Tafakari Dominika 24 Mwaka C wa Kanisa: Rehema na Huruma ya Mungu kwa Binadamu Mdhambi
Na Padre Efrem Msigala, OSA, Dar es Salaam.
Karibu Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa. Rehema na huruma ni fadhila na wema anaoonyeshwa mtu wakati kosa linapofanyika na adhabu kali inapotarajiwa. Rehema na huruma haiwezi kuoneshwa wakati hakuna kosa au dhambi iliyotendwa na mtu. Lakini pia utayari wa mkosaji kuomba msamaha kwa aliyemkosea. Kwa namna ya pekee mwanadamu mkosefu kuomba msamaha kwa Mungu na Mungu husamehe. Pamoja na rehema pia inahitajika neema ya Mungu katika safari ya toba na wongofu wa maisha ya mwanadamu ya kila siku. Katekismu ya Kanisa Katoliki namba 1989 inasema “Kazi ya kwanza ya neema ya Roho Mtakatifu ni wongofu, unaofanya kuhesabiwa haki kwa mujibu wa tangazo la Yesu mwanzoni mwa Injili, ikisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”Akisukumwa na neema, mwanadamu anageuka kuelekea Mungu na kuwa mbali na dhambi, hivyo kukubali msamaha na haki kutoka juu. Pamoja na hayo namba 1999 inaelezea kuwa “ Neema ya Kristo ni zawadi ya bure ambayo Mungu hutupatia kutoka kwa maisha yake mwenyewe, ikiingizwa na Roho Mtakatifu ndani ya roho zetu ili kuiponya kutoka kwa dhambi na kuitakasa”
Katika somo la kwanza tunaona tabia ya dhambi ya kukatisha tamaa ya watu wa Israeli waliokuwa na agano la upendo na Mungu. Mungu ambaye ni mwaminifu siku zote alishika sehemu yake huku Waisraeli wakiwakilisha wanadamu wasio waaminifu walimkasirisha Mungu sana kwa ibada ya miungu kwa kumfanya ndama na kumweka kama mungu wao, kitu ambacho Mungu alitahadharisha kuwa yeye ni Mungu mwenye wivu ambaye hangependa kushiriki utukufu wake na mwingine. Jambo hili lilimfanya Mungu akasirike na alimwambia Musa ashuke upesi kutoka mlimani akiwa tayari kuwaadhibu vikali watu kwa ajili ya dhambi yao ya kumwasi Mungu. Mungu alitaka hasira yake iwamalize,lakini Musa aliingilia kati kwa kumkumbusha Mungu kwamba aliwatoa Misri kwa kusudi na kwamba alifanya agano na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kwa hiyo, Mungu hakuwaangamiza. Musa aliwaombea msamaha na Mungu hakutekeleza hasira yake ndiko tunakoita rehema na huruma. Hii ni kwa sababu watu walitenda dhambi na adhabu kubwa ilitarajiwa. Hivyo wanapokea msamaha wa dhambi zao. Hiki ndicho anachozungumza Mtakatifu Paulo katika somo la pili kwamba alipata rehema kutoka kwa Mungu. Huruma ya Mungu ndiyo iliyomstahilisha toka kuwa mdhambi mkuu zaidi na kuwa mtume wa Kristo na Kanisa alilolikufuru na kulitesa. Naye anadhihirisha huruma na rehema toka kwa Mungu.
