Tafakari Dominika 19 ya Mwaka C: Imani Katika Matendo Matakatifu na Adili: Ushuhuda
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunayaangalia masomo ya dominika ya 19 ya mwaka C, masomo ambayo yanatuzungumzia juu ya Imani. Imani ni nguzo ya msingi katika ukristo wetu. Ndiyo tunu inayoakisi mafundisho, maadhimisho na mfumo mzima wa maisha ya mkristo. Imani ni mwanga na ni mlango, mlango ulio wazi daima na mlango unaotuingiza katika maisha ya muunganiko na Mungu (Rejea Papa Mstaafu Benedikto XVI, Porta Fidei, Mlango wa Imani n. 1) Nguzo hii ndiyo ambayo leo Maandiko Matakatifu yanatupatia fursa ili tuweze tuitafakari. UFAFANUZI WA MASOMO: Katika kuyapitia masomo ya dominika hii, nawaalika leo tuanze na somo la pili, somo ambalo linatuingiza moja kwa moja katika dhana hii ya imani. Tupo katika waraka kwa Waebrania (Ebr 11:1-2, 8-19) katika somo linalotupatia maana ya imani na kutupa mifano ya baadhi ya mashahidi wa imani katika Biblia. Tunasikia kuwa imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Hapa inayoongelewa ni imani ya kikristo. Imani ambayo msingi wake halisi sio kanuni za maisha au mfumo wa mafundisho au kitu kinachofanana na hicho. Msingi halisi wa imani ya kikristo ni nafsi ya Kristo mwenyewe. Ni wazi, Kristo huyu unamjua kwanza kupitia neno lake; anaeleza Mtume Paulo katika waraka wake kwa Warumi kuwa “imani chanzo chake ni kusikia” (War. 10:17).
Ni kwa njia hiyo ya kusikia, mtu anakutana na Kristo. Kinachombadilisha, kinachompa nguvu ya kusonga mbele na kinachomuongoza katika maisha ni Kristo mwenyewe. Bila nafsi ya Kristo Neno na mafundisho yote vinakosa kilicho kiini chake. Sasa katika imani, anayempa mtu uhakika wa mambo yanayotarajiwa ni Kristo. Tunapata uhakika kwa sababu Kristo amesema. Anayeweka bayana yale yasiyoonekana ni Kristo huyohuyo. Ni Kristo aliyeshuka duniani kuja kumdhihirisha Mungu asiyeonekana. Na kwa kuja kwa duniani amekuja kutufumbulia siri za Mwenyezi Mungu kuhusu wokovu wetu, siri za neema kubwa isiyoonekana, neema ya Mungu. Kutoka hapo, somo hili la waraka kwa waebrania linatupatia mifano ya mashahidi wa imani. Anatajwa Abrahamu baba wa imani aliyeianza safari ya imani asijue anakokwenda lakini akienda kuwa kuliamini Neno la Mungu. Inakumbukwa pia sadaka aliyokuwa tayari kuitoa, sadaka ya mwanae Isaka kwa kuwa tu aliliamini na kulitumaini Neno la Mungu. Wa pili anayetajwa ni Sara, mke wa Abrahamu kwa jinsi imani yake ilivyomwezesha kupata mtoto akiwa tayari amepita umri wa kibaiolojia wa kupata mtoto. Kwa kuwataja hawa wawili, somo linatukumbusha wengi ambao waliyasimika maisha yao katika msingi wa imani na hapo hapo kutuonesha kuwa imani hii tunayosisitiziwa leo sio jambo la nadharia.
Tukirudi sasa katika somo la kwanza, tunakutana na somo kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani (18:6-9). Ni somo ambalo linakumbushia tukio la waisraeli kuokolewa kutoka utumwani Misri. Somo hili linaonesha kipengele muhimu sana kuhusu imani. Linasema kuwa tukio hilo la ukombozi, Mungu alikuwa amekwishawaambia waisraeli mapema hata kabla halijatokea. Linasema “usiku ule baba zetu walitangulia kuonywa” yaani waliambiwa. Na sababu ya kuwaambia kabla ilikuwa ni ili wafurahishwe na viapo walivyovitegemea. Kumbe Mungu aliwaambia mapema ili awape matumaini na alitimiza wokovu ili awafundishe kuvitegemea viapo vya Mungu. Ni fundisho kumbe ambalo Mungu anaendelea kuwapa watu wake, fundisho la kuliamini Neno lake. Kile Mungu anachoahidi katika Neno lake kina manufaa kikishikwa kwa imani. Hatimaye, tunaingia katika somo la Injili. Tunaendelea kusoma kutoka Injili ya Luka (12:32-48) na katika dominika hii tunasikia mausia mbalimbali ambayo Yesu anayatoa kwa wanafunzi wake. Anawaita wanafunzi wake “kundi dogo”. Anawaambia “msiogope, enyi kundi dogo kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme”. Kundi hili dogo ndilo la wale walioweka tumaini la maisha yao kwake, kundi hili dogo ndilo Kanisa lake.
