Tafuta

Ni dominika inayotupa nafasi ya kutafakari mojawapo ya nguzo muhimu sana katika maisha ya mkristo, na nguzo hii ni sala. Ni dominika inayotupa nafasi ya kutafakari mojawapo ya nguzo muhimu sana katika maisha ya mkristo, na nguzo hii ni sala. 

Tafakari Dominika 17 Mwaka C wa Kanisa: Nguzo ya Sala Katika Imani

Leo tunayaangalia masomo ya dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa, dominika tunayoiadhimisha wiki hii. Ni dominika inayotupa nafasi ya kutafakari mojawapo ya nguzo muhimu sana katika maisha ya mkristo, na nguzo hii ni sala. Waamini wanahimizwa kujenga na kudumisha utamaduni wa sala kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu, ili kumshukuru, kumtukuza na kumsifu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Mitume wa Yesu wakamwambia Kristo Yesu: “Bwana utufundishe kusali kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.” Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayaangalia masomo ya dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa, dominika tunayoiadhimisha wiki hii. Ni dominika inayotupa nafasi ya kutafakari mojawapo ya nguzo muhimu sana katika maisha ya mkristo, na nguzo hii ni sala. Ufafanuzi wa masomo: Tuanze, kama kawaida yetu, kwa kuyapitia masomo yote matatu ya dominika na kuyaptia ufafanuzi. Somo la kwanza (Mwa 18: 20-32) linatuletea mazungumzo kati ya Mungu na Abrahamu. Ni mazungumzo yanayochukua sura kama ya mnunuzi anayembembeleza muuzaji ampunguzie bei ya bidhaa anayotaka kuinunua. Tunasema hivyo kwa sababu katika mazungumzo hayo, Abrahamu anamshawishi Mungu aishushe hasira yake dhidi ya miji ya Sodoma na Gomora asiiangamize. Anamwambia Mungu “utaharibu watu wema pamoja na waovu”? anasema “je, ukikuta katika Sodoma watu wema 50 utauangamiza?” Mungu anasema “hapana. Kwa ajili ya watu 50 sitauangamiza”. Abrahamu anapunguza idadi, “Je, watu wema wakiwa 45”? Mungu anasema “sitaangamiza”. Abrahamu anaendelea kupunguza na wanaendelea kuvutana hadi Mungu anasema akikuta watu wema 10 hataangamiza mji huo.

Anachokifanya Abrahamu ni sala. Ni maombezi anayoyafanya mbele ya Mungu kwa ajili ya wakosefu. Katika maombezi hayo ya Abrahamu ni vizuri kuona namna ambavyo Mungu anamsikiliza. Mungu ambaye hapo awali ni kama alikusukudia kuangamiza mara moja Sodoma na Gomora, kwa maombezi ya Abrahamu anakuwa tayari kubadili mawazo asiuteketeze mji kama katika mji atakuda idadi hiyo ambayo Abrahamu anaitaja. Hili ni somo linalotufundisha kuwa Mungu ni msikivu. Mungu anasikiliza sala za wale wamuombao: wale wamuombao kwa ajili yao au kwa ajili ya wengine. Sasa, Mungu ambaye ni mtakatifu wa watakatifu na ndiye utakatifu wenyewe ni kwa misingi gani anaweza kukaribiwa na mwanadamu na kuisikiliza sala yake? Mtume Paulo katika somo la pili (Kol 2:12-14) anawaandikia Wakolosai na kutufundisha sisi pia kuwa ni kwa njia ya ubatizo ambapo mwanadamu aliyekuwa amekufa kwa sababu ya dhambi, amefufuliwa pamoja na Kristo. Ni kwa njia ya ubatizo mwanadamu anapewa hadhi ya kuwa mwana sawa na Yesu mbele ya Mungu Baba. Ni kwa sababu hii sisi tunapata ujasiri wa kumuita Mungu – Baba. Yesu mwenyewe anapowafundisha wanafunzi wake sala, hilo ndilo neno la kwanza analowaambia walitaje: wamwite Mungu – Baba. Na ndivyo ilivyo. Mungu ni Baba yetu na sisi tu wanawe.

