Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan: Mchango wa Wanawake
Na Rais Samia Suluhu Hassan, Dar es Salaam, Tanzania.
Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kilikuwa ni hapo Dominika tarehe 11 Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam kwa Ibada ya Misa Takatifu, ambayo imeongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hotuba yake, amewapongeza WAWATA katika sera na mikakati ya kuwakomboa wanawake kiuchumi; karama na wito wa WAWATA; maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele sanjari na ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho haya yamekuwa na sura ya kiekumene, kidini na kitamaduni, kwa kuwashirikisha wawakilishi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, matendo makuu ya Mungu.
UTANGULIZI: Ninatambua kwamba WAWATA ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wote Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. WAWATA inajishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika Kanisa; na pia waweze kujiendeleza wao wenyewe katika familia na kuchangia katika pato la Taifa kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na haya yote yanaongozwa na dhamira yenu kuu: Kutumikia na Kuwajibika. Umoja wenu huu pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO)-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu huko nchini Ufaransa. Kumbe kupitia WAWATA mnashiriki katika kutunga sera na mikakati ya kuwakomboa Wanawake kiuchumi katika ngazi za Kimataifa. Haya yamejidhihirisha katika kazi zenu na mikono mlizoonesha na pia vipaumbele mlivyoainisha katika risala yenu ambavyo ni pamoja na: Malezi ya familia na kuwajali wenye mahitaji maalum bila kujali imani zao, na hapa mmezungumzia wafungwa magerezani, wagonjwa mahosipitalini, vituo vya kulelea Watoto yatima, wazee na kadha wa kadha.
Kutoa elimu ya mazingira na kutenga siku moja kila mwaka ambayo ni maalum kwa ajili ya kusafisha mazingira yanayowazunguka pamoja na kupanda miti. Kuwaandaa vijana kushiriki siasa na kuwahamasisha WAWATA kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kushiriki katika kutunga sera na sheria za nchi. Nimefarijika kusikia kuwa hata katika safu yenu ya uongozi wa WAWATA majimboni wapo madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa. Kuwajengea WAWATA uwezo na kuwaweka pamoja katika vikundi vya kuweka na kukopa ili wapate mtaji wa biashara ndogo ndogo za Kiuchumi; na sasa mna wazo la kwenda mbali zaidi na kuanzisha Microfinance ya WAWATA, hongereni sana. Kutoa elimu dhidi ya ulinzi wa Mtoto kwa kushirikiana na Serikali. Pamoja na mikakati hii mizuri mnashirikiana pia na madhehebu mengine kama UWAMAKDA – yaani Umoja wa Makanisa ya Dar es Salaam na pia TWIN – Tanzania Women Interfaith Network katika kutafuta suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo akina mama bila kujali Imani zao za dini. Hili ni jambo jema kwani siku zote tunatambua umoja unaleta matunda chanya na ya haraka zaidi.
KARAMA NA WITO WA WAWATA: Kwa kuzingatia karama na wito wa maisha katika Jumuiya yenu, mnaweza kuisaidia Serikali kushughulikia maridhiano katika familia, kushawishi ustahimilivu miongoni mwa wanajamii, kupendekeza mabadiliko katika Taifa letu kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni; na kwa kuyashughulikia hayo mtaweza kuonesha njia ya kupyaisha Taifa letu katika kuzingatia Dira ya Maendeleo ya 2025, Malengo ya “Afrika Tunayoitaka” ya 2063, na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030. Nimesikia katika risala yenu kuwa mmekuwa na mkakati endelevu wa utunzaji wa mazingira kila mwaka kuanzia mwaka 2018, na kuwa wakati mnaazindua Jubilei yenu Julai 2021 mlijiwekea lengo la kupanda miti 34,000 lakini mmevuka lengo na kuweza kupanda miti 530,416. Hongereni sana. Suala la Mazingira ambayo ni nyumba yetu sote, ni jambo ambalo Serikali yangu inalipa kipaumbele. Inapendeza kuona WAWATA mmelipa uzito wa kutosha na mnaendelea kutoa elimu kwa watoto wetu ili nao wakue wakitambua umuhimu wa kutunza mazingira nyumba ya wote.
MAENEO YANAYOHITAJI KUHIMIZWA: Kuna maeneo kadhaa ambayo yanahitaji kuhimizwa sana katika jamii yetu leo hii; na yahimizwe sana kwa kushawishi na kwa vitendo yapewe kipaumbele. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo: Malezi yenye uhakika wa ubora kijamii na kimaadili ya watoto na vijana. Elimu ya uongozi kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa kujikubali, kujiamini na kuwa na ujasiri wa kuthubutu kukabiliana na changamoto mbalimbali. Kushiriki kikamilifu katika shughuli na miradi mwafaka ya kiuchumi yenye tija na ufanisi kwa maisha ya familia. Kuanisha dhana halisi na ya kweli inayohusu maswala ya siasa, kwa kuzingatia ushiriki wa wananchi katika hatua zote zinazohusu uandaaji sera na katika kupata viongozi wa kisiasa wanawake ambao wanastahili. Kuendelea kutoa elimu kwa vijana juu ya matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano.
UTAFITI KATIKA KUOANISHA UTUME WENU NA SERA ZA NCHI: Jumuiya yenu inaweza kusaidia sana kufanya utafiti wenye mlengo wa kijinsia ili utume wenu utambulike katika jamii kwamba ni utume mwafaka kwa jamii, na unachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kweli ya kibindamu kwa raia wote wa Tanzania. USHIRIKIANO NA SERIKALI: Kama taasisi ya kijamii pia, Serikali inatarajia kuwa WAWATA itatoa ushirikiano mwafaka kama ambavyo imejitahidi kufanya katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Hiyo ina maanisha kwamba, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa katika historia ya nchi yetu, WAWATA mtatoa ushirikiano unaoongeza thamani katika uongozi wa nchi, uchumi wake na ustawi wake ambao ni mwafaka kwa hadhi na utu wa mwanadamu. Serikali ingependa WAWATA itumie karama zake kama wanawake na wazazi katika maswala ya kifamilia, ulinzi wa mtoto, malezi kamilifu na himilivu ya vijana, maswala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume na wanawake, na pia kwa wahitaji hasa wazee, wafungwa na Watoto yatima. Serikali iko tayari kusikiliza na kutoa msaada kwenu katika jitihada za maswala haya katika mipango na utekelezaji wenu.
TAMATI: Napenda kumalizia kwa kuwatakia WAWATA maadhimisho mema yenye furaha ya kweli, yenye matarajio ya baraka tele za Mwenyezi Mungu. Naamini katika miaka mingine hamsini, chini ya uongozi wa Kanisa lenu na kwa ushirikiano na Serikali mtaweza kutufikisha mahali ambapo tumetoka kwenye dhana ya usawa wa jinsia na tumefika kwenye mkamilishano wa kijinsia, na kwamba jambo la kuwa na Rais mwanamke litakuwa la kawaida; na mwisho lakini pia muhimu sana kwamba Tanzania yetu itakuwa ni jamii inayoishi utamaduni wa kijani katika kuhusisha maisha yake na utunzaji endelevu wa Tanzania kama bustani aliyotujalia Mwenyezi Mungu.