Tafakari Dominika 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Rushwa na Ubadhilifu!
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli Napoli, Italia.
Katika Injili Yesu anatupatia mfano wa “wakili dhalimu.” Wakili ni mtu aliyepewa kusimamia mali/biashara za mtu mwingine na hivyo mwisho wa siku alipaswa kutoa hesabu ya namna alivyosimamia mali za mmiliki: faida, hasara na hata changamoto. Ilikuwa ni kazi ambayo inamdai mtu uaminifu mkubwa. Wakili huyu anayetolewa mfano na Yesu hakuwa mwaminifu maana alitumia vibaya mali alizokabidhiwa kusimamia (ubadhilifu wa mali). Kitendo cha kutapanya mali za bwana wake kilikuwa na athari kubwa mbili: (i) alimchafulia sifa mwenye mali. Watu kwa vyovyote vile walimdharau au kumkejeli mwenye mali kuwa siyo mtu makini maana amempa kazi mtu ambaye hana uaminifu, tapeli tu mwenye kufanya ubadhilifu wa mali alizopewa kusimamia. Hali hii kwa vyovyote vile ilisababisha au ingesababisha watu wasiwe na ushirika naye katika biashara. (ii) Yeye mwenyewe wakili alijichafulia jina maana mbele za watu ni tapeli na hivyo hakuna mtu mwingine anayeweza kumwaminisha mali/biashara zake. Hawezi kupata tena ajira ya kuwa wakili. Kwa kuwa tayari kulikuwa na dalili za kuachishwa kazi ya uwakili, wakili huyu alitafakari cha kufanya ili hata atakapofukuzwa kazi basi apokelewe na watu wa kawaida maana siyo rahisi kupata tena kazi ya uwakili na yeye mwenyewe anasema, “kulima siwezi, kuomba naona haya.” Mwishoni wakili huyu atasifiwa siyo kwa sababu amewapunguzia watu madeni yao (maana nao ni ulaghai na ni kuendelea kumtia hasara mwenye mali), bali anasifiwa kwa jinsi alivyotumia maarifa, nafasi na muda wake mchache kutengeneza maisha yake ya baadaye. Huu ni mfano wa matumizi mabaya ya madaraka!
Habari ya ubadhilifu huu zilimfikia mwenye mali na hivyo kumtaka wakili wake kujiandaa kutoa hesabu ya uwakili wake. Hebu tuangalie kwa undani kidogo jinsi alivyokuwa mjanja katika maamuzi yake. Wakili huyu aliwapunguzia madeni wadaiwa wote. Tendo hili lina maana kubwa mbili: (i) linamrudishia mwenye mali sifa yake njema mbele za watu. Kwa kuwa yeye ni wakili tu chochote alichofanya basi watu walijua ameagizwa na mwenye mali. Hivyo watu waliopunguziwa madeni wao moja kwa moja walimwaga sifa na shukrani kwa mwenye mali. Hivyo bila shaka walimsifu mwenye mali kwa wema wake, kwa huruma yake na kwa kujali wengine. Hivyo kwa ujanja wakili huyu dhalimu anajenga mazingira ambayo yanamrudishia bosi wake sifa yake njema mbele za watu- sifa ambayo awali wakili aliifachua kwa matendo yake. (ii) lilimjengea urafiki na watu na kumwandalia mazingira ya kusaidiwa baadaye. Waliokuwa na madeni walimtazama wakili dhalimu kama mkombozi wao maana waliamini kuwa amewaombea punguzo la madeni kwa mwenye mali. Hivyo kama angefukuzwa kazi bado wangempokea na kumsaidia kwa kumbukumbu kuwa alishawahi kuwasaidia kupunguziwa madeni yao. Wakili huyu alitumia ujanja kuandaa maisha yake ya baadaye ikiwa atafukuzwa kazi. Kwa kweli hata leo “ujanja wa kiroho” unahitajika ili kuandaa maisha yetu ya baadaye baada ya Maisha ya hapa duniani.
