Kayanga,Tanzania:Hija ya Msalaba,Kalvario Kayungu:Heshimu Msalaba wa Kristo
Na Angella Rwezaula Vatican.
Kila tarehe 14 Septemba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Siku Kuu ya Kutukuka kwa Msalaba. Asili ya siku kuu hiyo ni ya kizamani sana, kwani Kanisa Katoliki, na makanisa mengi ya kiprotestanti na makanisa ya Kiothodox huadhimisha siku kuu hii ya kiliturujia, ikiwa inafanya kumbukumbuka kupatikana kwa Msalaba wa kweli wa Yesu na Mtakatifu Elena mnamo tarehe 14 Septemba 320, ambaye ni mama wa Mfalme Constantin na alitabaruku Kanisa la Kaburi Takatifu huko Yerusalemu mnamo mwaka 335, na tangu wakati huo masalia hayo yalioneshwa juu na Askofu wa Yerusalemu mbele ya watu, ambaye aliwaalika kuabudu Msalaba huo. Kwa mujibu wa utamaduni, Mtakatifu Elena alipeleka sehemu ya Msalaba mjini Roma ambapo baadaye eneo hilo likageuka kuwa Basilika ya Msalaba Mtakatifu wa Yerusalemu na sehemu nyingine ilibaki Yerusalemu.
Katika maadhimisho ya Misa takatifu ya siku hiyo, liturujia inaoneshwa na rangi nyekundu. Siku Kuu hiyo yenye ukuu na maana yake kwa kudhiirisha kuwa Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu. Msalaba ambao ni ishara ya wokovu wa dunia nzima. Kama Mtakatifu Paulo asemavyo kuwa kwake anaona fahari ya msalaba, ndiyo maana hata Mama Kanisa daima ameona fahari kuu ya kuutangaza utukufu na kuimba sifa za Msalaba wa Bwana wetu Yesu kristo, aliyekufa juu yake na kufufuka, tumaini letu daima la wakrisito wote.
Hija ya Jimbo katoliki la Kayanga katika kituo cha hija cha Kalvario Kayungu
Katika fursa hiyo Jimbo Katoliki la Kayanga Karangwe Tanzania, limefanya hija ya Msalaba iliyozinduliwa tangu mnamo mwaka 2011 katika Kituo cha Kalvario Kayungu kilichopo Parokia ya Kayungu tarehe 14 Septemba 2022. Misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza ikiudhuriwa na Mapadre, watawa na waamini walei kutoka maparokia yote ya jimbo ka Kayanga, waliofurika kwenye kilima hicho cha Kayungu, huku kwaya kutoka parokia zote wakiongoza nyimbo. Kwa neema ya Mungu hata baraka ya mvua iliweze kuwanyeshea waamni na hata maeneo yanayozungukia eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo cha Matangazo ya Radio FADECO, Radio ya jamii, Bwana Joseph Sekiku amebainisha kuwa misa ilikuwa nzuri na ya kupendeza. Katika mahubiri ya Askofu aliwashauri waamini kuheshimu Msalaba wa Kristu kwa kuamini msalaba kwamba ni Bendera ya ushindi kwa mkristo yeyote, anayeamini. Akiendelea katika mahubiri hayo aliezea juu ya madhumuni maalum ya kuanzishwa kwa vituo vya Hija jimboni, kwamba ni kutafuta namna ya kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili waamini wanaoamini Kristu na hivyo kwamba hawana budi kutumia vituo vya hija vilivyomo ndani na nje ya jimbo kusali kwa imani ikiwa ni nguzo pekee ya uponyaji wa magonjwa, changamoto za familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ilifanya mahojiano maalum na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza kuhusiana na Jimbo historia ya jimbo hilo ambapo katika mahojiano hayo marefu hata kuhusu kituo hicho na vingine alivitaja. Askofu akianza kueleza alisema, Jimbo Katoliki la Kayanga ni mojawapo kati ya Majimbo 34 ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Jimbo hili linaundwa na wilaya mbili ambazo ni wilaya za Karagwe na Kyerwa. Upande wa kaskazini linapakana na Uganda-Jimbo Kuu Katoliki la Mbarara. Upande wa Magharibi linapakana na Rwanda, na upande wa Mashariki linapakana na Wilaya ya Misenyi na kusini linapakana na wilaya ya Ngara nchini Tanzania.
