Tafuta

Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma anasherehekea Jubilei ya Miaka 25 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre. Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma anasherehekea Jubilei ya Miaka 25 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre. 

Mwaka wa Baraka Na Neema Jimbo Katoliki la Kigoma! Yumo Pd. Achiles N. Charukula!

Uteuzi Padre Evarist Anthony Guzuye, aliyekuwa Katibu wa Askofu na Katibu wa Jimbo ameteuliwa kuwa Makamu wa Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma. Ataendelea pia kuwa Paroko wa Janda na Meneja Msaidizi wa Shule ya Sekindari ya Mtakatifu Mathias Mulumba. Padre Achiles Narcis Charukula ameteuliwa kuwa Katibu wa Askofu na Katibu wa Jimbo “Chancellor." Kigoma Kumenoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma anayo kila sababu ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu anayoendelea kuwaonesha watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma na hususan katika kipindi cha Mwaka 2022. Jimbo hili limebahatika kumtoa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama ambaye maisha na utume wake unaongozwa na kauli mbiu ya Kiaskofu: Ukweli na haki katika upendo aliyewekwa wakfu na kusimikwa rasmi tarehe 4 Septemba 2022. Jimbo Katoliki la Kigoma kwa mwaka 2022 limebahatika kupata Mapadre wapya watano. Askofu Joseph Roman Mlola tarehe 11 Agosti 2022 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na kilele chake ni tarehe 26 Septemba 2022 kwa kuungana na Askofu Beatus Urasa wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Miaka 25 ya zawadi ya Daraja takatifu ya Upadre, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022.

Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Kigoma, hivi karibuni, wakati wa kukamilisha mafungo ya Mapadre wa Jimbo Katoliki la Kigoma, alimteuwa Mheshimiwa Padre Evarist Anthony Guzuye, aliyekuwa Katibu wa Askofu na Katibu wa Jimbo, “Chancellor” kuwa Makamu wa Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma. Ataendelea pia kuwa Paroko wa Janda na Meneja Msaidizi wa Shule ya Sekindari ya Mtakatifu Mathias Mulumba. Lakini, hii ndiyo “habari ya mujini” Padre Achiles Narcis Charukula ameteuliwa kuwa Katibu wa Askofu na Katibu wa Jimbo “Chancellor”. Viongozi hawa wawili walikuwa kiapo cha uaminifu kwa kazi na utume wao mpya. Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma akakiri pia Kanuni ya Imani katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa tarehe 23 Septemba 2022. Mafungo yaliongozwa na Padre Rogathian Msafiri kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika kipindi cha Juma zima, Mapadre Jimbo Katoliki Kigoma, walizama katika tema ya “Kumtazama Kristo Yesu, Kimbilio na Mwokozi wao katika hali mbalimbali za maisha.”

Askofu Christopher Ndizeye wa Kahama ni matunda ya Jimbo la Kigoma.
Askofu Christopher Ndizeye wa Kahama ni matunda ya Jimbo la Kigoma.

Kutoka Maktaba, tujikumbushe kidogo! Naitwa Frt. Achiles Narcis CHARUKULA. Nilizaliwa tarehe 2 Mei 1990 katika Kigango cha Mtakatifu Luka, Makere, Parokia ya Makere jimboni Kigoma, Tanzania. Mimi ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto tisa. Nilihitimu elimu ya kidato cha sita mwaka 2012 katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo, Jimbo Katoliki la Kigoma. Masomo hayo yalitanguliwa na elimu ya kidato cha nne niliyoipata katika shule ya sekondari Makere (2006-2009), na kabla ha yapo, elimu ya shule ya msingi ambayo nayo niliipata katika shule ya msingi Makere (1999-2005). Kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya uzamili ya Sheria za Kanisa katika Chuo kikuu cha Kipapa Urbaniana, Roma. Ikumbukwe kuwa nimeanza masomo haya baada ya kuhitimu masomo ya taalimungu hapohapo chuoni Urbaniana mwaka 2019, ambayo nayo yalitanguliwa na masomo na malezi ya falsafa niliyochota kutoka katika Seminari kuu ya Mtakatifu Anthony wa Padua -Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba.

