Tafakari Dominika ya 24 Mwaka C wa Kanisa: Huruma Na Upendo wa Mungu Vyadumu Milele!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuonesha jinsi huruma ya Mungu ilivyo kuu, haina mipaka ni ya milele. Mungu daima yuko tayari kumsamehe mkosefu anayetubu. Mungu daima anafurahi katika kusamehe na furaha ya kweli anayoweza kuipata mtu maishani ni kung’amua kwamba amesamehewa na Mungu. Waisraeli, Mwana mpotevu na Mtume Paulo ni mifano wazi inayotuonyesha huruma ya Mungu kwa mdhambi akiriye na kutubu makosa yake. Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut 32:7-11, 13-14). Itakumbukwa kuwa Masimulizi ya Agano la Kale yanaweka wazi upendo wa Mungu kwa Taifa la Israeli, kukosa uaminifu na shukrani kwa Taifa hili na huruma na msamaha wa Mungu ulivyojidhihirisha kwao kila walipotubu makosa yao ya kuvunja maagano na kumwasi Mungu. Somo la kwanza la dominika ya 24 mwaka C linasimulia jinsi wana wa Israeli walivyomwasi Mungu kwa kujitengenezea mungu wa ndama wa dhahabu, wakaiabudi na kuitolea dhabihu. Kwa tendo hili waliivunja amri ya kwanza ya Mungu (Kut 20:3-6) na kwa namna hiyo walivunja Agano na Mungu walilolifanya mlimani Sinai, Agano lililotanguliwa na tamko: “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri katika nyumba ya utumwa”, kisha ikafuata amri: “Usiwe na miungu mingine ila Mimi” (Kut 20:2).
Kwa kutenda dhambi hii, Mungu aliazimia kuwaangamiza na kuunda taifa jipya. Musa anachukua jukumu la kikuhani na kinabii, analiombea msamaha Taifa lake kwa Mungu kama walivyofanya makuhani na Manabii katika (Rejea 1Sam 12:19:23; Amo 7:2-5). Maombezi ya Musa hayategemei mastahili ya watu wake, bali yanategea upendo aminifu na huruma ya Mungu kwa watu wake iliyo ya milele na isiyo na mipaka wala ukomo. Kwa ajili ya sala ya Musa, Mungu akaughairi uovu aliokusudia kuwatenda watu wake, akawasamehe nao wakaishi. Nasi tukitambua na kukiri dhambi zetu Mungu Baba yetu ni mwenye huruma atatusamehe na kututakasa na uovu wetu wote. Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timotheo (1Tim 1:12-17). Paulo ni mzee na amemchagua kijana Timotheo kuwa Askofu wa Efeso. Paulo anamtia moyo kuwa atapata magumu katika utume huu. Mashaka na wasiwasi vitamtawala katika kuihubiri Injili, waamini wake wataweza kukata tamaa watakapokumbana na madhulumu, mateso na migawanyiko. Lakini asiogope kwani kuna furaha kubwa katika kufanya kazi ya Mungu.
