AMECEA:Yaliyojiri,umuhimu wa kujua asili ya AMECEA
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Katika Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki(AMECEA)uliofunguliwa Dominika tarehe 10 Julai, kwa misa Takatifu na ambao ulihitimishwa tarehe 18 Julai 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Laudato si” Utunzaji wa Mazingira Nyumba ya Wote”. Maaskofu ambao waliunganika kwa pamoja na wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, Tanzania walirudi kutazama nyuma jitihada zao zilizowaleta pamoja maaskofu wote wa Tanganyika ya wakati huo mnamo 1960 na kushuhudia kuzaliwa kwa Jumuiya ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katika Afrika Mashariki (AMECEA). Shirikisho hilo limetimiza miaka 61 tangu mkutano wa kwanza ulipofanyika mnamo tarehe 17 Julai 1961 nchini Tanzania, ambapo maaskofu wa AMECEA walitafakari njia ya kuweza kuthamini uwepo wa shirikisho hilo huku mada ya kwanza ikiwa juu ya “Mustakabali wa Kanisa Barani Afrika”. Mtaguso wa II wa Vatican ambao ulifanyikia katika Taasisi ya Mtakatifu Anselmo Roma mnamo Novemba 1964 ulitoa fursa nyingine tena kwa Maaskofu kujadili kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa II kuhusu masuala ya eneo lililo mbali na ardhi ya AMECEA.
Mkutano wa III uliofanyika Roma-Italia ulitoa jukwaa la kujadili Katiba ya Kwanza ya Jumuiya ya Kikanda (iliyopitishwa), mabadiliko ya jina kutoka ITEBEA (Baraza la Maaskofu wa Kikanda wa Afrika Mashariki) hadi AMECEA, wakimkaribisha Askofu Vincent McCauley kama Mwenyekiti wa Kwanza wa AMECEA. Mikutano mikuu iliendelea kufanyika wakichagua nchi baada ya nchi kufanya mkutano wao. Na ndiyo maana inakumbusha msema usemao: “Watu wasiojua historia, asili na utamaduni wao wa zamani ni kama miti isiyo na mizizi”. Ndivyo alielezea historia ya kuundwa kwa AMECEA, Askofu Method Kilaini, ambaye ni Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania. Na alielezea kwa shauku kubwa japokuwa hapakuwa na nafasi ya kutosha kuelezea yote, lakini wakati anawapisha wajumbe wengine, alionesha furaha kubwa ya kuonesha chimbuko na mafanikio ya kuzaliwa kwa shirikisho hilo hasa kwa malengo ya kichungaji na masuala ya pamoja katika shirikisho zima. Askofu Kilaini aliweza kuzungumzia kidogo kuhusu mada ya mazingira kwa ajili ya Maendeleo fungamani ya Binadamu akiwa na tumaini kwamba hiyo ni mada mojawapo ambayo itaweza kuleta mafanikio kwa vizazi vya sasa na zaidi vijavyo.
Padre Small: Utume wa Uwekezaji kusaidia utume wa Kanisa kwa shughuli za kuzalisha
Wawakilishi wa Taasisi mbali mbali nao walipewa fursa ya kutoa ujumbe wao kwenye Mkutano Mkuu wa AMECEA, ambapo Bwana Patrick Mujuni ambaye ni “Meneja wa utume wa Uwekezaji nchini Tanzania kwa niaba ya Padre Andrew Small, ambaye ni Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Uwekezaji (OMI), alisema: “Fedha zilizoko kwenye akaunti za uwekezaji za Kanisa zinatakiwa kutumika kwa ajili ya manufaa ya watu”. Ujumbe wake alisema “Ziwe fedha za Roma au Ujerumani au Marekani au hata Afrika, rasilimali ambazo zilikusudiwa maskini na waliotengwa lazima zitumike kwa ajili ya madhumuni hayo sasa. Ujumbe huo wa Padre Small ulieleza zaidi kwamba Utume wa Uwekezaji (Missio Invest) husaidia utume wa Kanisa kuhamasisha shughuli yoyote ya kuzalisha mapato kwa kutoa ujuzi na rasilimali za kifedha zinazohitajika.
