Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Tunda la Kwanza la Ukombozi: Imani ya Kanisa
Na Padre Efrem Msigala, OSA., - Roma.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News. Leo tunaadhimisha sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni. Ni sherehe ambayo kila mwaka inaadhimishwa tarehe 15 Agosti au siku za karibu ya tarehe hiyo. Kabla au baada. Kupalizwa kwa Bikira Maria mbinguni ni mojawapo ya mafundisho tanzu manne yanayo muhusu Bikira Maria katika Kanisa Katoliki, ambayo yamepelekea kuwa na sherehe nne kuu za Bikira Maria ingawa pia kuna sikukuu na kumbukumbu mbalimbali kwa heshima ya Bikira Maria. Sherehe hizo nyingine tatu ambazo ni sehemu ya mafundisho ya imani ni kama ifuatavyo: Januari 1, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu; Desemba 8, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Machi 25 Kupashwa Habari Bikira Maria kwamba atakuwa ni Mama wa Mungu na 15 Agosti Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni. Kwa hiyo Sherehe ya Kupalizwa mbinguni ilitangazwa na Papa Pius XII. Alitangaza na kufanya moja ya sherehe nne za Bikira Maria lakini pia kuwa ni fundisho la Imani kama tulivyosikia mwanzoni. Papa Pius XII aliifafanua mwaka 1950 katika Hati yake ya kitume Munificentissimus Deus kama ifuatavyo: Tunatangaza na kufafanua kuwa ni fundisho la sharti lililofunuliwa na Mungu kwamba Mama wa Mungu asiye na doa, Maria ambaye ni bikira milele, wakati maisha yake ya kidunia yalipokamilika, alichukuliwa juu mwili na roho hadi kwenye utukufu wa mbinguni.
Azimio na tamko hilo lilijengwa juu ya fundisho la 1854 la Kupashwa Habari kuwa Mama wa Mungu, ambalo lilitangaza kwamba Maria alichukuliwa mimba bila dhambi ya asili, na zote mbili zina msingi wao katika dhana ya Maria kama Mama wa Mungu. Papa alihalalisha dhana si kwa mamlaka ya Kibiblia bali kwa kiasi kikubwa juu ya: - "makubaliano ya jumla ya Kanisa" na kitaalimungu "kufaa" kwa mafundisho, Makubaliano ya Kanisa zima: yanamaanisha kwamba kile ambacho Kanisa kwa ujumla hufundisha na kuamini lazima kichukuliwe kuwa ni ukweli uliofunuliwa na hivyo usiopingika. Kanisa linaweza tu kufikia makubaliano hayo kupitia uongozi wa Roho Mtakatifu, na uongozi wa Roho Mtakatifu hauwezi kuwa mbaya. Kabla ya kutangaza fundisho hilo Papa Pius XII alihakikisha kwamba kweli kulikuwa na maafikiano katika Kanisa. Mnamo mwaka wa 1946 aliwaandikia maaskofu wote wa Kanisa Katoliki kama walifikiri kwamba Kupalizwa mbinguni kunapaswa kuwa fundisho la Kikatoliki au fundisho la imani, na b) makasisi na walei walikubaliana nao. Asilimia 99 ya maaskofu walisema ndiyo. Hivyo kutokana na maoni hayo alitangaza rasmi mwaka 1950 kuwa kupalizwa Bikira Maria mbinguni ni fundisho la imani na kanisa linaadhimisha kila mwaka 15 Agosti sherehe kubwa katika kanisa.