Mtume Paulo anasisitiza juu ya huruma ya Mungu na furaha aipatayo mdhambi anaposamehewa yeye akiwa ni mfano hai. Naye anashukuru kwa msamaha, neema na baraka alizozipokea kutoka kwa Kristo kwa dhambi zake ambazo zilikuwa ni matokeo ya ujinga, na kwa kutokuwa na imani sahihi. Lakini kwa neema na upendo wa Kristo aliweza kuongoka akiwa njiani kuelekea Damasko kuwakamata, kuwatesa na kuwaua wafuasi wa Kristo. Hivyo maisha yake yalibadilika na kuwa ya furaha kwa kukiri na kutubu makosa yake na kuanza maisha mapya. Paulo anatutia moyo akisema kama Mungu aliweza kumsamehe yeye aliyekuwa mtesi wa Kanisa, na kumfanya kuwa Mtume, basi yeyote yule anayetubu makosa yake atapokea msamaha. Kwa hiyo hatupaswi kuwa na mashaka kuhusu huruma ya Mungu. Kwa maisha yake yote, Paulo aliendelea kutafakari juu ya hali yake ya dhambi ya hapo kale, na juu ya ukarimu, wema, na huruma ya Mungu juu yake hata kusema; “Kwake yeye aliye mfalme wa milele, asiye kufa, asiyeonekana na aliye Mungu wa pekee, kwake, viwe heshima na utukufu, milele na milele. Amina (1Tim 1:17). Nasi pia tukifuata mfano wa Mtume Paulo, wa kuitikia mwito wa Kristo na kukiri madhaifu yetu, kuachana na maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya tukiongozwa na Roho Mtakatifu, huku tukimshukuru Mungu, maisha yetu yatajaa furaha hapa hapa duniani, furaha tutakayoifurahia katika utimilifu mbinguni.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 15:1-32) nayo inaifunua huruma ya Mungu isiyo na mipaka. Itakumbukwa kuwa Injili ya Luka, ni Injili ya huruma ya Mungu na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo. Msisitizo huu tunaona katika masimulizi yake kama vile: Mwanamke mdhambi (Lk 7:36-50); Zakayo mtoza ushuru (Lk 19:1-10), Sala ya Yesu kwa waliomsulubisha (Lk 23:34), na ahadi ya Yesu kwa mwizi aliyesulubiwa pamoja naye na kuomba msamaha (Lk 23:42). Katika sehemu ya Injili tunayoisoma dominika ya 24 mwaka C, Yesu anatufunulia huruma ya Mungu ilivyo kwa kutumia mifano mitatu; Kondoo aliyepotea (Lk 15:4-7), Shilingi iliopotea (Lk 15:8-10), na Mwana mpotevu (Lk 15:11-32). Mifano yote mitatu yaonyesha furaha ilivyo kuu mbinguni, juu ya mkosefu anayetubu na kumrudia Mungu. Ili kulielewa fundisho hili ni muhimu kutambua kwamba mifano yote mitatu inawalenga Mafarisayo na Waandishi kwa chuki waliyokuwa nayo kwa wakosefu na wadhambi na kwa Yesu kwa kuwapokea na kushiriki nao chakula kama inavyoanza sura hii ya 15 ya Injili ya Luka ikisema; “Watoza ushuru na wote wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize” Nao Mafarisayo walimnung’unikia Yesu wakisema; “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi na kula nao” (Lk 15:1-2). Lakini pia tutambue kuwa mifano hii mitatu inategemeana na kukamilishana kwa yenyewe lazima kuisoma na kuielewa kwa pamoja. Mifano miwili ya mwanzo yaani kondoo aliyepotea na shilingi iliopotea inasisitiza ukweli kwamba ni Mungu ndiye anayewatafuta watu waliopotea. Asili ya fumbo la ukombozi ni Mungu mwenyewe. Ndivyo tunavyopaswa kufanya hata sisi kuwatafuta na kuwasamehe waliotukosea. Hapa tunajifunza kuwa msamaha huanza kutolewa na aliyekosewa.
Na mfano wa Baba mwenye huruma kwa mwanae aliyepotea unaweka msisitizo juu ya namna Mungu anavyoheshimu uhuru wa binadamu. Mungu hatushurutishi kurudi kwake na kuomba msamaha. Lakini daima anatusubiri turudi kwake na kusema nimekosa nihurumie naye mara anatusamehe na kutufanya tena watoto wake na kutukaribisha katika ufalme wa mbinguni. Katika mfano huu tunaona kuwa baba mwenye huruma aliwapoteza watoto wake wote wawili. Tofauti ni kwamba yule mdogo alipotea nje ya nyumba kama kondoo aliyepotea nyikani na yule mkubwa alipotea ndani ya nyumba kama shilingi. Makosa ya mwana mpotevu ni mengi na mazito. Alidai urithi kwa baba yake wakati angali hai, hiyo ilikuwa sawa na kusema: “Baba utakufa lini? Baba kwanini unachelewa kufa? Baba huoni kuwa mda wako wa kuishi umeisha, kwanini unaendelea kutuzibia ridhiki yetu?” Pili aliuza urithi wake. Kwa tendo hilo, aliondoa mali toka katika familia yake na hivyo kutoiachia urithi tena. Tatu alikwenda nchi ya mbali. Hapa tunaona kuwa dhambi humtoa mtu kwa Mungu. Siyo Mungu anayejitenga nasi bali ni sisi kwa kutenda dhambi tunajiondoa na kumkimbia Mungu. Tunapomkimbia Mungu, tunakuwa gizani, tunakuwa na huzuni na masikitiko makubwa.
