Kanisa la Afrika Kusini kuendeleza mpango wa kuponyesha majereha kiroho na kimwili
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti, Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Afrika Kusini (SACBC) na Taasisi ya Uponyaji wa Kumbukumbu waliandaa warsha ya uponyaji wa kumbukumbu kwa mapadre katika Jimbo Kuu la Bloemfontein. Katika warsha hiyo, Askofu Mkuu Zolile Mpambani aliwakumbusha washiriki hao umuhimu wa kupokea uponyaji wa Mungu katika maisha yao ili wao wenyewe wawe waganga waliojeruhiwa. Askofu Mkuu alisisitiza kwamba “uponyaji wa maisha yetu ya nyuma yenye kuumiza ni safari ambayo tunafanya kupitia neema ya Kristo na warsha ya uponyaji wa kumbukumbu ambayo inapaswa kutumika kama moja ya hatua katika safari hiyo”. Aliwahimiza washiriki kufanya kazi kwa pamoja ili kutambua hatua za ziada baada ya warsha ambayo uponyaji wa mtu binafsi na wa pamoja unaweza kuendelea kufanyika.
Kuhama kutoka kuwa mwathirika na kuwa mshindi
Warsha hiyo iliendeshwa na Padre Michael Lapsley, Mchungaji wa Kianglikani na mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi ambaye mwaka 1990 alipoteza mikono miwili na jicho katika shambulio la bomu iliyokuwa kwenye barua lililofadhiliwa na Huduma za Siri za Afrika Kusini. Akishirikisha uzoefu wake na makauhani,Padre Lapsley alieleza kwamba “mapema kabisa baada ya bomu hilo nilitambua kwamba ikiwa ningejawa na chuki na tamaa ya kulipiza kisasi, ningekuwa mhasirika milele. Kwa maana hiyo niliamua kusafiri maishani mwangu kutoka kuwa mwathirika hadi mnusurika, hadi mshindi. Watu wengi wanashindwa kusafiri zaidi ya hili. Kuwa mshindi ni kuhama kutoka kuwa kitu cha historia na kuwa somo tena. Hiyo haimaanishi kwamba sitahuzunishwa kila nilichopoteza, kwa sababu nitakuwa na alama za kuharibika kabisa.” alisema.
Mpango wa uponyaji wa kumbu kumbu wa SACBC
Katika tafakari yake kwenye warsha hizo, Padre Stan Muyebe, mkurugenzi wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Afrika Kusini (SACBC), alieleza kuwa “ushiriki wa SACBC kitengo cha Haki na Amani katika mpango wa uponyaji wa kumbukumbu unatokana na kutambua kuwa mpango wa uponyaji wa kumbukumbu ni mwendelezo wa kazi ya Tume ya Ukweli na Maridhiano ya 1995-1996. Padre Muyebe aliendelea kubainisha kwamba wakati wa mpango huo (TRC), karibu watu 23,000 waliweza kusimulia historia zao za athari chungu za ubaguzi wa rangi katika maisha na familia zao. Padre Muyebe alisema wakati huo, hata hivyo, Afrika Kusini ilikuwa nchi ya watu milioni 55, na mpango wa uponyaji wa kumbukumbu ulitokana na kutambua kwamba si kila mtu atapata nafasi ya kusimulia historia zao kupitia mpango huo (TRC). “Kwa hiyo kulikuwa na haja ya kuunda jukwaa mbadala ambalo linahakikisha kuendelea kwa historia, uponyaji na upatanisho miongo kadhaa baada ya ubaguzi wa rangi,” aliongeza Padre Muyebe, pia kwamba, “Kama Kanisa, tumeshirikiana na taasisi ya uponyaji wa kumbukumbu ili kusaidia nchi ifanyie kazi uponyaji wake na upatanisho kupitia kusimulia historia”.
Uponyaji sio tu wa urithi wa uchungu wa ubaguzi rangi lakini hata wa kushindwa kwa uongozi
Kulingana maelezo ya Padre Muyebe uponyaji ambao nchi inahitaji sio tu kutokana na urithi wa uchungu wa ubaguzi wa rangi, lakini “Pia unatokana na urithi wa uvunjaji wa ahadi na kushindwa kwa uongozi katika miongo miwili ya demokrasia ya kikatiba. Pia ni kutokana na uzoefu wa hasara na huzuni unaohusishwa na janga la UVIKO-19”. Kwa njia hiyo alisema kwamba kuna hisia kuwa Afrika Kusini inapambana na majeraha ambayo hayajapona kutokana na ubaguzi wa rangi na majeraha mapya kutokana na janga la Uviko-19. “Majeraha haya ambayo hayajapona yanatumiwa na wanasiasa wanaopenda siasa kuzidisha ubaguzi, hofu, chuki na vurugu. Katikati ya haya yote, Injili inatualika kuleta ujumbe wa matumaini, ujumbe wa huruma ya Mungu, uponyaji, upatanisho, na msamaha wa dhambi zetu”, alisisitiza kuhani huyo.
