Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 20 Mwaka C wa Kanisa: Maisha ya Kikristo ni mapambano ya imani, ili kuifia dhambi na hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 20 Mwaka C wa Kanisa: Maisha ya Kikristo ni mapambano ya imani, ili kuifia dhambi na hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso.  

Tafakari Dominika 20 ya Mwaka C wa Kanisa: Maisha ya Kikristo Ni Mapambano ya Imani

Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 20 ya mwaka C, masomo ambayo katika dominika hii yanayagusa moja kwa moja maisha yetu ya kikristo na kutuonesha kuwa maisha ya kikristo, kimsingi, ni mapambano. Kukisimamia kile tunachokiamini, kupiga hatua kulifikia lengo la imani na kuyashinda majaribu, hayo yote ni mapambano mkristo anayopaswa kuyakabili kila siku.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunakwenda kuyaangalia masomo ya dominika ya 20 ya mwaka C, masomo ambayo katika dominika hii yanayagusa moja kwa moja maisha yetu ya kikristo na kutuonesha kuwa maisha ya kikristo, kimsingi, ni mapambano. Kukisimamia kile tunachokiamini, kupiga hatua kulifikia lengo la imani na kuyashinda majaribu, hayo yote ni mapambano mkristo anayopaswa kuyakabili kila siku. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza, kutoka kitabu cha nabii Yeremia (Yer 38:4-6, 8-10), kinatuletea mojawapo ya mateso ambayo nabii Yeremia aliyapitia  kwa sababu tu alichagua kusimama kidete katika kazi yake ya unabii. Somo linarejea tukio ambapo enzi za utawala wa Zedekia, ufalme wa Yuda ulihitaji kufana uamuzi wa kubaki koloni la Babeli au kuingia katika vita. Mfalme akatuma watu kwenda kwa nabii Yeremia ili kusikia sauti ya Mungu kuhusu jambo hilo.  Sauti ya Mungu kwa kinywa cha Yeremia ikawa ni ile ya kutokuiingiza nchi vitani. Sasa kwa vile mfalme Zedekia alizungukwa na washauri waliokuwa na mwelekeo wa kuipeleka nchi vitani, washauri hao hao walimwendea mfalme na kumwambia Yeremia ni msaliti wa nchi na anapaswa kuuawa.

Kusikiliza Neno la Mungu ni muhimu ili kutoa maamuzi makini.
Kusikiliza Neno la Mungu ni muhimu ili kutoa maamuzi makini.

Suala hapa halikuwa kuhusu ukoloni au uhuru, lilikuwa ni kuhusu kuisikiliza sauti ya Mungu. Na Yeremia kama nabii wa Mungu alijua upi ulikuwa mwelekeo wa washauri wa mfalme na upi ulikuwa mwelekeo wa mfalme. Wote walikuwa wamekwisha chagua vita. Yeremia hakupenda kupindisha ujumbe wa Mungu ili amfurahishe mfalme au washauri wake. Alichagua kusimamia kile alichokiamini, alichagua kusimama kidete katika wito wake.  Mazingira aliyokutana nayo Yeremia ni mazingira ambayo tunakutana nayo na sisi kila siku katika maeneo mbalimbali ya kazi, biashara, utume n.k. tunauhitaji uthabiti kama wa Yeremia katika ukristo wetu. Somo la pili (Ebr 12:1-4), lenyewe linayazungumzia maisha ya kikristo kama mashindano ya mbio. Ni mashindano ambayo wakimbiaji wote wamewekewa lengo la kufika. Anayefika mapema ndiye anayeshinda. Tofauti na mshindano hayo ambapo mshindi ni anayefika mapema, waraka kwa waebrania unaweka neno ambalo kwa kawaida kwenye mashindano hayo halipo. Neno hilo ni saburi. Ni neno linalobeba ndani yake subira, uvumilivu, kutokukata tamaa, bidii, kudumu n.k. na linafanya sasa mbio za maisha ya kikristo kuwa ni mbio ambazo ushindi sio kuwa wa kwanza kufika bali ushindi ni kufika. Njia ya imani si njia rahisi. Ni muhimu kulishika neno hilo, saburi, ili mkristo asikomee njiani akarudi bali asonge mbele daima hadi kulifikia lengo la imani ambalo ni kuuona uso wa Mungu.