Sala inarutubisha na kupyaisha imani
Sala inarutubisha na kupyaisha imani

Katika somo la Injili (Lk 10:38-42) Yesu anawafundisha wanafunzi wake kusali. Anaitikia ombi hilo tulilolinukuu mwanzoni mwa kipindi hiki, ombi la “Bwana utufundishe kusali kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.” Tunafahamu kuwa baadhi ya wanafunzi wa Yesu walikuwa ni wanafunzi wa Yohane Mbatizaji. Watakuwa wanajua namna Yohane alivyowafundisha kusali. Pia katika mazingira ya dini ya uyahudi, mazingira walimoishi wote, watakuwa wanajua namna wayahudi wanavyosali. Wao sasa ambao Kristo amekuja na upya wa mafundisho yake pamoja na upya wa maisha sala yao inatakiwa iweje? Yesu anawafundisha sala ya Baba Yetu, ambayo ni sala tunayoisali sote tulio wafuasi wa Yesu, lakini hapo hapo ni muhtasari wa namna ambavyo anapaswa kusali kila aliye mfuasi wa Kristo. Yesu anawaambia “mnaposali semeni Baba yetu uliye mbinguni” Tumekwisha eleza uzito wa hilo neno Baba. Ni neno linalomuweka mkristo katika uhusiano wa Baba na mwana. Mkristo anaposali, sala yoyote ile, anaalikwa kutambua kuwa kwa njia ya sala anaingia katika mazungumzo na Baba. Sala ni uhusiano wa mtu na Baba yake wa mbinguni. Sala sio kutamka maneno fulani yenye nguvu ya kutupatia tunachotaka. Ni uhusiano wa kiumbe na Muumba wake. Maneno tunayotamka ni maneno yanayotusaidia kuingia katika uhusiano huo. 

Sasa sala hii ya Baba Yetu inakuwa vipi muhtasari wa namna ambayo mkristo anapaswa kusali? Inayotuonesha kuwa sala ya mkristo huanza kwa kumtukuza Mungu “Jina lako litukuzwe”. Ni Mungu astahiliye kutukuzwa, kuabudiwa na kusifiwa. Tunapomtukuza Mungu tunatambua ukuu wake juu yetu na juu ya yote tunayoyapitia. Wale vijana watatu Shadrak, Meshak na Abednego katika kitabu cha Danieli walipotupwa katika shimo la wanyama wakali na hata katika tanuru ya moto sala yao ilikuwa ni kumsifu na kumtukuza Mungu. Paulo na Sila katika kitabu cha Matendo ya Mitume, walipokuwa wamefungwa gerezani, usiku kucha walisali na kuomba wakimsifu Mungu kwa nyimbo.  Baada ya kumtukuza Mungu, Yesu anaalika yule anayesali kujiweka chini ya mapenzi ya Mungu “utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”. Hii ni kutambua kuwa mkristo anaposali haweki kama kipaumbele kile anachotaka kumwomba Mungu bali anaweka kama kipaumbele kile ambacho Mungu anataka kitendeke katika maisha ya ya yule anayesali. Je hii inamaanisha kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo mkristo hapaswi kuweka katika sala kumuomba Mungu? Hapana.

Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu
Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu

Mkristo aweke ombi lake lote mbele ya Mungu kwa kutambua kuwa kile Mungu atakachojibu kufuatia ombi hilo ndicho Mungu katika mapenzi yake ameona ni chema zaidi kwake katika wakati huo. Ni kutambua kuwa tumo ndani ya maongozi yake Mungu, Mungu aliye na mipango yake juu ya maisha yetu. Mfano hai wa moyo huu katika sala ni Mama Bikira Maria na maneno yake kwa malaika “mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena.” Ni kutoka hapo mwombaji anaweka ombi kwa ajili ya mahitaji ya kimwili na ya kiroho kwa ajili yake au kwa ajili ya wale anaowaombea, walio hai au waliokwisha tangulia. Mwisho, katika maneno “utusamehe kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea” Yesu anatufundisha kuwa sala inatuwajibisha. Inatuwajibisha kwenda kuuishi msamaha, inatuwajibisha kwenda kujishugulisha, kwenda kuishi fadhila na tunu zile tunazozikiri katika imani yetu. Sala inapoisha ndipo sala inapoanza.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 17 ya mwaka C wa Kanisa yanatupa nafasi ya kutafakari juu ya sala na hasa juu ya maisha yetu ya sala. Nadharia ya sala au mafundisho kuhusu sala, si vigumu sana kuyajua. Changamoto inakuja pale ambapo tunatakiwa kutoka katika nadharia hiyo na kusali; kutoka katika kujua nini maana ya sala au nini umuhimu wa sala na kuwa watu wa sala; kuitoa sala kichwani na kuiweka moyoni. Bila kufanya hivyo sala ni ngumu na vigumu kudumu katika sala. Mtu ataanza kusali lakini atachoka mara moja na kuacha na wakati mwingine mtu anapoanza kusali ndipo mawazo ya kufanya vitu vingine yanakuja au ndipo umuhimu wa vitu vingine unakuja. Mtu anaishia kuahirisha sala: “nitasali baadaye”, yanapita masaa, zinapita siku bila kusali. Watakatifu wengi wametufundisha kuwa namna nzuri ya kujifunza kusali ni kusali kwa kufuata nyayo za waliofanikiwa kusali. Na mfano wa pekee tulionao katika Kanisa, mfano wa yule aliyefanikiwa katika kusali ni Mama yetu Bikira Maria. Mama huyu anaitwa malkia wa watakatifu wote kwa maana ndiye anayewaongoza watu kuufikia utakatifu akiwasaidia kuishi maisha ya sala.

Waamini wajifunze kusali kwa mahitaji mbalimbali.
Waamini wajifunze kusali kwa mahitaji mbalimbali.

Katika matokeo yake mbalimbali, matokeo ambayo Kanisa limeyaidhinisha, Bikira Maria amealika watu kusali na hapo hapo yeye mwenyewe akiahidi kuwa mwombezi na msaada wa wote wanaotaka kumfuasa Kristo kwa njia hiyo ya sala. Mwitikio wa Kanisa, mwitikio wa kujiweka chini ya shule ya sala ya Maria, umekuwa ni kuwaalika waamini wajiweke wakfu kwa Mama Maria. Kujiweka wakfu huku kwa maneno rahisi ni kujikabishi kwa Mama Bikira Maria ili yeye akushike mkono akuongoze katika njia ya sala. Hii ni changamoto ya kufuata kile ambacho Kristo Yesu mwenyewealikifanya pale juu Msalabani, alipomkabidhi Yohane kwa Bikira Maria, ni kama Yesu alimwambia, “Yohane ukitaka kuwa mfuasi wangu kamili fuata nyayo za Mama” na Yohane alichofanya ni kumkaribisha B. Maria nyumbani kwake. Kumbe kila mtu anaweza kujiweka wakfu mtu binasi, wanaweza kujiweka wakfu wanandoa na inaweza kujiweka wakfu familia nzima. Ni kwa nia hii hii Papa Francisko alitualika mwezi machi mwaka huu kuuweka wakfu ulimwengu mzima chini ya Mama Bikira Maria. Ninavutwa kukushirikisha nawe ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News kuwa katika kuupokea mwaliko wa dominika hii, mwaliko wa sala, kujiweka tayari kujifunza kusali na kuwa mtu wa sala kwa kupitia maongozi ya Mama yetu Bikira Maria.

Liturujia Dominika 17
22 July 2022, 18:20