Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma, upendo na msamaha wa Mungu unakita mizizi yake katika toba na wongofu wa ndani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma, upendo na msamaha wa Mungu unakita mizizi yake katika toba na wongofu wa ndani.  

Tafakari Dominika 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Toba, Wongofu; Huruma na Upendo wa Mungu!

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaonesha kwamba “Mungu ni mwenye huruma: huruma ya Mungu i wazi kwa wale wanaotubu na kumwongokea tena.” Ni kwa huruma ya Mungu sisi wadhambi tunapewa fursa ya kuwa karibu na Mungu (kumrudia Mungu) na ni kwa huruma ya Mungu sisi wadhambi tunastahilishwa kumtumikia Mungu.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli Napoli, Italia.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaonesha kuwa “Mungu ni mwenye huruma: huruma ya Mungu i wazi kwa wale wanaotubu na kumrudia Yeye.” Ni kwa huruma ya Mungu sisi wadhambi tunapewa fursa ya kuwa karibu na Mungu (kumrudia Mungu) na ni kwa huruma ya Mungu sisi wadhambi tunastahilishwa kumtumikia Mungu. SOMO LA KWANZA: Kut. 32:7-11, 13-14. Somo letu la kwanza linatufunulia kuwa “Mungu ni mwenye huruma kwetu sisi licha ya dhambi tunazotenda.” Musa alipopanda mlimani Sinai alikawia kushuka (rejea Kut. 32:1). Musa, ambaye anamwakilisha Mungu, alipokawia kushuka toka mlima Sinai kuliwafanya Waisraeli kutetereka kiimani: walidhani pengine Musa amekufa huko mlimani au amepatwa na jambo baya. Tukio hilo liliwafanya wafikiri kuwa sasa Mungu amesitisha mpango wa kuwakomboa (maana Musa kiongozi wao hajulikani kapatwa na nini), ama Mungu amesitisha mawasiliano nao au ameamua kuwaacha kabisa. Baada ya hali hiyo kujitokeza Waisraeli wanatafuta ufumbuzi wa yale waliyofikiri kwenye mawazo yao: wanatengeneza sanamu ya ndama wa dhahabu ili iwe mbadala wa Mungu na kisha kuisujudu na kuisifia kuwa ndiyo mungu aliyewatoa utumwani Misri.

Dhambi hii inamgadhabisha sana Mungu na anakusudia kuwaadhibu. Hata hivyo, Musa anaposhuka na kukuta hali hiyo anawaombea msamaha kwa Mungu na Mungu anawasamehe. Hapa tunajifunza kuwa “Mungu ni mwingi wa huruma na msamehevu pindi tumwombapo msamaha.” Hata sisi kuna nyakati tunafikiri Mungu ametuacha kwa kuwa tunadhani “anakawia” (anakawia kutufikishia ujumbe wake, amekawia kujibu sala zetu, amekawia kutupatia mahitaji yetu). Mara kadhaa tunadhani Mungu amesitisha kuwasiliana nasi au hana mpango na sisi. Hali hii inatupelekea kutengeneza “miungu ya bandia/ miungu ya sanamu” na kudai kuwa imetukomboa: tunatengeneza mungu-pesa, mungu-waganga, mungu-mali na mungu-miujiza (yaani badala ya kumtafuta Mungu tunatafuta miujiza). Tunajivunia kuwa mganga fulani ndiye aliyenikomboa kutoka kwenye umaskini, mhubiri fulani ndiye uliyenisaidia kunitoa kwenye mikosi na mikasa ya maisha, pesa zangu zimenitoa kwenye umaskini na kadha wa kadha. Wengi wetu tumejitengenezea miungu yetu ya kubumba. Hii ni dhambi kubwa sana. Hata hivyo, tukiomba msamaha wa dhambi hizi na kufanya toba ya kweli na kuamua kumrudia Mungu wa kweli, Mungu atatusamehe na kutuonesha huruma yake. Huruma ya Mungu huondoa dhambi zetu. Tuikimbilie huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, kwa kufanya hija ya kiroho, kwa kusamehe wenzetu na mengineyo.

