Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwamini: Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwamini:  

Tafakari Dominika 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Msalaba!

Ni katika kupenda bila kujibakiza hapo tunaweza kufikia hatua hata ya kutoa maisha yetu kwa ajili ya Mungu na jirani, ni hapa ndio Msalaba unapata maana kwenye maisha yetu ikiwa tu ni matokeo ya upendo. Msalaba kama matunda ya upendo ndio unakuwa ishara ya uzima na ushindi ukiwa; ni matunda ya upendo wetu kwa Mungu na jirani. Ushindi wetu ni katika kupenda!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Gharama ya ufuasi: Ni kwa Mungu tunajifunza maana na jinsi ya kupenda kwani Yeye ni Upendo! Msalaba hauna budi kuwa ni matokeo ya upendo wetu kwa Mungu na jirani. Kwa nini Msalaba katika maisha ya Mkristo; Kwa nini mateso na hata kifo? Ni maswali yanayotusumbua katika tafakari ya ufuasi wetu kwa Kristo. Ni maswali yasiyokuwa na majibu mepesi. Mkristo sio yule anayetafuta mateso na Msalaba, maana hata Kristo mwenyewe hakutafuta mateso na msalaba, maana wito wetu wa msingi ni upendo. Ni katika kupenda bila kujibakiza hapo tunaweza kufikia hatua hata ya kutoa maisha yetu kwa ajili ya Mungu na jirani, ni hapa ndio msalaba unapata maana kwenye maisha yetu ikiwa tu ni matokeo ya upendo na si kinyume chake.  Msalaba kama matunda ya upendo ndio unakuwa ishara ya uzima. Msalaba ni ishara ya ushindi ukiwa ni matunda ya upendo wetu kwa Mungu na jirani. Ushindi wetu ni katika kupenda ikibidi hata kutoa maisha yetu kama rafiki zake Yesu Kristo. Mpaka karne ya tatu ishara ya Ukristo ilikuwa ni picha ya mvuvi na samaki na kamwe haikuwa Msalaba kama leo hii.  Ni kuanzia karne ya nne baada ya Mtakatifu Helena, aliyekuwa mama wa mtawala wa Kirumi Constantino, ndio Msalaba ukaanza kutumika kama ishara ya ushindi. Hivyo kwa kuchagua Msalaba, hapo unachagua maisha, ingawa bado si rahisi kueleweka hata leo katika nyakati zetu tunapojaribu kuelezea Teolojia ya msalaba. Msalaba unapata maana tu ikiwa tunauangalia kama matokeo ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Fumbo Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake linapata maana kwani ni upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima, ni fumbo la upendo!

Msalaba unapata maana ya pekee ikiwa ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani
Msalaba unapata maana ya pekee ikiwa ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani

Dominika ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa tulimwona Yesu akiwa mezani katika nyumba ya mmoja wa wakuu wa mafarisayo, na leo tunaona yupo njiani akiwa na makutano. Yupo njiani kuelekea Yerusalemu, mahali ambapo atahukumiwa kifo, kuteseka, kufa na siku ya tatu kufufuka. Ni safari yake ya mwisho akiwa ulimwenguni baada ya kumaliza kazi yake ya kueneza Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ni safari ambayo hata wale rafiki zake wa karibu, yaani mitume walikuwa bado hawajaelewa mustakabali na hatima ya Bwana na Mwalimu wao. Mitume, kwao ushindi ni kuona Bwana na Mwalimu wao anakuwa mtawala kama watawala wa ulimwengu huu, na sio kuteseka na kufa kwa aibu pale msalabani na siku ya tatu kufufuka. Hilo lilikuwa ni jambo gumu si tu kueleweka bali hata kufikirika katika vichwa vyao. Mitume kama ilivyo kwetu leo tunahitaji ukombozi wa fikra, na hii ndio metanoia ya kweli, akili na namna zetu za kufikiri na kutenda lazima zikombolewe kwa nafasi ya kwanza. Ni katika mazingira haya Yesu anaona bado wafuasi wake hawajaelewa nini maana ya kuwa mfuasi. Anawageukia na kuanza kuwapa katekesi ya kina, juu ya nini maana ya kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, anatugeukia nasi leo katika Dominika hii ya leo ili tuweze kuelewa nini maana ya kuwa wafuasi wake. Yesu Kristo leo anatupa masharti matatu magumu ya kuwa wafuasi wake. Yesu anatueleza kinagaubaga bila kuupaka ukweli sukari maana ya kuwa mfuasi na hata hatari tutakazo kutana nazo katika safari yetu ya ufuasi.

