Maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.” Maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.”  

Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: Wosia Kwa Wanawake Wakatoliki

Askofu Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anasema, wosia ambao anapenda kuwapatia Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake ni kwamba, wawe ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Mfufuka inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani; kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuomba tena neema na baraka za kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anasema, wosia ambao anapenda kuwapatia Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake ni kwamba, wawe ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Mfufuka inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila anawataka WAWATA kamwe wasikate tamaa, kuvunjika wala kupondeka moyo wanapokabiliana na matatizo na changamoto katika maisha na watambue kwamba, kama wanawake, wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ndani na nje ya Tanzania. Katika kipindi cha miaka 50 ya WAWATA kwa hakika wametumikia na kuwajibika vyema katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania.

Askofu Msonganzila anawashukuru na kuwapongeza WAWATA: Ushuhuda
Askofu Msonganzila anawashukuru na kuwapongeza WAWATA: Ushuhuda

Askofu Msonganzila anapenda kuchukua fursa hii kuwatakia heri na baraka katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA hapo mwaka 1972. Swali chokonozi ni hili, Je, WAWATA katika Kipindi cha Miaka 50 wamechangia nini katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania na Ulimwengu katika ujumla wake! Kwa hakika WAWATA wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania, mfano bora wa kuigwa na vyama vingine vya Kitume. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuendelea kudumu katika kutangaza na kushuhudia imani, maisha adili na matakatifu yanayoshuhudiwa kila siku ya maisha yao. Waendelee kutekeleza wajibu na dhamana yao ya maisha ya kimama, kama walivyokuwa wale wanawake wa imani na watakatifu wanaosimuliwa katika Maandiko Matakatifu lakini zaidi akina Maria Magdalena na wenzake. Mtakatifu Maria Magdalena, yaani wa Magdala (Kwa lugha ya Kigiriki Μαρία ἡ Μαγδαληνή) ni mmoja kati ya wanafunzi maarufu zaidi wa Yesu wa Nazareti, hasa kutokana na sifa ya kuwa wa kwanza kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka. Rej.  Mk 16:9 na Yn 20:16.

Changamoto kubwa ni kuendelea kutafakari: Wito, utu, heshima, hadhi na haki msingi za wanawake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapenda kutambua ushiriki wao katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake kwenye ushuhuda wa imani sanjari na ukuu wa Fumbo la huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Wanawake wamekuwa ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni dhamana endelevu na fungamani inayojionesha kwa namna ya pekee katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaowaambata watu wote pasi na ubaguzi, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayowasindikiza waamini katika safari yao hapa duniani sanjari na kuwaonjesha maajabu ya Kazi ya Wokovu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Maria Magdalena ni mfano bora na Mwinjilishaji, aliyewashirikisha wengine furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu, kiini cha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha maisha na utume wa Kanisa katika ngazi mbalimbali za maisha. Mama Kanisa anapenda kuwashukuru na kuwapongezan wanawake wote kwa moyo na upendo wao wa kimama katika maisha na utume wa Kanisa.

Wosia kwa WAWATA: Mashuhuda wa imani, maadili na utu wema.
Wosia kwa WAWATA: Mashuhuda wa imani, maadili na utu wema.

Wanawake wanaalikwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wanawake waendelee kuwa ni mfano na kikolezo cha utakatifu wa maisha katika sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na katika majukumu ya kifamilia na kijamii. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila, anasema WAWATA wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Huu uwe ni utume wa pekee wanaopaswa kuutangaza na kuushuhudia. Wanawake katika Agano Jipya walipewa neema ya kuona na kushuhudia kaburi wazi. Hii ni changamoto ya kuishi na kuendelea kupyaisha imani na utume wao wa kimisionari, kwa kuamini na kufundisha kwamba: Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba, wao ni mashuhuda wa matukio haya makubwa yaliyoleta mageuzi makubwa ulimwenguni. Hii ni imani inayopaswa kwanza kabisa kutangazwa na kushuhudiwa kwenye kuta za familia, kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani” Koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia.” Hii ndiyo imani inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa na “Wanawake Wakomavu wa Imani” katika maeneo yao ya “kujidai” na katika jamii kwa ujumla wake. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila anakaza kusema, kamwe WAWATA wasiogope kuyatangaza na kuyashuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wao; wawe tayari kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazobubujika kutoka katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala.

WAWATA: Imani katika matendo
WAWATA: Imani katika matendo

WAWATA wasikate tamaa, kupondeka wala kuvunjika moyo kutokana na changamoto na matatizo mbali mbali yanayowaandama katika maisha na utume wao. Wawe na ujasiri na imani thabiti ili kukabiliana na changamoto na magumu yanayoweza kujitokeza katika maisha. Waendelee kujikita katika ushuhuda wa imani, maadili na utu wema. WAWATA watumike kama vyombo na mashuhuda wa Injili ya Upendo, kwa kuendelea kuadamana na Kristo Yesu katika njia yake ya Msalaba, tayari kusimama chini ya Msalaba kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na wale wanawake watakatifu, ili hatimaye kushuhudia kaburi wazi! Kwa njia hii WAWATA wataweza kuwajibika barabara katika majukumu yao kama wanawake na kama Wakristo wakomavu wa imani. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, anasema uwepo na ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni fursa kubwa ya kutambua kwamba, WAWATA wanayo nafasi adhimu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. WAWATA waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Yote haya yafanyikwe kwa sifa na utukufu wa Mungu kwa kuenzi na kuliadhimisha Kanisa nchini Tanzania.

Askofu Msonganzila WAWATA miaka 50
09 September 2022, 15:42