SOMO LA PILI: 1 Tim. 1:12-17: Somo letu la pili linatufunulia kuwa “Mungu anatuchagua kumtumikia si kwa sababu ya mastahili yetu bali kwa sababu ya huruma/rehema yake.” Leo Mtume Paulo anatueleza historia ya mwenendo wake wa zamani ya kwamba alikuwa mtu mwovu: mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri. Paulo, kwa kadiri ya mtazamo wetu wanadamu, asingestahili kuwa mhubiri wa Injili kwa sababu ya historia yake hii mbaya. Hata hivyo, kwa Mungu ni kinyume kabisa. Mungu hachagui wakamilifu au wale tu wenye historia nzuri au wema tu au walio bora zaidi, bali Mungu huchagua watu wadhambi, dhaifu, wanyonge na ambao wanaoonekana kuwa hawafai na kisha kuwapatia rehema ili wawe vyombo aminifu kwa huduma yake. Katika uhalisi Mungu/Kristo alikuja hasa kwa ajili ya watu wa wadhambi, wadhaifu na wenye mapungufu. Mungu yupo tayari kuwapatia rehema/huruma yake ili wawe wema na kisha kuwatumia katika utumishi wake mtakatifu. Mungu yupo tayari kuwastahilisha wale wasiostahili ilimradi tu wapo tayari kufungua mioyo yao ili kuruhusu neema ya Mungu kuwageuza wawe bora siku kwa siku. Mungu anaporuhusu tuteuliwe katika utumishi fulani hatupaswi kusahau kuwa si kwa mastahili yetu bali kwa huruma/rehema ya Mungu: hakuna chochote kizuri ndani yetu kinachomlazimisha Mungu kutupa majukumu fulani au kututeua kwa huduma fulani. Licha ya kuteuliwa kwa huduma mbalimbali tunapaswa kufahamu kuwa sisi si bora mbele za Mungu kwani tu wadhambi, wadhaifu, wenye mapungufu na pengine historia ya maisha yetu ya zamani/sasa haina tofauti na historia ya zamani ya Mtume Paulo. Hivyo, tutambue kuwa Mungu anaendelea kututumia/kutuchagua ili kutuunda zaidi na hatimaye tupate wokovu. Hivyo, huruma ya Mungu haiwaweki kando wadhambi/wadhaifu bali inatuvuta kwa Mungu.

SOMO LA INJILI: Lk. 15:1-31: Somo letu la Injili linatufunulia ujumbe kuwa “Mungu ni mwenye huruma nyingi kwa mdhambi anayetubu”. Katika Injili yetu ya leo Yesu anatoa mifano mitatu: kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na Mwana Mpotevu. Katika simulizi hizi kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na mwana mpotevu vinasimama kutuwakilisha “sisi wadhambi” ambao dhambi hututoa katika mikono ya Mungu lakini toba huturudisha kwake. Mifano miwili ya kwanza inaonesha jinsi Mungu anavyohangaika kuwarudisha wadhambi katika miliki yake: Mungu haridhiki kuona mtu anaishi katika dhambi. Simulizi la tatu ambao Yesu analitoa katika Injili yetu ya leo kwa miaka mingi limeitwa “Simulizi la Mwana Mpotevu”. Hata hivyo, tunashauriwa kuliita “Simulizi la Baba mwenye Huruma/Upendo” kwani uzito wa simulizi hili uko zaidi kwa Baba anayempokea kijana wake mdogo kwa huruma na upendo licha ya dhambi alizotenda.  Yesu ametoa simulizi hili ili kuwachangamotisha “Mafarisayo na Waandishi” ambao walijiona wao ni wema zaidi na hivyo kunung’unika baada ya kumuona Yesu akichangamana na watoza ushuru na wenye dhambi. Kimsingi mtoto mkubwa katika simulizi hili anawawakilisha “Mafarisayo na waandishi” kwani mtoto mkubwa alijiona ni mwenye haki mbele ya Baba yake na asiye na dhambi, na hivyo kumtazama mdogo wake kama mdhambi asiyestahili kusamehewa. Hulka ya kijana mkubwa inaakisi hulka ya Mafarisayo na waandishi: kujiona kuwa wao ni wenye haki zaidi na hivyo kuwatazama wengine kuwa ni wadhambi wasiostahili kusamehewa.

Mungu ni mwingi 2wa huruma na mapendo kwa wanotubu
Mungu ni mwingi 2wa huruma na mapendo kwa wanotubu

Yesu, kupitia simulizi la Baba Mwenye Huruma, anataka kufundisha kuwa hata wadhambi wana nafasi kwa Mungu (nafasi ya kumkaribia Mungu) ikiwa watafanya toba na kukusudia kuacha mwenendo wao wa dhambi. Hivyo, Yesu anaonesha hatua za kufanya hiyo toba na namna Mungu anavyompokea mdhambi baada ya kufanya toba. KWANZA, tutazame hatua za kufanya toba kutoka kwenye Simulizi la Baba Mwenye Huruma (Mwana Mpotevu): (i) Tafiti moyo. Maneno “alipozingatia moyoni mwake” yanaonesha kuwa mwana mpotevu aliingia ndani ya moyo wake na kujitafiti na kugundua kuwa alifanya makosa. Ni ndani ya mioyo yetu ndipo tunagundua madhaifu na mapungufu yetu. Kumbe hatua ya kwanza ya kuelekea toba ni kurudi ndani ya mioyo yetu na kujitathmini mahusiano yetu na Mungu, wenzetu na nafsi zetu wenyewe. (ii) Kukumbuka wema wa Mungu. Mwana mpotevu anakumbuka wema wa baba yake: “Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanakula chakula na kusaza…” Tunapofanya toba tujiulize ni mema mangapi ambayo Mungu ametutendea na kujihoji kama tuna uhalali wa kukaa mbali na Mungu anayetutendea mema mengi. (iii) Kukubali/kukiri dhambi/mapungufu yetu. Mwana mpotevu anasema, “nitakwenda… kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele zako.”