Kuchukia ndio kumpa Kristo Yesu nafasi anayostahili katika maisha yetu. Yesu leo anatualika kuchukia (Neno la Kigiriki ni mizein), ni kinyume na kawaida yake kwani daima anatualika kupenda, sasa inawezekanaje leo anatualika kuchukia baba, mama, mke, watoto, kaka, dada, na hata sisi wenyewe ili tuweze kuwa wafuasi wake. Yesu kila mara anapotualika kutafakari juu ya ufuasi wetu anatumia lugha ngumu na kali kwa nia moja tu hivyo tangu awali hatuna budi kufanya maamuzi ya dhati na magumu ili kuwa wafuasi wake. Ni Yesu anayetutaka tufanye maamuzi magumu, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, ndio ukombozi wa fikra, ni kukubali kuongozwa sio na mantiki ya ulimwengu huu bali ile ya Kimungu, ni kuwa na hekima na busara ya Mungu mwenyewe. Yesu hatuambii leo tusiwapende au tuwapende kidogo walio wa familia zetu au jamaa na marafiki zetu, hapana. Kusema hatuna budi kuchukia sio mwaliko wa kutokuwapenda au kuwapenda kidogo bali ni kubadili vichwa vyetu na kuanza kuongozwa na Injili, kuwa na mtazamo mpya na hivyo kutoa nafasi sahihi kwa wazazi, mke, watoto au ndugu na hata nafasi yetu sisi wenyewe kama kweli tunahitaji kuwa wafuasi kweli wa Yesu Kristo. Kuchukia ni kututaka tuwe tayari kuvunja hata mahusiano yetu ya karibu ikiwa yanatuweka mbali na Injili na wito wake Yesu Kristo. Ni kumpa nafasi ya kwanza Yesu Kristo na Injili yake katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ni kwa kufanya hivyo hapo kweli tunakuwa na upendo wa kweli kwa Bwana tunayemfuata katika maisha yetu. Kuchukia ni kumpa Mungu nafasi ya kwanza kabla ya mengine na wengine wote katika maisha yetu. Ni kujua nafasi stahiki ya Mungu katika maisha yetu, ni kuwa tayari kuupokea ukombozi wa fikra, yaani metanoia!

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa mashuhuda wa huruma na mapendo
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa mashuhuda wa huruma na mapendo

Katika ulimwengu wa leo neno upendo linatumika mara nyingi na labda ndilo neno linakosa kueleweka nini hasa maana yake. Ni kwa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza hapo tuna hakika ya kujifunza nini maana ya kupenda, kwani Mungu ni upendo! Ni kwa kumpa Mungu nafasi ya kwanza hapo kweli tunafanyika kuwa wana wa Mungu tunaoweza kuishi na kuenenda sio kwa kadiri yetu bali kwa kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe. Mama Teresa wa Kalkuta alipenda kusema; “Ni Mungu amenifundisha kupenda. Ni kwake pekee nimejifunza kupenda”.  Kumpa nafasi Mungu nafasi ya kwanza maana ni kukubali kuongozwa sio tena na mantiki ya ulimwengu huu bali na ile ya Mungu mwenyewe, ndio ukombozi wa fikra, yaani Metanoia ya kweli. Tunaweza kuona pia mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi na baba yake. Hakika Mtakatifu Francisko alimpenda baba yake hata pale ambapo baba yake alimlaani na kumtakia mabaya. Ni baba yake aliyekosa kujua maana ya upendo kwa kujawa na majivuno na umimi; palipo na majivuno na ubinafsi hapo hakuna nafasi ya upendo. Upendo wa kweli ni ule unaojisahau na hata kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine, ndio kujua kumpatia Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yetu. Nafasi ya kwanza sio ya baba au mama, sio ya mke au mume, sio ya watoto au ndugu au jamaa au marafiki au mali na vitu bali ni ya Mungu mwenyewe. Kubeba Msalaba ni matokeo ya upendo wa kweli.

