Tafuta

Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Maisha ya Kikristo yanapaishwa wa tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Maisha ya Kikristo yanapaishwa wa tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Tafakari Dominika ya 16 ya Mwaka C: Pyaisheni Maisha ya Kikristo Kwa Sala, Neno na Sakramenti

Waamini wanakumbushwa kwamba, bila ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao, hawataweza kuthubutu kusimama kwa jeuri yao wenyewe. Huu ni mwaliko wa kuendelea kushikamana na Kristo Yesu katika Neno, Sala, Sakramenti za Kanisa na huduma kwa jirani kama kielelezo makini cha imani tendaji inayomwilishwa kwenye ukarimu hasa kwa maskini na wahitaji

Na Padre Efrem Msigala, OSA., - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ujenzi na upyaisho wa maisha ya mwamini ni mapambano pevu na endelevu yanayohitaji neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Neema hii inapaswa kulindwa na kutunzwa kwa njia ya sala na kazi. Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka ameonesha ushindi mkubwa katika maisha ya wafuasi wake, chemchemi ya Injili ya matumaini kwa wale waliopondeka moyo na kukata tamaa; tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwenyezi Mungu anaendelea kuonesha nguvu yake katika kazi ya uumbaji inayopata utimilifu wake katika kazi ya ukombozi. Huu ndio ushindi wa Kristo Yesu unaomwezesha kujenga upya, Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na kupyaisha maisha ya waja wake. Waamini wanakumbushwa kwamba, bila ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao, hawataweza kuthubutu kusimama kwa jeuri yao wenyewe. Huu ni mwaliko wa kuendelea kushikamana na Kristo Yesu katika Neno, Sala, Sakramenti za Kanisa na huduma kwa jirani kama kielelezo makini cha imani tendaji. Somo la kwanza, kutoka Kitabu cha Mwanzo, 18:1-10, linahusu ziara ya Malaika katika umbo la kibinadamu kwa Ibrahimu. Aliwaonesha ukarimu mwingi. Mwishoni mwa ziara hiyo, malaika walimwahidi kwamba mke wake, Sara, ingawa alikuwa mzee, atapata mwana. Ibrahimu, baba wa mataifa mengi, anaitwa mtu wa imani. Hakupoteza imani katika Mungu hata katika nyakati zisizo hakika na zenye majaribu. Tukio hili lilionesha jinsi imani yake ilivyothawabishwa. Kutokana na imani aliweza kupata dhawabu kubwa ya uzao, baraka, eneo na sasa anaitwa baba wa imani.

Waamini wakisikiliza Neno la Mungu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa AMECEA
Waamini wakisikiliza Neno la Mungu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa AMECEA

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wakolosai (1:24-28). Anazungumza juu ya thamani ya mateso. Kwa kweli, alisema, “Nayafurahia mateso yangu kwa ajili yenu.” Aliteswa sababu ya kumtangaza Kristo. Alieleza hivi: “Katika mwili wangu natimiza yale yaliyopungua katika dhiki ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, ambao ni Kanisa. Kwa maneno mengine, anasema kwamba mateso yake ni kushiriki kwake katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa. Ni kwa njia ya mateso ya Kristo kwamba Kanisa linapokea neema nyingi. Wakristo wanapoungana na Yesu kutii mapenzi ya Baba, hii inahusisha mateso, lakini hii ndiyo njia ya kulifungua Kanisa kwa neema zaidi kutoka mbinguni. Kwa njia hii, tunakuwa wakombozi pamoja na Kristo, njia ambayo neema ya wokovu ya Kristo inaendelea kutiririka ulimwenguni. Yesu hakutuokoa na mateso. Alituokoa kupitia mateso. Injili ni ufafanuzi wa kawaida wa njia mbili tofauti za kumfuata Bwana: matendo na tafakari: “Ora et Labora” (sala na kazi) Martha anawakilisha ufuasi hai; ufuasi wa matendo au kazi.  Mariamu anawakilisha ufuasi wa kutafakari au sala.

Martha na Mariamu walikuwa na mawazo yao kuhusu kumtumikia Bwana. Martha alienda moja kwa moja jikoni na harakaharaka akawaandalia wageni wake maalum chakula. Alikuwa na mahangaiko mengi kwa sababu alikuwa akifanya kila kitu peke yake. Hivyo akapoteza uvumilivu hadi kumlalamikia mgeni kwa kukaa na ndugu yake bila kumsaidia shughuli za jikoni. Kwa upande mwingine, Maria hakujali kuhusu kazi ya jikoni. Aliketi miguuni pa Yesu na kusikiliza kila neno lake. Martha anawakilisha utume unaofanya kazi, wakati Mariamu mtume wa kutafakari. Ni yupi kati ya hao wawili aliyependelewa na Yesu? Martha alipoingia na kulalamika kwamba dada yake hakuwa akimsaidia, Yesu alimkemea hivi kwa upole: “Martha, Martha, unahangaika na kuhangaikia mambo mengi. Kuna haja ya kitu kimoja tu. Mariamu amechagua fungu lililo bora zaidi, wala hataondolewa kwake” (Lk 10:41-42). Je, hilo lamaanisha kwamba Yesu aliona maisha ya kutafakari kuwa muhimu zaidi kuliko maisha yenye utendaji? Bila shaka sivyo. Vyote viwili ni muhimu katika maisha ya kila Mkristo. Hata hivyo, Yesu alihakikisha kwamba tunaweka vipaumbele vyetu sawasawa: mambo ya kwanza kwanza.

