Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa: Kristo Yesu njia, ukweli na uzima; ni mlango wa mbinguni. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa: Kristo Yesu njia, ukweli na uzima; ni mlango wa mbinguni.  

Tafakari Dominika 21 Mwaka C wa Kanisa: Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima. Ni Mlango wa Mbinguni

“Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (rejea Mdo. 14:22). Ni ukweli huu ndio uliomsukuma Mtakatifu Mama Theresa wa Calkuta kusema, “Ikiwa mtu anatafuta dini nzuri ya kuingia basi asichague Ukristo.” Mama huyu anasema Ukristo siyo dini nzuri kabisa, siyo dini ya raha na starehe bali ni dini inayoambatana na mateso na utayari wa kujisadaka, Ushuhuda!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli) Italia.

Paulo na Barnaba, miongoni mwa Mitume maarufu wa uenezaji wa Injili ya Kristo kwa watu wa mataifa walisema kwa uthabiti ya kwamba, “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (rejea Mdo. 14:22). Ni ukweli huu ndio uliomsukuma Mtakatifu Mama Theresa wa Calkuta kusema, “Ikiwa mtu anatafuta dini nzuri ya kuingia basi asichague Ukristo.” Mama huyu anasema Ukristo siyo dini nzuri kabisa, siyo dini ya raha na starehe bali ni dini inayoambatana na mateso na utayari wa kujisadaka. Watakatifu hawa ambao ni mifano ya imani walisisitiza ukweli ambao Kristo Mwenyewe aliwaeleza wanafunzi wake na kwa namna ya pekee katika Injili yetu ya leo: “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba.” Mlango mwembamba ni kiashiria cha njia ngumu ya mateso, magumu na kujisadaka tunayopaswa kuipitia ili kuweza kurithi ufalme wa Mungu. Ukristo siyo lelemama! Tuone sasa masomo yetu kwa undani. SOMO LA KWANZA: Isa. 66:18-21: Somo letu la kwanza linatoka kwenye sura inayohitimisha kitabu cha nabii Isaya (yaani sura ya 66). Ni katika sura hii nabii Isaya anataka kuhitimisha ujumbe wake wa kinabii: kumjua Mungu, kumwabudu na kupata wokovu ni mwaliko kwa watu wa mataifa yote. Wayahudi waliamini kuwa wokovu ni kwa ajili yao peke yao na hivyo watu wa mataifa mengine hawahusiki. Walijiona wao ni taifa teule la Mungu na watakatifu sana na hivyo wengine hawana nafasi katika wokovu. Leo nabii Isaya anatufunulia ukweli halisi kuwa watu wote (watu wa mataifa yote na lugha zote) wana haki ya kumjua Mungu na haki ya kupata wokovu. Na ni kutoka kwa watu wa mataifa mengine Mungu atajiteulia makuhani na Walawi (watumishi wake) - hivyo kila mmoja ana fursa ya kumtumikia Mungu, bila kujali taifa analotoka au lugha anayaozungumza.

Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Ni mlango wa mbingu.
Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Ni mlango wa mbingu.

Somo letu la kwanza linatufundisha kuwa (i) watu wote wanastahili kumtumikia Mungu na kupata wokovu. Leo hii kuna Wakristo wana mtazamo kama wa Wayahudi wakifikiri kuwa wao peke yao ndiyo wanastahili kumtumikia Mungu au kupata wokovu- wanajiona kuwa wana hatimiliki ya wokovu. Utawasikia watu wa namna hii wakisema, “Ninyi ni wadhambi sana”, “Kabila letu ndilo linalotoa makuhani”, “Wewe siyo kabila/taifa letu hivyo huwezi kuwa Padre/Mtawa wa Jimbo/shirika letu” na mengineyo. Watu hawa wanafikiri wengine hawafai kupata wokovu kwani wanajiona wao ni bora na watakatifu zaidi kuliko wengine na ya kwamba wengine ni wadhambi sana wasiofaa kumtumikia Mungu au kupata wokovu. Watu wa namna hii wanasahau kuwa milango ya wokovu ipo wazi kwa watu wote. Wokovu u wazi kwa watu wote walio tayari kumpokea Mungu na kutimiza mapenzi yake. Yesu anaeleza pia jambo hili katika Injili yetu ya yetu anaposema, “Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.” Hii ni kuonesha kuwa ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kutoka pande zote za dunia. (ii) Tukivutwa na Mungu tunapaswa kuwa Sadaka kwa Bwana. Somo letu linasema, “Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana…” Sisi watu wa mataifa mengine tunapofanywa kuwa sehemu ya taifa teule la Mungu na kushirikishwa utukufu wa Mungu kwa njia ya Sakramenti tunazopokea tunapaswa kuwa Sadaka kwa Bwana: twapaswa kuitoa miili yetu kama sadaka kwa Bwana; twapaswa kutoa nafsi zetu kama sadaka kwa Bwana; tunapaswa kutoa mali na karama zetu kama sadaka kwa Bwana. Je, mimi na wewe ni sadaka kwa Bwana?

