Mkutano wa Lambeth 2022: Mambo makuu yanayojadiliwa ni: Athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na mapambano dhidi ya umaskini duniani. Mkutano wa Lambeth 2022: Mambo makuu yanayojadiliwa ni: Athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na mapambano dhidi ya umaskini duniani. 

Mkutano wa 15 wa Lambeth 2022: Mazingira, Vita Na Umaskini

Mkutano wa 15 wa Lambeth umezinduliwa rasmi tarehe 26 Julai kwa ibada rasmi na unahitimishwa tarehe 8 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kanisa la Mungu kwa Ulimwengu wa Mungu: kutembea, kusikiliza na kushuhudia pamoja.” Mkutano huu unapembua kwa kina na mapana maana ya ushirika wa Kanisa, mazingira, vita na mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Lambeth “Lambeth Conference” ni mkusanyiko wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kianglikan unaoitishwa na Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Canterbury lililoko nchini Uingereza kila baada ya miaka kumi. Mkutano huu kwa mara ya kwanza uliadhimishwa huko Lambeth, nchini Uingereza mnamo mwaka 1867 kwa kusimamiwa na Makanisa ya Amerika ya Kaskazini na kwa hakika imekwisha kugota miaka 155 tangu tukio hilo la kihistoria lilipoanizshwa. Ni mkutano wenye mamlaka ya hali ya juu, ambamo wajumbe wake, wanatoa ushauri kwa vipaumbele vya Kanisa Anglikan katika kipindi cha miaka kumi. Maadhimisho ya Mkutano wa Lambeth ni muda muafaka wa viongozi wa Kanisa kusali, kutafakari, kujenga na kuimarisha ushirika wa Kanisa unaosimikwa katika majadiliano mintarafu maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mkutano wa 15 wa Lambeth umezinduliwa rasmi tarehe 26 Julai kwa ibada rasmi na unahitimishwa tarehe 8 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kanisa la Mungu kwa Ulimwengu wa Mungu: kutembea, kusikiliza na kushuhudia pamoja.” Mkutano huu unapembua kwa kina na mapana maana ya ushirika wa Kanisa la Kiangalikan, ili kuitikia na kujibu changamoto, fursa na matatizo yanayojitokeza katika ulimwengu wa Karne ya 21.

Mkutano wa 15 wa Lambeth 2022: Mazingira, Vita na Umaskini Duniani
Mkutano wa 15 wa Lambeth 2022: Mazingira, Vita na Umaskini Duniani

Huu ni mkutano ambao umeitishwa na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikan duniani. Mkutano huu ulipaswa kuadhimishwa kunako mwaka 2020, lakini kutokana na janga kubwa la maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 likahailishwa na sasa linaadhimishwa. Huu ni mkutano unaosimikwa katika Maandiko Matakatifu na kwa namna ya pekee kwa mwaka huu, wanaongozwa na Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Petro kwa Watu wote unaokazia kwa namna ya pekee kabisa: Mafundisho ya Ubatizo, kweli kuu za kiimani katika Kristo Yesu na maisha adili kadiri ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Umuhimu wa kuvumilia mateso kwa saburi; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu na wokovu wa roho za watu unaopata chimbuko lake katika mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu. Maadhimisho ya Mkutano wa 15 wa Lambeth ni muhimu hasa katika nyakati hizi, ambamo walimwengu wanashuhudia: vita, kinzani na migawanyiko ya kila aina.

Hii ni fursa ya kutambua na kukiri mwelekeo wa Roho Mtakatifu katika utambuzi wa “Kanisa la Mungu kwa Ulimwengu wa Mungu” Jumuiya Waanglikan inapojizatiti katika mchakato wa kutembea, kusikiliza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake katika ushirika. Leo hii kuna mambo mengi ambayo yanawagawanya na kuwasambaratisha wanadamu, lakini changamoto kutoka kwa Kristo Yesu anasema, Askofu mkuu Justin Welby ni wito na mwaliko wa ushuhuda unaosimikwa katika ushirika, ili Kristo Yesu aweze kutangazwa na kushuhudiwa kwa walimwengu. Petro Mtume, katika maisha na utume wake, alikabiliana na changamoto pevu: mateso, hali ya kukata na kujikatia tamaa; furaha ya kuwa pamoja na Kristo Yesu, uhamisho na hali ya kutengwa na kunyanyaswa. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwomba Roho Mtakatifu, ili awasaidie Wakristo kutafuta na hatimaye, kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Mkutano wa 15 wa Lambeth: Ushirika na ushuhuda wa imani ya Kanisa
Mkutano wa 15 wa Lambeth: Ushirika na ushuhuda wa imani ya Kanisa

Kauli mbiu ya mkutano huu, iwasaidie viongozi wa Kanisa la Kianglikan kutembea, kusikiliza na kushuhudia kwa pamoja, changamoto kubwa kutoka kwa Kristo Yesu ni wote wawe wamoja! “Ut unum sint” kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha ushirika wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, kwa kujikita katika huduma kama kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika matendo. Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kushirikishana uzoefu na mang’amuzi kutoka katika Makanisa mahalia, ili hatimaye, kujielekeza zaidi katika huduma ya upendo kwa Mung una jirani. Tangu mwaka 2020, kumekuwepo na safari ya pamoja, iliyosaidia kupyaisha vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Huu ni muda ambao uliwawezesha Maaskofu wa Kanisa Anglikan, kukutana na kujadiliana kwa pamoja katika mitandao ya kijamii. Baada ya kusikilizana, awamu ya pili itakuwa ni ushuhuda wa ushirika kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi yatakayokuwa yamefikiwa katika Maadhimisho ya Mkutano wa 15 wa Lambeth huko nchini Uingereza kwa mwaka 2022.

Mkutano wa Lambeth

 

01 August 2022, 15:15