Tafuta

Kristo Yesu anasema “angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu alivyo navyo.” Kristo Yesu anasema “angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu alivyo navyo.”  

Tafakari Dominika ya 18 Mwaka C: Bila Mungu Yote ni Ubatili Mtupu!

Mafundisho ya Injili yanalenga kumsaidia mwanadamu kuipa mali nafasi yake inayostahili katika maisha, pasipo kupuuzia umuhimu wake wala kuikuza mali zaidi ya thamani yake. Hii yote ni kutahadharisha, mali isichukue nafasi ya nafsi ya mwanadamu na pia mali au mwenye mali wasigeuzwe miungu na kuanza kuabudiwa kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja Amri ya Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunayaangalia masomo ya dominika ya 18 ya mwaka C, masomo ambamo ndani yake tunaupokea mwaliko wa Kristo anayetuambia tujilinde na tujichunge dhidi ya kujilimbikizia mali kwa maana uzima wa mtu, uzima wetu haumo katika mali tunazomiliki. UFAFANUZI WA MASOMO: Kama kawaida ya kipindi hiki, tunaanza kwa kuyapitia na kuyatolea ufafanuzi masomo yote matatu ya dominika kabla ya kutoa tafakari fupi, tafakari ambayo kimsingi ina lengo tu la kuchokoza tafakari pana ambayo kila mmoja anaifanya kulingana na hali na mazingira aliyomo kutokana na masomo haya tunayoyapokea leo. Tunaanza na somo la kwanza. Somo hili linatoka katika kitabu cha Mhubiri (1:2, 2:21-23). Tunamsikia Mhubiri anasema “ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.” Ni kama mtu aliyekata tamaa ya chochote anachokifanya, ya kilicho mbele yake na ya maisha kwa ujumla. Kuelewa kile anachokimaanisha Mhubiri, tunapaswa kujua kuwa Mhubiri ni mojawapo ya vitabu katika Biblia, vitabu vinavyoitwa vitabu vya Hekima. Kwa ujumla, vitabu hivi vinatafuta kumpa mwanadamu ufunguo wa maisha kwa kupitia uzoefu au hekima.

Bila hehima ya Kimungu yote ni ubatili mtupu
Bila hehima ya Kimungu yote ni ubatili mtupu

Jambo moja kubwa ambalo vitabu hivi vinakuja kuonesha ni kuwa hekima hiyo, hekima ambayo inaweza kumsaidia na kumwongoza mwanadamu katika maisha yake ni ile ambayo chimbuko lake ni Mungu mwenyewe. Msisitizo unaotolewa daima ni kuwa kumcha Bwana ndio chanzo cha maarifa, kumcha Bwana ndio chanzo cha hekima. Sasa tukirudi katika somo la leo, maneno anayosema Mhubiri kuwa mambo yote ni ubatili, haya si maneno yake. Ni maneno anayoyachukua kutoka kwa wale wanaoifuata hekima bila hata chembe ya kumcha Bwana, yaani hekima isiyomtambua Mwenyezi Mungu. Anachokuja kukifundisha Mhubiri ni kuwa mwisho wa hekima ya namna hiyo ni kuona kila kitu hakina maana, kila kitu ni ubatili. Hekima hiyo ina hatari ya kuona kila kitu kuwa ni ubatili kwa sababu haiwezi kwenda mbele zaidi ya kile kinachoonekana. Hekima ya namna hiyo ipo na inaendela kusambaa hata nyakati zetu. Ndiyo hiyo inayotangaza daima kwamba huko mbeleni hali itazidi kuwa ngumu, ndiyo inayotangaza mwisho wa dunia, ndiyo ambayo haioni hata chembe ya matumaini katika nyakati ngumu za maisha na haiwezi kufanya hivyo kwa sababu haitambui kuwa ndani ya yale anayoyapitia mwanadamu ipo nguvu isiyoonekana ambayo ni nguvu ya Mungu.

Na hiki ndicho ambacho somo la pili linakuja kusisitiza. Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakolosai (Kol 3:1-5, 9-11) anasema “yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu”. Mtume Paulo anachokumbusha ni kuwa maisha ya mwanadamu yana wigo wa kibinadamu wa hapa duniani lakini pia yanao wigo ulio juu, wigo usio wa kibinadamu, wigo wa kimungu. Maisha yake kumbe hayategemei tu yale anayoyaona au anayoyapitia hapa chini bali yanategemea pia na yale yasiyoonekana, yale anayokusudia Mungu muumba wake na Muumba wa ulimwengu. Tuingie sasa kuliangalia somo la Injili (Lk 12:13-21). Ni somo ambalo kupitia mifano miwili inatupatia fundisho kuhusu mali na utajiri. Katika mfano wa kwanza, Yesu yupo anafundisha watu, ghafla anaibuka mtu mmoja katika hali isiyotarajiwa anamwomba Yesu awagawanyishe mali yeye na kaka yake. Hapo Yesu anatoa fundisho la kwanza kuhusu mali. Anasema “angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu alivyo navyo.” Hii choyo tunayosikia, katika lugha ya Kigiriki, lugha asili ya Maandiko kabla ya tafsiri linatumika neno pleoneksia linalomaanisha tamaa ya kujilimbikizia mali. Kumbe hapa Yesu anatutahadharisha dhidi ya hii tamaa, tamaa ya kujilimbikizia mali.

