Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 19 ya Mwaka C wa kanisa: Heri watumishi wale bwana akiwakuta wanakesha Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 19 ya Mwaka C wa kanisa: Heri watumishi wale bwana akiwakuta wanakesha 

Tafakari Dominika 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Msiogope Enyi Kundi Dogo! Kesheni!

Ni katika muktadha wa Kanisa la mwanzo lililokuwa linapitia mateso na madhulumu ya kila aina, hivyo walianza kukata tamaa na kuogopa kwa jinsi walivyokuwa wachache na mbaya zaidi wanachukiwa na ulimwengu: Mwinjili Luka anawaandikia kuwaimarisha kuwa wasiogope hawa walio kundi dogo. Ni maneno ya faraja na tumaini kwa Wakristo wa nyakati zote! Msiogope!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ni katika muktadha wa Kanisa la mwanzo lililokuwa linapitia mateso na madhulumu ya kila aina, hivyo walianza kukata tamaa na kuogopa kwa jinsi walivyokuwa wachache na mbaya zaidi wanachukiwa na ulimwengu: Mwinjili Luka anawaandikia sehemu ya Injili ya leo kuwaimarisha kuwa wasiogope hawa walio kundi dogo. Ni maneno ya faraja na tumaini si kwa Kanisa la mwanzo bali hata katika nyakati zetu tunaposafiri kama jumuiya ya waamini, kwani daima tunaona bado yule mwovu na nguvu zake zikilishambulia na kulitesa Kanisa. Kanisa daima linahakikishiwa ufalme wa Mungu maana sio kazi ya mwanadamu bali ni ya Mungu mwenyewe, na hivyo hatuna budi kusonga mbele maana ni Mungu anayeujenga ufalme wake ulimwenguni kwa kututumia sisi wanadamu dhaifu na wadhambi. Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa tulisikia juu ya mkulima tajiri mpumbavu, ambaye hakuweka akiba yake mbinguni, kwa kujali wengine na hivyo Mungu akamchukua na akaacha mali zake zote ulimwenguni. Tulitafakari na kuona ujumbe kusudiwa kuwa katika maisha yetu mali tulizo nazo sio zetu bali sisi tunawekwa kuwa waangalizi na mawakili wa mali hizo na hivyo hatuna budi kuzitumia kadiri ya maelekezo ya mwenye mali yaani Mungu mwenyewe. Wazo hilo linaendelezwa tena katika Injili ya leo. Injili ya leo inatualika nini tufanye ili nasi tusifanye makosa kama ya yule mkulima tajiri mpumbavu.

Kesheni kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha
Kesheni kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha

Papa Francisko anatualika tuwe matajiri kwa mfano wa Mungu mwenyewe aliye tajiri wa kweli, kwani daima anatushirikisha mema yake kwa upendo na ukarimu mkubwa. Hivyo utajiri wa mali na hata karama mbali mbali hatuna budi kuvitumia kwa mantiki ile ya Mungu mwenyewe, kuwa wema na wakarimu kwa wengine wanaokuwa wahitaji. Utajiri wa Mungu kamwe hautuachi katika uhitaji wa aina yeyote kwani daima anatushirikisha mema na utajiri wake kwa ukarimu usio na mfano. Sadaka ni kutenda haki, kuwapa wengine mastahili yao: Uzeni mlivyonavyo na mkatoe sadaka. Neno la Kiebrania Tsadakha, halikuwa na maana ya kutoa sadaka kwa wenye dhiki na shida bali lilikuwa na maana ya kutenda haki. Kumpa mwingine mastahili yake, ndio kusema kila kitu ninachokuwa nacho mimi kwa ziada basi hicho ni haki ya yule asiyekuwa nacho. Ni sawa na wazo tuliloliona Dominika iliyopita kuwa sisi ni waangalizi na mawakili tu wa kila mema tunayokuwa nayo bali mmiliki na mwenye mali ni Mungu mwenyewe hivyo hatuna budi kutenda haki, ndio tsadakha. Ni mwaliko wa kuwa watu wa haki, watu wakarimu na wenye kuwajali wengine wanaotuzunguka na wenye uhitaji.

