Tafakari Dominika 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma na Upendo wa Mungu kwa Mwanadamu Mdhambi
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Mwanadamu ni mwenye thamani isiyo na kifani mbele ya macho ya Mungu! Amani na Salama!Injili ya Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa inatuonesha thamani ya mwanadamu hata tunapokuwa wadhambi, na ndio huruma na upendo wa Mungu kwetu wadhambi na wakosefu, lakini zaidi sana furaha kubwa ya Mungu kwa kila mdhambi anapofanya toba na kurudi katika njia ya haki, kurudi katika mahusiano na ukaribu na Mungu aliye Baba na muumba wetu. Injili ya Luka ni Injili ya huruma ya Mungu, na inatuonesha sura halisi ya Mungu. Mifano anayotumia Yesu katika sehemu ya Injili ya leo inatualika na kutusaidia hasa kuweza kuelewa sura halisi ya Mungu. Mungu ni upendo na huruma! Mwinjili Luka anamwonesha Mungu, si tu Baba Mwema anayetuhurumia na kutusamehe dhambi na makosa yetu, bali anayetutafuta bila kuchoka kila mara tunapopotea katika dhambi mpaka atupate na hapo anakuwa na furaha kubwa. Si kwamba sisi tunamtafuta Mungu kwa nafasi ya kwanza, bali Mungu anatutafuta sisi kwanza tunaokuwa gizani kwa kutuangazia mwanga wa neema ya huruma yake, na pia kututoa katika wimbi la uchafu na ubaya wa dhambi. Tunaona leo mifano miwili ya kwanza au ya somo fupi la Injili ya leo ikimuonesha Mungu anayetutafuta kama kondoo aliyepotea na ile shilingi iliyopotea. Furaha ya Mungu ni wokovu wa mwanadamu, ni mwanadamu kubaki katika mahusiano naye!
Na hata katika mfano wa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu ambao kwa leo hatutautafakari, tunaona Mungu anaharakisha na kumkimbilia mwana anayerudi nyumbani, na hivyo baba yake kumfanyia karamu kubwa. Injili ya baba mwenye huruma au kama wengine wanavyopenda kuiita ya mwana mpotevu tuliitafakari vema Dominika ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima mwaka huu, hivyo leo naomba tubaki kutafakari zaidi mifano miwili kama nilivyogusia hapo juu, yaani ya kondoo aliyepotea na shilingi iliyopatikana tena. Mwanzoni tunaposoma Injili ya Luka 15:1-31 tunabaki na mshangao. Pamoja na kwamba Mwinjili Luka anatuonesha watoza ushuru na wenye dhambi walimkaribia Yesu ili kumsikiliza, mara moja anatuonesha kulikuwepo pia Waandishi na Mafarisayo walionung’unika kumuona Yesu akila na kunywa na wadhambi. Na hivyo, Yesu kwa mifano hii ya leo hadhira au walengwa wa mifano hiyo sio wadhambi bali wale watu waliojihesabia haki, na hivyo kidini na kijamii walionekana ni watu safi au wema wasio na dhambi.