Wito: Safari yangu ya wito ilianza katika uchanga wangu nilipokuwa katika kikundi cha watoto watumikiaji Altareni na kikundi cha Utoto Mtakatifu wa Yesu. Hakika ni katika kipindi hicho ambapo nilipenda sana kuwa padre katika maisha yangu. Nilivutwa na maisha ya mapadre waliokuwa wakihudumia parokiani kwetu Makere na kutamani kufahamu zaidi ni hatua zipi zinazoweza kumfikisha kijana kuwa padre. Aidha nilivutwa na unadhifu wa mafrateli waliokuwa wakija kuhudumu parokiani kwetu wakati wa likizo zao, mmoja wao akiwa ni Gambera wa sasa wa seminari ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo, (Pd. Patrick Tarcisius Mahinja). Hii si kwamba nimesahau masifu ya asubuhi yaliyokuwa yakisaliwa na mapadri na masista baada ya misa parokiani hapo. Ni dhahiri kwamba katika malezi nimejifunza kuwa maisha ya wenye daraja takatifu ni zaidi ya viashiria nilivyo viona mwanzoni. Ni utumishi kwa Mungu na kwa Kanisa lake bila kujibakiza, kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo aliye kuhani milele.

Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre wa Askofu Mlola.
Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre wa Askofu Mlola.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, licha ya kufaulu vema mtihani wa kujiunga na seminari ndogo na kuchaguliwa, sikuweza kwenda na badala yake nilijiunga na shule ya Sekondari ya Kata iliyotajwa hapo juu. Hata hivyo hii haikuzima kiu yangu ya kuwa Kasisi wa Kanisa Katoliki. Nilipiga moyo konde, ndoto yangu mtimani nikaihifadhi. Katika hili shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na wito, lakini pia kwa mapadre waliohudumu parokiani Makere ambao, si tu walinitia moyo kwa maneno na namna zao za maisha, bali pia walinielekeza na kunisaidia kujiunga na Seminari ndogo ya Iterambogo, kwa kidato cha tano na sita ambako huko wito wangu ulichanua zaidi. Katika muktadha wa maandalizi ya kupokea daraja takatifu ya Ushemasi, nimechagua maneno ya Mtakatifu Tomaso mtume “Bwana Wangu na Mungu Wangu” Yn. 20:28 si tu kwa sababu tuko katika kipindi cha Pasaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, bali pia ni namna yangu ya kukiri Imani yangu kwa Yesu Kristo mfufuka, ambayo pia ni imani yetu Wakatoliki, Imani ya Kanisa ambayo twajivunia kuikiri na kuishuhudia.

Mwaka 2022 ni Mwaka wa neema na baraka Jimbo Katoliki la Kigoma
Mwaka 2022 ni Mwaka wa neema na baraka Jimbo Katoliki la Kigoma

Aidha ni katika kuustajabia: ukuu na huruma ya Mungu katika safari yangu ya wito, kwa wema wake mwingi alionionyesha. Ninamshukuru nikikiri imani yangu kwake nikisema “Bwana Wangu na Mungu Wangu”. Ninamstaajabia Mungu nikitambua wazi kabisa kwamba, si kwa haki yangu ninaitwa kumtumikia Mungu katika Sakramenti ya daraja takatifu, bali ni kwa upendo na huruma yake kuu. Ndipo hapo ninapoungana na Mzaburi kusema “Ndiwe Mungu wangu nami nitakushukuru, ndiwe Mungu wangu, nami nita kutukuza”. Zab. 118:28. Ninapomshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na wito, Nawashukuru wazazi wangu Mzee Narcis Charukula na Mama Felista Paulo Mapengo kwa kushiriki kazi ya uumbaji na hivyo mimi nikazaliwa na kulelewa vyema, pamoja na hao nawashukuru wadogo zangu wote kwa kushiriki vema malezi yangu. Natambua na kushukuru mamlaka ya Kanisa jimboni Kigoma, na hivi namshukuru sana Baba Askofu Joseph Roman MLOLA, Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma na waandamizi wake wote kwa malezi, misaada ya hali na mali na kwa kukubali kwake kunipokea kati ya Makleri jimboni Kigoma mara tu nitakapopokea Daraja takatifu ya Ushemasi hapo 01.05.2021, kwa msaada wa Mungu.

Shukrani hizo zinamwendea pia Baba Askofu mkuu Paul Runangaza RUZOKA wa jimbo kuu katoliki Tabora, aliyenipokea katika nyumba ya malezi akiwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Kigoma mwaka 2013. Nawashukuru mapadre na watawa jimboni Kigoma na seminari zote nilizopitia, Iterambogo, Ntungamo, Bukoba na hapa Urbaniana kwa namna ambavyo kila mmoja amegusa maisha yangu. Ni ngumu kusahau mchango wa waseminaristi wenzangu, wema wa WAWATA jimboni Kigoma, watanzania walioko Roma, taifa lote la Mungu na wote wenye mapenzi mema. Eti wadaku wanasema, "Dogo ana upiga mwingi."

Jimbo Katoliki Kigoma

 

26 September 2022, 17:05