Tafakari Dominika 22 ya Mwaka C wa Kanisa: Upendo, Unyoofu Na Unyenyekevu Katika Huduma
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! “Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana.” Katika nyakati za Yesu na hata leo hii katika dini ya Kiyahudi mlo wa mchana wa siku ya sabato ulijumuisha ndugu, jamaa, na marafiki, na pia ni fursa muhimu, si tu ya kula pamoja bali pia kuendelea kuwa na wasaa wa kujadili juu ya Neno la Mungu walilolisikia katika Sinagogi, na hata pia kujadili mambo mbali mbali kama vile ya kijamii, kisiasa na hata masuala ya kifamilia. Ilikuwa ni fursa adhimu kabisa pale ambapo kati yao alikuwepo Rabi kuweza kujadili haswa maswali ya kidini, kiteolojia na hata kimaadili. Hivyo mafarisayo, waandishi na viongozi wa kidini walitumia fursa hizo kuweza kuwafundisha zaidi masuala ya kiimani wanapokuwa mezani. Na hata Yesu mara kadhaa alitumia fursa hizo za kuwa mezani kuweza kutoa mafundisho yake katika siku za sabato na hata nyakati nyingine. Na mezani pia si tu walikaa bila mpangilio, bali kulikuwa na sheria na taratibu zake za kuketi, hivyo mwenyeji aliketi katikati au sehemu ambayo angeweza kuhudumiwa kirahisi na kwa nafasi ya kwanza na pembeni yake waliketi wageni waalikwa mashuhuri na wengine waliketi pia kwa kadiri ya nyadhifa zao na umri wao. Meza iliakisi pia nafasi na wadhifa wa kila mshiriki katika mlo. Ni katika muktadha huo wa kuketi mezani kadiri ya wadhifa wa kila mwalikwa, ndio Yesu anatumia fursa hii kutupa mafundisho yake katika Dominika ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa Lk 14:1, 7-14.
Mwinjili Luka hazungumzii juu na jinsi ya kuketi tunapoalikwa kwenye sherehe au mezani, bali anatumia wasaa huu kuiasa jumuiya ya Wakristo aliyokuwa anawaandikia na hata jumuiya zetu leo ya namna ya jinsi ya kuenenda katika maisha yetu ya siku kwa siku. Yesu Kristo daima anawaonya wafuasi wake kutokujikweza au kujichukulia nafasi za heshima, na hivyo Injili ya leo haina lengo la kututaka tuchukue nafasi za mwisho ili tukwezwe na kupewa nafasi za heshima, ila lengo lake ni kutualika kubadili mtazamo wetu kama Wakristo. Ni kuwa na mtazamo mpya wa kuwa watumishi na wadogo kama vile Yesu Kristo mwenyewe alivyokuwa mtumishi wetu. Na ndio mwaliko ambao anatupatia Baba Mtakatifu Francisko wa kuishi kama Kanisa Kisinodi ambalo sasa maadhimisho yake yanaingia awamu ya pili ambapo kila mwamini mbatizwa anaalikwa kudumisha: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Hili Ndilo Kanisa linalosafiri na kutembea kwa pamoja kwa umoja na upendo, huku kila mmoja akitambua umuhimu wa mwingine hata anayekuwa mdogo au maskini kiasi gani. Kila mmoja ni kiungo hai katika kuujenga Mwili Fumbo wa Kristo, yaani Kanisa la Yesu Kristo kama jumuiya na familia ya watu wa Mungu.
Yesu Kristo leo, pamoja na kwamba ni mualikwa lakini haongei kama mualikwa bali kama mualika na hapo ndio tunaweza kupata ujumbe kusudiwa wa Injili ya leo. Ni Yesu anayetualika sote katika kuunda mwili fumbo wake yaani Kanisa, jumuiya ya waamini, sisi sote bila kujali nafasi au wadhifa tu waalikwa na kamwe asitokee mmoja wetu kujichukulia nafasi ya kuwa mualikaji. Ni wito wa kuenenda na kutembea kama Kanisa la Kisinodi, yaani kutembea pamoja katika ushirika, ushiriki na umisionari wa misheni ya Injili. Ni kwa kuwa na mtazamo huo tu hapo mashindano na mapambano yanayotokea katika jumuiya zetu tunaweza kuyaepuka, kwani kila mmoja wetu hana budi kujiona ni mualikwa. Mathalani kuwa Askofu au kasisi, au shemasi au mtawa au katekista mlei au kiongozi mlei wa jumuiya zetu, ni kwa kuwa na mtazamo sahihi kama anavyotutaka Yesu katika Injili, leo tunaweza kutambua zote ni nafasi za huduma na utumishi na udogo na kuwa wa mwisho na kamwe sio fursa za kuwa mabwana wakubwa na waheshimiwa au watawala wa wengine. Nafasi mbalimbali tunazokuwa nazo ni kwa ajili ya kuwahudumia wengine kwa upendo mkubwa na si vinginevyo. Nafasi za mbali mbali za utume wa utumishi kamwe tusiingie katika kishawishi cha kuwa watawala wa wengine wanaokuwa katika uangalizi wa huduma zetu mbali mbali. Ni mwaliko wa kuwa watumishi na wenye kuongozwa na upendo wa Kristo mwenyewe na kamwe sio kwa sifa na utukufu binafsi.