Hazina yetu inategemea tu kwa kutenda haki na ndio kuwajali wengine, kutumia mema au utajiri wa aina yeyote sio kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Na ndio wazo kuu katika Dominika ya leo tunaalikwa kuwa watumishi waaminifu na sio mabwana wakuu au wamiliki wa mema yanayowekwa mbele yetu na Mungu mwenyewe. Ni Dominika ya kuwa watumishi na mawakili waaminifu! Vyote tunavyokuwa navyo katika maisha si vyetu, bali ni vya Mungu mwenyewe, na hivyo hatuna budi kuvitumia kwa kuongozwa na mantiki ile ile ya upendo na wema na ukarimu wa Mungu mwenyewe kwa watu wake wote. Viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu ziwe zinawaka ndio mwaliko wa kuwa daima watumishi: Kanisa kama jumuiya ya waamini, ni nyumba ya Kristo Mwenyewe aliyetuachia utumishi, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutumikia kiaminifu. Yesu anatumia ishara mbili, viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu ziwe zinawaka. Lugha hii ilieleweka kwa watu wa tamaduni za Kiyahudi wa nyakati za Yesu, kwani kwa desturi mwenye nyumba alivaa kanzu ndefu na watumishi walipaswa kuvaa fupi na kujifunga viuno ili waweze kutumikia kirahisi. Walijifunga viuno vyao walipokuwa safarini au walipopaswa kufanyakazi fulani. Hivyo kila mara mtumishi alikuwa amejifunga kiuno tayari kutumika, na kuacha taa ikiwaka ndio kusema kuwa tayari muda wote kufanya utumishi. Yesu anatualika leo kuwa na viuno vilivyofungwa na taa zinazowaka, yaani kuwa tayari kutumikia daima katika maisha yetu bila kujali saa, wala nafasi au fursa au hali tunayokuwa nayo. Mfuasi wa Kristo hana saa wala majira, bali daima yupo tayari bila kujibakiza katika kutumikia kwa upendo kila anayekuwa mhitaji.

Waamini wajenge utamaduni wa sala za kiekumene
Waamini wajenge utamaduni wa sala za kiekumene

Anakuja kama mwivi sio kutuangamiza bali kutukomboa: Mfano wa pili unatushangaza kwani hatuuoni ukitumika katika Agano la Kale, Mungu anayekuja kama mwivi. Ni lugha hasi na yenye kuogofya na kukatisha tamaa. Ni katika Agano Jipya tunaona sura hii ya ujio wa Mungu kama mwivi inatumika kama tunavyosoma katika (1Wathesalonike 5:2 na 2Petro 3:10 na Ufunuo 3:3 na 16:15). Labda wengine tunapata picha kuwa Mungu anakuja kwa kutuvizia au ziara za kushtukiza kama tunavyosikia kwa baadhi ya wanasiasa wetu na viongozi katika jamii zetu. Kwa kweli hapana kwa kuwa Mungu wetu ni Baba mwema daima, kamwe hawezi kufanya matendo ya kutukomoa au ili atukute tukiwe hatupo tayari. Ni vema kutafakari vema la sivyo Injili inakoma kuwa Habari Njema, na inakuwa Habari ya kutisha na kukatisha tamaa na hilo sio lengo. Injili daima ni Euangelion, ni Habari Njema yenye kutuhakikishia amani na salama! Ujio wake daima ni neema kwetu, ni kairos kwetu. Natumaini wale mnaofuatilia tafakuri zangu mtakuwa mmekutana na tofauti ya kronos na kairos, ni maneno ya lugha ya Kigiriki yote yakiwa na maana ya muda, ila kairos sio muda wa kupimwa kama tunavyoweza kusema sasa ni saa moja asubuhi au mchana au mwezi au mwaka fulani bali ni neema za Mungu kwetu. Kila tunapomzungumzia Mungu tukumbuke tunatoka katika kronos, muda wa kupimwa na tunamzungumzia katika kairos, ndio wakati uliokubalika, wakati wa neema yaani wa Mungu mwenyewe. Tunaposema ni wakati wa Mungu maana yake ni wakati wa neema, ni wakati wa upendeleo wa Mungu kwa mwanadamu.