Hapa mwana mpotevu anakubali makosa yake na hivyo anatufundisha kukiri dhambi/mapungufu yetu. Hatuwezi kufanya toba na kupokea msamaha wa Mungu na jirani kama hatupo tayari kukiri dhambi/mapungufu yetu. Kukiri dhambi ni kuwa tayari kuwajibika kwa dhambi zetu bila kutafuta visingizio kama vya Adam na Eva vya kurushiana lawama. Wengi wetu huwa hatupo tayari kukiri/kukubali mapungufu yetu na badala yake tunafanya kila liwezekanalo kujisafisha ili tuonekana hatuna hatia. Tubadilike. (iv) Safari ya kumrudia Mungu- safari ya toba. Mwana mpotevu hakuishia tu kusema nitakwenda kwa baba yangu bali alianza kweli safari ya kurudi kwa baba yake. Hakuishia kutamani kurudi bali alifanya safari ya kurudi. Wengi wetu huwa tunatamani kumrudia Mungu lakini hatufanyi safari kwenda kumrudia Mungu. Tamaa pekee haitoshi. Tuanze kweli safari ya kumrudia Mungu kwa kujongea Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho, kwa kuwa na unyenyekevu, kwa kuwaomba msamaha wa dhati wale tuliowakosea, kwa kujinyima, kwa kujiadabisha sisi wenyewe (self-discipline) na mengineyo. PILI, tutazame jinsi Mungu anavyodhihirisha huruma na upendo wake kwa wadhambi: (i) Mungu humsubiri kwa hamu kubwa mdhambi arejee kwake. Tunaambiwa kuwa baba alimwona mwanae akingali mbali. Tendo hili la kumwona mwanae akingali mbali linaonesha kuwa daima baba huyu alikuwa na shauku ya kumwona mwanae anarejea tena kwake akiwa hai. Hii ndiyo hulka ya Mungu. Mungu haridhiki wala kutulia mdhambi akianguka dhambini bali daima anamngoja kwa hamu atubu na kurudi kwake.

Jifunzeni kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti
Jifunzeni kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti

Daima Mungu anamwonea huruma mdhambi. (ii) Mungu hajali historia ya nyuma ya mdhambi. Katika simulizi hili baba hapotezi muda kumuhoji mwanae ya kwamba alikuwa wapi na alikuwa anafanya nini baada ya kuondoka nyumbani na wala hamlaumu kijana wake kwa yale aliyofanya. Kadhalika, Mungu haitaji maelezo yetu mengi bali anatazama zaidi moyo uliopondeka. Historia ya nyuma ya mtu mdhambi si jambo la muhimu kwa Mungu. Jambo la muhimu kwa Mungu ni kuwa mdhambi ametubu na kuanza maisha mapya ya kiroho. (iii) Mungu huturudishia hadhi ya kuwa watoto wake tunapotubu. Baba anaagiza mwanae avikwe viatu ili kuonesha kuwa amekuwa si mtumwa bali ni mtoto wake (watumwa hawakuvaa viatu lakini mtoto alivaa viatu). Kwa kufanya toba na kuishi maisha mema tunarudishiwa hadhi ya kuwa wana wa Mungu na tunaunganika na Mungu (pete anavyovalishwa mwana mpotevu ni ishara ya kurejea kwa muungano na umoja kati yake na baba yake). Tusiogope kumrudia Mungu kwani ni Mwenye Huruma na Upendo mwingi, hasa kwetu sisi wadhambi. (iv) Mungu pamoja na miliki yake hufurahi sana mdhambi akitubu.

Wayahudi wakereketwa walikuwa na msemo wao kuwa “kuna furaha kubwa zaidi mbinguni kwa mdhambi mmoja akifutiliwa mbali [akifyekelewa mbali]”. Furaha ya baba baada ya mwanae kurudi nyumbani inaashiria furaha kubwa ya Mungu na miliki yake pale mdhambi mmoja anapotubu. Mungu hafurahii mdhambi akifutiliwa mbali. Mungu hafurahii kifo cha mtu mwovu, bali auache mwenendo wake mbaya apate kuishi. Kwa miaka mingi tumekuwa tukimtazama yule mtoto mdogo kwenye simulizi hili kama mwana mpotevu. Hata hivyo kijana mkubwa naye ni mpotevu, tena mpotevu mkubwa. Tofauti yao ni hii: “yule mdogo alipotea kwa muda tu” na “yule mkubwa alipotea jumla jumla.” Kijana yule mkubwa ndiye mpotevu haswa: kwa kujiona yeye ni mwenye haki kuliko yule mdogo, kwa kuona kuwa yule mdogo ni mkosaji zaidi na hivyo hastahili kupata msamaha wa baba yake. Hata sisi hatuna tofauti na kijana mkubwa kwani mara nyingi tunajiona sisi ni wema kuliko wengine na kuwaona wengine kana kwamba ni wadhambi wakubwa na hivyo wanastahili kuangamizwa. Hatuna tofauti na Mafarisayo na waandishi. Wote ambao tuna mtazamo kama wa huyu kijana mkubwa tumepotea, tena sana.

09 September 2022, 11:46