Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: Risala Kwa Rais Samia S. Hassan
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar es Salaam, Tanzania.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani; kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuomba tena neema na baraka za kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa.WAWATA katika risala yao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wameelezea historia ya WAWATA, Malengo ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA, Ombi kwa Serikali kuhakikisha kwamba, watanzania wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula kutokana na tishio la njaa kwa sasa pamoja na Bima ya afya ambayo ni nafuu kwa wengi.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan; pamoja na Viongozi wote wa Serikali ulioambatana nao katika hafla hii. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu wa Jimbo kuu Katoliki Mbeya. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Askofu Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei Katoliki Tanzania na Askofu wa Jimbo la Singida. Wahashamu Maaskofu Wakuu, Maaskofu; Viongozi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume wa kike na kiume, Mapadre pamoja na wakurugenzi wa Majimbo. Mheshimiwa Bi Winnie Muthiga - Mjumbe wa Kenya kweye Bodi ya Wanawake wakatoliki Duniani (WUCWO) na Bi Anastacia Musyimi Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kenya mkimwakilisha Rais wa WUCWO Bi Maria Lia Zervino Sevidora. Waasisi wa WAWATA, na kwa namna ya Pekee Bi Crecensia Jahari – Mtunza hazina wa Kwanza wa WAWATA. Viongozi wa Halmashairi ya Walei Taifa na Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Viongozi wa vyama vya kitume. Bi Shamim Khan – Mwenyekiti JUWAKITA, Bi Grace Mtawali, Mwenyekiti UWAMAKDA, Bi Amina Salum Khalfan Mwenyekiti JUWAKIZA Zanzibar. Wageni waalikwa – Mabibi na Mabwana – Miaka 50 ya WAWATA: Umoja, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.
SHUKRANI: Mheshimiwa Rais, Sisi Wanawake Watoliki Tanzania tunakushuru sana kwa kutenga muda katika ratiba yako ngumu kushiriki nasi siku hii muhimu. Tunapenda kukupongeza kwa uongozi mathubuti. Tunakupongeza wewe binafsi pamoja na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Mama WAWATA mwenzetu Mheshimiwa Bibi Anne Makinda kwa kazi kubwa inayoendelea ya sensa ya watu na makazi. Tunakuombea afya njema ya mwili na roho katika kutekeleza majukumu yako kama Rais na Mama wa familia.
WAWATA NI NINI: Mheshimiwa Rais, WAWATA ni Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 umekuwa na jukumu la kuwaweka Wanawake pamoja ili kutatua changamoto wanazokumbana nazo kila siku katika kulea familia. Tunashirikiana na Kanisa kutoa elimu ya kiroho ili kujenga familia yenye maadili na hivyo Taifa lenye uwajibikani. Tunatoa pia elimu ya kumsaidia mama kufanya shughuli za kiuchumi kuchangia pato la familia na Taifa. Tiketi ya kuwa mwanachama ni kuzaliwa na kubatizwa katika Kanisa Katoliki. Hakuna kiingilio wala ada ili kuwa mwanachama, hivyo tunawatambua Wanawake Wakatoliki kuanzia ngazi ya Jumuiya –tunaweza kusema ngazi ya shina. WAWATA pia inaunda wanachama wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO; hivyo tunashiriki kikamilifu katika kutunga sera na kupendekeza vipaumbele kwa vipindi vya miaka minne minne. WAWATA tumekuwa tukishirikiana na madhebebu mengine katika kushirikishana changamoto za akina mama kupitia umoja wa UWAMAKDA na TWIN hasa kujadili mambo yanayohusu haki na amani.
