Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa imani ya Kikristo. Fumbo la Umwilisho na Kashfa ya Msalaba. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa imani ya Kikristo. Fumbo la Umwilisho na Kashfa ya Msalaba. 

Tafakari Dominika 22 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu Ni Msingi wa Imani na Mapendo

Masomo ya Dominika ya 22 yanakazia juu ya umuhimu na faida ya fadhila hii ya unyenyekevu. Ni fadhila ya unyenyekevu ambayo itatuwezesha kujishusha na kuwa tayari kuwakaribisha katika mioyo yetu hata wale ambao machoni pa wengi wanaonekana hawana faida, hawana chcohote. Unyenyekevu unatuwezesha kuwafikia waliosukumwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli) Italia.

Mtakatifu Augustino wa Hippo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa katika mafundisho yake aliutazama unyenyekevu kama msingi wa imani ya Kikristo. Kwa uzoefu wake wa maisha Mtakatifu Augustino hatimaye alitambua kwamba ni mtu tu aliye na unyekekevu ndiye anaweza kumfuata Kristo ambaye ni Unyenyekevu Wenyewe maana “hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu” (Flp. 2:6-7). Na hivyo Mtakatifu Augustino anatupatia ushauri mzito kuhusu unyenyekevu (kujishusha) akisema, “Je, unataka kupanda? Basi anza kwa kushuka.” Masomo yetu yote matatu ya Dominika ya Dominika ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa yanakazia juu ya umuhimu na faida ya fadhila hii ya unyenyekevu. Ni fadhila ya unyenyekevu ambayo itatuwezesha kujishusha na kuwa tayari kuwakaribisha katika mioyo yetu hata wale ambao machoni pa wengi wanaonekana hawana faida, hawana chochote. Unyenyekevu unatuwezesha kuwafikia waliosukumwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Tuyatazame sasa masomo yetu kwa undani.

Unyenyekevu ni msingi wa imani na mapendo ya Kikristo.
Unyenyekevu ni msingi wa imani na mapendo ya Kikristo.

SOMO LA KWANZA: YbS 3:17-20, 28-29: Somo letu la kwanza linatoka kitabu cha Yoshua bin Sirah, ambaye inaaminika alikuwa mwalimu wa dini na “mwandishi wa Kiyahudi”- Jewish scribe (waandishi wa Kiyahudi walihusika kunakili maandiko kwa mikono kwa kuwa ugunduzi wa uchapaji ulikuwa bado. Pia waandishi walifundisha sheria za Kiyahudi, walifafanua maandiko na kufundisha namna ya kuenenda katika maisha na kupata mafanikio ya kweli. Kutokana na majukumu haya walipewa hadhi ya kuitwa “Rabbi” yaani “Mwalimu”). Kitabu cha Sira ni matokeo ya uzoefu wa Yoshua bin Sirah wa kufundisha Sheria za Mungu, maadili na masuala mengine ya kijamii.  Katika somo letu la leo Yoshua bin Sira anafundisha moja ya nguzo kuu ili kufanikiwa katika maisha. Nguzo hiyo ni unyenyekevu. Yoshua bin Sira anasisitiza unyenyekevu: kubaki mnyenyekevu pindi unapopata mafanikio katika maisha (mali/pesa/kazi), kubaki mnyenyekevu unapopata ukuu/ukubwa (cheo/madaraka), kubaki mnyenyekevu pale unapojaliwa kuwa na karama mbalimbali. Yoshua bin Sira anaweka wazi matokeo ya kuwa mnyenyekevu: unyenyekevu utamfanya mtu apate kibali machoni pa Bwana, yaani kadiri unavyokuwa mnyenyekevu ndivyo unavyopokea wingi wa neema na baraka kutoka kwa Mungu. Kadhalika, mtu asiye mnyenyekevu huwa na kiburi na madhara ya kiburi ni mtu kupatwa na matatizo yasiyokwisha na kuendelea kuwa mwovu zaidi. Hii ni kweli kabisa.

