Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Maana na Umuhimu Wake Kwa Waamini
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli) Italia
Kila Agosti 15 Mama Kanisa anaadhimisha SHEREHE YA KUPALIZWA MBINGUNI BIKIRA MARIA. Hii ni moja kati ya sikukuu 10 ambazo Mkatoliki anapaswa kuhudhuria Misa Takatifu kama isemavyo amri ya kwanza ya Kanisa: Hudhuria Misa Takatifu Dominika na Sikukuu zilizoamriwa (Sikukuu zilizoamriwa zipo 10, mojawapo ni Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria). Fundisho kuwa Bikira Maria alipalizwa Mbinguni Mwili na Roho ni kati ya mafundisho manne ya imani (Dogma) yanayomuhusu Bikira Maria ambayo ni lazima mwamini Mkatoliki kuyasadiki (Dogma). Mengine kuhusu Bikira Maria ni haya: Bikira Maria ni Mama wa Mungu, Bikira Maria ni Mkingiwa Dhambi ya Asili na Bikira Maria ni Bikira. Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa Kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Bikira Maria ni Mama yake Kristo Yesu, ambaye ni Mwana wa Baba wa milele, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu.
Swali letu la msingi leo ni hili: Kwa nini Mungu anampaliza mbinguni mwili na roho Mama yetu Bikira Maria? Kwa kifupi zipo sababu kubwa 4 zinazojibu swali letu:Bikira Maria anapalizwa mbinguni kwa sababu ni Mama wa Mungu Bwana Wetu Yesu Kristo kabla ya kutungwa mimba tumboni mwa Mama Bikira alikuwa na asili moja tu, yaani alikuwa ni Mungu tu. Injili ya Yohane inathibitisha ukweli huu: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yn. 1:1). Tangu Yesu anapotungwa mimba tumboni mwa Mama Bikira Maria anatwaa asili ya pili, yaani “anafanyika mtu” kwa kutwaa mwili wa kibinadamu kama Mwinjili Yohane anavyoeleza: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu” (Yn. 1:14). Hivyo kwa kipindi chote cha miezi 9 alichokaa tumboni mwa Mama Bikira Maria (na milele yote) Bwana Wetu Yesu Kristo alikuwa na asili mbili: Ni Mungu na ni Mtu, hivyo Bikira Maria alimbeba na kumzaa Mungu-mtu. Kwa sababu hii Bikira Maria huitwa Mama wa Mungu pia (alimzaa Nafsi ya Pili ya Mungu katika ubinadamu). Loo! Ni heshima kubwa namna gani unastahili mwili wa mama huyu ambapo ndani mwake alikaa Mungu-mtu? Mwili wa Mama Yetu Bikira Maria ulikuwa ni mwili mtakatifu sana na uliotukuka sana kwani ulikuwa ni Mwili wa Mama wa Mungu.
Je, Mungu/Yesu angeweza kuruhusu mwili mtukuka wa Mama huyu kuoza kaburini? La hasha! Ndiyo maana aliamua kumpaliza mbinguni mwili na roho Mama huyu Mpendelevu sana ili mwili wake mtakatifu na mtukuka (mwili uliombeba na kumzaa Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu katika mwili wa kibinadamu) usioze kaburini. Utangulizi wa Sherehe ya Kupalizwa mbinguni Bikira Maria unataja wazi kuwa alipalizwa mbinguni kwa kuwa ni Mama wa Mungu: “Nawe hukutaka kamwe aoze kaburini yeye aliyemzaa Mwanao, asili ya uzima wa vitu vyote.” Kumbe, kumzaa Kristo (kuwa Mama wa Mungu) ndiko kunamstahilisha Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Mwili wake (na roho yake) unapalizwa mbinguni maana ni Mwili wa Mama wa Mungu- mwili ambao katu haustahili kuozea kaburini. Bikira Maria alipalizwa mbinguni kwa sababu ni Mkingiwa dhambi ya asili na dhambi nyingine zote. Sababu hii tutaihusianisha pia na mapokeo/imani ya Wayahudi. Wayahudi waliamini kuwa mwili wa mtu mwenye dhambi huadhibiwa pia hata baada ya kufariki. Adhabu ambayo mwili wa mdhambi hupewa ni kuoza/kuharibika kwa mwili (corruption of the body). Hivyo, kwa Wayahudi, kuoza kwa mwili (corruption of the body) ni kielelezo dhahiri kuwa mtu huyo alikuwa na dhambi na hivyo anaadhibiwa (mwili unaoza) kwa sababu ya dhambi zake. Ili kuonesha dhahiri kuwa Bikira Maria hakuwa na dhambi Mungu aliamua kumpaliza mbinguni mwili na roho ili mwili wake usioze/kuharibika kaburini, jambo ambalo lingemfanya aonekane kuwa alikuwa na dhambi na hivyo mwili unaadhibiwa. Hivyo Bikira Maria anapalizwa mbinguni ili kuthibitisha kuwa ni mkingiwa dhambi ya asili na dhambi nyingine zote.
Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho kwa sababu ni Bikira daima. Hebu tuangalie maana nyepesi ya Bikira. Bikira ni mwanamke ambaye kizinda (hymen) chake bado hakijavunjwa kwa kuingiliwa na mwanamume. Kwa maneno rahisi Bikira ni mwanamke ambaye ameutunza mwili wake kwa usafi wa moyo kwa kutoruhusu kuingiliwa kimwili. Wapo wanawake duniani ambao ni mabikira katika maana halisi ya neno bikira. Hata hivyo, Mama yetu Bikira Maria ni bikira wa daima (kabla ya kumzaa Yesu, wakati wa kumzaa Yesu na baada ya kumzaa Yesu alibaki kuwa Bikira). Alitunza ubikira wake usiharibiwe na mwanamume ili kujiweka wakfu kwa Mungu (consecrated virgin). Kwa kuwa alitunza ubikira wake daima (yaani aliutunza mwili wake usiharibiwe na mwanamume kwa kuishi ubikira), Mungu naye alikusudia kuwa mwili wake usiharibiwe kaburini maana ulitunzwa vizuri kwa kiapo cha ubikira na ndiyo maana alimpaliza mbinguni mwili na roho ili azidi kuvitunza vizuri mwili na roho yake. Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho kwa sababu alishiriki kazi ya ukombozi. Bwana Wetu Yesu Kristo alitukomboa kwa mateso makali, kwa kifo chake msalabani na ufufuko wake. Baada ya mateso hayo makali na kifo, Mungu Baba alimpa tuzo la ushindi: Alimfufua, kisha akapaa mbinguni na kuketi kuume kwa Baba (yaani kutawala pamoja na Mungu Baba, rejea Mdo. 7:56).
Kwa maneno mengi Yesu baada ya kumaliza kazi ya ukombozi alipewa tuzo na Mungu Baba (tuzo la kufufuka, kupaa mbinguni na kuketi kuume kwa Baba). Tuzo hili hakulipata bure bure- alilipata baada ya kumkomboa mwanadamu kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kadhalika, Bikira Maria alishiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Alishiriki vipi kazi ya ukombozi wamwanadamu? Kwanza, kwa kukubali kwake kumchukua mimba Bwana Wetu Yesu Kristo (kwa “fiat” yake. “Fiat” ni neno la Kilatini lenye maana ya “Nitendewe”); Pili, kwa kuteseka pamoja na mwanae. Hakuna anayepata mateso mengi kama mama anayeshuhudia mwanae akiteseka. “Atesekapo mtoto, mama naye huteseka.” Huu ni ukweli dhahiri. Mateso yote aliyopitia Yesu katika safari yake ya ukombozi wa mwanadamu yalimtesa vikali mama yake pia. Hivyo, Mama Bikira Maria alishiriki ukombozi wa wanadamu kwa kushiriki mateso ya mwanae, ingawa kwa namna tofauti. Kwa kuwa Mama Bikira Maria alishiriki kazi ya ukombozi, naye alistahili kupewa tuzo. Tuzo analopatiwa Bikira Maria si jingine bali ni kupalizwa mbinguni mwili na roho na kufanywa malkia mbinguni (rejea Ufu. 12:1). Hivyo, Bikira Maria anapalizwa mbinguni kwa sababu alishiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu.