Kardinali Polycarp Pengo amewaasa watu wa Mungu Jimboni Singida kuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu kwani ni mema mengi aliwaotendea kwa kipindi cha miaka hii 50. Kardinali Polycarp Pengo amewaasa watu wa Mungu Jimboni Singida kuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu kwani ni mema mengi aliwaotendea kwa kipindi cha miaka hii 50.  

Jubilei ya Miaka 50 Jimbo Katoliki Singida: Kilele: Imani na Matumaini

Jubilei ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida: Lilianzishwa tarehe 25 Machi 1972 likiwa na Mapadre 15 wanajimbo wakiwa 4, Parokia 9, vigango 209, Makatekista 210, Mashirika ya kitawa na waamini 41,700 lina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu leo hii linapotimiza miaka 50 likiwa na Mapadre 74 Parokia 30 na Mashirika ya kitawa 30. Ni muda wa imani na matumaini.

Na Padre Deogratias Makuri, - Singida, Tanzania.

Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amewaasa watu wa Mungu Jimboni Singida kuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu kwani ni mema mengi aliwaotendea kwa miaka hii 50. Ameyasema hayo wakati wa mahuburi ya Misa Takatifu ya kilele cha Jubilei ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwa jimbo hilo, Dominika tarehe 21 Agosti 2022 kwenye Viwanja vya Kumbukumbu ya Askofu Mabula. "Tunashuhudia Jimbo la Singida likiwa ni miongoni mwa majimbo yanayostawi kwa kasi hapa nchini Tanzania. Ni Jimbo ambalo lipo katika hatua ya juu kabisa.  Tunaona tayari jimbo linajua miaka 50 ijayo litafanya nini na kwa kutazama idadi ya mapadre wanajimbo na wamisionari ambayo inatia moyo sana. Tuzidi kumwomba Mwenyez Mungu azidi kuwapa nguvu zaidi ya kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu wake." aliongeza Kardinali Pengo. "Jitahidini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa nguvu na vipaji vyenu. Mnaposherehekea Jubilei hii iwe ni chachu ya kuona uhitaji wa wenye shida kiroho na kimwili. Kanisa linapata nguvu pale linapoakisi kazi za Kristo. Mjawe upendo na kutenda haki ili Kristo Yesu azidi kutamalaki miongoni mwenu." aliasa Kardinali Pengo. Naye Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida akitoa neno la shukrani, " namshukuru Mungu kwa mema aliyonitendea na kulitendea Jimbo letu ninapoadhimisha miaka 25 ya Upadre tangu nimekuwa Padre na miaka 50 tangu kuundwa kwa Jimbo langu la Singida. Tunazidi kumwomba Mwenyezi Mungu ili kazi ya Mungu izidi kuonekana miongoni mwetu sote wanasingida kila mtu kwa nafasi yake."

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 Jimbo Katoliki Singida
Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 Jimbo Katoliki Singida

Jubilei Singida Umoja na Mapendo. Ni kauli mbiu ambayo kwa muda ya miaka mitatu imekuwa ikirindima ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Singida kama kauli mbiu ya kuchagisha maandalizi ya kiroho na kimwili katika maadhimisho ya kumshukuru, kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu kwa Jimbo hili la Singida kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Jimbo la Singida lililoanzishwa tarehe 25 Machi 1972 likiwa na Mapadre 15 wanajimbo wakiwa wanne, Parokia 9, vigango 209, Makatekista 210, Mashirika ya kitawa na waamini 41,700 lina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu leo hii linapotimiza miaka 50 likiwa na Mapadre 74 Parokia 30 na Mashirika ya kitawa 30. Hivyo mwaliko uliokuwa unavuma kotekote wa UMOJA na MAPENDO huku wakiwa na matumaini kwa Kristo Yesu na kuyakubali Mapenzi ya Mungu yatimizwe miongoni mwao ndio chanzo cha mafanikio haya makubwa ambayo leo wanasheherekea. Kifupi ni kuwa hizo kauli mbiu ambazo zinapatikana katika nembo zote tatu za awamu tatu za Maaskofu walioongoza Jimbo hili zimekuwa ni chachu ya maendeleo na mchakato ambao matunda yake wanasema mwenye macho haambiwi tazama. Baba Askofu Bernard Mabula ambaye aliongoza Jimbo la Singida kuanzia mwaka 1972 hadi 1999 nembo yake ilibeba maneno "Kristo Matumaini Yangu" alijikita katika kujenga matumaini kwa Kristo Yesu katika kuchochea mafanikio ya Jimbo kiroho na kimwili.  Alijenga msingi imara ambao alama zake zinaoneka vyema sasa hivi. Kipindi chake kilikuwa kigumu wakati huo kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na rasilimali watu, fedha na vitu katika ulimwengu wa nyakati hizo.