Jimbo Katoliki la Kayanga lilitangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 14 Agosti 2008, ambalo lilimegwa kutoka Jimbo Katoliki la Rulenge, na hatimaye kuzaliwa majimbo mapya mawili, yaani Jimbo Katoliki la Rulenge– Ngara, na Jimbo Katoliki la Kayanga. Mnamo mwaka 1929 ilianzishwa Vicarieti ya kitume ya Rulenge-Ngara kutokana ile Vicariate ya Kitume ya Tabora, ambapo mnamo tarehe 25 Machi 1953 Rulenge ilitangazwa kuwa Jimbo. Na mnamo tarere 14 Agosti 2008, ikamegwa Jimbo hilo Rulenge na kuanzishwa Jimbo Katoliki jipya la Kayanga.
Jimbo Katoliki la Kayanga lilizinduliwa mnamo tarehe 6 Novemba 2008, ambapo Askofu Almachius Vincent Rweyongeza aliwekwa wakfu akiwa Askofu wa kwanza wa jimbo hilo lenye kilomita za mraba 70,716 likiwa na wakazi zaidi ya laki 6 Wakatoliki wakiwa ni asilimia 60 Jimboni humo, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. ( na sensa ya mwisho ni 2022, itajulikana baadaye ni watu wangapi).
Askofu Rweyongeza akieleza juu ya jimbo lake alisema Jimbo la Kayanga lilianzishwa likiwa na Mapadri 24, hivyo kwa wastani, kila Padri mmojawao anahudumia waamini 11,200 katika Parokia 11 ilivyokuwa katika mwaka wa 2008, idadi ya watawa wa kike walikuwa 61 wa Shirika la Kijimbo. Katika muktadha huo, Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga anamshukuru Mungu kwa mafanikio ya kiroho yaliyopatikana Jimboni humo, hasa ongezeko la Mapadre, Watawa wa kike, na Makatekesta ambao wamekuwa chachu ya kuimarisha katekesi kwa waamini. Askofu anabainisha kuwa hadi sasa Jimbo hilo lina jumla ya Mapadre 51, Watawa 94 wa kike, na ongezeko la Makatekesta kutoka 398 katika kipindi cha mwaka 2008, na kufikisha idadi ya Makatekista 438 kwa mwaka 2022. Askfofu Almachius aidha, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka 14 tangu kuanza kwa Jimbo hilo kunako mwaka 2008 hadi mwaka huu 2022, kumekuwa na ongezeko kubwa la wahudumu, hasa Mapadre na miito ya Upadre, ambapo kwa mwaka huu amewapatia Daraja Takatifu Mapadre wapya watatu, na kufikisha idadi ya Mapadre 51 jimboni humo.
Mafanikio ya jimbo kayanga 2008-2022
Hakukosa kutotaja pia mafanikio mengine, hasa ongezeko la familia za Kikatoliki kupitia Sakramenti ya Ndoa Takatifu, hali iliyosaidia kupunguza ndoa za mseto, uchumba sugu, ndoa mgando, ndoa za mitala, pamoja na kupungua kwa ndoa za kiserikali. Miongoni mwa mafanikio mengine jimboni humo ni ongezeko la Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo kutoka Jumuiya 1,039 hadi kufikia Jumuiya 1657, pamoja na uwepo wa Vituo vya Hija ambavyo alivitaja kuwa ni ‘Zahanati za Kiroho’ kwa ajili ya kutibu mahangaiko ya waamini. Askofu Almachius alisema kuwa wakati jimbo linazinduliwa lilikuwa na Parokia 11 tu, Vigango 234, Jumuiya za Kikristu 1,039 na Mapadre 24, Masista wa Jimbo 61 wa Shirika la Mitume wa Upendo, Upendo ambalo ndilo Shirika la Jimbo Katoliki la Kayanga, wakiwamo Makatekista 398.
