Tafakari ya neno la Mungu, Dominika 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Kuwa mfuasi wa Kristo kuna gharama yake na gharama hiyo ni Msalaba. Tafakari ya neno la Mungu, Dominika 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Kuwa mfuasi wa Kristo kuna gharama yake na gharama hiyo ni Msalaba. 

Tafakari Dominika ya 23 Mwaka C wa Kanisa: Msalaba Ni Gharama ya Ufuasi Wa Kristo Yesu

Katika dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Neno la Mungu linazungumza nasi kuhusu gharama ya ufuasi. Kuwa mfuasi wa Kristo kuna gharama yake na gharama hiyo ni Msalaba. Ni hayo tunayasikia katika Injili ambapo Kristo Yesu mwenyewe anasema “mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mfuasi wangu.” Msalaba ni ufunuo wa Huruma!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Ni dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa. Katika dominika hii Neno la Mungu linazungumza nasi kuhusu gharama ya ufuasi. Kuwa mfuasi wa Kristo kuna gharama yake na gharama hiyo ni Msalaba. Ni hayo tunayasikia katika Injili ambapo Kristo Yesu mwenyewe anasema “mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mfuasi wangu.” Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tuweze kuupitia na kuupokea ujumbe wa Neno la Mungu kwa dominika hii. Kama ilivyo kawaida ya kipindi hiki, tunaanza kwa kuyapitia kwa kifupi masomo yote matatu na kuufafanua ujumbe wake. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 9:13-18). Ni sehemu ya sala ambayo Mfalme Sulemani alimtolea Mungu akimwomba paji la hekima. Tunalifahamu simulizi la Biblia ambapo Mungu alimwambia Sulemani aombe anachotaka naye angemjalia (Rej 1 Fal 3:4), yeye akaomba hekima. Katika kuomba hekima hiyo, Sulemani alianza kutambua ukuu wa Mungu, akaendelea kwa kulinganisha udogo wake na kazi kubwa aliyokuwa nayo kuliongoza taifa zima la Israeli na hatimaye akaeleza kuwa mwanadamu hawezi kuyapambanua wala kuyaelewa vema mambo yaliyo duniani na yaliyo mbinguni bila hekima itokayo kwa Mungu.

Msalaba ni alama na gharama ya ufuasi wa Kristo Yesu
Msalaba ni alama na gharama ya ufuasi wa Kristo Yesu

Sasa, somo letu la leo linatoka katika sehemu hii ya mwisho ya sala ya Mfalme Sulemani, sehemu inayomwonesha mwanadamu akipwaya katika kuyakabili mambo asipokuwa na hekima itokayo juu. Somo la pili tunalisoma kutoka katika waraka wa mtume Paulo wa Filemoni ((Flm 9b-10, 12-17). Paulo anamwandikia Filemoni kuhusu Onesimo ambaye alikuwa mtumishi wa Filemoni. Onesimo huyu alipotoka kwa Filemoni akakutana na Paulo akabatizwa na akawa mkristo. Paulo anamrudisha Onesmo kwa Filemoni akiambatana na hii barua. Ni nini ujumbe wa Paulo kwa Filemoni? Paulo anatambua kwamba zipo sheria na taratibu za kawaida kabisa katika jamii zinazoongoza mahusiano kati ya mtu na mfanyakazi - mtumishi wake. Paulo anamwomba Filemoni atambue kwamba imani yake ya kikristo inamtaka aende mbele zaidi. Wema ambao Filemoni anapaswa kumtendea Onesmo kama mtumishi wake, usibaki kuwa ni ule wema wa kawaida uliopo kwenye kanuni na sheria bali yeye aende mbele zaidi. Na hili, Paulo analisema waziwazi kuwa hamlazimishi Filemoni kwa sababu hataki wema wake uwe kama ni kitu cha lazima bali kiwe kwake hiyari.