Kilichowasumbua waandishi na mafarisayo ni jinsi Yesu alivyokuwa rafiki wa wadhambi na watoza ushuru. Yesu hakuwahubiria hawa wadhambi waache dhambi zao? Yesu anawapokea na kula na kunywa nao, ni nini maana yake? Hayo ni maswali waliokuwa nayo mafarisayo na waandishi, kwani hata nao walimtambua Yesu na kumuona kama mtu wa Mungu, kwa nini basi hafanyi kitu kuwabadili hawa walioonekana wadhambi na wakosefu? Yesu leo anatoa mifano mitatu kama jibu la maswali ya mafarisayo, ni mwito wake kwa mafarisayo kubadili vichwa na mitazamo yao, ndio ukombozi wa fikra au metanoia. Hata nasi leo tunaalikwa pia kubadili mitazamo yetu. Metanoia ya kweli ni ukombozi wa fikra, ndio kufikiri juu ya akili na mitazamo yetu, kuwaza na kufikiri kadiri ya mantiki ya Mungu, ni kuacha mantiki zetu na kuikumbatia ile ya Mungu mwenyewe kadiri ya mwanga wa taa ya Neno lake. Wadhambi ndio wanafananishwa na kondoo aliyepotea au shilingi iliyopotea, lakini cha kushangaza leo wapo ndani pamoja na Yesu wakila na kunywa na kinyume chake wanaobaki nje ni waandishi na mafarisayo waliojihesabia haki. Ndio kusema bila kubadili vichwa na mitazamo yetu, yaani ukombozi wa fikra tunajikuta ni sisi tunaobaki nje na kukosa kushiriki karamu, na furaha pamoja na Mungu mwenye huruma. Hatuna budi kwenda kwake si kama wenye haki bali daima kama wadhambi na wakosefu kama Mtume Paulo anayeshukuru wema na huruma ya Mungu kwake.
Kila mara Yesu anatumia mifano iliyokuwa inaakisi maisha yao ya kila siku. Wayahudi kama wachungaji, mfano wa kondoo aliyepotea ni mfano unaopokelewa na kueleweka kirahisi. Hivyo katika Biblia mara nyingi mfano wa Mungu kama mchungaji na taifa lake kama kondoo unatumika mara nyingi. (Zaburi 23; Isaya 40:11) Na hata Yesu anatumia pia lugha hiyo ya kondoo na wachungaji mara kadhaa katika Agano Jipya. (Marko 6:34). Mifano ya Yesu ya leo tunapotafakari tunakutana na ukosefu wa mantiki iliyo sahihi. Mchungaji anayeacha kondoo tisini na tisa na kwenda kumtafuta moja aliyepotea na kisha kurudi kwa furaha na kupita nyumba kwa nyumba akialika marafiki na majirani kufanya sherehe kwa kumpata kondoo huyo mmoja. Kila tunapojaribu kulinganisha thamani ya huyu kondoo na hiyo sherehe au karamu inayoandaliwa tunakosa uwiano wa mantiki na hata uhalisia. Na hata mfano wa Yesu tunaona anatoa nafasi kubwa kuzungumzia juu ya furaha na karamu kuliko hata ukweli wa kondoo mwenyewe aliyepatikana.
Ni katika muktadha huu tunapata ujumbe wa Injili ya Dominika ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Yesu anatuonesha jinsi gani Mungu anavyokuwa na furaha kwa kila mdhambi anapotubu na kuanza maisha mapya. Furaha ya Mungu ni kubwa hivi hata kualika wengine wote washiriki katika furaha hiyo. Ni furaha isiyoelezeka kwa kila mdhambi kurudi nyumbani kwa Mungu, kuanza tena maisha ya mahusiano ya Baba na mwana. Ni furaha inayoonesha thamani ya mwanadamu, kila mmoja wetu mbele ya Mungu ni wa thamani kubwa hivi hata sisi wenyewe hatuwezi kuielezea. Ni kana kwamba ni mimi tu, au ni wewe tu tunaoishi katika sura ya dunia, sisi ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu, kila mmoja wetu ni yule kondoo aliyepotea awali na kupatikana kwa neema na huruma ya Mungu. Mwanadamu anabaki kuwa mwenye thamani mbele ya Mungu hata anapokuwa mbali yake kwa maisha ya dhambi. Kila mmoja wetu ni wa thamani hivi Mwenyezi Mungu anatusumbukia kwa neema zake za msaada ili tuguswe nazo na kukubali kupokea huruma na msamaha wake wa daima. Huruma na upendo wa Mungu sio tu kwa wale wanaostahili, bali pia kwa wanaokuwa ni wahitaji wa huruma na upendo wake usio na mipaka wala kipimo.
