Haki Msingi Za Binadamu: Utu, Heshima, Ustawi, Maendeleo na Mafao ya Wengi Ni Muhimu Sana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtakatifu Mkuu wa Pili wa Vatican katika “Tamko juu ya uhuru wa dini, Haki ya mtu binafsi na ya jumuiya ya kuwa na uhuru wa kijamii na wa kiserikali katika masuala ya dini” wanatangangaza (declarat) kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubaliwa kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Aidha Mtaguso unatangaza kwamba haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Ni kutokana na hadhi yao kwamba watu wote, kwa sababu wao ni binadamu, yaani wamejaliwa kipaji cha akili na utashi na hivyo wanao wajibu binafsi, wanasukumwa na maumbile yao na kanuni za kimaadili kuutafuta ukweli, hasa unaohusu dini. Wanasukumwa pia kuambatana na ukweli, baada ya kuujua, na kuyaelekeza maisha yao yote kwenye matakwa ya ukweli. Lakini binadamu hawawezi kuitimiliza kanuni hii katika njia inavyodaiwa na maumbile yao, wasipopata uhuru wa ndani na kinga dhidi ya mashurutisho ya nje. Kwa hiyo haki ya uhuru wa dini, msingi wake si katika hisia za mtu binafsi (subiectiva personae dispositione), bali katika maumbile yake yenyewe (in ipsa eius natura). Kwa sababu hii, haki ya kinga hiyo hudumu hata kwa wale ambao hawalitimizi sharti la kutafuta ukweli na kuambatana nao. Utekelezaji wa haki hii hauwezi kuzuiwa iwapo hauleti ghasia katika jamii. Rej Dignitatis humanae, 2.
Haki Msingi za Binadamu zinatambuliwa ulimwenguni kote. Kilichoisukuma Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kunakuwa na mifumo thabiti ya Ulinzi wa Haki za Binadamu ni mateso, uhalifu na majanga makubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu uliofanyika wakati wa mapambano ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliyoanza kutimua vumbi tarehe 1 Septemba, 1939 na kumalizika tarehe 2 Septemba, 1945. Ni vita iliyo shuhudia ukatili na unyama wa hali ya juu unaoweza kufanywa na mwanadamu dhidi ya mwanadamu mwingine, hususan yule aliye dhaifu kimamlaka, kinguvu, kiuchumi, kisiasa, nk. Kwa hiyo, tarehe 10 Desemba 1948 Mataifa zaidi ya 50 chini ya Umoja wa Mataifa yalikutana na kutengeneza Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki Msingi za Binadamu. Tamko linakazia kuhusu: Utu na heshima ya binadamu: kiroho na kimwili na kwamba, kila raia anayo dhamana na wajibu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa na kuwa, utu na heshima yake, vinapaswa kuendelezwa katika ukamilifu wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutokana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, hapa kila mtu anapaswa kutambua kwamba, anawajibika kuchangia kwa ujasiri, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu zinazomwilishwa katika Matendo ya huruma: kiroho na kimwili; hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Haki na mshikamano ni dhamana ya kimaadili ambayo Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuimwilisha katika maisha na utume wao; kwa kuendeleza wema na huruma, ili kuwapunguzia mateso na mahangaiko wale wote waliovunjika na kukata tamaa ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na kitaifa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu na ushirikiano wa kimataifa na hata pale, itakapowabidi kwenda kinyume cha mkondo wa bahari! Hii ni fursa ya kuamsha dhamiri nyofu na kuendelea kujikita katika kulinda, kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu! Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Askofu mkuu Fortunatus Nwachwuku, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yaliyoko mjini Geneva, Uswis, amechangia kwenye Mkutano wa 51 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki Msingi za binadamu: Maji na Afya Bora; haki ya maendeleo inayosimikwa katika mshikamano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; amegusia kuhusu vita ya Urussi dhidi ya Ukraine pamoja na haki za wazee. Jumuiya ya Kimataifa lazima isimame kidete kulinda vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi.
Dhana ya maji safi na salama kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake! Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu! Jumuiya ya Kimataifa ina deni kubwa kwa maskini, ili kuhakikisha kwamba, hata wao wanapata maji safi na salama kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kama binadamu. Askofu mkuu Fortunatus Nwachwuku anasema, watu wana haki ya kupata maendeleo fungamani ya binadamu, yanayozingatia na kuheshimu: utu, ustawi na mafao ya wengi. Haki hii inasimikwa katika msingi wa mafao ya wengi na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Anasema, vita, kinzani na mipasuko sehemu mbalimbali ya dunia imepelekea wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna watu wengi ambao maisha yao yako hatarini.
Ni hatari sana, kusimika dhana ya ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa katika nguvu za kijeshi. Jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na uhuru unaowawajibisha wote. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amesikitika kusema kwamba, kuna wazee ambao wamesahaulika na kutelekezwa kama “magari mabovu” kutokana na mifumo mbalimbali ya ukoloni wa kiitikadi kuendelea kushambulia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Leo hii kuna wazee ambao wamefungwa gerezani kutokana na sababu mbalimbali, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, wananyimwa haki zao msingi zinazobubujika kutoka katika utu na heshima yao kama binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuangalia sheria, taratibu na kanuni zitakazosaidia kuhakikisha kwamba, haki msingi za wazee zinalindwa na kudumishwa. Wazee wapewe mahali maalum pa kutunzwa; walindwe dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa na hivyo kuondokana na utandawazi usiojali wala kuheshimu: utu, heshima na haki msingi za binadamu, hata kama bado wako kifungoni.