Pamoja na hayo, Utume wa Kristo kuwaokoa wenye dhambi ni tendo kuu la rehema lililoonyeshwa kwa ulimwengu. Alikuwa ni mwenye subira na rehema. Hayo tunasikia katika injili ya leo ambako nasi, tunakuwa sehemu ya Waandishi na Mafarisayo kila wakati tunapowadharau na kuhesabu tu makosa yao. Lakini pia tunakuwa sehemu ya watoza ushuru na wadhambi pale tunapotambua makosa yetu na kutubu. Mafarisayo na waandishi walikuwa kinyume na Yesu ambaye alishirikiana na wenye dhambi huku akilini mwao wakitamani wenye dhambi waadhibiwe na kutengwa. Hii ni huruma ya Yesu iliyompeleka kwa wenye dhambi. Katika sura ya 15 ya Injili ya Luka, Yesu anaeleza mifano mitatu kuhusu kupoteza, kutafuta, na kushangilia. Watu waliotengwa na jamii, wakusanya kodi, au watoza ushuru na watenda-dhambi wanamwendea Yesu wakiwa na hamu ya kusikia yale atakayosema. Katika Injili ya Luka, kusikia na kusikiliza ni ishara ya uongofu. Mafarisayo na waandishi, wakiwa bado wana mawazo potovu na Yesu, wanalalamika kuhusu yeye kushirikiana na watenda-dhambi, ambao wamekuwa wakimsikiliza na kuongoka. Kwa hiyo anawaambia mifano hii mitatu. Katika hadithi ya kwanza, mfano wa Kondoo aliyepotea, mchungaji anaacha nyuma ya kondoo tisini na tisa kutafuta kondoo mmoja aliyepotea. Anapompata, mchungaji hafurahii peke yake bali pamoja na marafiki pia majirani. Vivyo hivyo, Mungu hufurahi zaidi juu ya mtenda-dhambi mmoja anayetubu—kama watu waliofukuzwa ambao wamekuja kumsikiliza Yesu—kuliko wenye haki tisini na tisa kama Mafarisayo na waandishi. Hadithi ya pili, kuhusu mwanamke maskini ambaye haachi kutafuta hadi apate sarafu yake iliyopotea. Pia hadithi hii inasisitiza jambo hilo hilo.
Mfano wa tatu ni wa Mwana Mpotevu. Kama vile Kondoo aliyepotea na Sarafu Iliyopotea, hadithi hii (inapatikana tu katika Injili ya Luka) inamhusu mtafutaji. Baba mwenye huruma na upendo yuko katikati ya mfano huu. Ijapokuwa mwanawe anakimbia na urithi wa baba yake na kutapanya pesa hizo, baba anamngojea, akitumaini kurudi kwake. Mwana wake anaporudi, baba, “akiwa amejawa na huruma,” anakimbia ili kumkumbatia na kumsamehe kabla ya mwana huyo kusema neno la toba. Baba anaonesha furaha ya dhati na kuwaalika wengine kuungana naye katika furaha. Anafanya sherehe kwa kumpata mwanaye aliyepotea. Cha ajabu: mwana mkubwa ambaye amekuwa nyumbani na baba yake akachukia. Mwana huyu ambaye hakuondoka kamwe, kama Mafarisayo na waandishi wanaojiona kuwa waadilifu, anakataa kuingia katika nyumba ya baba yake ili kujiunga na kushangilia kwa kurudi mdogo wake. Amemtumikia baba yake. Amemtii. Lakini haikuwa kwa upendo kutokana na maelezo kwa baba yake anapodhihirisha kwa manung’uniko yake na kuzira. Jibu la baba linatufundisha kwamba utunzaji na huruma ya Mungu inaenea kwa wenye haki na wenye dhambi sawa. Tunapopotea, Mungu hatungoji kurudi kwetu. Anatutafuta kwa bidii. Na wakati waliopotea wanapopatikana, hufanya sherehe na kufurahi. Je sisi tunapokengeuka tunarudi kuomba msamaha kwa Mungu? Je tunawapokeaje wale waliokengeuka wanarudi katika kanisa?
Katika Dominika hii ya ishirini na nne kipindi cha kawaida cha Kanisa, tukiunganishwa na imani yetu katika Kristo Yesu, tunamtafakari Mungu aliye na huruma na upendo usiokuwa na kifani. Katika utangulizi wa kawaida namba mbili wa Misa siku za juma unasema: “…Mungu Mwenyezi na wa Milele, kwa wema uliumba mwanadamu, na alipohukumiwa kwa haki, kwa rehema na upendo ulimkomboa kwa Kristo Bwana wetu…” Huu utangulizi unaendana kabisa na masomo ya leo, ambapo Kanisa linatupa fursa nyingine nzuri ya kutafakari rehema na huruma ya Mungu. Hili limefunuliwa kikamilifu katika Mwanawe Yesu Kristo. Jambo moja muhimu kupitia katika masomo yote ya Dominika hii ni utayari wa Mungu kutukaribisha na kutupokea bila kujali ni kwa kiasi gani tumeanguka, tumemkosea, tumemuasi, tumekengeuka na kwenda mbali naye. Katika somo la kwanza tunaona Mungu ambaye ni mwaminifu kwa ahadi zake. Pia alionyesha kwamba upendo na huruma yake inapita hasira na hukumu yake. Akiwa Baba mwenye rehema na huruma, Mungu alisikia sala za Musa kwa niaba ya watu wake. Kwa hiyo, alitimiza ahadi yake kwamba: “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha na kuomba, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao…” ( 2 Nya 7:14 ). Hivyo tunapaswa kujifunza kutokana na somo hili, nguvu ya maombezi kwa ajili yetu wenyewe na kwa ajili ya wengine. Kama alivyofanya Musa, Kristo Yesu pia anaendelea kutuombea kila siku kwa Baba yake wa milele. Hii ni hasa katika sadaka ya Misa Takatifu. Kwa hiyo, tusichoke kuombeana sisi kwa sisi na kwa ajili ya ulimwengu wetu mbele ya Mungu wetu mwenye rehema na huruma. Kwa hiyo, ni lazima tumkaribie kwa sala daima kwani sala ni mawasiliano na Mungu.
