Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Injili ya Baba Mwenye huruma, upendo na saburi. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Injili ya Baba Mwenye huruma, upendo na saburi. 

Injili ya Baba Mwenye Huruma na Mwana Mpotevu! Huruma, Upendo na Uvumilivu wa Baba wa Milele

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Ni hapo tunaonja juu ya upendo, wema, huruma na uvumilivu wa Mungu usio na mipaka kwa wanadamu. Mwana mdogo anaomba kwa baba yake sehemu ya urithi inayomwangukia, haoni tena thamani ya mahusiano na baba yake, anamhesabu baba yake sawa na mfu, kwani anachoona kilichobaki kwa baba yake ni mali za urithi.

Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Ni simulizi linalokuja mbele yetu lenye kutuonesha sura halisi ya Mungu. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Ni hapo tunaonja juu ya upendo, wema, huruma na uvumilivu wa Mungu usio na mipaka wala kipimo kwetu wanadamu. Mwana mdogo anaomba kwa baba yake sehemu ya urithi inayomwangukia. Ndio kusema mwana mdogo haoni tena thamani ya mahusiano na baba yake, anamhesabu baba yake sawa na mfu, kwani anachoona kilichobaki kwa baba yake ni mali za urithi. Kwake baba yake hana thamani tena zaidi ya mali anayohitaji ili atoke na kwenda zake. Baba kwake ni mmoja anayembana kuishi uhuru wake, hivyo si tu anachukua sehemu ya urithi wake bali anajitenga na kwenda mbali naye. Hakika mali na vyote tunavyoweza kuwa navyo ni mali ya Mungu. Na hata uhuru wetu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa kuwa Mungu ni upendo, basi daima anaheshimu uhuru wa mwanadamu, kwani upendo huvumilia yote! Mwana mdogo anaenda nchi ya mbali na baba yake. Ni mwanadamu anayejiweka mbali na Mungu muumba wetu. Dhambi ni kujitenga na Mungu, ni kutumia mali na vyote anavyotujalia sio tena kadiri ya mapenzi yake bali kadiri ya mantiki na akili zetu. Kuacha kuongozwa na Neno lake na kufuata matakwa na tamaa zetu za kibinadamu. Mali, vitu, anasa na mambo ya namna hiyo vinaisha, sio vitu vya kudumu, na ndio tabia na silka ya dhambi, inadanganya, haitupi furaha na amani ya kudumu kama inavyoonekana mwanzoni. Pesa, mali, starehe, mamlaka na madaraka, umaarufu, na vingine vingi ni vitu vya kupita katika maisha, havitupi uhakika wa maisha yenye furaha na amani ya kweli. Akiwa nchi ile ya mbali, anatapanya mali zake zote na njaa kuu iliingia nchi ile. Ndio kusema kila tunapojitenga na Mungu na kwenda mbali naye, hapo tunaingia katika maisha yasiyo tena na ladha ya furaha na amani ya kweli. Maisha yanakuwa ya dhiki na shida kubwa kwani bila Mungu hatuwezi kitu. Bila Mungu tunabaki wakiwa na yatima na wenye dhiki kuu.

Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.
Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

Mwana yule mdogo si tu anapitia shida na dhiki kuu, bali kwa Myahudi kuishia kulisha nguruwe ni jambo lisiloweza kueleweka wala kuvumilika. Ni kinyume na dini na imani yao. Hivyo, hayo ni matunda na matokeo ya kuishi mbali na baba yake, ni kwenda na kuishi nchi ya wapagani naye kuenenda sawa na wapagani. Ni hali inayokuwa duni zaidi kufikirika kwa Myahudi ni kuishi upagani kiasi hata cha kula pamoja na nguruwe. Ni hapo tunaona mwana mdogo anafikiri moyoni mwake na kuukumbuka wema na upendo wa baba yake, na kufanya maamuzi magumu ya kurudi nyumbani na kuomba msamaha. Na kutaka asihesabiwe tena kama mwana, maana kadiri ya yeye alishavunja mahusiano ya baba na mwana kwa kuomba apewe sehemu ya urithi inayomwangukia. Anajishudha hadhi kwa kujiadhibu, kwani sasa anaona awe sawa na mtumwa au mtumishi wa baba yake. Cha kushangaza akiwa bado njiani, baba anamwona akiwa bado mbali, ndio kusema upendo unavuka mipaka ya kijiografia na muda. Upendo haundoki kwa sababu ya umbali, na ndio kusema huyu mwana mdogo pamoja na historia ile mbaya aliendelea kubaki ni mwana wake, hata kama mwana alivunja mahusiano na baba yake.  Baba anamwona na kumkimbilia na kumwangukia shingoni na kumbusu sana. Upendo unaona mbali na kutubusu hata kama tukatika hali ya uchafu na kunuka kiasi gani!  Ni hapa hatuoni baba akihesabu au kumkumbusha juu ya makosa aliyofanya, lakini mara moja anamrejeshea ile hadhi aliyoivunja yeye mwenyewe, kwa kumstahilisha kama mwana na tena mwana mpendwa sana. Ajabu juu ya wema na upendo wa huyu baba! Hatuwezi kuuelezea wema na huruma ya huyu baba mpaka pale nasi tunapoukimbilia wema na huruma ya Mungu katika maisha yetu.