Mapaji na karama za Mungu zijenge mahusiano na mafungamano ya kijamii.
Mapaji na karama za Mungu zijenge mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Na tukiangalia vizuri Injili inatuonesha kuwa tamaa hii inamfanya mtu kutokuona wala kutokufikiri kitu kingine isipokuwa mali na namna ya kuiongeza. Anaifanya mali kuwa ndio uzima wenyewe. Tunaona umati wa watu unaketi kumsikiliza Yesu anayejipambanua kama mwalimu. Yule mwenye tamaa ya mali haoni kama umati unavyoona. Yesu yeye hayupo kusikiliza mafundisho bali ni kama yupo kutafuta fursa na fursa anayoiona ni kumtumia Yesu kama mwamuzi wa kumshawishi kaka yake amgawie urithi wao. Tamaa inapofusha. Katika mfano wa pili ambao Injili ya leo inatupatia kuhusu mali na utajiri, tunasikia mfano ambao Yesu mwenyewe anautoa. Ni mfano wa mtu tajiri aliyefanikiwa kupata mavuno mengi aliyoweka akiba, tajiri ambaye baada ya mafanikio yote hayo ambayo aliyapata kwa nguvu na bidii zake akaona amekwishafikia upeo wa maisha, akajiambia “nafsi yangu pumzika sasa, ule, unywe, ufurahi.” Katika mfano huu Yesu anatuonesha kuwa lengo la maisha ya mwanadamu sio hilo. Kupata mali au utajiri sio lengo bali ni njia au mojawapo ya namna ya kumuwezesha mtu kuishi vema mahusiano yake na Mungu na watu. Upeo wa maisha ya mwanadamu na hatima yake vinapatikana kwa Mungu tu. Yesu anafundisha anayehitaji kujitajirisha na ajitajirishe kwa Mungu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 18 ya mwaka C wa Kanisa yanatupa tafakari juu ya mojawapo ya vipengele nyeti katika maisha ya mwanadamu: kipengele kinachohusu mali. Kuhusu kipengele hiki ni kama mwanadamu daima anajikuta katikati ya misukumo miwili. Msukumo wa kwanza, tunaoweza kuuita wa dunia au jamii, ni ule unaomtaka ajitafutie mali kwa bidii na maarifa, wakati mwingine kwa haraka na kwa njia zote halali ili aishi vema na msukumo wa pili, ule wa Injili, ni ule unaoonekana kumuwekea breki au kumpunguzia spidi ili asiyafikie malengo hayo. Tangu mwanzo kabisa inabidi kuweka wazi kuwa Injili haifundishi kuwa mali kama mali ni dhambi. Mafundisho ya Injili yanalenga kumsaidia mwanadamu kuipa mali nafasi yake inayostahili katika maisha, pasipo kupuuzia umuhimu wake wala kuikuza mali zaidi ya thamani yake. Hii yote ni kutahadharisha,  mali isichukue nafasi ya nafsi ya mwanadamu na pia mali au mwenye mali wasigeuzwe miungu na kuanza kuabudiwa. Kupokea vizuri fundisho hili, ni muhimu tukarudi katika fundisho la amri ya kwanza ya Mungu.

Utu na heshima ya binadamu vinapata asili yake kwa Mungu.
Utu na heshima ya binadamu vinapata asili yake kwa Mungu.

Katika amri hiyo Mungu anasema “usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilichomajini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia.” Kwa bahati mbaya na kimakosa amri hii imechukuliwa daima kama ni amri inayokataza matumizi ya picha au sanamu katika nyumba za ibada. Undani wa amri hii unakataza kuunda hasa ndani ya fikra au moyo wa mwanadamu vile ambavyo mwanadamu ataelekeza maisha yake yote kwake na kumuweka Mungu pembeni. Vitu hivi kimsingi sio vibaya na sio dhambi. Vinageuka kuwa vibaya, na vinageuka kuwa dhambi pale ambapo anavipa nafasi ya kwanza katika maisha yake na kuiacha pembeni nafsi yake, ubinadamu wake na Mungu mwenyewe. Vinaweza kuwa ni madaraka, vinaweza kuwa ni mali, vinaweza kuwa ni chakula au vilevi, vinaweza kuwa ni umaarufu n.k na mtu yuko tayari kufanya chochote na kwa namna yoyote ile ili avipate na aendelee kuvipata. Hivyo ndivyo vinyago na ndizo sanamu ambazo Mungu hataki tuzichonge.

Hataki tuzichonge kwa sababu yeye amemuumba mwanadamu awe kiumbe huru, awe juu ya viumbe vyote na amtumikie Mungu pekee. Vinyago na sanamu hizi zinaondoa uhuru wa mwanadamu na zinamfanya mateka. Badala ya kuwa juu ya viumbe vyote, yeye ndio anakuwa chini na vile alivyovitengeneza mwenyewe vinakuwa juu. Matokeo yake si tu anamweka Mungu pembeni, bali anakuwa mpinzani wake.  Hekima ya Maandiko Matakatifu katika kitabu cha Mithali inasema ikimwambia Mungu “usinipe umaskini wala utajiri. Usinipe utajiri nikakusahau nikasema “Bwana ni nani”? Wala usinipe umasikini nikaiba na kulitaja bure jina la Mungu wangu.Unilishe chakula kilicho kadiri yangu (rej. Mith 30:7-9).  Tuupokee mwaliko wa Kristo, mwaliko wa kujilinda na kujichunga ili mali na harakati za kutafuta maisha mazuri zisiwe kwetu ibada kama ile ya sanamu, tukausahau ubinadamu wetu wala wa wenzetu; tukamsahau na Mwenyezi Mungu. Tuombe neema ya kutumia mali na nafasi zetu kwa ajili kuuinua ubinadamu na kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Liturujia D18
30 July 2022, 10:28