Katika somo la Injili (Lk 12:49-53), Yesu anasema “msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani, sivyo, bali mafarakano.” Ni maneno makali sana. Na anaendelea kuonesha namna mafarakano hayo yanavyoweza kutokea kati ya ndugu, kati ya baba na mwana, kati ya mama na binti yake n.k. Kwa maneno haya Yesu anataka kuturudisha katika mstari na kutuonesha kuwa Neno ambalo Yeye amekuja kulipanda katika mioyo yetu sio suala la “mwendo ni uleule” au “biashara inaendelea”. Anatuonesha kuwa ukristo unamuhitaji mtu kuwa tayari kubadilika hata na hasa wakati ule ambapo mabadiliko hayo yatalazimu kuingia katika mafarakano ili kulinda utambulisho wa imani. Mafarakano anayozungumzia Yesu, kabla ya kuwa mafarakano ya nje kati ya watu wanaotuzunguka, awali ya yote ni mafarakano ya ndani. Ni mafarakano ya ndani kwa sababu Neno la Mungu likipokelewa kazi yake ya kwanza ni kuuchoma. Mara nyingi tumesikia katika Maandiko Matakatifu “watu walipolisikia neno walichomwa moyoni.” Ni neno linalomsukuma mtu kubadilika na hapo hapo Neno hilo hilo ndio huo moto wenyewe unaoleta mabadiliko. Na mabadiliko haya sio kazi ya siku moja, siyo kazi ya mara moja bali ni kazi endelevu. Yapo pia mafarakano ya nje hasa pale ambapo mkristo ambapo mkristo anajikuta anashawishiwa kuirahisisha imani yake ili aendane na matakwa ya ulimwengu unaomzunguka. Kuupokea ujumbe wa Kristo leo ni kutambua kuwa katika mazingira hayo tunahitaji kusimama kidete. Imani ambayo mkristo anasimama kidete kuilinda, kimsingi ndiyo imani itakayomlinda mkristo huyo huyo katika mapambano yake.

Maisha ya Mkristo ni mapambano yanayohitaji subira.
Maisha ya Mkristo ni mapambano yanayohitaji subira.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii ya 20 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yamejikita katika kutualika kuyapokea maisha ya kikristo kama mapambano ya imani, ni vizuri kujiuliza mwaliko huu unanigusa vipi katika maisha yangu binafsi? Katika maisha yetu kuna wakati tunakabiliwa na hofu ya kukosa uthubutu katika imani. Hofu ya kuzama katika imani, hofu ya kusimama kidete katika imani na hofu ya kuwa tofauti. Tunataka imani inayoendana na vipaumbele vyangu, imani inayoendana na kazi zangu na isiyoutikisa mfumo wangu wa maisha. Ndugu yangu imani isiyokuchokoza siyo imani, imani isiyokuaachia maswali siyo imani, imani ambayo hata mara moja haikuweki njia panda mahali ambapo unajikuta unajiuliza hapa nifanye nini: nikane imani nipate kazi au nishike imani niendelee kutafuta kazi? Nikane imani nioe au niolewe au nishike imani niendelee kutafuta mchumba n.k. Imani kwa asili yake ni chokozi. Yesu anasema amekuja kushusha moto. Ni moto unaounguza lakini ni moto ambao ndio nguvu yenyewe inayotenda kazi ndani yetu. Tuupokee mwaliko huu wa imani ambao Yesu anatupatia. Na kama Yeye mwenyewe anavyosema “tutweke hadi kilindini” tuzame ndani katika imani yetu na kwa njia ya imani hiyo tutaufikia wokovu aliotuandalia.

Liturujia D20
12 August 2022, 16:39