Ushauri anaoutoa Yoshua bin Sira unatuhusu na sisi pia. Tunapaswa kuwa wanyenyekevu.  Mtu mnyenyekevu hutambua kuwa Mungu ndiye kila kitu kwake, hutambua kuwa mali na ukuu alivyopata vimetoka kwa Mungu na hivyo anapaswa kuvitumia kwa faida ya wote na hutambua pia kuwa yeye ni duni/mnyonge/mdhaifu mbele ya Mungu. Kwa bahati mbaya watu wengi tukifanikiwa tunapata kiburi: tunajiona sisi ni miungu, tunajiona kuwa hatumhitaji Mungu (hatushiriki mambo ya dini), tunajikweza wenyewe, tunajiona tunajitosheleza kwa kila kitu, tunajihudumia wenyewe, tunawadharau wengine na kuwaona hawana msaada wowote katika maisha yetu, tunatumia mali/madaraka/pesa zetu kuwanyanyasa wengine na mengineyo. Matokeo haya ya kukosa unyenyekevu hutufanya tusipate kibali machoni pa Bwana: tunajitenga na Mungu, tunajitenga na watu na mafanikio yetu ambayo yanatupa kiburi yanakuwa ya muda tu kwa sababu Mungu hana nafasi katika maisha yetu. Katika somo letu la Injili ya leo tutamsikia Yesu akisisitiza juu ya unyenyekevu (kujishusha) kwa kusema “ajidhiliye [anayejinyenyekesha] atakwezwa.” Ni kweli kabisa. Watu wanyenyekevu hukwezwa na Mungu kwani hupata mafanikio ya kweli: huwa na mahusiano mazuri na Mungu, huwa na mahusiano mazuri na wenzao na hupata baraka nyingi kutoka kwa Mungu.

Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu
Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu

SOMO LA PILI: Ebr. 12:18-19, 22-24: Katika somo letu la pili Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania analenga kutufunulia kuwa “kwa njia ya agano jipya lililofanywa kwa sadaka ya Kristo Msalabani mwanadamu anaweza kumfikia Mungu kwa urahisi, tofauti na ilivyokuwa kwenye agano la kale.” Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania katika somo letu la leo analinganisha ibada za agano la kale na ibada za agano jipya. Anatueleza ufanisi ulio bora zaidi wa yale yaliyofanywa na Kristo katika Agano Jipya akilinganisha na yale yaliyotendeka katika Agano la kale: yale yaliyotukia katika mlima Sinai yalikuwa ya kutisha sana lakini yanayofanyika katika mlima Sayuni (Yerusalemu ya Mbinguni) ni ya amani na furaha. Kimsingi Mlima Sayuni unaozungumziwa katika somo letu la pili ni Yerusalemu ya mbinguni. Kwa maneno mengine sadaka ya Kristo imefanya agano kati ya Mungu na mwanadamu: agano ambalo siyo la kuogofya kama la Mlimani Sinai bali ni agano la upendo na amani kati ya Mungu na mwanadamu, agano ambalo limemfanya mwanadamu kuwa huru kumsogelea Mungu na kuisogelea Yerusalemu ya mbinguni. Ni agano ambalo linaonesha Unyenyekevu ambapo Mungu anajishusha na kuteswa na kufa msalabani kwa ajili yetu.  Swali la msingi ni hili: Je, fursa ya kumsogelea Mungu na kufunguliwa milango ya Yerusalemu ya mbinguni tunaitumia vizuri tukingali hapa duniani? Ili tuweze kuujongea Mlima Sayuni (Yerusalemu ya Mbinguni) ni lazima kutokuwa na makandokando ya dhambi: kiburi, majivuno, zinaa, dhuluma na mengineyo.

SOMO LA INJILI: Lk. 14:1, 7-14. Katika somo letu la Injili, Bwana Wetu Yesu Kristo anapigilia msumari fundisho kutoka Somo letu la Kwanza: “unyenyekevu ni moja ya masharti ya kuingia mbinguni.” Mara nyingi Yesu alitumia mazingira ya kawaida kuelezea mafumbo ya imani. Leo amealikwa chakulani na mmoja wa wakuu wa Mafarisayo na anatumia fursa hiyo kufundisha vigezo viwili vya kutuwezesha kuingia mbinguni. Kabla ya kuingia kwa undani katika tafakari ya somo hili la Injili ni vizuri kudokeza jambo moja kubwa: ingawa mara kadhaa Yesu amekuwa akikosoa mfumo wa maisha ya Mafarisayo na kuwaeleza ukweli (rejea Lk. 11:39, 40, 42), leo ameingia katika nyumba ya mmoja wa wakuu wa Mafarisayo na kula naye chakula. Kwa tukio hili tunafundishwa kuwa: kumkosoa mtu na kumweleza ukweli siyo sababu ya kujenga uadui na chuki kati yenu. Leo Yesu anapoalikwa chakulani anagundua mambo mawili: (i) wageni waalikwa wanachagua vitu vya mbele, (ii) mwenyeji wao (mwalikaji) amealika wale wa hadhi (caliber) yake tu na wenye uhusiano naye: bila shaka Mafarisayo wenzake/matajiri wenzake tu na ndugu zake tu. Ni kutokana na mapungufu haya Yesu anataka kuonesha vigezo vya kuingia mbinguni: kutambua unyonge wetu/kujishusha mbele za Mungu na kujali mahitaji ya watu wengine bila kufikiria malipo. Kutoka kwenye Injili tumeambiwa kuwa wageni waalikwa walichagua viti vya mbele.

Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake juu ya Msalaba.
Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake juu ya Msalaba.

Kwa nini walichagua viti vya mbele? Kwa sababu walijiona wao ni bora zaidi kuliko wengine, wao ni waheshimiwa sana, wao wanapaswa kuhudumiwa kwa ukaribu zaidi kuliko wageni wengine- walifanya hivyo ili kutambulika, kuonekana kwa urahisi zaidi, kutukuzwa, kupata sifa, kujionesha wao ni wa maana zaidi. Hizi zote ni dalili za kukosa unyenyekevu. Matokeo ya kutaka kuonekana, kutafuta heshima, kutambulika au kutafuta umaarufu ni kupatwa na AIBU BAADAYE (KUFEDHEHESHWA): “Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma.”  Hivyo mwaliko wa Yesu ni kututaka kujishusha na kuwa wanyenyekevu mbele ya Mungu. Mnyenyekevu ni mtu ambaye anatambua ukuu wa Mungu na wala siyo ukuu wake yeye mwenyewe; mnyenyekevu ni mtu anayetambua kuwa ana mapungufu/udhaifu mbele ya Mungu, mnyenyekevu ni mtu anayetambua kuwa watu wengine wana nafasi/mchango wao katika maisha licha ya hali zao za maisha. Unyenyekevu huu ndiyo kigezo cha kuirithi mbingu. Kadhalika, Yesu aligundua kuwa mwenyeji wao (mwalikaji) amealika tu wale wa hadhi/aina yake (matajiri/marafiki zake tu n.k) akijua kuwa kwa namna moja au nyingine watamlipa tu (labda siku nyingine nao wataandaa sherehe/chakula na kumwalika pia au watamsaidia akiwa na shida).

Ekaristi Takatifu ni Karamu ya maisha ya uzima wa milele.
Ekaristi Takatifu ni Karamu ya maisha ya uzima wa milele.

Hii ndiyo sababu Yesu anasema, “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.” Yesu hataki tufanye mambo ili baadaye tupate malipo. Yesu anataka tuwatendee mema hata wale ambao twawaona kuwa hawana thamani wala hawana cha kutulipa. Hiki ni kigezo cha kuingia mbinguni: kutenda wema kwa watu wote bila kuweka mbele maslahi binafsi. Somo la Injili linatuhusu na sisi pia kwani tunayo pia mapungufu mawili aliyoyagundua Yesu alipoalikwa chakula: Kwanza, wengi wetu tunafikiri kuwa sisi ni bora zaidi kiroho na hivyo tunastahili kuingia mbinguni (kukaa viti vya mbele) na kuwaona wengine hawafai. Wengine tunajikweza katika maisha ya kiroho: bila mimi Jumuiya/Kigango/Parokia itakufa. Wengine tunapenda kujitukuza, kuabudiwa, kusifiwa, kujionesha na hata kutafuta umaarufu kwa kuwaangamiza/kuwachafua wengine. Huku ni kukosa unyenyekevu. Mt. Augustino anatupatia ushauri mzito kuhusu unyenyekevu/kujishusha akisema, “Je, unataka kupanda? Basi anza kwa kushuka.” Tena Waraka wa Mtume Yakobo kwa watu wote unatuambia kuwa, “Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza” (4:10); Pili, tunapenda kushirikiana/kufanya kazi na wale tu wenye uwezo au wale walio marafiki/ndugu zetu. Hii ni dhambi ya ubaguzi. Mara nyingi huwa hatuwafikirii watu wa kawaida katika utendaji wetu wa kila siku kwa sababu tunawaona kana kwamba hawana thamani au hawana cha kutulipa. Ni mara ngapi watu wenye uwezo wanafanya sherehe na kualika tu wale wenye uwezo? Mara ngapi watu wenye uwezo wanatoa visingizio vya kutohudhuria Jumuiya ikiwa wanasalia kwa mtu maskini? Ni mara ngapi tunafanya kazi na marafiki/ndugu zetu tu? Mara ngapi tunashirikiana kwa misingi ya ukabila au mahali tutokapo? Tafakari, fanya toba na wongofu wa ndani. Dominika Njema

26 August 2022, 14:18