Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa sala katika maisha na udumifu wake. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa sala katika maisha na udumifu wake. 

Tafakari Dominika 17 Mwaka C wa Kanisa: Katekesi Kuhusu Sala

Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Kuna mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Kuna Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Salini!

Na Padre Efrem Msigala, OSA., - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya mwaka C. Uzee ni kipindi cha neema na baraka. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii. Mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi thabiti ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2022 anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wazee kwani wao ni “chakula” kinacho rutubisha maisha yao; hekima na busara inayofichama katika jamii ya watu.” Ni katika muktadha huu, wazee wanapaswa kuadhimishwa, ndiyo maana anasema Mama Kanisa ameanzisha Siku ya Wazee Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Dominika ya Nne ya Mwezi Julai na kwa mwaka huu ni Dominika tarehe 24 Julai 2022, yaani Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi zake kuhusu Fumbo la Maisha ya Sala anasema, ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Kuna mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Kuna Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli.

Watoto wajengewe utamaduni wa kusali kunzia kwenye familia
Watoto wajengewe utamaduni wa kusali kunzia kwenye familia

Katika Katekesi kuhusu Fumbo la Sala, Baba Mtakatifu amekwisha wahi kupembua kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake na kwamba, Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala si lelemama yataka nguvu ya ndani. Amegusia kuhusu fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala! Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ndiyo mada iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya mwisho! Katika Dominika hii tunasikia umuhimu na uvumilivu katika sala kwenye maisha ya kila siku. Tunahitaji kusali bila kukata tamaa.  Somo la kwanza linahusu hatima ya Sodoma na Gomora. Mungu alichoshwa na upotovu na matendo machafu dhidi ya asili ya watu. Mungu aliamua kuharibu miji hiyo miwili. Lakini Abrahamu alimwomba Mungu kwa ajili ya watu. Abrahamu anatupa mfano wa sala ya dhati na ya ndani. Alizungumza na Mungu kana kwamba anazungumza tu na mwanadamu mwingine. Alikuwa mtu wa karibu sana na Mungu katika sala. Alijadiliana na Mungu, na alianza kubembeleza kama mfanyabiashara akitaja idadi ya watu waadilifu. Alianza na watu hamsini waadilifu, kisha akashuka mpaka akafika kumi. Mungu alikubali kuuokoa mji kama kungekuwa na watu kumi waadilifu. Mungu ni mwenye haki, lakini pia ni mwingi wa rehema. Alisikiliza kwa subira sala za Ibrahimu zenye uchungu. Lakini kama ilivyotokea, ni wazi hakukuwa na watu kumi waadilifu  pale. Sodoma na Gomora zilichomwa sababu ya maovu yaliyokithiri miji yote miwili.

Somo la pili ni kutoka Waraka Mtakatifu Paulo kwa Wakolosai 2:12-14. Anazungumza juu ya ubatizo. Katika Yesu, tulibatizwa, na hii ilitufanya kuwa watoto wapendwa wa Mungu na warithi wa ufalme Wake. Tunahakikishiwa na Mtakatifu Paulo kwamba, Mungu daima atakuwa na neema na huruma kwetu kwa maana sisi ni watoto wake wapendwa. Injili ya Luka 11:1-13 inatupa fundisho la Yesu juu ya sala ya Baba yetu. Ni sala fupi kuliko katika Injili nyingine. Lakini fundisho sio tu kuhusu fomula au kanuni ya sala. Fupi au ndefu. Bali pia inatukumbusha kwamba Mungu ni Baba yetu mwenye upendo na mwema, bora zaidi kuliko baba yeyote wa kibinadamu.  Ni baba wa kila mmoja ndiyo maana tunasema Baba yetu. Kwa hivyo, tunapaswa kuomba kwa upole, ukaribu na imani kamili kwa Baba yetu mwenye upendo kwa kuwa anatutazama kama watoto Wake wapendwa. Luka anakazia zaidi mafundisho ya Yesu kuhusu sala kuliko Wainjili wengine. Pia anamtaja Yesu katika sala kuliko wengine. Katika somo la leo, tangu mwanzo wa Sura ya 11 ya Injili yake, Luka anatoa msingi wa mafundisho ya Yesu kuhusu sala. Inajumuisha Yesu akifundisha sala kwa wanafunzi wake baada ya yeye kusali na hivyo kuombwa na wanafunzi wake awafundishe kusali, kama vile Yohane Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.