Kuna haja ya kuwa na uwezo wa kusimulia historia na hitaji la kusikilizwa
Wakati wa warsha Padre Michael Lapsley alielezea uwezo wa kusimulia historia, juu ya jinsi kila historia inahitaji msikilizaji na jinsi sisi sote tuna historia ya kusimulia ili tuweze kuponywa kihisia na kiroho.” Padre Lapsley alisema moja ya mapambano makubwa maishani ni historia kutambuliwa na kutambuliwa maumivu ya watu. Wakati wa warsha hiyo ya uponyaji wa kumbukumbu katika Jimbo Kuu la Bloemfontein, washiriki kwa hiyo walipata fursa ya kushirikishana wao kwa wao historia zao za maisha zenye kuumiza na kujadili jinsi ya kufanya mchakato wa safari ya kutoka kuwa mwathirika hadi kufikiwa kuwa mshindi, kutoka katika kumbukumbu za kujiangamiza hadi kufikia kumbukumbu zinazoleta uhai. Warsha pia ilijadili uwezo wa kusimulia historia na uponyaji wa kumbukumbu katika parokia na jinsi hii inavyo husishwa na wito wa kuwa Kanisa la Kisinodi.
Changamoto katika wito wa kikristo wa kuwa Kanisa la Kisinodi na nafasi ya kusikiliza Roho Mtakatifu
Kuhusiana na hilo, Padre Stan Muyebe alitoa maoni yake kwamba “imesemwa mara nyingi kuwa moja ya changamoto katika wito wetu wa kuwa Kanisa la Sinodi ni jinsi gani ya kutoa nafasi za kweli za kumsikiliza Roho Mtakatifu akizungumza kupitia wale walio pembezoni mwa Kanisa. Kanisa hili ni muhimu.” Padre muhyebe aidha aliongeza kusema kuwa watu pia wasipoteze mwelekeo wa changamoto ya ziada ambayo, “Katika muktadha wa pengo kubwa kati ya matajiri na maskini nchini Afrika Kusini, changamoto nyingine katika wito wetu wa kuwa Kanisa la Sinodi ni uwezo wa Kanisa katika kutengeneza fursa na kutoa fursa, majukwaa ambayo yangeruhusu wale walio pembezoni mwa uchumi wa Afrika Kusini kupata historia zao na hadhi yao kutambuliwa na wale walio madarakani.
Je tunahitaji nini kusikiliza mahitaji yote ya wenye mahitaji katika jamii?
Padre Muyebe akiendelea alisema kwamba kuna maswali ambayo yanahitaji kutafakari: “Tunahitaji nini ili kuunda majukwaa kama haya kwa watu wasio na makazi, vijana wasio na ajira, wahamiaji/wakimbizi, wanawake wanaonyanyaswa, walemavu wa mwili, wafanyakazi wa shamba, wagonjwa waliokuwa kwenye migodi zamani, wale wanaoishi katika mazingira yasiyo ya kibinadamu katika makazi duni na mengine? Je, tunahitaji kufanya nini ili kusikiliza na kutambua kile ambacho Roho Mtakatifu analiambia taifa kupitia uzoefu wa wale ambao jamii imewaweka pembezoni mwa uchumi? Padre Muyebe kwa kukazia alisema hayo ni baadhi ya maswali yanayopaswa kuulizwa katika mchakato wa safari ya kuwa Kanisa la Kisinodi, Kanisa la Sinodi linaloitwa kuwa Msamaria mwema katika mazingira ya kukosekana kwa usawa wa kiuchumi.
Mwendelezo wa warsha hizi katika majimbo ya Aliwal Kaskazini,Kimberely na Mariannhill
Mnamo 2021, warsha kama hizo zilifanywa na mapadre katika majimbo ya Aliwal Kaskazini, Kimberely na Mariannhill. Warsha za uponyaji wa kumbukumbu zinafanywa chini ya msingi wa mpango wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Afrika Kusini (SACBC), hasa uthibitisho wake wa uponyaji na upatanisho kama sehemu muhimu ya uinjilishaji Kusini mwa Afrika. Warsha zinasisitiza kwamba uinjilishaji kama ushiriki katika utume wa uponyaji na upatanisho wa Kristo unahitaji malezi endelevu ya mapadre kama waponyaji waliojeruhiwa. Inalazimu kuwekwa kwa Kanisa kama mponyaji aliyejeruhiwa, kile ambacho Papa Francisko anakiita Kanisa kama hospitali ya kambi baada ya vita.