Kwa asili Mungu ni upendo wenyewe, hivyo udhaifu na unyonge wake ni upendo, maana Mungu hajui kuchukia wala kuangamiza bali daima anatupenda hata tukiwa wadhambi na wakosefu kiasi gani. Naomba kusisitiza hili maana kinyume chake ni kufanya kufuru, ni kukosea kuitambua sura ya Mungu. Mifano ya Injili ya leo ni katekesi nzuri na rahisi inayoonesha sura halisi ya Mungu. Kinyume chake ni kufanya uzushi na kufanya kufuru. Kinyume chake tunabaki kuwa na sura isiyo sahihi ya Mungu, na hivyo kujikuta tunajiweka nje na kukosa kushiriki furaha na sherehe ya kupokea huruma na upendo wa Mungu kama anavyosema Mtume Paolo katika somo la pili la Dominika ya leo. Injili ni Habari njema kwetu kwani daima inatuangaza na kutusaidia kuonja wema na huruma ya Mungu kwetu. Ni mwaliko wa daima kwetu kujiweka karibu na Mungu ili tuweze kushiriki furaha yake ya milele. Muunganiko na Mungu ni hakika ya furaha na amani ya kweli mioyoni na nafsini mwetu. Papa Francisko daima anapenda kutumia msemo wa Kihispania unaosema: “Mungu anasamehe daima, mwanadamu mara kadhaa, na maumbile ya asili kamwe hayatusamehi makosa yetu.” Anaendelea kutukumbusha daima kuwa ni sisi tunaochoka kwenda mbele ya Mungu na kuomba msamaha lakini Mungu kamwe hachoki kutusamehe makosa na madhambi yetu. Ni jinsi gani tunabaki na mshangao kukutana na ukweli huo juu ya huruma na msamaha wa Mungu kwetu!
Marabi walirudiarudia kwa desturi mafundisho yao ili yaweze kueleweka vyema kwa wanafunzi wao, na ndio "pedagojia" anayotumia leo Yesu katika mifano hii ya huruma ya Mungu. Na si kwa makosa Mwinjili Luka anatuonesha ni kwa jinsi gani Yesu alitaka fundisho hili lieleweke vema na kwa uwazi juu ya sura halisi ya Mungu, ni huruma na upendo usio na kifani, usioelezeka na hata kueleweka kwa akili na mantiki zetu za kibinadamu. Mungu anayetusamehe daima hata madhambi makubwa kiasi gani mbele ya macho yetu ya kibinadamu. Mfano wa pili, ni wa shilingi iliyopotea katika nyumba. Tunaona mwanamke akifanya kila juhudi na bidii ili kuipata pesa ile iliyopotea. Ndio kusema jinsi gani Mungu hawezi kutulia tunapokuwa mbali naye, tunapokuwa tumepotea, maanake mbali na macho yake yenye huruma na upendo. Tumeumbwa kukaa na kubaki sote mbele ya macho ya Mungu na si kinyume chake. Mwanamke yule anawasha taa ili kuitafuta shilingi ile, ndio kusema taa inayoweza kutusaidia katika maisha ya kila mfuasi wa Yesu Kristo ni Neno la Mungu, ni kwalo tunang’amua na kutambua kusudi na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Hivyo Neno lake ni taa na mwanga wa miguu yetu kama anavyotuambia Mzaburi. Mungu anatutafuta tena kwa bidii na uvumilifu mkubwa, anatusubiri kila mmoja wetu kurejea na kubaki katika mahusiano ya upendo naye. Sisi sote ni wadhambi na hivyo tunahitaji huruma na upendo wake ili tuweze kushiriki katika ile furaha na sherehe ya milele. Habari ya msamaha na huruma ya Mungu, ni habari njema kwetu, kwani tunakiri na kutambua kuwa daima tunaenda kinyume na mapenzi yake. Hivyo, kila mara tuzidi kumuomba ili tutambue ni Yeye anayetutafuta sisi kwanza kwa njia ya neema zake za msaada. Nawatakia Dominika na tafakari njema.