Katika somo la pili Mtume Paulo anatukumbusha kwamba, kama yeye, sisi sote ni mazao ya rehema ya Mungu. Hivyo Mtume Paulo anasimulia jinsi wokovu wake ulivyowezekana kwa maombezi na rehema ya Kristo. Kwa hiyo, kama Paulo, na tuchukue fursa ya rehema hiyohiyo ya kuokoa ya Mungu kwa wokovu wetu wa milele. Pia tuwe na shukrani kwake, anayetuonea huruma kwa njia ya Kristo. Katika Injili ya Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa, Kristo Yesu alishutumiwa kwa kuwakaribisha wenye dhambi. Kupitia matendo na mifano yake, alionesha jinsi alivyo na rehema na huruma kwetu. Licha ya dhambi zetu na ukaidi wetu, Kristo Yesu yuko tayari kutukaribisha tena kwake. Kupitia moyo wake wa rehema na huruma, yuko tayari kufanya mambo yote kuwa mapya kwa ajili yetu tena. Haijalishi itamgharimu kiasi gani. Kwa hiyo, kama mwana mpotevu, ni wakati wa kukubali mwaliko huu. Ni wakati wa kurejea kwa Mungu mwenye rehema na huruma ambaye rehema yake inapita hukumu na ghadhabu yake. Mungu amefanya kurudi kwetu kuwa rahisi sana kupitia Yesu Kristo. Kwa hivyo, tunachohitaji ni kujitambua wenyewe. Kwa unyofu, na kwa unyenyekevu ni lazima tufanye uamuzi muhimu sana kama yule mwana mpotevu: “Nitaondoka mahali hapa na kurudi kwa baba yangu.” Hatupaswi kuona haya kutubu, kuongoka na kumrudia Mungu baba yetu kwa sababu: “Fadhili zake hazikomi kamwe, na rehema zake hazikomi kamwe. Ni mapya kila asubuhi, na uaminifu wake ni mkuu” (Maombolezo 3:22-23).
Pamoja na hayo ndugu mkubwa hana roho ya msamaha na huruma; Alishikilia sana dhambi ya zamani ya ndugu yake mdogo na kukataa kuona majuto na toba. Alidumaa katika maisha ya kiroho na aliona tu maisha ya dhambi yaliyopita na sio yaliyotubu ya sasa. Kwa Mungu kuna msamaha na ukamilifu wa rehema. Yeye si mwepesi wa hasira na ni mwingi wa rehema. Tusitende kama Waandishi, Mafarisayo na kaka mkubwa wa mwana mpotevu anayeshikilia dhambi za wengine badala yake tunapaswa kutenda kama Yesu ambaye anapuuza makosa yetu kwa urahisi na anatusamehe dhambi zetu kubwa na kisha kutukaribisha tena. Na tuwe tayari kusamehe na kuwakaribisha waliotukosea kwa kuwaonyesha rehema. Na tukumbuke kwamba heri wenye rehema kwa maana watapata rehema. Tunaomba rehema za Mungu zitupate kila tunapokosa njia yetu na kwa subira iturudishe kwenye kifua chake cha rehema. Tumuombe Mungu ili tuweze kuhisi kujuta katika njia zetu za dhambi kama zaburi ya leo na kumwomba Mungu na wanadamu kwa ajili ya rehema wakati wowote tunapotambua dhambi na makosa yetu.