Tafuta

Kumbukizi hii ni kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, aliyewawezesha Padre Vincent Boselli na Sr. Maria Rosaria Gargiulo, ASC kutumia vipaji na karama zao kwa ajili ya mafao ya watoto. Kumbukizi hii ni kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, aliyewawezesha Padre Vincent Boselli na Sr. Maria Rosaria Gargiulo, ASC kutumia vipaji na karama zao kwa ajili ya mafao ya watoto. 

Miaka 20 ya Kijiji Cha Matumaini Dodoma: 2002-2022: Imani, Matumaini na Mapendo

Kijiji cha Matumaini kilianza na watoto watatu, waathirika wa UKIMWI. Leo hii, kina watoto 145, kati yao kuna wavulana 62 na wasichana 83 wanaoishi kwenye nyumba 13 zinazohudumiwa kwa mtindo wa familia, ili kuhakikisha kwamba, watoto wote wanaonja huruma na upendo kutoka kwa wazazi wao, wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao: kiroho, kimwili na kiakili.

Na Padre Vincent Boselli, C.PP.S. -Dodoma, Tanzania.

Kumbukizi la Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Kijiji cha Matumaini kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, tarehe 17 Agosti 2022 linazinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Mgeni rasmi kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria De Mattias, Dodoma, ili kuwajengea wanafunzi mazingira bora zaidi ya kujifunzia. Kijiji cha Matumaini kinachoendeshwa na kusimamiwa na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu kwa kushirikiana na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Tanzania, kilizinduliwa rasmi tarehe 17 Agosti 2002. Mwaka 2022, kinaadhimisha kumbukizi la Miaka 20 ya Huruma, Upendo na Matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa watoto wanaoishi katika hali na mazingira magumu. Kumbukizi hii ni kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, aliyewawezesha Padre Vincent Boselli na Sr. Maria Rosaria Gargiulo, ASC kutumia vipaji na karama zao, kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema, kuanzisha Kijiji cha Matumaini. Kijiji kilianza na watoto watatu, waliokuwa wameathirika kwa Ugonjwa wa Ukimwi. Leo hii, Kijiji cha Matumaini kina watoto 145, kati yao kuna wavulana 62 na wasichana 83 wanaoishi na kutunzwa kwenye nyumba 13 zinazohudumiwa kwa mtindo wa familia, ili kuhakikisha kwamba, watoto wote walau wanaonja huruma na upendo kutoka kwa wazazi wao, wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao: kiroho, kimwili na kiakili.

Kijiji cha Matumaini kimekuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watoto wengi
Kijiji cha Matumaini kimekuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watoto wengi

Katika kipindi cha miaka 20 kuna Wasamaria wema, waliojisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo ili kuhakikisha kwamba, watoto wa Kijiji cha Matumaini wanakuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kati yao ni Bwana Gigi Marini, Antonio Grossi, wengi walimtambua kama “Bomba Loro” aliye hakikisha kwamba, Kijiji cha Matumaini kinapata mfumo bora wa huduma ya maji. Wengine ni Marino Marelli, Frizza Giani, Anna Maria Bartolomei. Hawa wametangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Mchango wao utaendelea kupigwa chapa katika maisha ya watoto wa Kijiji cha Matumaini, Dodoma. Akina Hassani, Regina na Jackiline, wanakumbukwa kwani walipokelewa Kijijini hapo, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, akapenda kuwapumzisha kwenye usingizi wa milele. Kwa hakika wanaendelea kuwaombea wadogo zao katika safari hii ya imani na matumaini. Kijiji cha Matumaini, kimekuwa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Wazazi walezi, Madaktari na wauguzi; Walimu na wafanyakazi wote wanaounganishwa kwa pamoja na kifungo cha upendo na matumaini kwa wale walipondeka na kuvunjika moyo.

Ujenzi wa miundo mbinu na majengo yanayoonekana na kuendelea kukipamba Kijiji cha Matumaini ni mchango kwanza kabisa wa Mtakatifu Yohane Paulo II aliyechangia ujenzi wa nyumba ya kwanza ya Kijiji cha Matumaini na kufunguliwa rasmi tarehe 17 Agosti 2022 na Askofu mkuu Luigi Pezzuto, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania. Kijiji hiki ni mchango mkubwa wa Wasamaria wema kutoka Italia, Canada na Tanzania hata katika umaskini wao. Kijiji cha Matumaini kilianza mchakato wa ujenzi wa shule ya awali na msingi ili kuwapatia watoto fursa ya kujiendeleza kimasomo wakati huo huo wakiendelea kupata tiba ya kurefusha maisha. Ilikuwa ni vigumu kuwapeleka watoto wa Kijiji cha Matumaini kwenye shule za kawaida kutokana na ukweli kwamba: wangeweza kutengwa kutokana na unyanyapaa. Idadi ya watoto ilikuwa inaongezeka kwa kasi na kwamba, watoto hawa walikuwa wanahitaji kupata tiba kwa wakati muafaka. Ujenzi wa shule ya msingi, sekondari pamoja na kidato cha tano na sita ni mkakati wa kutaka kuvunja upweke miongoni mwa Watoto wa Kijiji cha Matumaini kwa kuwashirikisha wanafunzi kutoka katika maeneo ya jirani kusoma na kuishi pamoja na watoto walioathirika kwa Ukimwi. Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Matumaini inaonesha mafanikio makubwa katika elimu.