Kutoka katika Injili tunafundishwa mambo yafuatayo: (i) Tutapaswa kutoa hesabu ya uwakili wetu katika vyote tulivyokabidhiwa. Tuwapo hapa duniani tukumbuke kuwa Mungu ametukabidhi mali nyingi tuzitumie na kuzisimamia kwa niaba yake: imani, muda, karama, vyeo na nyadhifa, utumishi na usimamizi wa familia, jamii, kanisa na taifa kwa ujumla. Ni lazima kuwa waaminifu katika majukumu tuliyokabidhiwa maana baada ya uwakili wetu hapa duniani tutaitwa mbele ya mwenye mali kutoa hesabu ya uwakili wetu. Kwa bahati mbaya wengi wetu tumekosa uaminifu katika uwakili wetu hapa duniani kwani tumetapanya mali tulizopewa kuzisimamia: tumetumia muda vibaya kwa starehe na anasa, tumejinufaisha wenyewe kupitia mali za umma, tumezika karama na vipaji vyetu, tumeshindwa kutimiza majukumu yetu ya kusimamia familia, jamii, kanisa na taifa katika mapana yake. Tunapaswa kuwa mawakili waaminifu. Yesu anasisitiza kuwa uaminifu unapimwa kwanza kwa/katika mambo madogo madogo. Wizi, ubadhilifu, uzembe na vilema vingine huwa vinaanza kwa kudharau mambo madogo madogo. Maandiko Matakatifu yanasisitiza uaminifu katika mambo madogo madogo “Anayepuuza mambo madogo ataanguka kidogokidogo” (YbS 19:1) na tena mmoja wa walimu wangu wa Seminari Kuu Kibosho alikuwa daima anasema, “Daima mtu mkubwa huaibishwa kwa vitu vidogo vidogo” akitolea mfano kuwa kitendo cha mtu mzima kukosa leso ya mafua iuzwayo Tshs. 200/= kinaweza kumwaibisha mtu huyu akiwa na mafua na hana leso.
Uaminifu ni msingi mkubwa katika maisha. Tutimize kwa uaminifu jukumu letu la uwakili. (2) Tunapaswa kuwa wajanja kurekebisha mwenendo wetu sasa ili kujenga taswira nzuri na halisi ya Kristo aliyetuaminisha uwakili wa imani. Vyote tulivyonavyo (tukiwemo na sisi wenyewe) ni mali ya Kristo/Mungu. Mungu ametufanya mawakili wa mali zake: maisha, imani, wito na mengineyo. Tunaposhindwa kuishi kulingana na hadhi na utume wetu, basi tujue kuwa tunaharibu pia hadhi ya Kristo mwenyewe kama ambavyo wakili dhalimu aliharibu sifa njema ya bwana wake kwa kutokuwa mwaminifu katika jukumu alilokabidhiwa. Kwa bahati mbaya hata sisi kuna nyakati tunaishi na kutenda mambo ambayo hata wapagani wanatushangaa kama kweli sisi ni Wakristo na kama kweli tumefundishwa hivyo na Kristo. Sasa katika hali kama hii tunapaswa kuwa wajanja katika kufanya maamuzi ambayo yatarudisha siyo tu sifa yetu njema mbele za watu bali hasa taswira njema na halisi ya Kristo aliyetupa jukumu la uwakili. Ujanja ni pamoja na kugeuza mwenendo wetu wa maisha (wongofu), kujongea sakramenti ya kitubio na kujenga mahusiano mazuri na watu, kwa kutaja tu machache. (3) Utumishi wetu kwa Mungu unapaswa kuwa kipaumbele chetu cha kwanza.
Yesu anatambua wazi kuwa mali, licha ya kumsaidia mwanadamu katika maisha yake ya kawaida, bado zinamweka mwanadamu katika hatari ya kukosa uzima wa milele. Katika mahangaiko yake mwanadamu anashawishika tuzitumikia mali badala ya kumtumikia Mungu. Mali zimewekwa ili zimtumikie mwanadamu na wala siyo mwanadamu azitumikie mali. Kwa bahati mbaya tumejikuta tunazisujudi mali tukidhani zinatatua shida zetu zote, tukidhani zinaleta furaha na amani, tukidhani zitatuwezesha kujitosheleza na hivyo kutomuhitaji Mungu. Hii ndiyo hatari ya mali. Leo Yesu anatukumbusha kuwa hatuwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja: “Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.” Mungu ni Muumba na mali ni kiumbe. Ni mpuuzi tu anayeweza kuchakua kiumbe na kukitumikia. Malizinapaswa kutusaidia kumtumikia Mungu na watu. Dominika njema.