Awamu ya pili ambayo ilikuwa na nembo Mapenzi ya Mungu yatimizwe ilikuwa chini ya Baba Askofu Desiderius Rwoma ilijikita katika kuimarisha mafanikio yaliyokuwepo kichungaji na kiuchumi. Mpaka awamu hii inaisha mwaka 2013 jimbo lilikuwa na mafanikio makubwa na mazuri kiroho na kimwili. Awamu ya tatu ambayo ndio hii ya Askofu Edward Mapunda inaongozwa na kauli mbiu ya UMOJA NA MAPENDO. Jimbo linaposherekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kuna mengi ambayo wanajimbo wanaamini bila Mungu yasingetendeka. Leo wanasingida wanapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo wanayofuraha kuonesha kukua kwa jimbo kiimani, kwa idadi ya waamini, mawakala wa uinjilishaji, taasisi na miundombinu. Kwa sasa jimbo lina waamini 196,797, Parokia 30, parokia teule 6, Vigango 361, Mapadre 108, (kati yao 76 wanajimbo akiwemo Askofu Edward Mapunda, 32 wa Mashirika). Kuna Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume 32; Waseminari wakuu 56, nyumba 6 za malezi ya kitawa, seminari ndogo tatu zenye waseminari wadogo 494 na Makatekista 583. Kwa Upande wa Huduma za jamii zipo Hospitali 4, Vituo vya afya 3, Zahanati 9, Sekondari 7, Shule za Msingi 12, Vyuo vya ufundi 3, Chuo cha Ualimu 1, Chuo cha Afya 1, Chuo cha Makatekista 1; Kituo cha Kichungaji 1, Vituo vya walemavu na wazee 3, Watoto Yatima 1 na shule za chekechea 30 na vyama vya kitume na Jumuiya ndogondogo za Kikiristo zimeongezeka na kuimarika maradufu kwa hapa ni mahali pa kujichotea amana na utajiri wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Sala na huduma ya upendo kwa jirani kama kielelezo cha imani tendaji.

Umoja na Mshikamano wa watu wa Mungu Jimboni Singida
Umoja na Mshikamano wa watu wa Mungu Jimboni Singida

Maadhimisho haya ya dhahabu ya Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo la Singida yanaenda sambamba na maadhimisho ya Jubilei ya fedha ya Mhashamu Edward Mapunda Askofu wa Jimbo la Singida kwani alipadrishwa tarehe 23.11.1997 na Mhashamu Askofu Bernard Mabula. Padre Edward Mapunda alifanya uchungaji katika nafasi mbalimbali hadi tarehe 5 Julai 2015 alipowekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida. Pamoja naye waliokuwepo wapadrishwa wenzake watano ambao ni Mapadre: Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania, Gabriel Choda, Titus Kachinda, Karoli Kidamui na Conrad Munna. Kwa mara ya kwanza hii ilikuwa ni idadi kubwa ya Mashemasi kupadrishwa jimboni Singida. Pia walipadirishwa mapadre watatu wanasingida wa mashirika mwaka huo kwa tarehe tofauti hao ni Chesco Msaga, C.PP.S., Kaimu Katibu mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC Gregory Mkhotya, C.PP.S., na Damasi Missanga, SJ., Tunawapongeza Wajubilanti hawa pamoja na wenzao waliohudhuria toka majimbo na mashirika mbalimbali ya kitawa na kazi za kitume.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameziomba taasisi za dini nchini Tanzania kuendelea kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuiongoza nchi vizuri na kutimiza dira yake ya uwekezaji katika sekta ya uzalishaji, kutengeneza ajira, kukuza uchumi na kujenga Tanzania yenye umoja, upendo na mshikamano. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa rai hiyo mkoani Singida aliposhiriki katika Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida na Miaka 25 tangu Askofu Mapunda alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na kusema Rais Samia ana dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo ni vema kumuombea ili yale aliyodhamiria kwa ajili ya nchi yaweze kutimia. Aidha amesema kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya jamii katika sekta mbalimbali za maendeleo zikiwemo za afya, maji na elimu hususani maeneo ya pembezoni. Wakati wanasingida wanampongeza Askofu wao kwa utume uliotukuka, wakati huo huo wanamshukuru sana Mwenyezi Mungu kuwapatia Askofu huyu ambaye kwao ni zawadi kubwa isiyomithilika. Askofu Mapunda, mara zote yuko mbele yao kuonesha njia.  " ... upo katikati yetu kama baba na kututia nguvu, uko nyuma yetu kuhakikisha hapotei hata mmoja na upo juu yetu kama rejea-Kuhani Mkuu.  Umeendelea kujenga Umoja na Mapendo ya jimbo kama chachu ya ushuhuda wa Kiinjili. Hongera Baba yetu.

