Tafuta

Fumbo la mateso na kifo linapata mwanga wake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; alfa na omega; mwanzo na mwisho. Fumbo la mateso na kifo linapata mwanga wake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; alfa na omega; mwanzo na mwisho. 

Hayati Padre Laurenti C. Magesa: Tafakari Kuhusu Fumbo la Kifo!

Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Fumbo la Kifo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo.

Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Mateso na kifo vinapata maana yake katika Fumbo la Pasaka.
Mateso na kifo vinapata maana yake katika Fumbo la Pasaka.

Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.

Baba Mtakatifu anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duniani Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!

Padre Magesa anakumbukwa na wengi kwa utume wake miongoni mwa vijana
Padre Magesa anakumbukwa na wengi kwa utume wake miongoni mwa vijana

Padre Laurenti Magesa Cornelli alizaliwa Agosti 10, mwaka 1946, Mwiringi Mugango Wilaya Musoma, Mkoa wa Mara; akiwa ni mzaliwa wa 9 kati ya wazaliwa 11 wa Mzee Cornelli Magoti Mujora na Mama Odiria Nyakwesi Chuma. Laurenti alipata Sakramenti za kukamilishwa kuingizwa katika Ukristo yaani: Ubatizo, Kipaimara na Komunio Takatifu katika Parokia ya Nyegina, Jimbo Katoliki la Musoma. Laurenti alipata Elimu ya Msingi katika shule ya Msingi Mabui Merafuru mnamo Mwaka 1954 hadi 1957, baadaye alijiunga na Seminari ndogo ya Mtakatifu Pio wa X Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma kuanzia mwaka 1958 hadi 1961. Kwa elimu ya Sekondari alijiunga na Seminari ndogo ya Bikira Maria, Nyegezi Jimbo kuu la Mwanza mwaka 1962 hadi 1968. Baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari, Laurenti alijisikia kuitwa kumtumikia Mungu mintarafu Daraja Takatifu ya Upadre wa Jimbo na hivyo kuamua kutuma maombi ya kujiunga na malezi na majiundo ya Kipadre. Laurenti alikubaliwa kujiunga na kuanza safari yake hiyo.  Na mara baada ya kukubaliwa alitumwa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua, Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba kwa masomo ya Falsafa kuanzia mwaka 1969 na kuhitimu mwaka 1970.

Mnamo mwaka 1971, Frt. Laurenti alitumwa tena Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Jimbo Kuu la Tabora kwa masomo ya Taalimungu hadi mwaka 1974. Mwaka 1973 alipewa daraja ya Ushemasi, na hatimaye akapewa daraja ya Upadre Juni 21, mwaka 1974 na Askofu John Rudin, M.M. kwenye viwanja wa Shule ya Msingi Mwembeni, Musoma mjini. Mara baada ya kupadrishwa Padre Laurenti Magesa alianza utume wake Parokiani Nyarombo kunako mwaka 1974. Amehudumu pia katika Parokia na Taasisi zifuatazo: Musoma mjini na kupata mafanikio makubwa katika utume kwa vijana ambao wengi wao wamekuwa ni Mapadre na watawa ndani na nje ya Tanzania. Makoko Center, Iramba, Masonga, Sirari, Ingri, Mwisenge, Bukama na Baraki Sisters Farm. Baada ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, Padre Laurenti Magesa alijiendeleza kielimu kwa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paulo, Canada mwaka 1977 hadi 1978, na baadaye shahada ya uzamivu mwaka 1982 hadi 1985 katika chuo kikuu hicho hicho cha Mtakatifu Paulo, Ottawa, nchini Canada. Padre Laurenti amefundisha katika Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora, Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA, Nairobi nchini Kenya, Maryknoll Institute of African Studies - Nairobi, Maryknoll School of Theology – Newyork Marekani, Catholic University of Nijmegen – Uholanzi, Chuo cha Hekima na Tangaza nchini Kenya. Pia amekuwa ni mwana taalimungu nguli wa Taalimungu ya Kiafrika na ameandika vitabu vingi na kutoa semina katika maeneo mengi duniani.

Ugonjwa wa Saratani ya Kongosho tangu Septemba, 2021 ukawa Msalaba wake.
Ugonjwa wa Saratani ya Kongosho tangu Septemba, 2021 ukawa Msalaba wake.

Padre Laurenti Magesa alianza kuugua Saratani ya Kongosho mwezi Septemba 2021, na alianza matibabu katika Hospitali ya Agakhan jijini Dar-es-salaam, matibabu aliyoendelea nayo hadi umauti ulipomfika tarehe 11 Agosti 2022; akiwa na umri wa miaka 76 na siku moja. Tunatoa shukrani za dhati kwa wote waliokuwa na mchango katika maisha ya Padre. Laurenti Magesa toka kuzaliwa kwake, malezi yake yaani wazazi, ndugu jamaa na marafiki.  Vile vile tunamshukuru sana Baba Askofu Michael Msonganzila kwa upendo wake wa kibaba kwa Padre Magesa na hasa kwa namna ya pekee kabisa ukaribu na uwepo wake wakati wa ugonjwa wake. Pia tunawashukuru mapadre wote waliohudumu naye katika urika na hata kumsaidia katika mazingira mbalimbali. Aidha kwa namna ya pekee sana tunatambua mchango mkubwa wa madaktari, wauguzi wa Hospitali ya Agakhan Dar es salaam na wote wenye mapenzi mema waliojitahidi kunusuru maisha ya Padre Laurenti Magesa. Tunanatoa pia shukrani nyingi kwa kila mmoja aliyeko hapa na hata asiye hapa kwa jinsi mlivyokuwa pamoja nasi katika kipindi hiki cha majonzi. Michango yenu ya hali na mali imekuwa ni faraja kubwa kwetu. Tunakushuruni sana nyote, Mungu awabariki. Hakika tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi Padre Laurenti Magesa Cornelli kwa mengi sana hasa kwa mchango wake mkubwa katika uchungaji na tasnia ya elimu kwa ujumla. Tuzidi kumwombea sana ili Mungu Mwenyezi hakimu mwenye huruma amsamehe mapungufu yake ya kibinadamu na hatimaye ampokee kwake mbinguni.

Padre Magesa
17 August 2022, 16:12