Kwetu sisi leo, barua hii ya Paulo kwa Filemoni inatualika tutambue dhamana ambayo ukristo wetu unatupatia. Ni dhamana ya kutokubaki katika mstari wa ukawaida, ni dhamana inayotutaka twende mbele zaidi. Ni fundisho linaloakisi maneno ya Yesu mwenyewe aliyesema “haki yenu isipozidi ile haki ya waandishi na mafarisayo hamtaingia katika ufalme wa Mungu” (rej. Mt 5:20). Katika mwendelezo wa dhana hii kuhusu dhamana ya ukristo wetu, somo la injili linaizungumzia dhamana hiyo kama gharama ya kuwa mkristo, gharama ya kumfusa Kristo. Gharama hiyo ni mtu kuwa tayari kuubeba msalaba wake na kushika njia nyuma ya Kristo. Haya si maneno mepesi. Katika wakati huo wa Yesu, maneno haya kubeba Msalaba yalikuwa sawa na kumaanisha hukumu ya kifo. Waliobebeshwa Misalaba walikuwa ni wale waliohukumiwa kifo. Kumbe kuwa mkristo, Yesu anakufananisha na kukabiliana na adhabu ya kifo. Kwa maneno haya, Injili ya leo inatuonesha kuwa ukristo sio lelemama. Kumfuasa Kristo sio jambo jepesi. Linahitaji mtu ajitoe na ajikite kisawasawa katika imani. Vinginevyo atayumba, na atayumba sana. Na ili kujikita katika imani, mkristo anaalikwa kumtanguliza mbele Kristo na kumpa Yeye nafasi ya kwanza katika maisha yake. Ni hiki anachokimaansha Yesu anaposema  “yeye asiyemchukia baba na mama na mke na wanawe na ndugu zake na hata nafsi yake mwenyewe hawezi kuwa mfuasi wangu.” Yesu hafundishi chuki wala migawanyiko katika familia. Hiyo ni kazi ya yule mwovu. Anaalika kumtanguliza Yeye kwanza, kumpenda Yeye kwanza na kutafuta kumpendeza Yeye kwanza kabla ya nafsi zetu, kabla ya watu walio karibu nasi na kabla ya vitu. vinavyotuzunguka.

Kila mwamini amepewa Msalaba wake ajitahidi kuubeba kwa imani.
Kila mwamini amepewa Msalaba wake ajitahidi kuubeba kwa imani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyapokea masomo ya dominika hii ya 23 ya mwaka C wa Kanisa, tunachota nini cha kuisindikiza tafakari yetu katika juma hili. Binafsi ninawaalika turudi katika neno lile la Yesu, neno la mtu kubeba msalaba wake na kumfuasa. Kristo ameukomboa ulimwengu kwa njia ya msalaba. Na kwa jinsi hiyo ametufundisha na kutuonesha kuwa njia ya msalaba ndiyo njia ya wokovu. Hakuna njia nyingine mbadala wala hakuna njia nyingine ya mkato. Kwa sababu hiyo, Yesu mwenyewe amempa kila mmoja wetu njia yake ya msalaba ili kwa njia hiyo aweze kuifuata njia ya wokovu. Neno hili la Yesu siku ya leo ni neno basi linalokuja kutuimarisha na kututia nguvu ili tuendelee kuibeba kwa furaha na matumaini misalaba yetu tukimfuasa Kristo. Kishawishi ni kikubwa cha kuutupa msalaba na kubadili njia, kishawishi ni kikubwa cha kutamani misalaba ya wengine tukidhani ni myepesi kuliko ya kwetu na kishawishi ni kikubwa cha kukata tamaa tukidhani ni sisi tu tulio na misalaba ilhali wengine wakiwa na ahueni. Hekima ile ambayo mfalme Sulemani aliiomba ndiye Roho Mtakatifu anayekuja kutuangaza ili tuyatambue na kuyazingatia yanayompendeza Mungu na ni Roho anayetutia nguvu katika safari yetu ngumu ya njia ya msalaba. Tuiombe nasi hekima hiyo ya kimungu ili maisha yetu yasiongozwe na utashi wa kibinadamu pekee bali yaongozwe na Roho wake Mtakatifu.

Liturujia D23

 

03 September 2022, 15:35