Mungu anakuja kwetu sio kwa nia na lengo la kuiba au kutuangamiza, bali ili atukomboe na kutupa uzima wa milele; Ujio wa Mungu kwetu daima ni wakati wa neema, ni kairos! Kama mwivi ni wazi ni lugha inayoogofya bali ni kututaka tuwe tayari daima kwani kuwa mfuasi wa Kristo ni maisha ya daima na hivyo hakuna likizo ya kuishi imani yetu, Imani haina likizo! Imani ni maisha yetu ya siku kwa siku, Injili ni kuhusu maisha yetu ya kila siku. Lugha inayotumika ni kutuonesha uzito wa kukesha tukiwa na viuno vimefungwa na taa zetu zikiwa zinawaka, ni ujumbe muhimu na wa lazima kwa ajili ya wokovu wetu. Imani yetu inajengwa katika mahusiano yetu ya ndani na ya daima na Mungu mwenyewe. Ni urafiki unaotudai na kututaka kubaki waaminifu daima kwani Yeye ni mwaminifu daima! Heri watumishi wale bwana akiwakuta wanakesha: Mfano wa tatu ni jibu la Yesu kutokana na swali la Mtume Petro. Pamoja na kwamba sote kama wafuasi na rafiki zake Yesu Kristo tunaalikwa kuwa watumishi waaminifu, bado pia kuna wale wenye nafasi maalumu zaidi katika jumuiya zetu na ndio leo hii mashemasi, makasisi na maaskofu kwa namna ya pekee kabisa. Ni angalisho kwao pia kukumbuka kundi si lao ila daima ni la Kristo na wao wamewekwa kuwa waangalizi na mawakili tu, na kamwe wasigeuke kuwa mabwana wakubwa na watawala bali wanapewa utume wa utumishi na Yesu Kristo mwenyewe.

Imani thabiti ni kinga dhidi ya woga na wasi wasi usio na mashiko
Imani thabiti ni kinga dhidi ya woga na wasi wasi usio na mashiko

Ni angalisho kwa makuhani kukumbuka kuepuka kishawishi cha kudhani kuwa ndio wenye kundi bali daima ni kundi la Kristo, yaani Kanisa lilikokabidhiwa kwa kupakwa mafuta ili kutumikia watu wake. Hapa kuna mengi tunaweza kusema ila itoshe tukumbuke kuwa sisi sote ni watumishi labda katika ngazi mbali mbali bali mwenye kundi ni Yesu Kristo mwenyewe. Na hivyo tutumikie kila mmoja kwa nafasi yake aliyokabidhiwa na mwenye kundi yaani Yesu Kristo. Maisha ya Ukristo kamwe sio maisha ya ukubwa na utawala kama ambavyo tunaweza kuangukia katika kishawishi hicho, na ndio tunasikia mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko akiwakumbusha makuhani kuwa na harufu ya kondoo, kujidogosha katika hali zote ili kuwa kweli watumishi waaminifu. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni mfano kwetu pale anapowasihi mahujaji wanaofika kwake kutokubusu pete au mkono wake, ndio kusema anatambua nafasi yake kuwa ni mtumishi tu mdogo kama ulivyokuwa moto wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, lakini zaidi sana Yesu Kristo mwenyewe anayesema amekuja duniani kutumikia na sio kutumikiwa. Ni udogo na utumishi ndio unakuwa kweli kitambulisho cha mmoja anayependa kuwa mfuasi na rafiki yake Bwana wetu Yesu Kristo. Kishawishi chochote cha kupenda ukubwa na utawala na heshima ni kinyume na Injili yake Yesu Kristo! Wapendwa tunaalikwa kuwa daima watumishi wadogo, tena wenye kujifunga viuno vyetu na taa zetu ziwe zinawaka, maisha yetu yawe taa ya kuwavuta wengine kwa Kristo kwa njia ya utumishi wetu wa aina yeyote ile

