Mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini unapaswa kuwa ni utambulisho wa Mama Kanisa: Kristo Yesu anajifunua kwa waja wake kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Maskini. Mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini unapaswa kuwa ni utambulisho wa Mama Kanisa: Kristo Yesu anajifunua kwa waja wake kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Maskini. 

Tafakari Neno la Mungu Dominika XV: Huruma na Upendo Kwa Jirani

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia : upendo na huruma ya Mungu inayopenya katika moyo na akili ya binadamu. Huu ni mchakato wa kupyaisha juhudi za kichungaji, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni chemchemu ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 15 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii kupitia Musa, Paulo na Yesu yanatufundisha sheria ya kweli iletayo wokovu kwamba matendo ya huruma kwa jirani yakiongozwa na upendo ni utimilifu wa Sheria na Torati yote, ndiyo amri kuu ya mapendo njia ya wokovu wetu. Katika somo la kwanza la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kumb 30:10-14), Musa anatuambia kuwa kama tukizishika Amri na maagizo ya Mungu, hakika tunao wokovu. Si vigumu kuzishika Amri na sheria za Mungu maana hazitoki nje ya mtu, haziko mbali hata tuseme nani ataenda kutuletea, zi karibu tena zinatiririka kutoka ndani ya moyo wa mtu na wala si ngumu kuzifuata, jambo moja tu linahitajika nalo ni upendo kwa Mungu na jirani. Kumpenda Mungu maana yake ni kushika amri zake ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzifahamu na kuzitekeleza akitaka na kufanya maamuzi na kunuia kuzishika. Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 1:15-20); linatueleza kuwa Kristo yu tangu milele na katika Yeye vimeumbwa vyote. Tena Mungu anataka viumbe vyote vipate utimilifu na upatanisho katika Kristo peke yake. Somo hili lina historia yake. Kolosai ulikuwa mji uliostawi sana, wenye idadi kubwa ya Wakristo, na wengi wao waliongokea Ukristo kutoka Upagani. Wakolosai hawakuhubiriwa Injili na Paulo bali na Epaphras. Historia inasema kuwa Wakristo wa Kolosai waliogopa sana mizimu kwasababu kabla ya kuuongokea Ukristo waliamini juu ya nguvu ya mizimu. Hivyo baada ya kuongokea ukristo walikuwa na mawazo mkanganyiko kuhusu mizimu. Walishindwa kutofautisha kati ya roho walio wema na roho walio waovu, malaika na mashetani.

Ulimwengu unawahitaji wasamaria mwema, mashuhuda wa huruma ya Mungu
Ulimwengu unawahitaji wasamaria mwema, mashuhuda wa huruma ya Mungu

Wakiongozwa na baadhi ya walimu wa uongo na wazushi, walianza kutilia mashaka kama imani kwa Kristo, ilitosha kuwaokoa kutoka katika mashaka yao. Kadiri yao, mizimu nayo ilikuwa na nafasi kubwa katika wokovu wao, kwa hiyo walikuwa na imani nusunusu nyingine kwa Kristo na nyingine kwa miungu yao. Paulo akiwa gerezani Roma, Epapharas alimtumia habari za walimu hawa wa uongo na mafundisho yao kwa Wakristo wa Kolosai. Ndipo Paulo akawaandikia barua ili kusahihisha uzushi ule akifundisha kuwa; Kristo ni juu ya wote na yote. Ni juu ya watu wote na roho zote. Kila mtu na kila kitu kiko chini ya utawala wake kwa sababu katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana. Yeye ndiye anayeviwezesha kuwepo. Bila yeye ulimwengu wote hauwezi kuwapo. Tukumbuke kwamba, kila alichoumba Mungu, mwanadamu, malaika na viumbe vyote ni vyema. Roho chafu na ovu ni matokea ya uasi dhidi ya Mungu. Yesu alijimwilisha, akawa mwanadamu, ili atupatanishe na Baba kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kupatanishwa kwetu na Mungu ni kazi ya Kristo mwenyewe. Alifufuka kutoka wafu, na kwa sababu hiyo, yeye ni mzaliwa kwanza katika viumbe vyote, kati ya wengi waliokufa katika Bwana na wamekwisha kufufuka katika utukufu wa Mungu. Yesu ndiye mwanzo na mwisho wa maisha yetu. Yeye ni alpha na omega. Kumbe Paulo anatufundisha kuachana na malumbano kuhusu aina ya Roho, wema na waovu, kinachohitajika ni kuungana na Kristo, katika maisha ya Roho Mtakatifu. Tukiwa na Kristo hakuna roho mchafu atakayetugusa kama tumeunganika na Kristo.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 10:25-37), ni simulizi la shauku ya mwana-sheria kutaka kujua maoni ya Yesu, kuhusu utata wa wingi wa sheria zilizoongezwa na Walimu wa dini ya Kiyahudi kutoka Amri 10 za Mungu alizompatia Musa hadi kufikia sheria 613, huku wakisisitiza kuwa hakuna anayeweza kuokoka pasipo kuzishika Amri hizo. Mwalimu huyu anauliza maswali mawili. Swali la kwanza: “Mwalimu, nifanye nini, ili nipate kuurithi uzima wa milele? (Lk 10:25). Katika Injili ya Marko na Mathayo tunasoma: “Mwalimu katika Torati ni Amri ipi iliyo kuu?” (Mk 12:28, Mt 22:35). Yesu hatoi jibu la moja kwa moja bali anamwuliza huyu mwanasheria swali: “Imeandikwa nini katika Torati? Wasomaje? (Lk 10:26). Yeye akiwa ni mwalimu wa sheria ya Musa anajua wazi majibu ya swali lake. Ndiyo maana bila kusita anatoa jibu akinukuu Kumbukumbu la Torati na kitabu cha Walawi: “Mpende Bwana Mungu wako kwa Moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako” (Kumb 6:5, Wal 19:18). Kila Myahudi, hata mtoto mdogo angetoa jibu hili, kwani lilikuwa ni sehemu ya sala yao waliyojifunza tangu utotoni.

Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni utambulisho na vinasaba vya Kanisa
Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni utambulisho na vinasaba vya Kanisa

Likafuata swali la pili: “Na Jirani yangu ni nani? (Lk 10:29). Kwa maneno mengine; “Ni yupi ninayepaswa kumpenda na yupi ninapaswa kumchukia? Itakumbukwa kuwa Wayahudi wa wakati ule, walijua kwamba upendo ulikuwa ni kwa ajili ya Wayahudi tu. Watu wa mataifa mengine/wapagani, hawakustahili kupendwa. Upendo kwa jirani uliwahusu Wayahudi tu. Kwa hiyo mtu yeyote wa mataifa hakustahili mahusiano na Myahudi, na ikiwa mtu wa mataifa alimdhuru Myahudi, alistahili adhabu ya kifo. Yesu anasahihisha mtazamo huo kwa simulizi maarufu la Msamaria mwema akitufundisha kuwa kila aliyeumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu ni Jirani yetu, anastahili kupendwa, kuheshimiwa na kusaidiwa anapokuwa katika shida. Itakumbukwa kuwa Wayahudi na Wasamaria walikuwa na chuki ya mda. Kihistoria, Wasamaria walikuwa ni uzao mchanganyiko wa Wayahudi na Wapagani. Katika dini yao walikubali “Vitabu 5 tu vya Musa – Torati vingine vyote walivikataa. Hawakuruhusiwa kuabudu katika Hekalu la Yerusalemu hivyo walijenga Hekalu lao huko Gerizim. Katika hali hii Wayahudi waliwaona Wasamaria kama “Wazushi.” Kwa Myahudi kumwita Myahudi mwenzake “Msamaria” lilikuwa tusi kubwa sana ndiyo maana mara kadhaa, walimwita Yesu “Msamaria”: “Je, sisi hatusemi vema ya kwamba, wewe u- “Msamaria,” nawe una pepo?” (Yn. 8:48). Yesu alipoongea na mwanamke msamaria pale katika kisima cha Yakobo (Yn 4:1-19) mitume walimshangaa sana na hawakumuelewa.

Yesu akiwa na wanafunzi wake walikataliwa chakula na malazi katika vijiji vya Wasamaria. Hivyo kwa chuki ya kiyahudi kwa Wasamaria, Yohane na Yakobo walipoona hayo walimwambia Yesu: “Bwana wataka tuagize, moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize? (Lk 9:51-56). Naye Yesu akawakemea kuwa hawajui ni roho gani aliyonayo. Yesu ili kuwafundisha wayahudi ubaya wa chuki alimsifia mkoma msamaria aliyetakaswa na kurudi kutoa shukrani (Lk17:18) na katika mfano wa msamaria mwema aliyemhudumia kwa upendo Myahudi aliyekuwa katika hatari ya kufa. Katika mifano hii miwili anatufundisha kuwa upendo unapita sheria na uadui wote na kipimo chake ni matendo ya huruma. Katika simulizi la Msamaria mwema Yesu anasema: “Mtu mmoja alishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko…” Kutoka Yerusalemu mpaka Yeriko ni umbali wa kilomita 30. Njia hii ilikuwa ikijulikana kama “Njia ya Damu” kwa sababu watu wengi walimwaga damu yao katika njia ile kwa kuvamiwa na maharamia – Wanyang’anyi. Kumbe, mtu anayesimuliwa katika mfano huu alikuwa mhanga wa maharamia – wanyang’anyi. “Kwa nasibu, kuhani mmoja alishuka kwa njia ile, na alipomwona majeruhi yule alipita kando akaenda zake. Na Mlawi, vivyo hivyo.” Hawa wawili - Kuhani na Lawi, yawezakuwa walitoka kusali, na kutolea sadaka katika Hekalu la Yerusalemu ambapo walisoma pia sharia za Musa/Torati, lakini hawakuelewa kuwa matendo ya huruma ni utimilifu wa sheria na torati yote, yanapita sheria. Kutenda matendo ya huruma ni kwenda zaidi ya sheria. Mlawi na kuhani, walipomwona mtu aliyekuwa anajeruhiwa na kuachwa nusu mfu, kwa kufuata sheria walipita pembeni.

