Tafakari Dominika 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Matumizi Halali ya Mali za Dunia: Huduma ya Upendo
Na Padre Efrem Msigala,OSA, - Dar es Salaam.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News, Karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 25 ya Mwaka C wa Kanisa. Kristo Huwatetea Maskini na Wanyonge Katika jamii. Dominika hii ya ishirini na tano ya mwaka C kipindi cha kawaida, Kanisa linatuagiza kutafakari mtazamo wetu kuhusu fedha, vitu vya kimwili, na hasa, mtazamo wetu kwa maskini na waliotengwa. Dhuluma, uroho wa madaraka na uonevu ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo yameendeleza umaskini katika jamii zetu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanazingatia uhuru wa mtu katika mambo ya kiuchumi kuwa ni tunu msingi na haki ya mtu asiyoweza kuondolewa ambayo inapaswa kuenziwa na kulindwa. Kila mtu anayo haki ya kukuza kipaji cha ubunifu wa kiuchumi na kutumia kihalali vipaji vyake katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kupata matunda ya haki za kazi yake. Rej. Mafundisho Jamii ya Kanisa, 336. Katika somo la kwanza, Nabii Amosi analaani ukosefu wa haki na uonevu dhidi ya maskini. Aliandika wakati ambapo matajiri walichukua ardhi yote na "kuwafanya watumwa" maskini katika mashamba yao. Walisafirisha chakula nje ya nchi ili kujipatia pesa zaidi, huku maskini wakifa kwa njaa.
Leo, tunakabiliwa na hali kama hizo ulimwenguni pote. Ingawa wengine hawawezi kumudu mlo mmoja kwa siku, wengine wanapoteza pesa kwa miradi isiyo na faida kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Wengine humwaga chakula wakati jirani hawana chochote. Wakati mwingine, kisingizio tunachotoa ni kwamba maskini ni wavivu, wakati huo huo wapo ambao wamenyang’anywa hata maeneo yao na wenye nguvu kifedha au madaraka. Ukweli ni kwamba kuna tamaa nyingi; kama za madaraka, utajiri kwa njia isiyohalali, tamaa ya mali na pia ukosefu wa haki na ufisadi katika ulimwengu wetu. Kitu ambacho nabii Amosi alikiona nyakati zake na leo pia katika jamiii zetu. Kitu kingine ambacho nabii Amosi anagusia ni wafanyabiashara wanaotengeneza mizani kimtindo ili kuwaibia watu wanaponunua bidhaa zao na wapo hata nyakati zetu. Nabii Amosi anasema “...mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu...” hali hiyo ilikuwepo enzi za Amosi na nyakati zetu wapo watu wasio waaminifu katika biashara zao. Kanisa halijawa nyuma katika swala la maisha ya kijamii.
Papa Leo XIII baada ya kuona hali halisi ya kijamii nyakati zake alitoa waraka kujibu swali kubwa la kijamii, akaandika Barua ya kwanza ya Kichungaji inayoitwa Rerum Novarum, yaani “Mambo Mapya” Barua hii inachambua hali ya wafanyakazi wa mishahara ambao waliishi katika hali mbaya isiyo ya kiutu kutokana na kugandamizwa na waajiri wao na pia wenye madaraka. Barua pia inachambua masuala ya kijamii na kisiasa ili kuruhusu tathmini kufanyika katika mwanga wa Injili. Hati hii inaorodhesha dosari zinazopelekea matatizo ya jamii, kuweka pembeni itikadi ya misingi ya usawa na kusababisha haki za wanyonge kukosekana. Hivyo basi kanisa limeendelea kutoa mafundisho sahihi juu ya mafundisho ya jamii katika msingi wa injili. Mtakatifu Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Timoteo anatusihi tuombe kwa ajili ya kila mmoja hasa, wafalme, watawala na viongozi katika serikali zetu ili watende haki. Anasema “kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka...”. Sala ni muhimu kwa uongofu na kwa hekima. Viongozi wetu kwa nafasi mbalimbali, wakiongoka wakawa na hofu ya Mungu na wakawa na hekima watasaidia kukomesha ufisadi, dhuluma na uonevu katika jamii na mifumo mibovu au mifumo gandamizi.
Hilo ni muhimu sana kwa sababu kama vile Mtume Paulo anavyosema: “Mungu anataka kila mtu aokolewe na kupata ujuzi kamili wa kweli.” Ukweli huu ni kwamba, kuna Mungu mmoja tu, na kwamba sisi sote ni watoto wake. Katika Waraka wa Pili kwa Timotheo tunaambiwa kwamba “Mungu anataka wote waokolewe” na kwamba ni “mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na wanadamu, yaani Yesu Kristo” Anatupenda sote kwa usawa, na anatamani sote tufanikiwe na kuwa na afya njema, na pia roho zetu zifanikiwe. Mara tu tunapoelewa hili, ubinafsi utatoweka, na tutaanza kuzingatia maslahi na manufaa ya wengine. Ni mapenzi ya Mungu kwamba sisi sote tuokolewe. Hii ni pamoja na kuokolewa na njaa. Inamaanisha kuokolewa kutokana na udhalimu, ulafi na ufisadi ambao umeharibu ulimwengu wetu na kuwaacha wengi kuwa maskini, wengi kukosa haki zao na wengi kunyanyaswa. Injili ya leo, Yesu anatukumbusha ukweli kwamba pesa na vitu vya kimwili havidumu milele. Kwa hiyo, anatushauri jinsi ya kuzitumia bila kupoteza wokovu wetu. Kuna msemo kwamba: "Njia bora ya kuwekeza ni kuwekeza kwa maskini." Kwa hiyo tujifunze kuwekeza kwa maskini ili kuboresha hali zao. Kujilimbikizia mali bila kuzitumia kuwasaidia wenye uhitaji ni uchoyo na ubinafsi. Pesa na mali huwa na thamani pale tu vinapotumiwa kwa busara kuwasaidia wale wanaotuzunguka na kwa huduma mbalimbali za kanisa.
Haina thamani ya kudumu pale ambapo tunashikilia kwa bidii fedha na mali kuliko Mungu, na kwa hasara ya maskini. Pia, ni watu wasiomcha Mungu pekee wanaotumia mali zao kuwakandamiza maskini na wanyonge. Hii ni kwa sababu, wao ni kama “mpumbavu asemaye hakuna Mungu” (Zab 14:1). Kinyume chake, mwenye hekima hutumia mali yake kuwasaidia wenye uhitaji na kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kanisa na hivyo, kujiwekea mali mbinguni. Kwa hiyo, ni muhimu kujua kwamba tunapobarikiwa na Mungu kwa mali, sisi ni watumishi wake tu. Utajiri hutolewa kwetu kwa madhumuni ya kusaidia na kuboresha maisha ya wale wanaohitaji na ujenzi wa kanisa lake. Haijakusudiwa sisi na familia zetu tu. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na hisani nayo. Hatimaye, tusiwadanganye maskini na wahitaji kwa ajili ya kujinufaisha kiuchumi. Hii ni kwa sababu, aina yoyote ya udhalimu au ukandamizaji dhidi ya maskini au wanyonge humlilia Mungu kwa ajili ya kulipiza kisasi kama damu ya Abeli ilivyofanya (Mwanzo 4:10). Kristo ndiye mtetezi wa maskini na waliotengwa.