MALENGO YA JUBILEI: Mheshimiwa Rais, tulipofanya uzinduzi wa Jubilee tarehe 25 Julai 2022, tulijiwekea malengo ambayo ni pamoja na: Malezi ya familia na kuwajali wenye mahitaji maalum bila kujali Imani zao. Tuliwatembelea wafungwa magerezani, wagonjwa mahosipitalini, vituo vya kulelea Watoto yatima, wazee na kuwapa zawadi. Tulitoa elimu ya mazingira ili kuijali nyumba ya wote sawasawa na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Katika kipindi cha mwaka mmoja tulijiwekea lengo la kupanda miti 34,000 lakini kwa takwimu za Juni 2022 tumepanda miti 530, 416 na tunaendelea. Tumetoa elimu kwa vijana (WAWATA chipukizi) pamoja na WAWATA na kuwahimiza kuwania nafasi za uongoizi katika siasa. Tumetoa elimu ya ujasiriamali – kama ulivyoona kwenye maonyesho yetu. Tulitoa elimu dhidi ya ulinzi wa Mtoto kwa kushirikiana na Serikali.
Napenda kutoa Shukrani za dhati kwako Mheshimiwa Rais kwa kuwepo kwa Dawati la Jinsia. Waliitikia kila mara tulipowaomba kuja kutoa elimu dhidi ya ulinzi wa mtoto. Kwa kushirikina na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, tulitoa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga, mafuno maalum kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa kujiwekea akiba lakini zaidi, umuhimu wa kila familia kuwa na BIMA ya AFYA. Tulikuwa na lengo la kujenga upya nyumba ya WAWATA iliyopo Ilala, hatukukamilisha lakini ramani iko tayari. Lengo ni kuwezesha WAWATA kujiendesha bila utegemezi. Tulikuwa na lengo la kuanzisha Microfinance ya WAWATA. Mradi wetu wa kukopesha tuliusitisha mwaka 2019 baada ya Benki kuu kutoa miongozo ya kufanya biashara ya fedha. Tumefanya vikao na Benki kuu na tupo katika hatua za kuandaa miongozo ili tuweze kusajili Microfinance. Lengo ni kuwapatia WANAWAKE mikopo midogo midogo ili waweze kuchangia kukuza na kuboresha uchumi wa familia, Kanisa na Taifa katika ujumla wake.
OMBI KWA SERIKALI: Mheshimiwa Rais, tunapofanya Jubilei ya miaka 50 tunaamini safari ndio kwanza imeanza ya kuimarisha umoja wetu na pia kujenga mahusiano bora zaidi na Wanawake wenzetu wenye dini na wasio na dini katika kutatua changamoto zinazomkabili mwanamke katika ulimwengu mamboleo. Tuna mambo mawili ambayo tunaiomba serikali yako tukufu itusaidie: Takwimu zisizo rasmi zinaonesha dalili ya kutokuwepo chakula cha kutosha mwaka huu 2022 hadi msimu ujao wa kilimo kutokana na mavuno hafifu katika msimu unaomalizika na hali ya hewa isiyokuwa rafiki. Tunatambua linapotokea baa la njaa, wanaoathirika zaidi ni Wanawake na Watoto! Tunaiomba serikali yako kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji na uhakika wa chakula na hivyo kutunusuru na athari za baa la njaa. Tunaipongeza serikali kwa juhudi kubwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha upatikanaji wa Bima nafuu ya Afya. Hata hivyo bado huduma hii haijawafikia wengi hasa wanawake ambao asilimia kubwa wanaishi vijijini. Bila kuwa na Bima ya afya uhakika wa kupata huduma za afya bado ni mdogo kwani wengi wetu tupo katika kundi la wale wasioweza kupata milo mitatu kwa siku na hivyo hatuna akiba kwa ajili ya dharura. Tunaiomba serikali yako tukufu kuona namna ya kuyasaidia makundi maalum kupata Bima nafuu ili kuwa na uhakika wa kupata huduma bora ya afya.
TAMATI: Napenda kumalizia kwa kukushuruku Mheshimiwa Rais kwa juhudi zinazofanywa na serikali yako kuleta maendeleo endelevu kwa Wananchi wa Tanzania. Tunakuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kushiriki shughuli za Maendeleo na vipaumbele vya Serikali katika kuifikia Tanzania tunayoitamani.