Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Mama Kanisa anatangaza na kushuhudia wema, ukarimu na ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu mdhambi. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa: Mama Kanisa anatangaza na kushuhudia wema, ukarimu na ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu mdhambi. 

Tafakari Dominika 24 ya Mwaka C: Wema, Ukuu Na Huruma ya Mungu

Leo tunayatafakari masomo ambayo yanaweka katika upande mmoja udhaifu na upotevu wa mwanadamu na katika upande wa pili yanaweka ukuu, wema na huruma ya Mungu Baba. Ni mwaliko wa kutambua kuwa safari yetu ya imani ni safari ambayo ukuu, wema na huruma ya Mungu Baba huja kutusaidia kuushinda udhaifu na upotevu wetu ili kutuwezesha kuufikia wokovu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanaweka katika upande mmoja udhaifu na upotevu wa mwanadamu na katika upande wa pili yanaweka ukuu, wema na huruma ya Mungu Baba. Ni masomo basi yanayotualika kutambua kuwa safari yetu ya imani ni safari ambayo ukuu, wema na huruma ya Mungu Baba huja kutusaidia kuushinda udhaifu na upotevu wetu ili kutuwezesha kuufikia wokovu. ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Kutoka (Kut 32:7-11, 13-14) na linatuletea tukio la waisraeli kutengeneza ndama ya dhahabu na kuanza kuiabudu kama mungu wao. Ni wakati ambapo waisraeli wako jangwani katika safari yao ya kuelekea nchi ya ahadi, Musa kiongozi wao ameitwa na Mungu mlimani Sinai ili apokee maneno ya Agano na amri kumi. Musa anachelewa kurudi kutoka mlimani, waisraeli wanatengeneza sanamu ya ndama na kuanza kuiabudu. Hii ni dhambi ya uasi kwa Mungu aliyewakomboa na ni dhambi ya upotevu kwa maana wanatoka katika njia inayowapeleka nchi ya ahadi na wao wanashika njia nyingine.

Waisraeli wanafikia hatua hii ya uasi kwa sababu wapo jangwani. Jangwani hakuna maji, hakuna mimea, hakuna chakula hakuna hali nzuri ya hewa. Ni mahala ambapo hakuna uhakika wa maisha na mtu hajui afanye nini. Zaidi ya hayo, wanajikuta wako peke yao kwa sababu Musa kiongozi wao yuko mbali. Wanachofanya ni kujitafutia mahali pa kushika na mahali pa kuwapa uhakika. Na wapapotafuta kufanya hivyo bila Mungu, wanaingia katika dhambi ya uasi, dhambi ya kuabudu miungu wengine; dhambi ya ushirikina. Upotevu wa mwanadamu. Somo la Injili linaendeleza dhamira hii hii ya upotevu wa mwanadamu linapotupatia mifano mitatu ambayo Yesu anaitoa kuhusu kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na mwana mpotevu (Lk 15:1-32). Mifano hii ya Yesu haikomei tu kuonesha upotevu, inakwenda mbele zaidi kuonesha jibu la Mungu katika upotevu wa mwanadamu. Jibu hilo la Mungu ni jibu la wema na huruma yake ambayo daima ni ya ajabu na hushangaza. Katika mfano wa kondoo aliyepotea, ajabu ya wema na huruma ya Mungu inajitokeza katika mchungaji ambaye yuko tayari kuwaacha kondoo 99 walio salama ili aende kumtafuta yule mmoja aliyepotea. Katika mfano wa shilingi iliyopotea, ajabu ya wema na huruma ya Mungu inajionesha katika mwanamke ambaye anatumia gharama kubwa kutafuta shilingi iliyopotoea na akishaipata anatumia gharama kubwa zaidi kufanya sherehe.

Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli
Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli

Na katika mfano wa mwisho wa mwana mpotevu, ajabu ya wema wa Mungu inaonekana katika baba anayempokea na kumfanyia sherehe mtoto aliyeasi kiasi cha kumkwaza yule ambaye alibaki nyumbani akishughulika na kazi za nyumbani. Hilo ndilo jibu la Mungu kwa upotevu wa mwanadamu ili kwa wema na huruma yake mwanadamu apate kurudi kutoka upotevu wake aishi. Mtume Paulo tunayemsikia katika somo la pili (1 Tim 1:12-17) anatoa ushuhuda wa kuwa mmoja wa waliosaidiwa na huruma ya Mungu kurudi katika njia ya imani kutoka katika upotevu. Anasema hapo mwanzo alikuwa mtukanaji, mwenye kutesa watu na mwenye majivuno. Aliipokea neema ya Mungu na neema hiyo ikamtia nguvu hadi kumfanya kuwa mtumishi wa Mungu na mtumishi wa wale wale aliokuwa akiwatesa. Mtume Paulo anakuwa shuhuda kuwa udhaifu na upotevu wa mwanadamu haviwezi kuwa na neno la mwisho kuhusu maisha ya mwanadamu endapo mwanadamu atakubali kuupokea wema na huruma ya Mungu inayookoa.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, mazingira ya somo la kwanza la leo yanaelezea chimbuko na matokeo ya dhambi ya kubudu sanamu iliyo dhambi ya kuabudu miungu wengine. Mazingira hayo ni jangwani, mahala ambapo waisraeli walijikuta hawana mahitaji yao, wapo katika hali ya kukosa na hawana uhakika na kesho yao kwa sababu kiongozi wao Musa alikuwa mbali. Ndugu zangu, mazingira hayo ya jangwani ndio mazingira ya kila siku ya maisha yetu. Katika maisha mwanadamu daima hujikuta katika uhitaji na katika ile hali ya kutokuwa na uhakika wa mambo kadhaa kuhusu maisha yake ya kesho. Upo uhitaji wa fedha, upo uhitaji wa kazi au ajira, upo uhitaji wa mwenza wa ndoa, upo uhitaji wa mtoto katika ndoa n.k. Sasa katika kutafuta vitu kama hivi vinavyokosekana katika maisha ya mtu kulingana na uhitaji wake ipo hatari ya kugeuza uhitaji wenyewe au vitu mtu anavyodhani vitamtimizia uhitaji wenyewe kuwa mungu mwingine, na hivyo mtu akavishikilia na kuviishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Ibada ya sanamu haimaanishi tu kuingia moja kwa moja katika ushirikina au kuwa na sanamu inayoonekana. Ibada ya sanamu inaanza katika kile ambacho mtu anakijenga kwanza kichwani na kukiweka moyoni kuwa ndio mhimili wa maisha yake na ndicho kilichomwezesha au kupata anachokosa au kutunza alichokikosa na hicho anakipa nafasi kubwa kuliko nafasi ya Mungu katika maisha yake.

Sakramenti za Kanisa ni chemchemi ya huruma, neema na baraka za Mungu
Sakramenti za Kanisa ni chemchemi ya huruma, neema na baraka za Mungu

Matokeo ya ibada ya sanamu ni yapi? Licha ya kuwa ni dhambi dhidi ya amri ya kwanza ya Mungu, ibada ya sanamu hizi mtu anazozijenga moyoni zinaidhalilisha ile hadhi ya kimungu ambayo Mungu mwenyewe ametupatia siku ya ubatizo wetu. Mfano huu tunauona katika Injili ambapo mwana aliyeondoka nyumbani alijikuta kwanza akifanya kazi ya kulisha nguruwe na tena kutamani kula pamoja na nguruwe hao kwa sababu hakuwa na wa kumpa chakula. Katika tamaduni za Wayahudi, nguruwe alikuwa ni mnyama ambaye hawakuruhusiwa hata kumsogelea kwa sababu alikuwa najisi. Mwana huyu kwa kosa lake la uasi alijikuta si tu akimsogelea mnyama najisi bali alijigeuza yeye kuwa kama nguruwe kwa kutamani kula anachokula nguruwe. Dhambi inadhalilisha hadhi ya mwanadamu, dhambi ya kuabudu miungu wengine inadhalilisha hadhi ya kimungu ambayo Mungu mwenyewe ametupatia. Na haya ndiyo matokeo ya ibada kwa sanamu. Wema na huruma ya Mungu baba inayotangazwa daima na Kanisa na inayotangazwa katika masomo yetu vituvute kutoka upotevu wetu tuweze kurudi nyumbani kwa Mungu baba mwenye huruma ili tuupate wokovu.

Liturujia Dominika 24
09 September 2022, 15:05