Ni kundi dogo kwa sababu utume linaouchukua ni ule wa kuwa chachu au hamira ambayo kidogo kidogo inaleta mabadiliko katika jamii kubwa. Kumbe mafundisho haya ambayo Yesu anawapa ni mafundisho ya kuwaimarisha na kuwasaidia wauishi vema uamuzi wao huo, uamuzi wa imani ambao wameuchukua baada ya kukutana na Yesu na baada ya kuyasikia maneno yake. Anawaambia wasiogope. Hofu, hasa ile hofu ya maisha au hofu ya kuhusu mambo yajayo haitoki kwa Mungu. Hofu ni silaha ya adui kuwavunja moyo walio na matumaini kwa Mungu. Anawaambia wekeni hazina yenu mbinguni, wekeza katika yale yadumuyo, yale yatakayokusaidia katika ulimwengu huu na ule ujao. Kwa kiswahili tunasema “usiache mbachao kwa msala upitao”. Anaongeza kusema “viuno vyenu na viwe vimefungwa na taa zenu ziwe zinawaka”. Huu ni mwaliko wa kukesha na kujiweka tayari. Ni muhimu kukesha kwa sababu katika safari ya imani kishawishi cha kujisahau ni kikubwa. Viko vitu vingi njiani vinavyoweza kumpotezea mtu lengo na kuipoteza imani yake. Mwaliko wa kukesha ni mwaliko pia wa kuwa wavumilivu mbele ya changamoto za kiimani zinazomkabili mtu mmoja mmoja na zinazolikabili kanisa katika ujumla wake. “Msiogope enyi kundi dogo” ni mwaliko wa kuumbuka daima mwaliko wa kuifurahia imani.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii ya 19 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yamejikita katika kipengele cha imani, ni vizuri kujiuliza mwaliko huu wa imani unaamsha hisia gani ndani yangu? Ni wazi imani ya mtu, ukubwa au udogo wake, anayeijua kwa undani ni Mungu peke yake. Na hicho ndio kitu ambacho kinatusaidia kutokuhukumu wengine kuhusu kiasi cha imani yao. Kumbe jambo la uhakika na la manufaa analoweza kulifanya mtu kuhusu imani ni kutafakari yeye mwenyewe mahala ilipo imani yake. Ni hapa ninashawishika kuweka mbele yako ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News mafundisho au miongozo mikuu miwili, kati ya mingi tuliyonayo kuhusu imani. Fundisho au mwongozo wa kwanza ni ule unaopatikana katika Biblia. Mtume Yakobo katika waraka wake anasema “imani bila matendo imekufa” (rej. Yak 2:14-18). Anasema: Yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani lakini matendo ya maisha yake yanaonesha kinyume na hicho anachosema? Je hiyo imani ya kusema tu nina imani, namwamini Mungu, inaweza kumwokoa? Anamalizia Yakobo fundisho lake akisema “nioneshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu”.
Fundisho la pili ni lile ambalo Papa Francisko hulitoa daima anapozungumzia utakatifu wa maisha ya mkristo. Katika mafundisho yake hayo, Papa Fransisko husisitiza kutuonesha kuwa ushuhuda wa imani tunaoitwa kuutoa si ule wa kufanya mambo makubwa, mambo ambayo mara nyingi huvuta hisia za watu. Anasema, ushahidi wa imani tunaoitwa kuutoa ni wa kufanya mambo yale ya kawaida, mambo ya kila siku ya maisha, mambo ambayo huenda hakuna hata anayeyatambua lakini tuyafanye kwa nguvu ya imani yetu. Mifano ambayo Papa anaitoa ni ile ya kutoka katika familia zetu. Namna wazazi wanavyotunza familia zao, namna wanandoa wanavyopokeana na kuvumiliana katika mapungufu yao, namna watoto wanavyowatunza wazazi au ndugu, namna ambavyo familia inakabiliana na nyakati ngumu kama vile kuuguza wagonjwa wa muda mrefu, kupokea kifo cha mwanafamilia, kukabiliana na magomvi au chuki za kifamilia ambapo wakati mwingine mmoja anakubali kubeba lawama au mzigo wote n.k Yote hayo tunapoyafanya kwa nguvu ya imani yetu, huo ni ushuhuda mkubwa sana wa imani na ndio utakatifu wa maisha ya kawaida. Tuhitimishe tafakari yetu hii ya leo kwa sala kama ile ambayo wanafunzi walimwambia Yesu, nasi tuseme pamoja nao kwa ajili yetu “Tuongezee imani Bwana."