Jubilei Singida imevuta watu wengi kutoka ndani na nje ya Jimbo la Singida
Jubilei Singida imevuta watu wengi kutoka ndani na nje ya Jimbo la Singida

Baba Mapunda, Jubilee Singida! Pamoja nawe tunaendelea kumshukuru Mungu kwa mema mengi aliyotujalia wanasingida." Alisema Padre Francis Lyimu ambaye ni Wakili wa Askofu wa Jimbo la Singida akiwakaribisha wageni kwa adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei. "... Kwa namna ya pekee tunawashukuru sana majirani zetu, kwa ukarimu na upendo wao kwa kudumisha historia hii muhimu ya Uinjilishaji wa kina ndugu zetu wanajimbo Kuu la Tabora, jimbo kuu la Dodoma, jimbo la Kondoa na kwa namna ya pekee wajukuu wetu wote wa Jimbo Katoliki la Mbulu ambao leo wamefika kwa wingi sana kutoa shikamoo.  Tunayofuraha kwa namna ya pekee kuishukuru serikali na vyombo vyake katika ngazi zote kwa kuwa mwezeshaji na mbia muhimu katika utume wa Jimbo letu kwa maendeleo mfungamano ya mkoa wetu na watu wake. Uwepo wenu hapa leo ni ishara wazi ya ushirikiano mzuri kati yetu.  Ni sala yetu mahusiano haya mema yaendelee. Aidha tunawashukuru viongozi na waamini wa dini na madhehebu mbalimbali mkoani kwetu kwa ushirikiano mzuri na wa muda mrefu. Tunazishukuru asasi mbalimbali za umma na binafsi kwa mahusiano wezeshi ya maendeleo ya watu wetu. Tunawashukuru wahisani wetu wote wa nje na ndani hawa ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Jimbo letu. 

Padre Liyimu alisema, "Tunawashukuru wale wote waliowezesha sherehe hii kwa michango yao mingi na mikubwa. Mungu awazidishie zaidi kwa ukarimu wenu. Miaka hamsini imetimia na sasa tunaangalia mbele kwa matumaini makubwa ya kiwajibu yaani uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini na sababu ya utume wa Jimbo Katoliki la Singida. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria Mama wa Kanisa mtuombee ili kanisa jimboni Singida liendelee kuwa wakala muhimu wa Injili hadi ukamilifu wa dahari." alimalizia Padre. Lyimu. Maadhimisho hayo ya Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo la Singida yamehudhuriwa na Maaskofu 33, Abate, Mkuu wa majeshi mstahafu Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Mapadre 507 kutoka ndani na nje ya jimbo, masista 812, Mheshimiwa Mwigulu Lameki Nchemba Waziri wa Fedha na Mipango, Mkuu wa mkoa wa Singida ndugu Peter Serukamba, Mawakili na Wawakilishi wa Maaskofu, Wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume.  Waheshimiwa Wakuu wa wilaya, Waheshimiwa Wabunge na wawakilishi wa wananchi katika ngazi mbalimbali, viongozi wa serikali, viongozi wa vyama vya siasa na taasisi za umma, viongozi wa dini na madhehebu ya dini, mafrateli na waamini maelefu kutoka ndani na nje ya nchi. Tunawatakia wanasingida wote na mapadre wajubilei wote maadhimisho mema na mafanikio mema katika kugeukia ungwe nyingine ya utume baada ya Jubilei.

Jubilei Singida

 

23 August 2022, 16:12