Tunaenda mbali kama vile kifo kilivyo mbali na uhai – maisha. Kwa tendo hilo aliinyima familia yake huduma yake na katika maisha ya kifamilia hayo ni makosa mazito sana. Huko mbali alikoenda alitapanya na kufuja mali zote kwa anasa, akila na kunywa pamoja na makahaba. Dhambi inatufanya tupoteze uzima wa Mungu ndani yetu, maisha ya kiroho tuliyoyapokea kwa batizo. Tunapotenda dhambi tunapoteza furaha na amani ya moyo na zaidi sana uzima wa milele. Hatimaye alijishikamanisha na mwenyeji mmoja tajiri ndiyo kusema alijiuza na kufanywa mtumwa wa kulisha nguruwe, mnyama najisi - mchafu – haramu (Walawi 11:17, Kumb 14: 8). Hii ilikuwa hatua ya kutisha kabisa kutoka kuwa Mwana – Mtu Huru – Mfalme hadi kuwa Mtumwa chini ya shetani. Na shetani akisha kutuhadaa kwa kutushawishi kutenda dhambi kwa ahadi zake nzuri na za kuvutia, baada ya kutenda dhambi, ahadi zake hutoweka badala ya kutupa raha, anatulipa aibu, mateso na mahangaiko. Pamoja na hayo yote alipojichunguza moyoni, akajutia matendo yake, akaamua kurudi kwa Baba yake na kuomba msamaha. Matunda ya toba yake ni msamaha na kufanywa tena mwana katika familia. Hii inatuonyesha kuwa huruma ya Mungu ni ya milele na upendo wake kwetu sisi wanae ni mkubwa kiasi kwamba hakuna dhambi ambayo Mungu hawezi kuisamehe isipokuwa hii ya kufuru kwa Roho Mtakatifu yaani kukata tamaa na kushindwa kuomba msamaha.
Kwa upande mwingine yule mwana wa pili, naye alipotea lakini ndani ya nyumba kama shilingi. Kwa kiburi, chuki na wivu anamkataa ndugu yake na hata kumwambia baba yake “Alirudi huyu mwanao aliyekula mali zako pamoja na makahaba ukamfanyia sherehe” (Lk 15:28-30). Kumbe hata yeye ni mpotevu. Baba yake anatoka kumtafuta na kumsihi arudi ndani, afurahi pamoja na familia yake. Yesu hasemi kama Baba huyu alifanikiwa kumpata mwanae mkubwa? Kila mmoja ajiulize yeye ni kijana yupi aliyepotea ndani ya nyumba kama shilingi au aliyepotea nje ya nyumba kama kondoo nyikani? Kanisa ni jumuiya ya wenye dhambi waliosamehewa. Katika jumuiya yetu, ni karibisho gani tunalowapa ndugu zetu waliovunjika moyo kwa dhambi zao? Tukumbuke daima kuwa dhambi inatufanya kuwa watumwa, lakini ni hamu ya Mungu kutuweka huru tena na kuturudisha nyumbani. Mwaliko kwetu ni kwamba hakuna aliyemkamilifu kila mmoja ana makosa na dhambi zake. Kila mmoja anapotea kwa namna yake. Basi tusikate tamaa bali tuzingatie moyoni ukuu wa upendo na huruma na Mungu Baba, nasi tujirudi na kujisemea moyoni; “Nitaondoka nitakwenda kwa Baba yangu, kwa mama yangu, kwa Mke wangu, Mume wangu, dada yangu, kaka yangu, familia yangu na ndugu zangu” na kumwambia nisamehe nimekosa. Tujue kwamba Mungu, Baba Mwema anatungojea. Tumwombe Roho Mtakatifu atujalie neema zake ili nasi tutambue mwito wa kuomba msamaha kwa Mungu na kwa ndugu zetu ili tuweze kuishi kwa amani na furaha maisha ya hapa duniani na kushirikishwa yale ya mbinguni mara baada ya Mungu kumtuma mjumbe wake – kifo – kuja kutuita turudi kwake. Tumsifu Yesu Kristo.