SOMO LA PILI: Ebr. 12:5-7, 11-13: Wakristo wanaoandikiwa waraka kwa Waebrania walikuwa ni Wakristo waliokuwa wanakabiliwa na mateso makubwa kutokana na imani yao kwa Kristo. Hivyo, mwandishi anawaandikia Wakristo ili kuwaeleza faida ya mateso (the value of suffering). Mwandishi anawataka Wakristo wenzake watambue kuwa Mungu ameruhusu wapatwe na mateso siyo kwa lengo la kuwakomesha/kuwaangamiza bali kuwaandaa kupata matunda yaliyo bora kabisa. Mwandishi anatumia mfano wa baba ambaye anamwadhibu mwanae: ingawa mtoto anayeadhibiwa hafurahii adhabu (maana adhabu inaumiza, huleta huzuni), Baba anayetoa adhabu ana lengo la kumrudi, kumfunza na kumjenga zaidi ili awe mtu bora zaidi. Baba hatoi adhabu kwa mwanae kwa sababu anamchukia mwanae bali anasukumwa na upendo kwa mwanae ili mwanae awe mtu bora zaidi- nia ni kumfunza na kumjenga/kumuunda zaidi. Hivyo, mwandishi anawahimiza Wakristo wayatazame mateso wanayopitia kama fursa ya kujengwa, kuundwa, kufunzwa na kutakaswa zaidi ili kupata wokovu. Hivyo, Wakristo wanapaswa kuona faida ya mateso, wasiyatazame kama hasara kwao Mara nyingi sisi wanadamu tunayatazama mateso (magonjwa, misiba inayotukumba, changamoto za familia, ndoa na kazi, usaliti katika mahusiano, kutengwa na ndugu au marafiki, kupoteza kazi, kufilisika kibiashara, changamoto za wito na mengineyo) kama hasara kwetu badala ya kutambua kuwa Mungu anayatumia mateso ili kutujenga, kutuunda na ili tupate wokovu. Hivyo, hatuna budi kuyapokea na kuyakubali mateso kama njia ya kutupatia wokovu. Pia tutambue kuwa kuna nyakati hatuwezi kubadili matukio katika maisha bali twaweza kubadili mtazamo wetu juu ya matukio hayo: hatuwezi kuzuia mateso, bali twaweza kubadili mtazamo wetu juu ya mateso.

Jitahidini kumtafuta Kristo Yesu Mlango wa mbinguni.
Jitahidini kumtafuta Kristo Yesu Mlango wa mbinguni.

SOMO LA INJILI: Lk. 13:22-30: Somo letu la Injili linatufundisha kuwa ni “lazima kuteseka na kuwa tayari kuacha dhambi ili kuingia mbinguni.” Yesu akiwa njiani kuelekea Yerusalemu ili kutimiza ukombozi wa mwanadamu kwa ajili ya mateso, kifo na ufufuko wake anakutana na swali kutoka kwa mtu mmoja ambaye hatajwi kwa jina. Swali la mtu huyu ni juu ya idadi ya watu watakaoingia mbinguni: “Je, Bwana, watu watakaookolewa ni wachache? Labda tuangalie kwanza msingi wa swali lake. Wayahudi waliamini kuwa wao ni taifa teule la Mungu na ya kwamba kitendo cha mtu kuzaliwa Myahudi kinamhakikishia mtu huyo kuingia mbinguni. Hivyo mawazo haya yaliwafanya Wayahudi waamini kuwa wao peke yao ndiyo watakaoingia mbinguni. Mtu huyu anaposema “wachache” anamaanisha Wayahudi tu, wengine (walio wengi) hawana nafasi ya kuokoka. Mtu huyu anauliza swali hilo ili kupata uhakika juu ya wanachoamini toka kwa Yesu. Hata hiyo, Yesu hatoi jibu kwa swali hilo (yaani hasemi kama watakaookolewa ni wachache au wengi). Kwa nini Yesu hatoi jibu? Kwa sababu swali lenyewe siyo la msingi: kujua idadi ya watu watakaookoka siyo jambo la msingi. Jambo la msingi kwa Yesu ni namna gani tutakuwa miongoni mwa hao watakaookolewa pasipo kujali kama ni wachache au wengi. Hivyo, Yesu anatoa maelezo ya namna ya kuingia kwa kutumia lugha ya picha: Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba.

Hebu tutazame taswira ya mlango anaozungumzia Yesu. Kwa kawaida miji ya zamani (ikiwemo miji ya Israeli) ilizungushiwa ukuta na kuwa na geti kubwa kwa mbele. Geti hili kubwa lilikuwa na milango midogo miwili upande wa kulia na upande wa kushoto (kama vilivyo viwanja vingi vya mpira wa miguu hapa Tanzania). Mlango huo (mlango mdogo upande wa kulia au wa kushoto wa lango/geti kubwa) ndiyo Yesu anauita mlango mwembamba. Ili mtu aweze kuingia kwa kupitia mlango huo mwembamba ilikuwa ni lazima (i) asiwe na mzigo mkubwa ambao ungeweza kuwa kero/bughuza wakati wa kupita mlangoni (maana mlango wenyewe ni mdogo na mwembamba) na (ii) aingie kwa kujibanabana/kujiminya au kwa ubavu ubavu (kama ambavyo watu hufanya wakati wa kuteremka kwenye daladala ikiwa kuna watu wengi waliosimama). Hivyo, kupita kwenye mlango huo ilikuwa ni shida/mateso kiasi. Hivyo, kwa kutumia picha ya mlango mwembamba Yesu alilenga kufundisha njia kubwa mbili ambazo mwanadamu anapaswa kutumia ili apate wokovu (kuingia kwenye uzima wa milele): (i) Kutokubeba mizigo ya dhambi ambayo ni vikwazo katika harakati za kuingia mbinguni na (ii) kuwa tayari kuteseka (maana haikuwa rahisi kupitia mlango mwembamba) ili kuingia mbinguni.

Wafundisheni watoto wenu adabu na kuwarithisha tunu bora za Kikristo
Wafundisheni watoto wenu adabu na kuwarithisha tunu bora za Kikristo

Nasi Wakristo wa zama hizi somo la Injili linatuhusu pia. Suala la msingi siyo kujua idadi ya watakaookoka bali namna ya kupata huo wokovu. Hivyo, Injili inatufundisha kuwa (i) Wokovu unapatikana kwa njia ya mateso (kwa njia ya mlango mwembamba). Kama ambavyo haikuwa rahisi kwa watu kupita kwenye mlango mwembamba, hata sisi tunafunuliwa kuwa njia ya kupata wokovu siyo rahisi kwani ni njia inayotupasa kuteseka. Kuteseka ni pamoja na kukubali taabu/magumu katika maisha ya hapa duniani: magonjwa, wajibu wetu kama Wakristo, mikasa ya maisha, usaliti katika mahusiano, kutengwa/kukataliwa, kupingwa, kunyanyaswa kwa ajili ya Kristo na hata kuuawa. Je, mimi na wewe tupo tayari kuteseka? Wengi hatupendi kuteseka ili kupata wokovu bali tunapenda kupata wokovu kwa njia rahisi, njia inayokwepa mateso/taabu/mahangaiko ya dunia: kupambana na mateso kwa gharama yoyote ile, kutendewa miujiza, kuhubiriwa Injili ya utajiri wa haraka haraka, nk. Kwa ujumla hatutaki mateso. Tusisahau kuwa, “Watu waliotembea karibu sana na Kristo ndiyo waliokumbana na mateso makubwa.” Hivyo, mateso ni sehemu ya kutembea pamoja na Kristo. Tuyapokee mateso na kuyatoa kama sadaka kwa Mungu. (ii) Ili kuingia mbinguni ni lazima kutokuwa na “mizigo.”

Ili kupita kwenye mlango mwembamba ilikuwa ni lazima mtu asiwe na mzigo ili kuondoa usumbufu wakati wa kupita kwenye mlango huo. Hata sisi tunaalikwa kuacha mizigo yetu ili kuingia mbinguni- kuacha mizigo ya dhambi. Kwa bahati mbaya wengi wetu bado tunabeba mizigo ambayo inakuwa kikwazo kwetu kuingia mbinguni: udhalimu, uzinzi, uzandiki, ubinafsi, uchoyo, rushwa, uchawi, tamaa ya mali na vyeo, ngono, ulevi, mauaji na mengineyo. Ni lazima kuacha mizigo hii kama tunataka kuingia mbinguni. (iii) Wokovu ni kwa ajili ya watu kutoka mataifa yote. Ukweli huu umedokezwa pia katika somo letu la kwanza: “Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote… mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema Bwana.” Wokovu upo wazi kwa watu wote wanaoishi vyema ukristo wao (wakiepuka udhalimu). Wokovu hauji tu kwa kusema, “Nilikuwa nashiriki sana sherehe za Jumuiya/Parokia,” “Nilikuwa nahudhuria Misa za asubuhi,” “Nilikuwa naimba sana kwaya,” Nilikuwa nahubiri vizuri sana”. Haya yote hayatatufaa kuingia mbinguni ikiwa maisha yetu yamejaa udhalimu. Tukiishi maisha ya fadhila milango ya wokovu ipo wazi kwetu sisi sote.

 

 

20 August 2022, 16:06