Wema, huruma na upendo wa Mungu hauna mipaka.
Wema, huruma na upendo wa Mungu hauna mipaka.

Yeye asiyependa hajamjua Mungu bado. (1 Yohane 4:8). Mwana mkubwa anaingia mara moja, yule ambaye alibaki nyumbani na baba miaka yote, yule ambaye aliendelea kutumika nyumbani akiwa jirani au karibu au katika ushirika na baba yake. Ni huyu ambaye kwa haraka haraka tungeweza kusema ndio mwana na mtoto mwema kuzidi ndugu yake mdogo. Hapa tunaonja kuwa hata mwana mkubwa, hakuwa na mahusiano mema na sahihi na baba yake na ndugu yake mdogo. Hata naye mtazamo wake ni ule ule kama wa ndugu mdogo pale awali, kwani kwake baba ni mali, ni vitu na baada ya ndugu mdogo kuchukua sehemu inayomwangukia, basi vyote vinavyobaki sasa ni mali yake peke yake. Moyo wake umejaa vitu na mali na sio tena mahusiano na baba wala ndugu yake mdogo. Na ndio hali inayoweza kuwa ndani mwetu. Kutaka mema yote yawe yetu katika maisha ya siku kwa siku, na hivyo kujawa na chuki na wivu dhidi ya wengine.  Wivu sio upendo uliokithiri bali ni ukosefu wa upendo! Haitoshi kuwa karibu na baba bali lazima kuuvaa moyo wa baba na ndio mwaliko kwetu kuwa wema na wenye huruma kama Mungu alivyo! Ni baba peke yake katika simulizi hili anayebaki na mahusiano ya upendo wa kweli kwa wana wake wote wawili, upendo na huruma. Na hi indio sura halisi ya Mungu kwetu, sura ya upendo na huruma kwa kila mmoja wetu. Na ndio fundisho kuu katika masimulizi haya matatu ya somo la Injili ya Dominika ya leo.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na saburi.
Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na saburi.

Mtakatifu Francisko wa Assis akiwa katika kijiji cha La Verna, mara nyingi akiwa anasali mbele ya Msalaba, alionekana akilia na kutokwa na machozi huku akitamka maneno haya: “Upendo haupendwi!” Kwake anauonja na kuuona upendo wa Mungu pale Msalabani, unaotualika nasi kuupenda kwani asiyependa hamjui Mungu! Ni mara ngapi nasi tumewaka moto wa upendo ndani mwetu kwa Mungu na kwa jirani? Hatusali au hatuendi kanisani kwa kuwa tunahitaji muujiza fulani katika maisha yetu, bali iwe ni kwa sababu tunampenda kweli Mungu na jirani. Sala ni mahusiano ya upendo kwa Mungu kwa nafasi ya kwanza, ni kuingia katika na kuuonja upendo na huruma ya Mungu kwetu. Ni mara ngapi tunauangalia Msalaba na kuwa na tafakari ya kina kuwa hapo ni upendo na huruma na msamaha wa Mungu kwetu wadhambi? Msalaba ni upendo na huruma ya Mungu kwetu wadhambi na wakosefu. Tusali na kumuomba Mungu ili daima nasi tudumu wenye mahusiano mema na sahihi naye na ndugu zetu. Mahusiano ya upendo na huruma, mahusiano ya Mungu aliye muumbaji na mgawaji wa mema yote kwetu, lakini kutumia mema yote sio kadiri ya mpango na mapenzi yetu bali kadiri ya mapenzi yake aliyetuumba. Nawatakia tafakuri na Dominika njema!

10 September 2022, 14:55