Imani tendaji inamwilishwa katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi
Imani tendaji inamwilishwa katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi

Lakini Yesu alimkemea Martha kwa upole kwa sababu ya kuhangaika sana na kuhangaikia mambo mengi. Na hasa akifanya kwa manung’uniko tena mbele ya mgeni. Kwa upande mwingine, alikubali uamuzi wa Maria wa kuketi na kusikiliza kila neno alilosema. Kwa kweli, “mtu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Huduma ya bidii ya Martha ilikosa mchango wa kiroho na nuru sababu ya manung’uniko hata kama ni muhimu sana. Ndio maana alikuwa na shughuli nyingi na wasiwasi juu ya mambo mengi. Usikivu wa Maria kwa maneno ya Yesu lazima ulimpa mwanga wa kutosha na msukumo wa kuanza huduma yenye matunda na yenye kujenga, isiyo na wasiwasi. Dhamira ya Dominika hii ni imani katika Bwana. Abrahamu hakuwa na wasiwasi kuhusu kutokuwa na mtoto. Alikuwa na uhakika kwamba Mungu hatasahau ahadi yake. Na alizawadiwa kwa zawadi ya mwana, Isaka na baadaye uzao uliongezeka vizazi hadi vizazi. Mtakatifu Paulo alikabiliwa na matatizo mengi sana katika kueneza Injili kwa Mataifa. Lakini hakukatishwa tamaa na mateso hayo. Badala yake, aliyakubali kama njia yake ya kushiriki mateso ya Kristo. Katika Injili, Yesu alimfanya Martha atambue kwamba katika utendaji na utumishi wa aina yoyote kwa Mungu, imani ni muhimu, ili kusiwe na haja ya kuhangaika. Kwa hiyo, mtu anapaswa kuchukua muda wa kutulia na kusikiliza Neno la Mungu kwa imani kamili na kutumaini katika hekima na maongozi yake. Hivyo kuunganisha matendo na sala kwa Mungu.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika hii ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa, tunaalikwa tujitahidi kumkaribisha Kristo Yesu rafiki na mgeni wetu. Leo, kanisa linakumbusha umuhimu wa ukarimu. Ni wema wa Kikristo na wajibu wetu kwa wengine. Pia, anatukumbusha haja ya kuwa makini na Kristo Mgeni wetu. Muhimu zaidi, tunashauriwa kutozingatia zaidi vitu vya kimwili kuliko mambo ya kiroho. . Katika somo la kwanza, Abrahamu alionyesha ukarimu wake kwa kuwapokea na kuwakaribisha wageni katika nyumba yake. Kwa bahati nzuri kwake, wageni walikuwa ni wajumbe kutoka kwa Mungu. Sio tu kwamba aliwakaribisha chini ya paa yake, alishughulikia sana mahitaji yao ya kimwili. Vivyo hivyo alitilia maanani ujumbe na maagizo yao. Kwa hiyo, kupitia ukarimu wake, alionyesha hali yake ya kiroho. Kwa hili, Mungu aliamua kuthawabisha na kubariki nyumba yake. Sehemu muhimu sana ya ukarimu ni kuzingatia watu. Wakati fulani, kile ambacho watu wanahitaji kutoka kwetu si vitu vya kimwili tu, bali umakini wetu. Leo, ni wazi kwamba Wakristo wengi wanakosa hali hiyo. Hii ni licha ya ukweli kwamba tunafanya kazi nyingi katika nyumba ya Mungu. Kwa hivyo msemo usemao: “Mtu ana wakati kwa ajili ya kazi ya Mungu, lakini hana wakati wa Mungu mwenye kazi.” hata hatuna muda wa kutafakari kiroho.

Kazi ni utimilifu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Kazi ni utimilifu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Katika baadhi ya familia zetu, tunatilia maanani kila jambo lingine, lakini hatuzingatii sana ukuaji wa kiroho wa washiriki wa familia zetu. Tuna muda kwa ajili ya shughuli za kijamii, lakini muda kidogo au hakuna wa kuomba pamoja au kujifunza neno la Mungu pamoja. Tunahitaji kuimarisha uhusiano wetu na Kristo, kwa kuketi karibu naye tukiwa familia, kwa kuzingatia yale anayotuambia. Kristo anahitaji usikivu wetu, kwa sababu ana jambo jipya la kutufundisha kila siku. Anataka kutumia wakati mzuri na sisi kila siku. Kwa hiyo, hatupaswi kuruhusu chochote kutuzuia kumkaribisha, au kuondoa uangalifu wetu kuondoka katika uwepo wake. Anataka tuishi daima katika uwepo wake wakati. Zaburi inatukumbusha kwamba: “Wenye haki wataishi mbele za Bwana!” Waamini tujitahidi kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu pamoja na sala inayomwilishwa katika huduma kwa Mungu na jirani. Utamaduni wa kusikiliza ni dhana inayopewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Dominika ya 16
14 July 2022, 07:07