Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Jimbo Katoliki Shinyanga! 11 Septemba 2022 Ni Kwa Mkapa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania. Jumuiya hii ilianzishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kunako mwaka 1972 kwa lengo la kuwasaidia wanawake kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! WAWATA Jimbo Katoliki la Shinyanga, hivi karibuni imefunga rasmi maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA ngazi ya Jimbo katika ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Liberatus Sangu na mahubiri kutolewa na Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha kwenye Kanisa kuu la Ngokolo, Jimbo Katoliki la Shinyanga. Ibada ya Misa Takatifu ilitanguliwa na maandamano makubwa ya WAWATA Shinyanga kama alama ya kumshukuru Mungu kwa uwepo na ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji” na kilele chake ni tarehe 11 Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin William Mkapa, Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. Msisitizo ni kwamba, hii ni Siku ya Wanawake Wakatoliki Tanzania na wala si siku ya…! Wasije wakafanya vitu vyao! Askofu Liberatus Sangu amewakumbusha watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Shinyanga kwamba, ustawi na maendeleo ya Shinyanga vitaletwa na watu wa Shinyanga wenyewe. Kumbe ni wajibu wao kujifunga kibwebwe kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Na kuendelea kujikita katika ushirika na mafungamano ya kijamii; kwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu Liberatus Sangu amewapongeza WAWATA kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya kulitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali, lakini zaidi kwa kukazia umoja, ushiriki na utume wao kwa Kanisa. Amempongeza pia Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha kuwa ni kati ya viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na jukumu la kuasisi uanzishwaji wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ambayo kwa mwaka 2022 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania, UWT, ndugu Gaudentia Mugosi Kabaka, kwa niaba Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewapongeza WAWATA katika maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1972. Amewataka WAWATA kuendelea kujielekeza zaidi katika kutoa elimu kwa jamii, ili kuenzi na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mafungamano ya kijamii kwa kuachana na vitendo viovu! Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa WAWATA kama chama cha kitume kinachopata msingi na chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na hivyo wanashiriki katika kazi ya uumbaji, ukombozi na uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. WAWATA watambue kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukabidhiwa dhamana ya kushiriki katika kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto wao. WAWATA ni wazazi, walezi na walimu: sifa kuu zinazowatambulisha katika familia ya watu wa Mungu, kumbe wanapaswa kujitambua na kuheshimu wajibu huku wakiendelea kuwajibika na kutumikia. Washirikiane na waamini wengine kama vile watawa wa kike, ambao kimsingi ni sehemu ya WAWATA. Dhana hii imechukua muda mrefu kuweza kukita mizizi yake miongoni mwa Watawa wa kike nchini Tanzania anasema, Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu. Kwa pamoja wanapaswa kusimama kidete na hivyo kushiriki katika utume wao kwa kutambua kwamba, wanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume.
Amewataka WAWATA chipukizi, wahamasishwe, ili kusaidia kuwaanda WAWATA wa leo na kesho sanjari na kuwasaidia wasichana wa Kikatoliki kujitambua na kujiheshimu kwani hii, ni sehemu ya utekelezaji wa unabii wao kwa kusoma alama za nyakati kwa kusimama dede kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. WAWATA wasimame kidete kuinua na kuupyaisha utu wa binadamu na kuendelea kujikita katika upatanisho, kwa kutambua ubaya wa maneno. Katika utekelezaji wa dhamana na wito wao wa kuongoza, daima Bikira Maria awe ni mfano wao, ili kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; upendo na mshikamano wa dhati. WAWATA Wajitahidi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani. Kazi ya uumbaji inapata utimilifu wake katika Kristo Yesu mkombozi wa dunia, aliyesadaka maisha yake kwa mateso, kifo na ufufuko.
Bikira Maria chini ya Msalaba akawa ni WAWATA wa kwanza, kazi ambayo iliendelezwa na Mitume wote baada ya Sherehe ya Pentekoste ile ya kwanza. WAWATA waendelee kutumainia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, aliyejaa neema na baraka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani, huku wakiendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa upande wake, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa amewataka WAWATA kuhakikisha kwamba nuru yao inaangaza, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa: kwa moyo wa huruma na upendo; kwa kurithisha fadhila za Kimungu, yaani: imani, matumaini na mapendo katika familia zao na jamii katika ujumla wake. Wawe wanyenyekevu na watiifu kwa Mungu na Kanisa. Wawe walinzi na warithishaji wa kanuni maadili na utu wema. Watambue na kuheshimu dhamana na nafasi ya Baba wa familia. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; wawe ni madaraja yanayowaunganisha watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. WAWATA wawe walinzi wa kwanza wa watoto wao, kutokana na changamoto nyingi zinazoibuliwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, ili kujenga na kudumisha upendo, mshikamano na uadilifu wa uumbaji.