Mawazo ya Kibiblia: Ingawa hakuna Maandiko ya uthibitisho wa wazi katika Biblia kwa dhana ya Maria, baadhi ya mada za kibiblia zinaweza kutoa mwanga juu ya fundisho hili. Kwa mfano, wazo la kuchukuliwa juu mbinguni lina kielelezo fulani katika Maandiko. Enock alichukuliwa mbinguni bila kuona kifo (Waebrania 11:5), na Eliya alisukumwa mbinguni na magari ya moto mwishoni mwa maisha yake (2 Wafalme 2:11). Ikiwa Mungu aliweza kuchukua watu hawa waadilifu wa Agano la Kale, ni hakika inawezekana kwamba Yesu angeweza kuchukua mama yake mwenyewe pia. Zaidi ya hayo, kwa kuwa Biblia inamtaja Maria kuwa mfuasi wa kwanza Mkristo, inafaa kwamba awe wa kwanza kupokea baraka za kumfuata Kristo. Katika Agano Jipya, Maria anaonyeshwa kama wa kwanza kusikia Neno la Mungu na kulikubali hivyo akasema: “mimi mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.... Pia akasema “Moyo wangu wa Mwadhimisha Bwana” (Luka 1:38, 45). Anaitikia neno la Mungu upesi na kwenda haraka kumsaidia Elizabeti. Maria anaendelea kuwa mwaminifu kwa mwanawe, akimfuata hata msalabani (Yohana 19:25–27), ambapo anapitia utimilifu wa unabii wa Simeoni aliyesema: “nawe Maria upanga utaingia ndani ya nafsi yako” ( Luka 2:25-27. 35). Maria anadumu katika imani katika maisha yake yote. Na tunaambiwa pia katika kitabu cha matendo ya Mitume alikuwa pamoja na mitume wamekusanyika baada ya mwanawe kupaa mbinguni (Matendo 1:14).
Hivyo Agano Jipya linatoa taswira ya wazi ya Maria kama mfuasi wa kwanza na mkuu wa Kristo, ambaye alisikia Neno la Mungu na kuliweka moyoni mwake. Kwa kuwa mojawapo ya baraka zilizoahidiwa kwa wanafunzi wote waaminifu ni ushindi juu ya kifo, ilifaa Maria, ambaye ni mfuasi wa kwanza na kielelezo cha Kristo, awe wa kwanza kupokea baraka hiyo. Hivyo, Wakatoliki wanaamini kwamba pendeleo la ufufuo lililoahidiwa kwa wakristo wote waaminifu alipewa kwanza Maria na kwa njia ya pekee kabisa. Maria alipata ufufuo na utukufu wa mwili wake wakati maisha yake ya kidunia yalipomalizika. Hivyo, dhana yake—ambayo inabubujika kutokana na ushiriki wake wa pekee katika ushindi wa Kristo kama mama wa Mwokozi na kama wafuasi wa kwanza na waaminifu zaidi wa Kristo—tunatarajia nasi kushiriki katika utimilifu wa ushindi huo ikiwa tutastahimili kama wafuasi wa Kristo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 966 inasema: “Mwishowe Bikira Msafi, aliyehifadhiwa bila doa lote la dhambi ya asili, wakati mwendo wa maisha yake duniani ulipokamilika, alichukuliwa juu mwili na roho katika utukufu wa mbinguni, na kuinuliwa na Bwana kama Malkia juu ya vitu vyote, ili apate kufanana zaidi na Mwana wake, Bwana wa mabwana na mshindi wa dhambi na mauti.” Kupalizwa kwa Bikira Mbarikiwa ni ushiriki wa pekee katika Ufufuko wa Mwanaye na kutarajia ufufuo wa Wakristo wengine:
Katekisimu inafundisha kwamba Maria alichukuliwa kwenda mbinguni wakati mwendo wa maisha yake duniani ulipotimia. Kanisa halitangazi kama Maria alikufa na kisha kuchukuliwa mbinguni au kama alichukuliwa kabla ya kufa. Inaacha fursa zote mbili wazi. Hata hivyo, wengi wa wanatheolojia na watakatifu katika karne zote wamethibitisha kwamba Maria alipata kifo—si kama adhabu ya dhambi bali kulingana na mwanawe, ambaye alikufa kwa hiari kwa niaba yetu. Katika kuunga mkono maoni hayo ya mwisho, Mtakatifu Yohana Paul wa Pili Papa alisema, “Mama si mkuu kuliko Mwana ambaye alipitia kifo, akiipa maana mpya na kuibadilisha kuwa njia ya wokovu.” Pili Katekisimu inathibitisha kwamba, Maria alichukuliwa mwili na roho katika utukufu wa mbinguni mwishoni mwa maisha yake ya duniani. Moja ya matokeo ya dhambi ya asili ni uharibifu wa mwili (KKK, 400; Mwanzo 3:19). Ikiwa Maria alikuwa amejaa neema na hakuteseka na dhambi ya asili, inafaa kwamba yeye, kama mwanawe, asingepata uharibifu wa mwili kama huo.