Leo hii naomba nikiri hata kati yetu wadarajiwa kumekuwa na mapambano, na chuki, na hata magomvi kwa kukosa kuielewa na kuiishi Injili ya Yesu Kristo, kwani badala ya kuona nafasi zetu ni katika kuwa watumishi na wadogo mara nyingi zimekuwa chanzo cha kujikweza na kujitafutia heshima na matajamala ya pekee na binafsi. Yesu Kristo anatualika kubadili vichwa vyetu kwani aliye mkubwa ni yule anayekuwa mtumishi kama yeye, na hivyo kujifunga na kutumikia wengine na si kusubiri kupata heshima, masilahi binafsi na sifa kama mantiki ya ulimwengu huu. Baada ya Yesu kuwahubiria walioalikwa sasa anamgeukia mfarisayo aliyewaalika na kumtaka pia kubadili mtazamo wake. Ilikuwa ni desturi na kawaida si tu katika nyakati za Yesu bali hata katika nyakati zetu leo kuwaalika watu wa hadhi yetu, watu wanaoweza nao kutualika kesho au keshokutwa. Yesu anamwalika kuwageukia watu wanaosetwa na kudharaulika na kutengwa na ndio maskini, walemavu, vipofu na viwete. Ni kuwaalika wale wasiokuwa na kitu cha kutulipa. Ni kuwaalika kama Mungu anavyotualika kwani hakuna hata mmoja wetu hata awe tajiri au mwenye uwezo kiasi gani wa kuweza kumlipa Mungu. Ni kualika bila kutarajia chochote na ndio upendo wa Kimungu tunaopaswa kuwa nao, upendo usio na masharti wala kujitafutia faida yake wenyewe.
Kwa Wayahudi aina ya watu kama viwete, vipofu, walemavu hawakuruhusiwa hata kuingia Hekaluni pale Yerusalemu, hivyo Yesu anawaalika kubadili vichwa vyao kwa maana ya mtazamo wao wa kufikiri na kutenda. Labda hata leo tunapokuwa na sherehe zetu iwe katika ngazi ya familia zetu mara nyingi wanaingia ukumbini wale tu waliochangia, bahati mbaya hiyo ipo hata katika makusanyiko na sherehe za Kanisa. Mara ngapi katika sherehe zetu za upadrisho au uaskofusho au jumuiya ndogo ndogo za Kikriso au Kiparokia tunawakumbuka wahitaji au watu wenye dhiki na kushiriki nao meza ya sherehe? Naomba nisitoe jibu wala hukumu ila tuingie ndani mwetu na kujihoji ni mara ngapi tunawajali na kuwakumbuka maskini au watu wenye mahitaji maalumu katika mikusanyiko ya sherehe zetu? Lakini pia maskini, vipofu, viwete na walemavu si tu watu wenye shida na ulemavu wa kimwili bali pia wale wenye shida za kiroho, watu wanaokuwa mbali au kujisikia mbali na Mungu, je ni mara ngapi tumewapa nafasi hawa na kujisikia kuwa Mungu anawapenda na kuwaalika washiriki naye karamuni? Ni kwa jinsi gani kama jumuiya ya waamini tumewaweka karibu wanaokuwa mbali na Mungu? Ni mara ngapi tumekuwa wakali na kuwatenga na hata kuwafungia huduma na masakramenti ya Kanisa badala ya kuona namna za kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usio na mipaka wala kipimo? Ni maswali yakututafakarisha katika Dominika yetu hii ya leo. Yesu leo anatualika kupenda bila masharti, kupenda kama vile Mungu anavyotupenda bila kutubagua, Mungu anatupenda sote iwe tuwe wema au wadhambi bila upendeleo wowote. Upendo wa Mungu sio kutuacha katika uduni na hali ya kupotea bali sote tuweze kuonja huruma yake ya Kimungu, na hapo ndio kuufikia wokovu wetu. Tafakari na Dominika njema.