Kijiji cha Matumaini chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Kijiji cha Matumaini chemchemi ya imani, matumaini na mapendo

Hizi ni juhudi za waalimu kutaka kuwajengea wanafunzi wao uwezo wa kiakili, ili baadaye waweze kujitegemea na kuwategemeza ndugu zao. Ni matumaini makubwa ya Kijiji cha Matumaini kinachoendeshwa na Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu kwamba, watoto wa Kijiji cha Matumaini wanaoendelea kukua kwa kimo na busara, siku moja watafanikiwa kuhitimu masomo yao katika medani mbali mbali za maisha na kurudi kuwasaidia watoto wengine wanaoendelea kupambana na ugonjwa wa Ukimwi ndani na nje ya Kijiji cha Matumaini, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza Injili ya Furaha na Matumaini kwa wale waliokata tamaa kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Kijiji cha Matumaini kilifanikiwa kujenga Maabara, PMTCT kwa ajili ya wanawake wajawazito, CTC kwa ajili ya tiba ya Wagonjwa wa Nje, OPD pamoja na wagonjwa wa ndani pamoja na Zahanati kwa ajili ya tiba kwa watoto wachanga. Kijiji cha Matumaini, pia kinaendelea kujiimarisha katika mchakato wa kujitegemea kwa kuanzisha Huduma ya Kuoka Mikate pamoja na shamba linaloendeshwa kwa kilimo bora.

Kijiji cha Matumaini kiliwahi kuwa na idadi ya watoto 180, wote hawa walipatiwa tiba, malezi na makuzi makini. Leo hii kuna baadhi yao waliohitimu hata vyuo vikuu na wengine wameanza maisha yao kama watu wazima, kwa hakika Mwenyezi Mungu, chemchemi ya matumaini anapaswa kupewa sifa na shukrani. Baadhi ya watoto waliolelewa na kutunzwa kwenye Kijiji cha Matumaini, baada ya masomo katika taasisi mbalimbali wameajiriwa Kijijini hapo, ili kuendeleza kile kifungo cha upendo, kwa kuwalea na kuwatunza wadogo zao. Haya ni matukio na mafanikio makubwa yaliyoimarisha fadhila ya matumaini. Kijiji cha Matumaini kilianza kama Zahanati ya kutoa huduma ya Dawa za Kurefusha Maisha, ARV. Huduma ziliendelea kuimarika mwaka hadi mwaka, kiasi cha kupata ruhusa kutoka Wizara ya Afya na kukigeuza Kijiji cha Matumaini kuwa ni Kituo cha Afya, kwa ajili ya huduma kwa watoto na watu wazima. Maabara ya Kijiji cha Matumaini inatoa huduma muhimu kama vile “Ultra Sound”. Kijiji cha matumaini kimeendelea kutoa huduma bora ya elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hataarishi, jambo la kujivunia na kumshukuru Mungu. Kijiji cha Matumaini kimetoa huduma ya malezi na makuzi kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu. Shule ya St. Maria De Mattias ni kati ya shule zinazofanye vizuri zaidi mkoani Dodoma na hata Kitaifa.

Kijiji cha Matumaini ni matunda ya ushirikiano na mshikamano wa upendo
Kijiji cha Matumaini ni matunda ya ushirikiano na mshikamano wa upendo

Changamoto kubwa kwa sasa ni kodi ambayo Kijiji cha Matumaini kinapaswa kulipa kwa Serikali, ili hatimaye, fedha hii itumike kwa ajili ya kuendelea kuboresha mazingira ya kuishi na kujifunzia kwa watoto hawa sanjari na kuendelea kujitegemea zaidi. Kijiji cha Matumaini kinapania kujenga mabweni kwa watoto wa nje, maabara kwa ajili ya kujifunzia, ili kuwapatia wanafunzi wanaopata elimu hapa Kijijini, ujuzi na maarifa ya kupambana vyema na hali pamoja na mazingira yao. Msamaha wa kodi Kijiji cha Matumaini unaweza kuwa alama ya matumaini na maboresho zaidi. Kijiji cha Matumaini kinaushukuru uongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa msaada wake wa elimu na tiba ya uhakika kwa wagonjwa wanaopata huduma kutoka katika Kijiji cha Matumaini. Shukrani za dhati ziwaendee Kampuni ya Pyramid Pharmacy, Kampuni ya The Big Five na USAID kwa kuchangia vifaa tiba katika Kijiji cha Matumaini. Tangu mwanzo, Serikali ya Tanzania imeonesha upendeleo wa pekee kwa Kijiji cha Matumaini, kwa kukipatia ardhi ya kutosha kwa shughuli mbalimbali; kwa kukipatia Wahudumu wa Afya pamoja na misaada mbalimbali ya hali na mali. Shukrani za dhati kutoka katika sakafu ya moyo wa waasisi, watoto na wahudumu wa Kijiji cha Matumaini, ziwaendee watanzania wote waliowaonesha na kuwaonjesha tone la upendo watoto wa Kijiji cha Matumaini katika kipindi cha miaka yote ishirini. Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena! Wasamaria wema, wasisite kuwatembelea, kuwasaidia na kuwafariji watoto wa Kijiji cha Matumaini na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwajenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kijiji cha Matumaini
16 August 2022, 16:26