Askofu aliongeza kusema: “Wahenga wetu wamesema “daima mwanzo ni mgumu’” ugumu huu ulitokana na shida za kiuchumi, hasa kuweka miundombinu ya msingi ya kichungaji na kijamii. “Namshukuru Mungu wakati jimbo linazinduliwa, Kanisa Kuu la Mtakatifu George, Kayanga, lilikuwa limekwisha jengwa na kutabarukiwa na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge - Ngara, mnamo tarehe Mosi Septemba 2008, siku tano kabla ya kuzinduliwa kwa Jimbo Katoliki la Kayanga”. Askofu Rweyongeza anasema kwamba alipokabidhiwa Jimbo la Kayanga hakuwa na uzoefu wowote wa kuzindua jimbo, hakuwa na ujanja wala mbinu za kuongoza jimbo hilo. Hivyo, aliandika katika Ngao yake ya Kiaskofu akijisalimisha kwa Bwana kwa kutumia maneno yasemayo: “Mimi ni Mtumishi wa Bwana.” Nilijisalimisha kwa Mungu kwa kutumia maneno ya Bikira Maria. Nilimkabidhi yote Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu asipojenga Jimbo Katoliki la Kayanga, wajengao wanajisumbua bure, nami nikiwa mmojawapo. Kusema kweli, Mwenyezi Mungu amenitendea makuu kwa kipindi cha miaka 14, kwani nimeshuhudia mafanikio makubwa,” alisema Askofu.
Ukosefu wa mapadre wa kutosha
Askofu Rweyongeza nasema vile vile kuwa licha ya idadi ndogo ya Mapadri wanaotoa huduma za kiroho Jimboni humo, anashukuru pia mchango wa Makatekesta ambao ni wasaidizi wa karibu wa Mapadre, hasa Vigangoni na Vijijini, kwa sababu Parokia moja inakuwa na vigango zaidi ya 30 ambavyo vinahudumiwa na Mapadre wawili, hivyo Makatekesta wanasaidia sana kutoa huduma za kiroho kwa waamini wao. Hadi sasa lisema kuwa kuna ongezeko la Parokia, kutoka 11 katika kipindi cha mwaka 2008, na kufikia idadi ya Parokia 20 mwaka huu 2022, zenye Mapadre wenye makazi maalum katika Parokia hizo. “Mapadri bado ni wachache kulingana na idadi ya Waamini Jimboni humu, kwani baadhi ya Parokia moja moja anaishi Padre mmoja tu, ambapo inakuwa ni kazi ngumu. Hata hivyo naamini kwamba Mungu ndiye anayeweza kutufanikishia kwa kuwategemeza katika Utume wa Kanisa licha ya uchache wao.”
Ongezeko la vyama vya kitume jimboni
Mbali na hayo, Askofu Rweyongeza amesifu ongezeko la Vyama vya Kitume Jimboni humo, ambavyo ni uhai wa Kanisa na Jimbo, na alivitaja kuwa ni Utoto Mtakatifu, WAWATA, UWAKA, VIWAWA, Lejio ya Maria, Wafransiskani na vyama vingine vya kitume, ambavyo ni chachu ya mafanikio ya kiroho Jimboni humo. Askofu Rweyongeza aliwasifu pia Viongozi wa Halmashauri Walei Katoliki (HAWAKA), ambao ni washiriki wenza katika shughuli za uchungaji ambao umejengwa na viongozi wanaojituma, ili kuhakikisha Jimbo linasonga mbele kiimani. Sambamba na hayo kwa upande wa taasisi za Dini, alivitaja uwepo wa Vituo vya Hija ambavyo alisema ni kama “Zahanati za Kiroho’”zinazosaidia Waamini wengi Wakatoliki na wasio Wakatoliki kwenda kuchota neema na baraka kutoka katika vituo hivyo vya hija na maisha ya kiroho. “Nilivizindua Vituo hivi vya hija wakati Jimbo lilipoanza. Nikaona kwamba hili ni hitaji kubwa la kuwasaidia Waamini na jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kiroho, kiimani na uponyaji, nikiamini kwamba Vituo hivi vya Hija ni zahanati za kiroho.”alisema .