Shirika la Utume wa Uwekezaji, (Missio Invest) lilianzishwa kwa ajili ya kutoa utaratibu wa ufadhili endelevu kwa majimbo chini ya mamlaka ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, liliozinduliwa katika mkutano wa AMECEA nchini Malawi mnamo mwaka 2014 na sasa inafanya kazi katika nchi 10 ambapo zaidi ya dola milioni 10 zimewekezwa katika zaidi ya mabilioni 50. Asilimia 50 ya mikopo hiyo ni katika mipango ya kilimo endelevu lakini pia imeanza kukopesha shule na hospitali zikiwemo taasisi za fedha. Hadi sasa imerekodi kiwango cha ulipaji cha asilimia 99%. Katika hotuba iliyosomwa na Bwana Mujuni, Padre Small alibainisha kwamba haihamishiki rasilimali kutoka Kaskazini hadi Kusini tu kama mashirika mengine ya misaada, lakini kwamba, dhana kuu ya Utume wa Uwekezaji (Missio Invest) ni kuhamisha hatari ambazo watu hubeba na kuwashirikisha watu wengine katika mikoa mingine. “Kipimo cha kimaadili cha juhudi zozote za pamoja ni uwezo wa kila mshiriki kubeba kile anachoweza kustahimili.
Kwa kufafanua zaidi alisema kwa muda mrefu sana, Kanisa Barani Afrika limeombwa kutimiza utume bila fedha zinazohitajika huku likibeba hatari zote zinazohusika katika miradi yenye maendeleo makubwa,”. Padre Small alisema kuwa maendeleo yamezalisha dhuluma kwa kizazi na hivyo inahitaji kurekebishwa. Hii ni dhuluma ya kizazi ambayo inahitaji kusahihishwa na Utume wa Uwekezaji (Missio Invest) inayowakilisha njia mpya kabisa ya kufikiria mahusiano yetu ili yawe na msingi wa roho ya kuheshimiana kati ya watu”, aliwaambia Maaskofu. Kwa kusisitiza zaidi alisema, Kanisa limeitwa kuwa mwanga katika mwanga wa uwepo wa Mungu unaookoa, na hata hivyo, haliwezi kufanya lolote ikiwa hakuna watumishi wa kidini, hakuna miundo, hakuna waseminari au wanovisi, hakuna shule au zahanati au vituo vya kutwa. “Matumaini na matamanio ya Mungu kwa ajili yetu na mipango yake ya wokovu hatimaye itakatishwa tamaa na kubatilika ikiwa hakuna Kanisa. Hilo ndilo lengo ambalo Utume wa Uwekezaji (Missio Invest) una malengo ya kufikia”.
Profesa Pius Yanda:Kanisa ina wajibu wa kupambana na uharibifu wa mazingira
Profesa Pius Yanda wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Tanzania wakati wa kutoa ujumbe wake wa Mshikamano kwa wawakilishili wote wa Mkutano wa AMECEA alibainisha kuwa Kanisa lina mchango mkubwa katika kupambana na uharibifu wa mazingira ili kunusuru sayari na hapo ndipo wanatakiwa kujihusisha katika mijadala ya namna bora zaidi inaweza kuingia na kuwa sehemu ya suluhisho. “Lazima tusimamie mazingira si kwa manufaa yetu wenyewe bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Tukishindwa kutunza mazingira tunamoishi, tutapata taabu. Tabia za binadamu zinahusika na uharibifu wa mazingira unaochochewa na faida ya kiuchumi na mali, na hatua za Kanisa zinahitajika ili kuokoa sayari hii” alisisitiza Profesa Yanda.
Akizungumzia umuhimu wa mfumo wa ikolojia, Profesa Yanda alisema kwamba viumbe vyote vilivyo hai ni muhimu kwa ajili ya maisha ya binadamu na ubora wa maisha kwa wote, kwa kuwa vina mchango mkubwa katika kutoa chakula, nishati, dawa na vifaa mbalimbali muhimu kwa ajili ya afya ya binadamu, ustawi na kudumisha asili. Zaidi ya watu bilioni 2 wanategemea kuni ili kukidhi mahitaji yao ya msingi ya nishati; hii ni wazi hasa kwa kurejea maeneo ya vijijini ambako hawana umeme, hivyo wanategemea sana maumbile. Profesa aliendelea kusema kwamba takriban watu bilioni 4 wanategemea hasa dawa asilia kwa ajili ya huduma zao za afya na hii pia ni ukweli. Pamoja na kwamba serikali zinafanya juhudi kubwa katika kutoa huduma za kisasa za matibabu, wengi bado wanategemea sana dawa za asilia. Profesa Yanda Katika hotuba yake, Profesa huyo aliwaomba nchi za Afrika kujiandaa na mahitaji madogo ya maliasili kadri idadi ya watu inavyoongezeka kwamba: “tunapaswa kujiandaa katika kuunda mfumo wa usimamizi ambao unaweza kukabiliana na uharibifu unaotarajiwa wa maliasili na mfumo wa Ikolojia kwa ujumla”, alisisistiza Profesa Yanda.
Ikumbukwe: Mkutano Mkuu wa AMECEA kwa kawaida hufanyika kila baada ya miaka minne. Kwa maana hiyo viongozi hao walihitimisha kwa kuchagua mada na nchi mwenyeji kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa 21 ujao utakaofanyika mnamo 2026 jijini Kampala Uganda.