Mpendwa msikilizaji: Akizungumza juu ya Sherehe ya Kupalizwa kwa Bikira Maria kwa umati wa watu waliokusanyika kwenye Malaika wa Bwana katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Agosti 15, 2017, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na haya ya kusema: "Kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni tunamtaka atuletee tena sisi, familia zetu na jumuiya zetu neema ya kipekee ambayo lazima tuombe kila wakati kabla ya neema zingine ambazo pia ni muhimu kwetu - neema ambayo ni Yesu Kristo." Pamoja na hayo, katika Injili ya Luka tunasoma baada ya kuingia nyumbani kwa Elizabeti, baada ya maelezo ya Elizabeti tunaona Utenzi wa Bikira Maria wa kumsifu Mungu, Magnificat. Katika sifa zake, anasema, "Moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu inashangilia katika Mungu Mwokozi wangu." Maneno haya yanaonyesha furaha ya Maria katika upendo na uaminifu wa Mungu kwa vizazi vyote. Kwa waaminifu wote, Mungu anaahidi uzima wa milele. Ni tumaini hili haswa ambalo linaonyesha nguvu ya Kupalizwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Kupalizwa kwa Bikira Maria Mbinguni mwaka 2021 alisema, utenzi wa “Magnificat” unasikika katika liturujia. Wimbo huu wa sifa ni kama "picha" ya Mama wa Mungu. Maria "anafurahi katika Mungu kwa sababu ameutazama unyenyekevu wa mjakazi wake" (rej Lk 1:47-48).
Siri ya Maria ni unyenyekevu. Unyenyekevu wake ndio uliovutia macho ya Mungu kwake. Jicho la mwanadamu daima hutafuta ukuu na hujiruhusu kustaajabishwa na kile kinachong'aa. Badala yake, Mungu haangalii sura. Mungu hutazama moyo (rej. 1Sam 16:7) na anavutwa na unyenyekevu. Leo, tukimtazama Maria aliyechukuliwa kwenda mbinguni, tunaweza kusema kwamba unyenyekevu ndiyo njia iendayo Mbinguni. Zaidi ya hayo, “Ndiyo” ya Maria kuwa Mama wa Yesu na imani yake katika maneno na matendo ya Yesu hutuelekeza kwenye maana ya kuwa mfuasi wa kweli wa Bwana. Tuombee neema ya utayari kupokea mapenzi ya Bwana. Tukio la Upendo: Hata hivyo Kupalizwa Baadhi ya mababa wa kanisa walitumia maelezo haya kuwa Yesu kwa upendo alimchukua mama yake kutokana na yale ambayo Maria alifanya kwa upendo kwake katika maisha yake ya hapa duniani. Hivyo ni kwa upendo huo naye Kristo amemchukua mama yake na kumpeleka mbinguni. Mt. Yohane Paulo II Papa alisema kwamba Kupalizwa kwa kweli lilikuwa tukio la upendo, ambalo hamu ya Maria ya kuwa pamoja na mwana wake hatimaye ilitimizwa. Kwa kweli, picha nyingi za Kupalizwa zinaonyesha Maria akiinuka kwa utukufu juu ya wingu kwenda mbinguni, akipokelewa na malaika kwa furaha. Tuombe nasi tujaliwe upendo wa dhati katika maisha yetu ya kila siku.