini wajichotee nguvu na neema kutoka katika Neno la Mungu na Sala kwa ajili ya huduma
Waamini wajichotee nguvu na neema kutoka katika Neno la Mungu na Sala kwa ajili ya huduma

Mungu ni upendo na Mungu ni ukarimu. Ukarimu ni uwepo wa kimungu ndani yetu. Unapofanya tendo la ukarimu unaakisi uwepo wa Mungu ndani yako. Tunapowakirimia wenzetu wenye mahitaji mbalimbali twafanya tendo la Kimungu. “Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa na Mungu, maana huwapa maskini chakula chake (Mithali 22:9). Ibrahimu anapewa hakikisho hilo na baraka hizo mbele ya Mungu kwa ukarimu alioonyesha kwa wageni nao wakamwambia; “Bwana asema, hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume”. Ni baraka toka kwa Mungu kwa ukarimu wake. Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto barua yake ya pili anasema; “Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Kor 9:6-7). Ni kwa maana hii ukarimu hugeuka kuwa neema na baraka ambazo ndiyo hazina yetu tunayojiwekea mbinguni kama anavyotuambia Yesu; “Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako” (Mt. 6:19-21). Mzaburi anasisitiza; “Heri amkumbukaye mnyonge, maana Bwana atamwokoa siku ya taabu” (Zab. 41:1).

Kujikusanyaji na kujiwekea hazina mbinguni kunafanyika kwa kujikusanyia mali za duniani na kuzitoa kwa kuwapa wenye shida wasioweza kujikusanyia, wanyonge na wahitaji kwa moyo wa ukarimu na upendo, na ni katika kuwasaidia wahitaji, muujiza hufanyika, vitu hugeuka kuwa neema, na neema hizo huwekwa mbinguni kwenye hazina yako, ambapo ndipo utakuwa moyo wako (Mt. 6:21). Kwa hiyo kadri ulivyo na neema hizo kwa wingi mbinguni, wakati utakapokuwa umekwenda kuzimiliki, nawe utaweza kuwagawia wanaokuomba msaada wa neema hizo, nazo haziishi, kama ule unga wa mjane wa Sarepta aliyemsaidia mwenye shida Nabii Elia, na baada ya tendo hilo la ukarimu, unga wake haukupungua, wala mafuta katika chupa hayakwisha (1Fal. 17:16). Neema hizo za mbinguni, ndizo zinaweza kufanya miujiza hapa duniani wakati tuombapo sala zake, yeye akiwa mbinguni. Hii ndiyo maana, wakati Kanisa linapofanya mchakato wa kumtangaza mtu kuwa Mtakatifu, linaomba muujiza unaopatikana kutokana na maombezi yake yenye nguvu za neema alizonazo mtumishi wa Mungu mwenye kufanyiwa mchakato huo.

Sala ya mtu aliyejaa neema husikilizwa haraka mbele ya kiti cha Mungu, halikataliwi, majibu yanatokea mara moja. Kwa hiyo kadri mtu alivyo na neema hizi kwa wingi katika hazina yake, ni kadri hiyohiyo anavyoweza kutusaidia kwa msaada wa sala zake. Kama neema ni kidogo hataweza kutupatia, maana hataweza kutoa zaidi ya alichonacho. Ndiyo maana michakato ya kumtangaza mtu aliyekufa mwenyeheri na baadae utakatifu wake, kwa wengine miujiza inatokea haraka mfano kwa Baba Mtakatifu Yahane Paulo II na Mama Theresa wa Calcutta. Hii ni kwa sababu wanazo neema kwa wingi. Kwa wengine miujiza inachelewa au hata kukosekana kabisa; kwa sababu hazina ya neema waliyojiwekea mbinguni ni ndogo. Haya mambo ni mazuri sana tufanye hima kuwa na moyo wa ukarimu ili tujiwekee hazina mbinguni lakini haya yote yafanyike kwa upendo, na sio kwa woga kwamba, nisipofanya matendo ya huruma sitaenda mbinguni au kwamba nitatupwa katika moto wa milele.

Sala na Kazi ni chanda na pete
Sala na Kazi ni chanda na pete

Mtakatifu Basili anasema; “Kama tukiacha kutenda dhambi kwasababu ya woga, tuko katika hatari ya kuwa watumwa; kama tukishikilia ushawishi wa mishahara tutafanana na mamluki au askari wa kukodiwa; mwisho kama tukitii kwa ajili ya uzuri wenyewe na kwasababu ya upendo kwake, tuko katika nafasi ya wana na watoto wa Mungu”. Hivyo upendo ndio utawale katika kutenda matendo ya huruma, maana ajuaye ni Mwenyezi Mungu, yeye atayapima matendo yote kwa kipimo sahihi (1Sam. 2:3). Tusiyafanye matendo ya huruma ili watu watuone na kutusifu, maana tukifanya hivy hatutapata thawabu yetu machoni pa Mungu mbinguni (Mt. 6:5). Kama lengo la kufanya matendo ya ukarimu, ni kuonekana na kupata sifa kwa watu, basi hiyo ndiyo thawabu yako, yaani, sifa na mashangilio ya watu wanayokupatia na hivyo usitegemee thawabu mbinguni kwani umezipata hapahapa duniani, huna chochote mbinguni. Bali katika kufanya matendo ya ukarimu iwe ni kwamba mapendo ya Kristo yatimiliki (2Kor. 5:14), na Mungu Baba aonaye sirini atakujazi (Mt. 6:6).

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anasema; baada ya ugeni hapa duniani, natumaini kwenda na kukufurahia wewe, lakini, sitaki kujiwekea akiba ya mafao ya mbinguni. Nataka nitumikie pendo lako tu mwishoni mwa maisha haya, nitatokea mbele yako nikiwa na mikono tupu, kwani sikuombi uhesabu kazi yangu. Haki yetu yote inalawama machoni pako. Nataka tu, nivikwe katika haki yako mwenyewe na nipate kutoka kwenye pendo lako miliki yako ya milele. Mambo ya kusema kwamba nimefanya matendo mengi ya huruma; kwamba nimesaidia maskini wengi, nimelisha wenye njaa wengi, nimenywesha wenye kiu wengi, nimehudumia wagonjwa wengi na kazi nyingi sana nimefanya; hayo si hoja kwa Mungu, kwani, sawa umefanya hayo yote tena kweli ni mengi, lakini kama huna upendo, si kitu, yote ni bure. Jambo la msingi ni kwamba, usitumikie haki, bali upendo, kwani upendo ni kila kitu na ndio unaotustahilisha kuupa ufalme wa mbinguni. Nenda nawe kafanye hivyo ili upate kibali machoni pa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 16 Ukarimu
15 July 2022, 15:52