Kisheria hawakuwa na kosa lolote kwani walitimiza sheria ya kutojitia unajisi kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Walawi sura 21: “Kwa utaratibu wa kiibada kamwe kuhani asijitie unajisi kwa ajili ya kugusa maiti ya mtu wake ye yote, isipokuwa maiti ya jamaa yake wa karibu, kama vile mama yake au baba yake, mwanawe au binti yake, ndugu yake, au dada yake asiyeolewa ambaye anamtegemea kwa kuwa hana mume, kwa ajili ya hao aweza kugusa maiti na kujitia unajisi. Kamwe asijitie unajisi mwenyewe kutokana na wale watu ambao anahusiana nao kwa kuoana” (Wal. 21:1-4). Na Yesu kila mara aliwakumbusha kuwa: “Lakini nendeni mkajifunze: Nataka rehema, wala si sadaka, kwa maana sikuja kuwaita wenye haki ila wenye dhambi” (Mt 19:13). “Lakini kama mngalijua maana ya maneno haya: Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasiona hatia” (Mt 12:7). Nabii Hosea aliwafundisha; “Maana nataka fadhili wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa” (Hos 6:6). Simulizi linaendelea kusema; “Lakini Msamaria mmoja, katika kusafiri kwake, alipofika hapo, alipomwona, alimhurumia…” Akamfunga jeraha zake, baada ya kuzitia mafuta na divai, dawa bora aliyokuwa nayo kwa wakati ule.

Injili ya Msamaria Mwema itangazwe na kushuhudiwa kwa maskini na wahitaji zaidi
Injili ya Msamaria Mwema itangazwe na kushuhudiwa kwa maskini na wahitaji zaidi

Akampandisha juu ya mwanapunda wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Akamkabidhi mwenye nyumba ya wageni, amtunze mpaka atakaporudi. Akalipa gharama zote za kumtunza na kumuuguza. Itakumbukwa aliyekuwa ameangukia mikononi mwa wanyang’anyi ni Myahudi. Yesu anahitimisha mfano wake kwa kumwambia Mwalimu wa Sheria atoe hukumu ni nani aliyekuwa jirani wa yule majeruhi: “Waonaje, kati ya hao watatu, ni nani aliyekuwa jirani yake? Mwalimu wa Sheria hakuthubutu kutamka neno “Msamaria” akajibu: “Ni yule aliyemwonea huruma”. Yesu akimwambia; “Nenda nawe ukafanye vivyo hivyo” (Lk 10:37). Msamaria mwema kwa tendo lake la huruma, akisukumwa na upendo kwa Mungu na jirani anatimiza sheria kwa utimilifu wake na anapata dhawabu machoni pa Mungu. Kumbe gharama ya ufalme wa mbinguni ni ile ile kwa wote; “Upendo kwa Mungu na jirani” tena “upendo usio na ubaguzi”. Na kila mwanadamu, ni jirani yetu haijalishi ni rafiki au ni “Adui”. Na kumpenda jirani ni kuzishika sheria zote 613.

Tunaalikwa kuonesha matendo ya huruma, nayo ni saba ya kimwili na saba ya kiroho. Kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika nguo walio uchi, kuwatembelea wafungwa, kuwakaribisha wageni, kuwatembelea wagonjwa, kuwazika wafu, kuwafundisha wasio na ujuzi, kuwaonya wakosefu, kuwashauri walio mashakani, kuwafariji wenye huzuni, kuvumilia kwa saburi maovu tutendewayo, kuwasamehe waliotukosea, na kuwaombea wazima na wafu. Huenda tusikutane na mtu aliyevamiwa na wanyang’anyi katika maisha yetu, lakini kila siku tunakutana na watu waliojeruhiwa: Kihisia, kisaikolojia au kimahusiano. Hawa nao wanahitaji faraja na huruma yetu. Katika mazingira tunakoishi wapo maskini, wajane, yatima, watoto wa mitaani, makahaba, wagonjwa, wafungwa katika magereza ya roho na mwili, ni baadhi tu ya watu waliojeruhiwa. Tuwaendee hawa kama alivyofanya msamaria mwema nasi tukafanye vivyo hivyo. Huu ndio utume wetu sote na hii ndiyo tiketi ya kuurithi ufalme wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 15 Mwaka C
07 July 2022, 14:52