Yesu Kristo anatualika kutoogopa, ndio kusema kuwa na imani daima. Mwandishi mmoja wa Kiitalia Luigi Santucci aliwahi kuandika simulizi hili dogo: “Siku moja uoga ulikuja kugonga mlangoni kwangu. Lakini imani ikatoka kwenda kumfungulia mlango na ilipofika mlangoni hakumkuta tena bwana uoga; uoga ulikimbia” Uoga daima unakimbizwa na imani. Tukiwa wenye imani kweli basi tutaweza kuhamisha milima, ndio kusema tutaweza kuhamishi yale yote yanayoonekana kuwa ni magumu na yenye kushindikana kwa jicho la nyama. Maisha yetu hayana budi kuwa kweli ni maisha yenye kuakisi imani, na hapo tunaweza kuyashinda magumu na vishawishi vya maisha ya hapa ulimwenguni. Na imani ni kukubali kukutana na Mungu na kumruhusu aongoze na kutawala maisha yetu. Mwanataalimungu na mwanafalsafa Soren Kierkegaard aliwahi kufananisha kanuni ya Kifizikia ya Archimedes nje ya kweli za kimaumbile ya kidunia na mtu anayesali kweli kwa moyo wake wote: mtu anayesali kweli basi huyo anaweza kuiamisha dunia, ni jambo la kushangaza kama duniani angelikuwepo mtu mwenye imani na kusali namna hiyo basi tungeshuhudia miujiza mingi hasa pale anapoingia katika chumba chake cha ndani cha sala.” Na ndio kitu tunachoweza kusema hata nasi tukiwa na imani ya kweli na tukisali huku tukiongozwa na hiyo imani thabiti basi hakuna jambo litakalotuogopesha na kutushinda, kwani hakika tutahamisha milima. Hakika tukiwa na Mungu hakuna jambo litakalotushinda wala kutuogopesha. Kristo daima anasafiri na Kanisa lake, hata katika nyakati zile za dhoruba na kuchafuka kwa bahari daima yupo pamoja nasi, na ndio maana anatualika leo tusiogope!

Waamini wajifunze kujiaminisha mbele ya Mungu kwa imani na sala
Waamini wajifunze kujiaminisha mbele ya Mungu kwa imani na sala

Wapendwa Kristo anatualika sote kila mmoja kwa nafasi yake kuwa mtumishi mwaminifu na anayekesha, akiwa na taa inayowaka na ndio utayari wetu wa kumtumikia mwingine kwa upendo na kila wakati ninapohitajika kufanya hivyo kwani sijui siku wala saa. Tukumbuke tunakutana na Yesu Kristo kila siku kwa ndugu zetu wanaokuwa wahitaji wa upendo na utumishi wetu wa aina yeyote ile. Katika sura ya mwingine nakutana na Mungu muhitaji, naalikwa kutumikia bila kuweka masharti, kupenda bila kujibakiza. Upendo hauna likizo! Upendo hauna muda, ni wa daima! Basi tumuombe Mungu aliye asili ya wema wote atujalie nasi neema zake za kupokea wito wake wa kuwa watumishi waaminifu katika maisha yetu ya ufuasi. Imani haina likizo, imani ni maisha ya daima, imani ni kujifunga kiunoni na kutumikia kwa upendo na hapo kweli tunaweka akiba yetu mbinguni, akiba isiyooza milele. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

03 August 2022, 17:15