Waamini watambue mambo muhimu katika sala: Imani
Waamini watambue mambo muhimu katika sala: Imani

Kristo Yesu anawafundisha sala ya Kikristo maarufu zaidi, Baba Yetu, au Sala ya Bwana. Baada ya hapo anatoa mfano juu ya jirani anayeendelea, na hakikisho kwamba Mungu husikia maombi yetu.  Baada ya kuwafundisha wanafunzi wake sala rahisi ya kila siku, Yesu anaendelea kuwahakikishia kwamba Mungu hujibu sala. Kwanza anasimulia mfano wa jirani mwenye bidii ambaye anamwomba rafiki mkate usiku wa manane. Rafiki huyo tayari yuko kitandani na hana nia  ya kusumbua familia yake kwa kufungua mlango. Lakini kwa sababu jirani ni mwenye kuendelea kuomba bila kuchoka, mtu aliyelala huamka na kumpa kila anachohitaji. Ikiwa jirani yuko tayari kutusaidia ikiwa tunadumu vya kutosha, Mungu asingeweza kujibu maombi yetu? Fundisho hili linahitimisha kwa ukumbusho kwamba ikiwa tutatafuta, tutapata jibu. Ikiwa baba wa kibinadamu, pamoja na makosa yake yote, anajua jinsi ya kuwapa watoto wake zawadi nzuri, je, Baba yetu wa mbinguni hatatupa sisi zaidi? Mambo muhimu katika sala ya mkristo: Sala ni mawasiliano na Mungu. Hasa zaidi, sala ni kuinua roho zetu kwa Mungu. Ni mawasiliano ya pande mbili. Ni uhai wa nafsi zetu. Ni "oksijeni ya roho", kulingana na Mtakatifu Padre Pio. Katika sala tunakutana na Mungu. Tunakuwa kitu kimoja na Mungu. Ndio maana mtu anayesali ana nguvu kwa sababu Mungu yu ndani yake.

Mambo Muhimu ya sala: Imani - Tunaomba kwa sababu tuna hakika juu ya nguvu za Mungu, na tunaamini upendo na utunzaji Wake. Mtu ambaye hana imani hakika hataomba. Unyenyekevu - Tunapoomba, tunakubali ukweli kwamba Mungu ndiye chanzo cha kila kitu katika maisha yetu. Sisi si chochote bila Mungu. Kwa hiyo, katika sala, tunainama chini kwa unyenyekevu, tukimwomba Mungu msaada, pamoja na msamaha Wake kwa ajili ya dhambi zetu na kutostahili. Bila unyenyekevu, hakuwezi kuwa na sala ya kweli. Mawasiliano – sala ni mawasiliano yetu na Mungu. Daima ni mawasiliano ya pande mbili. Tunazungumza na Mungu; Yeye Anasikiliza. Mungu huzungumza nasi; tunapaswa kusikiliza. Mababa wa Kanisa wanawahimiza waamini kusali sala zote na maombi kila wakati katika Roho, huku wakikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote. Kukesha na kufunga daima ni sehemu ya utaratibu wa maisha ya mwamini, lakini kusali bila kukoma ni sheria. Hii ni bidii inayobubujika kutoka katika mapendo. Ni kinyume kabisa cha uzito wa uvivu na kwamba, pambano kamili la sala ni lile la mapendo ya unyenyekevu, matumaini na ya kudumu. Haya ni mapendo yanayofungulia nyoyo za waamini mambo makuu matatu yanayotoa uhai wa imani juu ya sala. Daima inawezekana kusali. Sala ni hitaji la lazima kwa maisha. Sala na maisha ya Kikristo ni sawa na chanda na pete, vinategemeana na kukamilishana. Rej. KKK 2742 – 2745. Kwa kuwa Mungu anajua kila kitu tunachohitaji, kwa hiyo, sala inapaswa kuwa zaidi ya kumsikiliza Mungu badala ya kuzungumza. Ndiyo maana tunahimizwa sio tu kusoma novena na vitabu vya maombi, lakini pia tunahitaji wakati mwingine ukimya katika tafakari kusikiliza Mungu anasema nini kwetu.

Dominika 17
20 July 2022, 15:51