Kituo cha Kalvario Kayungu na Kituo cha Lourdes Bugene
Kalvario Kayungu ni miongoni mwa Vituo vya Hija jimboni humo, kilichozinduliwa septemba 14 mwaka 2011 kwa heshima ya Msalaba Mtakatifu. Pia, kituo kingine cha hija cha Lourdes Bugene kilijengwa kwa heshima ya Bikira Maria wa Lourdes na Afya ya Wagonjwa, kikizinduliwa tarehe 11 Februari 2012 sambamba na siku ya wagojwa ulimwenguni ifanyikayo kila mwaka. Askofu Rweyongeza alisema kuwa familia ya Mungu Jimboni humo huwa wanafanya hija za kijimbo kila ifikapo tarehe 11 Februari Kitaifa na Kimataifa huko Lourdes Bugene katika kuadhimisha sikukuu ya Bikira Maria wa Lourdes, Afya ya Wagonjwa. Kadhalika wanafanya hija za kijimbo, kitaifa na kimataifa huko Kalvario Kayungu kila ifikapo tarehe 14 Septemba kwa heshima ya Kutukuka kwa Msalaba.
Uwekezaji katika taasisi za kijamii
Licha ya Jimbo hilo kuwa miongoni mwa majimbo machanga nchini Tanzania, limewekeza katika taasisi mbalimbali za jamii, hususan zinazogusia masuala ya Elimu kama vile shule, vituo vya afya hospitali na zahanati, pamoja na tasisi za mazingira (CHEMA). Askofu Almachius alisema : “Tuna taasisi muhimu sana Jimboni ijulikananyo kama CHEMA, kifupi cha Community Habitat Environment Management, kama mwitikio kwa Baba Mtakatifu kuhusu barua yake ya kitume ‘Laudato Si’ , inayohusika hasa na utunzanji wa mazingira.” Alifafanua kwamba Taasisi ya CHEMA inashughulika na mazingira, kama vile upandaji miti na utengenezaji wa vitalu mbalimbali vya miti mbalimbali ya matunda na miti ya mbao, kivuli na biashara. Pia, ikiwemo utengenezaji wa majiko sanifu yanayotumia kuni kidogo, au majiko yanayotumia unga wa mbao kunusuru uangamizaji wa miti kwa ajili ya kujipatia kuni na mkaa, sanjari na ufugaji wa nyuki.
Uharibifu wa Mazingira
Katika kuendeleza suala hili Askofu Rweyongeza alibainisha kwamba uharibifu wa mazingira ni moja kati ya changamoto zinazolikumba Jimbo hilo, hususani uharibifu wa vyanzo vya maji; ukataji wa miti kiholela; uchomaji moto misitu; na utumiaji wa sumu kuua magugu kwa kulima mazao ya muda. “Jimbo langu limekumbwa na uharibifu wa mazingira, kwani mtu anakata mti wa miaka 30 ili apande mazao ya haraka kujipatia pesa ya haraka, bila kuangalia ni aina gani ya uharibifu wa mazingira anaousababisha.” Kupitia taasisi ya CHEMA, Askofu Rweyongeza alisema kwamba anahimiza watu waoteshe miti ili kuhakikisha wanatunza uoto uliopo kwa sababu ya uharibifu wa mazingira, kwani ni hatari katika maisha ya binadamu na viumbe vyote. “Jimbo Katoliki la Kayanga linao msitu wa mfano kuhakikisha kwamba mazingira yanatunzwa, nami namshukuru Mungu nina msitu wangu wa mfano ambao unaitwa bustani ya Edeni, ambako lengo ni kutunza miti ya asili ya matunda ambayo imeshatoweka. Nimepanda miti ya Kibiblia ambayo ni mizeituni, mitende, mitini na mizabibu, ambayo ninayo kwenye shamba langu la ekari 05”.