Sharti la pili, ndilo kubeba Msalaba wetu na kumfuasa.  Ni mwaliko si tu wa kukubali kuteseka na kusetwa kwa ajili ya Injili, bali ni maisha ya kuwa tayari kuwa mashahidi wa Upendo wa Mungu, tunateseka na kutaabika kwa sababu moja tu yaani upendo wa Bwana wetu Yesu Kristo na Injili yake. Wito wetu ni kupenda daima hata kama inatubidi kutoa sadaka ya maisha yetu. Lazima kuketi na kujitathmini kabla ya kumfuasa Kristo Yesu. Yesu pia anatumia fursa hii ya leo kutupa mifano miwili, wa kwanza ndio ule wa mkulima anayejenga mnara shambani kwake, kwa sababu kubwa ya ulinzi dhidi ya wevi na wanyama waharibifu. Anayeketi kwanza kabla ya kuujenga kuona kama ana pesa na uwezo wa kuukamilisha, na ndivyo tufanyavyo kila mara kabla ya kuanza mradi mkubwa katika maisha yetu, lazima kufanya tathmini ya kina kuona kama tunaweza kufikia malengo. Ni mwaliko pia hata katika maisha ya ufuasi kuketi na kujitafakari kabla ya kuanza kumfuasa Yesu Kristo. Ni mwaliko kwa kila mbatizwa na si tu kwa wale wanaoitwa kwa maisha ya wakfu kama mapadre na watawa, kila mmoja wetu hana budi kuketi na kujitathmini katika kumfuasa Yesu Kristo.

Ushuhuda wa Injili upewe kipaumbele  cha kwanza.
Ushuhuda wa Injili upewe kipaumbele cha kwanza.

Mfano wa pili ndiye mfalme anayeketi na kujitathmini kabla ya kwenda vitani. Maisha ya ufuasi ni vita dhidi ya yule mwovu shetani hivyo hatuna budi kuketi kila mara na kujitathmini kabla ya kwenda vitani. Hivyo maisha ya ufuasi ni maisha ya kufanya maamuzi magumu, huo ndio wito wetu anaotualika Yesu kuutafakari katika Dominika ya leo, si kwamba Yesu anataka kutuvunja mioyo, la hasha, bali kutuweka wazi tangu mwanzo kuwa maisha ya ufuasi hayana budi kuwa ni matokeo ya maamuzi magumu na ya dhati kabisa ya kila mmoja wetu. Ni wito wa maisha wenye magumu na changamoto zake, na hivyo hatuna budi tangu mwanzoni kufanya maamuzi ya dhati. Lazima kuacha yote ili kumfuasa kweli Kristo Yesu. Sharti la tatu na labda ni gumu kuliko yote ndio kutojishikamanisha na mali au vitu ili kuwa wafuasi wake. Yesu hasemi kuwa tutoe msaada wa pesa kidogo bali yote tuliyo nayo, eeeh sio mchezo ni hitaji gumu na zito. Wengi leo hii wanapenda kuona mwaliko huu ni kwa wachache tu hasa wale wanaoamua kujitoa kwa maisha ya wakfu, ila naomba niseme ni mwaliko kwa kila mmoja. Ni mwaliko kama nilivyosema hapo juu wa kubadili vichwa vyetu kwa maana ya kuipa pesa na mali nafasi stahiki na sio kuchukua nafasi ya kwanza ile ya Mungu na Neno lake katika maisha yetu. Yafaa kila mmoja kuketi na kujiuliza katika maisha yangu ni nini kinakuja kwa nafasi ya kwanza, moyo wangu upo katika mali au katika kumpenda Mungu na Neno lake? Nawatakia Dominika na tafakari njema.

01 September 2022, 08:50